Monday, November 13

Wanaosubiri kuchimbiwa vyoo vya msaada waelezwa wasahau


Mkuu wa wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma, Louis Bura ametathmini baadhi ya watu wasivyojituma kisha akawaambia wanaotegemea msaada wa kuchimbiwa vyoo wasahau kwa kuwa haitatokea wakaupata katika kipindi hiki.
Bura hakuishia hapo, bali alikwenda mbali zaidi na kusema hata wale wanaosubiri msaada huo kutoka kwa wafadhili ni wazi wamepitwa na wakati kwa vile mambo hayo hayapo tena.
Kauli hiyo aliitoa jana wakati wa shughuli ya kuweka mazingira safi na afya salama wilayani Kibondo kupitia mradi unaotekelezwa katika vijiji 10 kwa kuhamasisha jamii kuchimba na kutumia vyoo bora ili kutunza vyanzo vya maji.
“Muda wa kusaidiwa na mjomba hata kuchimba choo haupo tena, wananchi tujue kwamba mambo yanayohusu ulinzi wa afya zetu ni lazima tuyagharamie kwani siku tukiugua magonjwa yatokanayo na kutumia maji machafu au ukosefu wa vyoo ndipo tutakapoona umuhimu,” alisema Bura.
Mratibu mradi kutoka shirika la TCRS, Terry Raphael alisema mradi huo unalenga kuielimisha jamii juu ya matumizi ya vyoo bora na usafi wa mazingira.
Ofisa afya, maji na usafi wa mazingira kutoka shirika la misaada la Norway (NCA), Zakayo Makobero aliwataka wakazi wa Kibondo kutumia ujuzi waliopata kuelimisha wengine juu ya umuhimu wa kulinda vyanzo vya maji na kuvitumia kwa usahihi.

No comments:

Post a Comment