Monday, November 13

CCM, Chadema wanavyotifuana kwenye kampeni za udiwani


Mwenyekiti  Chadema Taifa, Freema Mbowe
Mwenyekiti  Chadema Taifa, Freema Mbowe akizungumza wakati wa Mkutano wa kampeni wa uchanguzi  mgodo wa udiwani  Kata ya Reli uliofanyika katika Uwanja wa Serengeti  Mjini Mtwara jana. Picha na mpigapicha Wetu 
Siku 17 tangu kuanza kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata 43 nchini, vyama vya CCM na Chadema vimeendelea kupimana ubavu.
Kampeni za uchaguzi huo zilianza Oktoba 27 na zitahitimishwa Novemba 25. Uchaguzi umepangwa kufanyika Novemba 26.
Akizungumzia mwenendo wa kampeni hizo, katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Elias Mpanda alisema jana kuwa chama hicho hakitumii nguvu kubwa kwa kuwa kina uhakika wa kushinda kata zote nane mkoani humo.
Alisema hilo linatokana na kazi zinazofanywa na Rais John Magufuli ambaye ni mwenyekiti wa CCM kwa kuwa amefungua njia na kila mmoja anaona utendaji kazi wake, hivyo chama hicho kinaaminiwa.
Mgombea udiwani wa Kata ya Muriet (CCM), Francis Mbise aliwaomba wananchi kumchagua ili kuibadili kata hiyo kwa kuhakikisha huduma ya maji inapatikana.
Kwa upande wake, mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amemshauri Rais Magufuli kusikiliza kilio cha wananchi kuhusu Katiba Mpya.
Akizungumza katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni za udiwani Kata ya Moita wilayani Monduli, Lowassa alisema nchi inakwenda vizuri kwa katiba iliyo bora na kwamba, nchi inaongozwa kwa umoja na hakuna nchi ambayo inaongozwa na mtu mmoja.
Lowassa alisema haiwezekani katika uchaguzi mgombea mmoja anapata kura milioni sita lakini hapati kitu na mshindi anapata kura milioni nane.
“Mimi walinipa kura milioni sita na Magufuli alipata kura milioni nane na kutangazwa mshindi sasa haiwezekani kura sita milioni kutosikilizwa,” alisema na kuongeza kuwa, katika nchi nyingine aliyepata kura milioni sita anapata nafasi.
Aliwataka wananchi wa Moita kumchagua mgombea wa Chadema, Loburu Lomyaki akisema kata hiyo ni miongoni mwa alizowezesha maendeleo wilayani Monduli alipokuwa mbunge.
“Hapa kuna maji, umeme, shule mbili za kata na maendeleo mengine nawahakikishia sintowasahau,” alisema.
Chadema kamwe haitakufa
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema siku atakayoingia kaburini ndiyo wasaliti watafanikiwa kukivunja chama hicho.
Alisema ametoka mbali akiwa na watu anaowaamini na waliojiita wanamapinduzi ambao baadaye waliteleza.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo katika Kata ya Reli mkoani Mtwara, alisema silaha pekee ya kusonga mbele katika siasa za upinzani ni kuungana.
Alisema mwaka 2015 alijaribu kwa kila hali kufanikisha hilo kwa kuwataka alioamini wana mapinduzi wenzake kuweka masilahi yao pembeni na kuangalia mustakabali wa Taifa.
“Niliwaambia wenzangu Dk Wilbroad Silaa weka masilahi yako pembeni, Profesa Ibrahim Lipumba weka masilahi pembeni na nikajiambia Mbowe weka masilahi pembeni. Cha kushangaza Profesa Lipumba na Dk Slaa wakateleza, mimi nimekomaa na wasaliti waliowarubuni wao wamejaribu kwa kila hali kuivunja Chadema, lakini wamegonga mwamba na ninasema litafanikiwa hilo siku nikiingia kaburini,” alisema Mbowe.
Kuhusu umuhimu wa Katiba Mpya, Mbowe alisema upo palepale na si takwa la watawala bali ni la wananchi.
“Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kwa Katiba hii mtu akiamua kuwa dikteta anakuwa kwa sababu inampa mamlaka makubwa Rais,” alisema Mbowe.
Kukosekana Nyalandu
Aliyekuwa mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu aliyejiondoa CCM alishindwa kupanda jukwaani mjini Mtwara katika mkutano wa Chadema.
Mbowe akihutubia mkutano wa kampeni ya uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Saranga jijini Dar es Salaam alisema amempokea Nyalandu na jana na angeungana naye kwenye mkutano mjini Mtwara.
Hata hivyo, kukosekana kwa ndege inayofanya safari kati ya Dar es Salaam na Mtwara kumemsababishia Nyalandu kushindwa kuhudhuria mkutano huo.
Mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano na mambo ya nje wa Chadema, John Mrema alisema Nyalandu aliyekuwa Nairobi nchini Kenya kumjulia hali Tundu Lissu amekosa ndege ya kwenda Mtwara.
Mke wa mgombea jukwaani
Stella Mang’ati, mke wa mgombea udiwani Kata ya Kitwiru, Manispaa ya Iringa kwa tiketi ya CCM, Baraka Kimata alipanda jukwaani kumuombea kura mumewe akitumia fursa hiyo kujibu maswali kadhaa aliyodai yameibuliwa na wapinzani kwamba amekuwa hafuatani na mumewe kwenye kampeni.
“Maswali mengi nimeyapata hata ninyi mmeyasikia, wanasema mnatembea na mgombea hana mke waambieni leo mmeniona,” alisema.
Kimata aliyekuwa diwani wa kata hiyo kupitia Chadema kabla ya kujiuzulu na kuhamia CCM alisema baadhi ya miradi alishindwa kuitekeleza kutokana na kutokuwa na maelewano mazuri na viongozi wake wa juu.

No comments:

Post a Comment