Monday, November 13

Wanafunzi 400 wanavyopokezana darasa


Mkuu mpya wa mkoa wa Geita, Robert Lughumbi amekutana na jambo jipya katika elimu baada ya kuambiwa madarasa mawili yenye wanafunzi 400 yanachangia chumba kimoja.
Mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Nyarubanga wilayani hapa, Boaz Masalu amemwambia Lughumbi kuwa, shule yake yenye wanafunzi 1, 799 ina vyumba sita vya madarasa, hali inayosababisha baadhi ya darasa kukaliwa na wanafunzi zaidi ya 300.
Mwalimu huyo akamweleza mkuu wa mkoa ambaye aliteuliwa hivi karibuni na Rais Magufuli kuwa, wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili wanaofikia 400 wanachangia chumba kimoja kusomea na hupokezana kwa zamu. Shule hiyo pia inakabiliwa na upungufu wa matundu ya vyoo na kwa sasa ina matundu manne yanayotumiwa na wanafunzi 1,799. Kutokana na upungufu wa vyumba vya madarasa 8,000 vinavyoukabili mkoa huo katika shule za msingi, Lughumbi ameanza kampeni ya ujenzi kupitia michango na nguvu ya wananchi pamoja na wadau.
Kwa kuanzia ameanza kuhamasisha ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa kuchimba msingi katika shule hiyo inayokabiliwa na upungufu wa vyumba 34 vya madarasa. “Haiwezekani Geita inayosifika kwa utajiri wa dhahabu karibia kila eneo liendelee kukabiliwa na changamoto ya uduni wa huduma za kijamii na maendeleo ikiwamo upungufu wa vyumba vya madarasa, lazima tufikie lengo na sera ya elimu ya darasa moja kutumiwa na wanafunzi wasiozidi 45,” alisema Lughumbi.
Katika hafla ya kuhamasisha ujenzi wa madarasa shuleni hapo, mifuko 200 ya saruji ilipatikana kupitia michango ya wananchi, viongozi wa halmashauri, ofisi ya mkuu wa wilaya na mbunge wa Geita pamoja na ile ya mkuu wa mkoa.
Akishukuru kwa niaba ya wananchi, diwani wa Luenzera, Jeremia Misango aliwataka wananchi kujitokeza kuchangia miradi ya maendeleo katika maeneo yao badala ya kutegemea Serikali na wafadhili.

No comments:

Post a Comment