Sunday, August 20

Katibu Soko la Sido ashikiliwa kwa uchochezi

Mfanyabiashara wa Soko la Sido mjini Mbeya

Mfanyabiashara wa Soko la Sido mjini Mbeya akilalamikia kitendo cha Serikali kuwazuia kujenga vibanda vya kudumu ndani ya soko hilo lililoteketea kwa moto.Picha na Godfrey Kahango 


Wakati hali ya amani na utulivu ikiwa imerejea katikati ya Jiji la Mbeya baada ya kutokea vurugu juzi mchana, jeshi la polisi limesema linawashikilia watu 18 akiwamo Katibu wa Wafanyabiashara wa Soko la Sido, Alanus Ngogo kwa tuhuma za kuchochea vurugu hizo.
Juzi mchana, polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi, maji ya kuwasha na upupu kuwatawanya wanafabiashara wa soko hilo waliokuwa wamegoma kutekeleza agizo la Serikali la kuwataka kutoendelea na ujenzi wa vibanda vya kudumu ndani ya soko hilo ambalo liliteketea kwa moto na kuunguza mali zote usiku wa kuamkia Agosti 15 mwaka huu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohammed Mpinga aliliambia gazeti hili jana kwamba baada ya kutokea kwa vurugu kuna watu waliokuwa katika soko hilo la Sido waliingia na kufunga barabara kuu ya Tanzania-Zambia kwa mawe na magogo huku wakipiga mawe magari yaliyokuwa yakipita.
“Katika tukio la juzi tuliwakata watu 18 hawa kosa lao ni kuingia barabarani na kuanza kupanga mawe na magogo na kuzuia magari yasipite barabara kuu ya Tanzania-Zambia kuanzia Kabwe hadi Mafiati.
“Lakini yule katibu wa soko (Alanus Ngogo) yeye anatuhumiwa kwa kosa la uchochezi kwani juzi ile mimi nilipopanda jukwaani na kuwataka watu wote waende nyumbani kwao kwa usalama wao yeye alichukua kipaza sauti na kuanza kuwahamasisha watu wasiondoke eneo lile akitamka ‘tutakesha hapa hapa’ na maneno mengine ya kukashifu,” alisema Kamanda Mpinga.
Alisema watuhumiwa wote wanaendelea kuhojiwa na baada ya kumalizika kwa mahojiano watapandishwa kizimbani kujibu tuhuma zao.
Kuhusu hali ya usalama, Kamanda Mpinga alisema ulinzi katika jiji hilo umeimarishwa na polisi wapo doria muda wote na watu waliamka alfajiri kuendelea na shughuli zao maeneo mengi hususan Soweto, Kabwe, Manjelwa hadi Mafiati ambako juzi biashara zilifungwa kutokana na usalama kuwa mdogo.
Hata hivyo, Serikali ya Mkoa wa Mbeya kupitia kwa Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Paul Ntinika ilisisitiza kusimamia msimamo wake wa kutowaruhusu wafanyabiashara hao kuendelea na ujenzi wa vibanda vyao tofauti na ombi lao kutaka kuruhusiwa.
Ntinika aliwataka wafanyabiashara hao kuwa na hali ya utulivu na uvumilivu kwa kusubiri siku tano zilizotengwa na Serikali ili kupisha kamati maalumu iliyoundwa kufanya tathmini ya hasara iliyojitokeza kutokana na janga hilo pamoja na kuchunguza kiini cha moto huo.

MWANAMKE MTANZANIA ASHINDA TUZO YA MHASIBU KIONGOZI




Maelfu ya Watanzania wanaishi Uingereza. Wapo wanaoonekana kwenye mitandao jamii na wanaoendelea na shughuli zao bila kusikika. Joyce Materego ni mfano huo. Baada ya kumaliza masomo 2004 alianza kazi ya uhasibu. Anasema mhasibu ni mtu anayeelewa na kutathmini vyema hesabu.
“Kazi yangu ni kuhakikisha fedha zinazoingia ni nyingi kuliko zinazotoka,”anasema. Materego anafafanua kuwa uhasibu ulihitaji kutimiza mitihani 14 kipindi cha miaka 10. Hati inayotolewa ya ACCA (Jumuiya ya Wahasibu Duniani – Association of Chartered Accounts) hutambuliwa popote pale kama walivyo walimu, madaktari na kadhalika. Mafunzo je? Huhusu sheria, kodi, uchumi na kadhalika.
“Unajengwa kisaikolojia kuwa wewe ni mlinzi. Kama daktari anavyoaminiwa na maisha ya watu, wewe unafadhiwa na fedha za watu na makampuni,” anasema.
Badala ya kuchukua miaka 10, Mtanzania huyo alimaliza mafunzo miaka minne tu. Ana bidii sana.
Karibuni aliteuliwa kati ya wafanyakazi wanaowatia wenzao changamoto. Picha iliyotolewa na jarida la kisekta la Focus, kibaruani inaonyesha kasimama na wanaume wawili wa Kizungu na zawadi zao. Nywele sio za bandia, zimesukwa butu kubwa linalotukuza Uafrika. Ni naadra siku hizi kuona mwanamke akisuka namna hiyo. Kila analofanya Materego lina maana na uzito fulani. Mbali ya kulea wanawe wanaosoma sekondari, huenda kazini alfajiri - siku tano kwa wiki na kurejea kuwapikia na kuwahudumia kila siku.
Ingekuwa Tanzania angeajiri mtu wa kufanya kazi nyumbani. Ulaya hilo halipo.
Mbali na kulea, Materego ni mjuzi sana wa lugha na mara kwa mara huajiriwa kama mkalimani wa Kiswahili na Kiingereza fasaha..
Anafanya wapi kazi?
Kaajiriwa na shirika la fadhila linalohudumia watoto maskini la Child Poverty Action Group (CPAG). Mwaka 2015, CPAG ilidai asilimia 28 ya watoto wa Uingereza ni hohehahe. “Ulimwengu mzima” anatathmini. “Tunatakiwa tujue kuna watu wanaoishi maisha ya fahari na duni. Hata Uingereza tuna tatizo hilo. Kampuni yangu inachojaribu ni kuongea na Serikali kuhakikisha wanasiasa wanabadilisha mwongozo wa jinsi fedha za Serikali zinavyotumika kuinua hali ya watoto katika uduni, wawe sawa na wengine.
Unaweza kukuta mtoto anayekulia hali duni kiasi hali nzuri, akienda shule hasikilizi vizuri na hivyo vyote afya kwa mtoto vinachangia mtoto kufanya kazi vizuri.”
Kwanini akapewa tuzo?
Tuzo ilihusiana na namna anavyowasiliana vizuri na wafanyakazi wenzake na wateja wa shirika. Huo ni mfano mzuri wa baadhi ya Watanzania (tusiowajua) wanaolea, huku wakichapa kazi na kutoiaibisha nchi yetu ugenini. Ni siri pia ya undani wa Watanzania. Sisi ni watu waungwana sana kwa ujumla, wageni husema. Tuzo si fedha, bali cheti cha uongozi katika masuala ya fedha. Alisisitiza kuwa usimamiaji wa fedha ni suala muhimu katika sekta na vitengo vyote vinavyotawala dunia zikiwamo kampuni za kibiashara, taasisi za wilaya na mikoa, kiserikali, huduma katika jamii, sanaa na hata uchumi wa nyumbani.
Tumpe hongera mama huyo wa watoto. Kama walivyosema Mwalimu Julius Nyerere na mpigania haki za watu weusi nchini Marekani, Malcolm X ukimuelimisha mwanamke unaelemisha Taifa zima.

Mahakama yazuia bomoabomoa kwa nyumba 286 Dar


Dar es Salaam. Wakati operesheni ya ubomoaji wa nyumba zilizoko ndani ya umbali wa mita 121.5 kutoka katikati ya Barabara ya Morogoro ikiendelea maeneo ya Kimara mpaka Kiluvya jijini Dar es Salaam, Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi imeziwekea kinga ya muda nyumba 286 zinazohusika.
Uamuzi huo wa Mahakama ulitolewa juzi na Jaji Leila Mgonya kutokana na maombi ya zuio yaliyowasilishwa mahakamani hapo na wakazi hao 286 wa maeneo ya Ubungo- Maji hadi Kiluvya wakiomba itoe zuio la muda hadi kesi yao ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Maombi hayo ya zuio la muda kusubiri uamuzi wa kesi ya msingi yamepangwa kusikilizwa Agosti 30 baada ya upande wa wajibu maombi (Serikali) kuwasilisha hati ya kiapo kinzani.
Hata hivyo, wakati wakisubiri usikilizwaji wa maombi ya zuio la muda, wananchi hao kupitia kwa wakili wao, Benito Mandele waliwasilisha maombi ya dharura wakioomba mahakama hiyo iamuru hali iendelee kuwa kama ilivyo kwa sasa hadi maombi hayo yatakaposikilizwa.
Jaji Mgonya anayesikiliza shauri hilo alikubaliana na maombi hayo na kuamuru hali iendelee kuwa kama ilivyo kwa sasa hadi tarehe hiyo ya maombi hayo yatakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Akizungumza na Mwananchi baada ya kutolewa kwa uamuzi huo, wakili Mandele alisema kuwa waliamua kupeleka maombi hayo ya kudumisha hali iliyopo kwa sasa baada ya kuona Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) wameanza kutekeleza operesheni hiyo wakati maombi yao ya zuio yakiwa bado hayajasikilizwa.
Kwa uamuzi huo, Tanroads ambayo ndiyo mtekelezaji wa operesheni hiyo haitaweza kuzigusa nyumba hizo hadi hapo mahakama itakavyoelekeza vinginevyo baada ya usikilizwaji wa maombi hayo ya zuio la muda kusubiri kesi ya msingi kumalizika.
Wakili Mandele alisema kuwa watakachofanya baada ya kupata hati ya amri hiyo ya mahakama wataitoa nakala nyingine na kuwagawia kila mdaiwa kwa ajili ya kuiweka kwenye nyumba yake.
Katika kesi ya msingi namba 284 ya mwaka 2017, wananchi hao wanaiomba mahakama itamke kuwa wao ni wamiliki halali wa maeneo hayo yenye mgogoro na kwamba hawapo katika hifadhi ya barabara.
Pia, wanaiomba mahakama hiyo iamuru kuwa kama Serikali inata kuwahamisha na kuyachukua maeneo yao, basi iwalipe fidia stahiki kwa mujibu wa sheria.
Tanroads imetoa notisi kwa wakazi wote walipo katika umbali wa mita 121.5 kutoka katikati ya barabara ya Morogoro kila upande, kuanzia Ubungo - Maji hadi mpakani mwa Dar es Salaam na Pwani kuvunja nyumba zao kwa madai kuwa wapo kwenye hifadhi ya barabara.
Hivyo, Tanroads waliwataka wananchi hao kuondoka katika maeneo hayo ili kupisha upanuzi wa barabara hiyo.
Wananchi hao wanapinga amri hiyo wakidai kuwa wanaishi katika maeneo hayo kihalali kwa kuwa wana hatimiliki halali na hawapo kwenye hifadhi ya barabara, huku wakihoji sheria iliyotumika kuidhinisha umbali huo wa mita 121.5.
Kutokana na hali hiyo, wananchi hao wameamua kwenda mahakamani katika makundi tofauti na kufungua kesi tofautitofauti kupinga operesheni hiyo wakidai kulipwa fidia kama Serikali itawahamisha.
Mbali na kesi hiyo iliyotolewa amri hiyo, pia kuna kesi nyingine mbalimbali ambazo ziko katika hatua mbalimbali.
Kesi hizo nyingine ni ile iliyofunguliwa na Abdallah Maliki kwa niaba ya wenzake 570 ambao ni wakazi wa maeneo ya Kimara, Mbezi na Kiluvya dhidi ya Tanroads na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kwa upande mwingine.
Shauri jingine ni maombi ya kibali cha kufungua kesi ya uwakilishi kupinga operesheni hiyo lililofunguliwa na Ephrahim Kavishe na wenzake wanne ili wawe wawakilishi wa wenzao zaidi ya 198 ambao ni wakazi wa Kimara Stop Over na Mbezi.
Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye ni mmoja wa wajibu maombi hayo amewawekea pingamizi akiiomba mahakama hiyo iyatupile mbali maombi hayo huku akiainisha kasoro mbalimbali za kisheria.
Maombi hayo yanasikilizwa na Jaji Crencecia Makuru na amepanga kutoa uamuzi kuhusu pingamizi hilo Agosti 30, uamuzi ambao ndio utakaotoa hatima ya maombi hayo kama yataendelea kusikilizwa au yatatupiliwa mbali.     

Ukusanyaji michango ya harusi sasa kwa mbinde


Moshi. Wakati kiwango cha michango ya harusi inayochangwa na marafiki kikiporomoka kwa kasi nchini, washereheshaji (Ma-MC) wameanza kutumia mashine za kielektroniki za EFD ili kutoa stakabadhi.
Baadhi ya washereheshaji (ma-MC), wameenda mbali na kuwataka wenye kumbi zinazotumika kwa sherehe hizo kutowaruhusu washereheshaji ambao hawatawaonyesha kuwa wanatumia EFD.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa ile ari ya uchangiaji harusi iliyokuwapo miaka ya nyuma imeporomoka kwa kasi kubwa sasa.
Kulingana na uchunguzi huo, katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, harusi za kifahari zilizokuwa zikifungwa ni nyingi kulinganisha na miaka miwili iliyopita kutokana na ugumu wa maisha.
Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, bajeti ya chini ya harusi au kumuaga bibi harusi (send off), ilikuwa kati ya Sh5 milioni na Sh7 milioni wakati kiwango cha juu kilikuwa zaidi ya Sh60 milioni.
Hata hivyo, sasa mambo yamekuwa tofauti kwani bajeti za harusi zinazopangwa na wanakamati zinakusanya kati ya asilimia 50 na 75 tena ni kwa wale wenye ndugu wenye uwezo.
Ugumu kukusanya michango
Uchunguzi huo umebaini kati ya kazi ngumu kwa sasa ni ukusanyaji wa ahadi za michango ya harusi, send off au kitchen party kutokana na kile kinachoelezwa kuwa watu ni wagumu kutimiza ahadi zao.
Chanzo kimoja kimedai kuwa kila mtu analia mambo yamebadilika na kwamba unapoonekana unafuatilia sana michango wapo watu ambao hufikia hatua ya kuzuia mawasiliano ya simu.
“Huu usawa wa sasa si kabisa. Kila mtu analia hana hela sasa hizo za kuchangia harusi anazitoa wapi? Ukiona mtu anakuchangia harusi zama hizi mshike sana huyo,” alidokeza mshereheshaji mmoja.
Mkazi wa Pumuwani mjini Moshi, Ewald John alisema anazo kadi tatu za harusi za marafiki wa karibu, lakini ameshindwa kuwachangia kwa sababu hali ya kifedha imekuwa ngumu. “Mimi nina kadi tatu, lakini mbili zimeshapita. Sio kwamba nilikuwa sijui lakini kiukweli sina pesa nafanyaje? Nafikiri Watanzania sasa tubadili aina ya maisha, hii michango haitawezekana,” alisema.
Mshereheshaji mashuhuri nchini, Sijabu Kiata alisema kiujumla hali ya maisha imebadilika na hata harusi zinazofanyika sasa si za gharama kubwa kulinganisha na miaka mitano au 10 iliyopita.
“Watu hawana pesa wala hilo sio suala la kuuliza. Kuna harusi unaenda unakuta inapita round (mzunguko) moja tu ya vinywaji kabla ya chakula na nyingine wakati wa chakula, basi,” alisema.
Wakili wa kujitegemea wa jijini Arusha ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini, alisema kama michango ya harusi ingekuwa ya lazima, basi ingebidi watumike madalali kuikusanya.
“Katika kazi mojawapo ngumu kwa sasa ni kukusanya michango ya harusi. Unaweza hata mkapishana kauli na mtu unayeheshimiana naye pale anapokwambia hali ni ngumu. Hali imebadilika,” alisema na kuongeza:
“Huko tunapoelekea itabidi mtu anayetaka kuoa ajiandae mwenyewe na marafiki zake wa karibu, tena unaalika watu wasiozidi 20 mkitoka kanisani mnaenda hotelini mnakula mnarudi nyumbani”.
Mkurugenzi wa Mfinanga Block Supply ya Mbezi Beach jijini Dar es Salaam, Hussein Mfinanga alisema kutokana na mabadiliko ya maisha hivi sasa anafikiria kusitisha uchangiaji wa harusi.
“Huko nyuma mtu anakupa kadi na anakwambia kama humchangii kuanzia Sh100,000 basi usimchangie. Sasa hivi peleka kadi na masharti hayo uone kama utachangiwa,” alisema.
Mfinanga alisema siku za nyuma kuna harusi ilikuwa mtu akichanga Sh20,000 anapewa kadi ya mtu mmoja (single) na wale wanaochangia zaidi ya Sh50,000 ndio wanapewa kadi ya watu wawili, akisema hilo litafutika.
Ma-MC, TRA nao watoa neno
Baadhi ya washereheshaji waliozungumza na Mwananchi jana walipongeza hatua ya Serikali kuwataka waanze kutumia mashine za EFD, lakini wakataka kuwapo mfumo wa kuwabana ma-MC wote.
Kiata alisema japokuwa ni mpango wa Serikali wa kuwataka washereheshaji wote kulipa kodi na kutumia mashine za EFD, utekelezaji wake ni wa kusuasua.
“Mimi nina mashine ya EFD tangu mwaka jana lakini wengi hawana na hii maana yake hawalipi kodi. Hii si sahihi. Ni lazima TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) ije na mfumo unaoeleweka,”alisema.
“Maisha yamebadilika hakuna pesa kabisa unaweza kukaa mwezi mmoja hujapata kazi na bahati mbaya hii kazi imeingiliwa, watu wanashusha bei hawana EFD mashine, ni vurugu tu.”
“TRA waziamuru hizi kumbi zinazotumika kwa hizi sherehe kuhakikisha kuwa kila MC anayeingia katika ukumbi aonyeshe risiti ya EFD aliyomkatia mwenye harusi. Lazima kuwe na usawa.”
Mshereheshaji mwingine, Ntoly Mayombola alisema hakuna MC anayepinga kutumia mashine hizo, lakini tatizo ni ughali wake kulinganisha na vipato vya washereheshaji.
“Tatizo unainunuaje? Unalipwa Sh100,000 au 150,000 au 200,000 lakini tunaambiwa mashine ni zaidi ya Sh700,000. Bado huu mfumo Serikali inatakiwa itoe bure hizo mashine,” alisema Mayombola.
Msimamo wa TRA
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Walipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo alipongeza hatua ya baadhi ya washereheshaji kuanza kutumia mashine hizo.
“Tunataka (washereheshaji) wote waingie kwenye kutoa risiti za EFD na mwaka jana tulikaa nao na wako willing (tayari) kutumia hizo mashine. Tunaendelea kuwahamasisha wafanye hivyo mapema,” Kayombo.
Kayombo alisema matumizi ya EFD yatawasaidia Ma-MC kupata kazi kwa vile wananchi hivi sasa wana mwamko wa kudai risiti za kielektroniki na kwamba, wasio nazo inawanyima kazi kubwa hasa za Serikali.   

Askari wadaiwa kuruhusu magari mabovu barabarani

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Fortonatus Musilimu (kulia) na askari wa kikosi chake kikagua moja ya mabasi ya abiria jana alfajiri  katika Kituo Kikuu cha Mabasi jijini Mbeya katika ukaguzi wa kushitukiza, ambapo mabasi kadhaa yalikuwa na ubovu katika mfumo wake wa usukani, tairi vipara na matatizo mengineyo na kuyazuia.  Picha na Godfrey Kahango 
Mbeya. Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Fortunatus Musilimu ameagiza askari saba wa kikosi hicho katika Kituo Kikuu cha Mabasi Mbeya waondolewe kituoni hapo kwa madai ya kuruhusu mabasi mabovu kubeba abiria.
Kamanda Musilimu alimuagiza Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Mbeya (RTO) Butusyo Mwambelo kutekeleza amri hiyo jana baada ya kufanya ukaguzi wa kushtukiza katika mabasi na madereva eneo hilo.
“Hawafanyi kazi ipasavyo na hii inatokana na kukaa kituo kimoja zaidi ya miaka mitano,” alisema Kamanda Musilimu.
Pia, alisitisha mabasi matano kutoendelea na safari baada ya kubaini hitilafu kwenye mfumo wa usukani na magurudumu.
Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) Mkoa wa Mbeya, Denis Daud alisema chombo cha moto lazima kifanyiwe ukaguzi na maofisa wa polisi kama kina sifa ya kuingia barabarani.
Mdau wa usafiri, Mohamed Abdalah alisema ukaguzi uliofanywa na kamanda unaisadia kubaini mabasi ambayo hayaruhusiwi kuwapo barabarani. 

Maalim Seif aendelea kulia na hujuma akimlima barua msajili


Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad ameendelea kulia na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kutokana na kile alichodai ni hujuma anazozifanya dhidi ya chama hicho akishirikiana na Profesa Ibrahim Lipumba.
Maalim Seif alieleza hayo juzi katika barua yake ya kumjibu Jaji Mutungi kuhusu hatua yake ya kuwatambua Profesa Lipumba kama mwenyekiti halali wa CUF na Magdalena Sakaya kama kaimu katibu mkuu wakati viongozi hao walisimamishwa uanachama kwa tuhuma mbalimbali.
Katibu mkuu huyo alifikia uamuzi wa kumjibu Jaji Mutungi baada ya ombi lake la kuwafukuza uanachama wabunge wawili; Sakaya (Kaliua) na Maftaha Nachuma (Mtwara Mjini) kugonga mwamba kutokana na msajili kumtambua Sakaya kama kaimu katibu mkuu kufutia maelezo aliyopewa na Profesa Lipumba.
Profesa Lipumba alimweleza Msajili kuwa Maalim Seif ameshindwa kutekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja na kutofika ofisi ya chama hicho zilizopo Buguruni, hivyo akamteua Sakaya ambaye ni Naibu Katibu Mkuu Bara kukaimu ukatibu mkuu.
“Kwa mujibu wa katiba ya CUF mimi, Maalim Seif bado ni katibu mkuu wa chama hiki na nipo hapa nchini, ni mzima na nina akili timamu. Na nafasi yangu haiwezi kukaimiwa na Sakaya ambaye tulishamsimamisha uanachama,” inaeleza barua hiyo.
“Mheshimiwa msajili, nashangaa kwa maelezo yako. Mimi ninavyojua ni kuwa kiongozi anakaimiwa ikiwa hayupo nchini au hawezi kutekeleza majukumu yake. Hivyo ndivyo katiba ya CUF ya 1992 (toleo la 2014) kifungu cha 105 (1) kinavyoeleza.”
Aliongeza kuwa Jaji Mutungi alipokea barua ya Profesa Lipumba Machi 16, 2017 huku yeye akiwa hapa nchini akiendelea na shughuli za chama hasa katika ofisi ya makao makuu ya chama hicho iliyopo Zanzibar kwa mujibu wa katiba ya CUF.
Maalim Seif alisema cha kushangaza Msajili wa Vyama vya Siasa alitoa uamuzi kutokana na maelezo ya mwenyekiti anayetambuliwa na ofisi yake. Kutokana na hilo, mwanasiasa huyo alimtaka Jaji Mutungi kuangalia katiba ya CUF ya mwaka 1992 (toleo la 2014) kifungu Na. 1 (2) vinavyoeleza kwamba makao makuu ya chama hicho yatakuwa katika Mji Mkuu wa Zanzibar na anuani yake itakuwa kama itakavyoamuliwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa.
Alisema kifungu cha 1 (3) kinaeleza kwamba kutakuwa na Ofisi Kuu ya Makao Makuu ya Chama Dar es Salaam na anuani yake itakuwa kama itakavyoamuliwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa.
“Kwa mantiki hii, Mheshimiwa Jaji Mutungi wewe mwenyewe umeshawahi kuyatembelea makao makuu hayo au bado ofisi iliyopo Buguruni, Dar es Salaam ndiyo Ofisi Kuu ya Makao Makuu?” inahoji barua ya hiyo. Maalim Seif ambaye pia aliwahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, alisema kesi mbalimbali zinazohusu mgogoro wa CUF zimefunguliwa Mahakama Kuu na kwamba, ni vyema Jaji Mutungi angetumia busara kumweleza Profesa Lipumba asubiri hukumu ya mahakama na endapo angekataa msajili na ofisi yake ingejitenga naye.
Mbali na hilo, Maalim Seif alidai kwamba msajili katika barua yake alieleza kwamba amejiridhisha na maelezo ya Profesa Lipumba kuwa yeye hafiki Buguruni na ameshindwa kufanya kazi, lakini hakumtafuta au kumuita ama kumuuliza ili kupata maelezo yake kujua ukweli wa kilichoandikwa na mwenyekiti anayemtambua. 

Zipo nyakati ambazo ni bora kuwa mzazi peke yako




Ni vema kufahamu kwamba kukuza na kulea mkiwa wazazi wawili ni njia bora na yenye manufaa zaidi kuliko kuwa mzazi mmoja. Lakini kama kwa kuwa wazazi wawili wenye misuguano na ugomvi inaleta usumbufu ya akili na moyo kwa watoto basi ni bora kubaki mzazi mmoja kwa afya ya watoto kuliko mkawa wawili na kuleta uharibifu mkubwa kwa wengi.
Pamoja na kwamba kuwa wazazi wawili ni njema sana, mara nyingine inakuwa ngumu sana kubaki wawili. Unakuta mpo pamoja kama wazazi lakini majukumu yote yahusuyo watoto anayafanya mzazi mmoja na wala watoto hawaoni mchango wa mzazi mwingine, labda haonekani katika kipato wala uwepo wake nyumbani, na kuwepo kwake kunakuwa bora kutokuwepo kabisa. Katika nyakati kama hizi wasaidie watoto wako au mwanao kuwa mwenye heshima, kuheshimu watu na mazingira yao, wafundishe kuwa na upendo kwa wanaowazunguka, usikatishwe tamaa au kuhofu kubeba majukumu peke yako kwasababu mazingira yameshakulazimu, unaweza kuzipunguza athari kwa kuwaweka watoto mbali na mzazi mwingine mwenye uharibifu kwao kuliko kung’ang’ania kuwa wote pamoja na hatimaye ukawaharibia watoto picha ya maisha.
Imeonekana mara nyingi kwamba watoto wa familia za mzazi mmoja wanaweza kujifunza kujituma na kuchukua majukumu mapema zaidi kuliko watoto wa familia za wazazi wawili. Hii ni kukuonyesha kwamba sio mara zote athari ni lazima kuwa hasi tu pale ambapo mzazi analazimika kulea na kukuza watoto au mtoto akiwa pekeyake. Weka vipaumbele katika mambo yaliyo chanya na wafundishe watoto wako hayo, wafundishe pia kuwa na mitazamo chanya katika maisha ya kila siku, usisahau kuwa mzazi kioo “a good model” kwao ili katika kuyatengeneza maisha yao wakutazame wewe kama mfano kwao. Wasaidie kujua kwamba ziko nyakati wanaweza kufanya mambo mazuri pale ambapo dunia na mazingira yanawaletea mambo ya kuumiza.
Baadhi ya usumbufu unaowakumba
Pamoja na kwamba yapo kuna usumbufu mwingi, upo unayowasumbua wazazi hawa zaidi. Kwa mfano; ile hali ya kuhakikisha unafanya kila kitu peke yako bila ya wakumlaumu endapo kitu hicho hakitafanyika vile kilivyotakiwa kifanyike. Unakuta mzazi wa hali hii anafahamu kwamba kama anataka kitu au vitu fulani vinatakiwa kufanyika basi hakuna wakuvifanya isipokuwa yeye mwenyewe.
Hata kama maranyingine unawatu au marafiki wa kukusaidia, lakini wawezakujikuta unalazimika kufanya baadhi ya vitu wewe mwenyewe. Kukubaliana na kuchukuliana na hali hizi ni sehemu mojawapo ya muhimu sana katika kuwezana na changamoto hii kubwa. Siku utakayoshindwa kujifunza kutokana na mazingira yanayokuzunguka ndiyo siku utakayoanza kutoweka.
Baadhi ya faida kwa watoto wa familia za mzazi mmoja
Baadhi ya watoto wanaotoka katika familia hizi wameonyesha uwezo mkubwa katika kusaidia kazi za nyumbani na hata kuwajali au kuwahudumia wadogo zao. Hali hizi huwafanya kupevuka na kuyaelewa maisha kwa haraka zaidi kuliko wale wa familia zenye wazazi wawili ambao wanawafanyia karibu kila kitu.
Watoto wa familia za mzazi mmoja wameonekana kuweza kujitegemea mapema zaidi na kujisimamia wenyewe katika ufanyaji wa mambo, wamekuwa na uwezo zaidi kwenye utatuzi wa matatizo binafsi na hata katika kubeba majukumu. Wanaweza kujifunza pia kwamba maisha sio wakati wote yanakuwa rafiki ingawa bado yawapasa kujeuza hali kuwa njema kutoka katika hali tete wanazokutana nazo. Kama wazazi wataweka utaratibu mzuri wa watoto kuwa na muda na wazazi wote katika nyakati tofauti basi mara nyingine watoto wanaweza kuwa na wakati mzuri na bora na kila mzazi pekeyake tofauti na muda waliokuwa wanapata wakati wazazi hawa wakiwa pamoja.

AFRIKA KUSINI

MAKAMU WA RAIS MHE. SAMIA SULUHU HASSAN KATIKA MKUTANO WA 37 WA WAKUU WA NCHI NA SERIKALI SADC MJINI PRETORIA AFRIKA KUSINI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan jana tarehe 19 Agosti 2017, amehudhuria  ufunguzi rasmi wa Mkutano wa 37 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika – SADC mjini Pretoria Afrika Kusini akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.
John Pombe Magufuli.
Mhe. Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa taarifa fupi kuhusu majukumu ya SADC Organ kwa kipindi cha Agosti 2016 - Agosti 2017 kwa niaba ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa SADC Organ anayemaliza muda wake.
Makamu wa Rais amewasilisha kwa Wakuu wa Nchi na Serikali taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya SADC Organ kwa kipindi cha Agosti 2016 hadi Agosti 2017 kwa niaba ya Mwenyekiti wa SADC Organ anayemaliza muda wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Taarifa hiyo inaelezea hali ya kisiasa, kiulinzi na kiusalama katika Kanda katika kipindi tajwa hususan katika Nchi za DRC, Madagascar na Lesotho.
Aidha taarifa hiyo pia imetoa mapendekezo ya namna ya kutatua changamoto zinazoendelea kuikabili Kanda katika maeneo ya siasa, ulinzi na usalama.
Taarifa hiyo pia imeelezea hali ya demokrasia na chaguzi zilizofanyika kwa kipindi cha 2016/2017 kwa nchi wanachama.
Katika Mkutano huu Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan amekabidhi Uenyekiti wa Asasi ya SADC ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama kwa Angola, baada ya Tanzania kukamilisha kipindi cha Uongozi wake chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Mkutano huu wa SADC uliofunguliwa rasmi  na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini ambaye ni Mwenyeji wa Mkutano wa 37 wa SADC, ulitanguliwa na mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Troika Mbili uliofanyika tarehe 18 Agosti, 2017
Mkutano wa Troika Mbili umefanyika kwa kuzingatia mapendekezo ya Mkutano wa Mawaziri wa Kamati ya Asasi ya Ushirikiano wa Siasa,Ulinzi na Usalama (SADC MCO) uliofanyika Dar es Salaam tarehe 20 na 21 Julai, 2017 ambapo Mawaziri waliona ipo haja ya kuitisha Double Troika pembezoni mwa Mkutano huu wa 37 ili kujadili pamoja na mambo mengine, hali ya ulinzi na usalama.
Troika Mbili inahusisha nchi wanachama sita ambao kwa sasa ni Swaziland, Tanzania, Afrika Kusini, Angola, Botswana na Msumbiji.
Serikali ya Afrika Kusini ambayo ni mwenyeji wa Mkutano huu wa 37 wa SADC na Mwenyekiti imependekeza kuwa kaulimbiu ya Mkutano wa 37 iwe ni Kushirikiana na Sekta Binafsi katika kuendeleza Viwanda na Kuongeza Thamani ya Bidhaa.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa Uenyekiti wa SADC kutoka kwa Mfalme Mswati III, Rais wa Afrika Kusini Mhe. Jacob Zuma amesisitiza nchi wananchama kutekeleza kwa vitendo Kauli Mbiu ya Mkutano wa 37 wa SADC juu ya kushirikiana na Sekta Binafsi katika kuendeleza Viwanda na Kuongeza Thamani ya Bidhaa kuwa ndio njia pekee ya nchi za Jumuiya hiyo kupiga hatua kimaendeleo.
Rais Zuma amesisitiza nchi za Afrika kufanyakazi kwa bidii na kuhakikisha rasilimali za nchi  zinatumika kwa faida ya maendeleo yay a kweli.
Wakuu wa Nchi na Serikali wamepokea taarifa ya utekelezaji wa Mkakati wa Maendeleo ya Viwanda wa SADC 2015 - 2063 ambao ulipitishwa katika Mkutano wa Dharura uliofanyika tarehe 29 Aprili, 2015 mjini Harare, Zimbawe.
Mkakati huu unalenga kuzifanya nchi za SADC kuwa na uchumi wa viwanda na kushiriki zaidi katika  mnyororo wa thamani kikanda na kimataifa  na hivyo kuongeza kasi ya maendeleo kwa wananchi wake.
Mkutano wa 37 wa Wakuu wa Nchi na Serikali (SADC) utahitimishwa hapo kesho Jumapili tarehe 20 Agosti 2017, kwa kutolewa Tamko (Communique) litakaloelezea yaliyojiri katika Kikao cha Wakuu wa Nchi na Serikali.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika picha ya pamoja na Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika – SADC mjini Pretoria Afrika Kusini 

Masauni: Polisi, Temesa na NIT kuungana kukagua magari nchini


Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Dkt. Mussa Mgwatu (kushoto), akimpokea Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni wakati Mwenyekiti huyo alipofanya ziara katika ofisi hizo zilizopo Keko Mwanga, jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kuangalia jinsi gani Baraza lake linaweza kufanikisha Utekelezaji wa Mapendezo ya Kamati iliyoundwa na Baraza hilo ili kukabiliana ajali za barabarani nchini.  
Na Felix Mwagara (MOHA)
MWENYEKITI wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amesema Baraza lake litakutana kujadili uwezekano wa Jeshi la Polisi, Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) pamoja na Chuo cha Usafirishaji (NIT) ziweze kuungana ili kufanya ukaguzi wa lazima wa magari kwa lengo la kuondoa ajali nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana mara baada ya kumaliza ziara yake ya kutembelea ofisi za Temesa na Chuo cha NIT, Masauni alisema ziara yake ilikua na mafanikio makubwa, hivyo anatarajia kukutana na Wajumbe wa Baraza lake katika vikao vyao na kuwasilisha uzoefu alioupata mara baada ya kuzitembelea Taasisi hizo za Serikali. 
“Nimeshuhudia Temesa na NIT mambo ambayo sikuyatarajia, inaonyesha kwamba katika vita ya kuzuia ajali nchini hatutaanza sifuri, tunasehemu fulani ya kuanzia, tutaanza na utaratibu wenye mfumo mzuri ambao utaweza kutekelezwa ili kufikia malengo ya kuwa na utaratibu wa lazima wa ukaguzi wa magari yote ambayo yanatumika katika nchi yetu,” alisema Masauni na kuongeza;
“Lengo la mipango hiyo ni kuhakikisha tunakuwa na magari mazuri ambayo hayawezi kusababisha ajali, hivyo nitawasilisha katika kikao hicho chha Baraza uzoefu huu nilioupata baada ya ziara hii ili nijadiliane na wajumbe wenzangu tuone jinsi tutakavyokubaliana kuhusiana na mafanikio niliyoyapata baada ya ziara hii.”
Pia alisema lengo la kuunganisha nguvu kwa kuungana kwa taasisi hizo za Serikali ni kufanikisha zaidi makabiliano ya ajali za barabarani, ambapo kwasasa Jeshi la Polisi pekee ndilo linalofanya ukaguzi wa lazima nchini, hivyo nguvu inahitajika endapo kutakua na muungano wa taasisi hizo ikiwa na lengo moja la kuijenga Tanzania.
Hata hivyo, Masauni aliongeza kuwa, katika kufanikisha hilo, kuna umuhimu wa kumtafuta mshauri mwelekezi ili afanye utafiti wa kina ili aweze kushauri jinsi ya kuvitumia vyombo na taasisi zetu zilizopo nchini, nini kifanyike ili kuweza kufikia muafaka wa namna bora ya kuweza kufanya ukaguzi wa magari wa lazima uanze  kazi haraka iwezekanavyo ili kuweza kupunguza ajali za barabarani ambazo nyingi zinasababishwa na ubovu wa magari.
Masauni akiwa Temesa alitembelea karakana ya utengenezaji wa magari na kujionea kazi mbalimbali ambazo zinafanywa na wataalamu katika karakana hiyo inayotengeneza magari ya Serikali pamoja na watu binafsi, ambapo aliona watalaamu wa Taasisi hiyo wanavyotumia vifaa mbalimbali vya matengenezo ya magari ikiwemo uwepo wa mashine ya kisasa ya kukagulia magari kwa njia ya umeme.
Alipokuwa katika Chuo cha NIT, Masauni alifanikiwa kupata taarifa fupi ya historia ya chuo hicho pamoja na kozi mbalimbali zinazotolewa chuoni hapo zikiwemo za masuala ya usalama barabarani. Pia alitembelea sehemu ya kisasa ya ukaguzi wa magari chuoni hapo pamoja na madarasa ya Wahudumu wa Ndege pamoja na Marubani ambapo ni kozi ipya ya masuala ya anga inayotarajiwa kuanzishwa chuoni hapo hivi karibuni.
Aidha, Mkuu wa Chuo hicho, ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Profesa Zakaria Mganilwa, alisema chuo chake kina kituo kilichofungwa mitambo ya kisasa ya kukagua magari ambapo kituo hicho kina uwezo wa kukagua magari mia sita kwa siku.
“Kama utaratibu utaweza kuwekwa wa kukagua magari, chuo kipo tayari kwasababu mitambo ipo na tumeajiri vijana ambao wanauwezo mkubwa wa kuhudumia idadi hiyo ya magari kwa siku,” alisema Mganilwa.

Masauni alimaliza ziara yake ya siku moja ambayo ilikua na lengo la kufanikisha utekelezaji wa mapendekezo ya Kamati iliyoundwa na Baraza lake la Usalama Barabarani katika hatua ya kukabiliana na ajali za barabarani ambazo zinasababishwa na mambo makuu matatu, moja ni matatizo ya kibinadamu, pili matatizo ya miundombinu, na tatu ubovu wa magari au vyombo vya moto ambako ndio lengo kuu la kuunganisha taasisi hizo ili kupata nguvu zaidi katika ukaguzi wa magari nchini.

KIKAO CHA KAMATI YA KATIBA, SHERIA NA HADHI ZA WACHEZAJI KUKAA LEO NA KESHO

Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), inatarajiwa kuketi kwa siku mbili Agosti 20 na 21, 2017 kupitisha usajili, lakini kabla kupitisha itasikiliza malalamiko kutoka baadhi ya timu na vituo vya kuibua na kukuza vipaji vya soka zinazodai fidia baada ya wachezaji wao kusajiliwa na klabu nyingine msimu wa 2017/18.

Viongozi au Wawakilishi wa Klabu zifuatazo hawana budi kufika Azam FC, Pamba FC, African Lyon, Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Singida United, Tusker FC, Young Africans, Njombe Mji, Majimaji, KMC, Ndanda FC, Coastal Union,  Stand United, Rhino FC, Mbao FC, Toto Africans, Stand United, Mbeya City na Lipuli. Pia wameitwa wachezaji Mbaraka Yussuf na Frank Hamisi.


Klabu na vituo vya kuibua na kukuza vipaji vilileta malalamiko yao TFF kudai fidia mbalimbali kama vile za mafunzo; ada ya usajili; ada za maendeleo na kuvunjwa kwa mikataba kutoka katika timu walizochezea hadi msimu uliopita.

Baadhi ya malalamiko yaliyopokelwa TFF ni ya Majimaji ya Songea dhidi ya Azam FC ya Dar es Salaam kuhusu mchezaji Idd Kipangwile.

Alliance ya Mwanza imelalamikia Pamba pia ya Mwanza kuhusu mchezaji Juma Nyangi ambako madai hayo yamekwenda mbali zaidi yakisema kuwa mchezaji husika amebadili jina kwa lengo la kudanganya.

Kwa upande wake, African Lyon imeondokewa na wachezaji 19 na inadai fidia katika timu, wachezaji kwenye mabano za Majimaji (Saleh Malande); Lipuli (Hamad Manzi, Lambele Reuben na Mussa Nampoka); Young Africans (Rostand Youthe Jehu); Tusker FC (Abdul Hilal) na Ndanda kwa wachezaji Hamad Tajiri na Baraka Majogoo.

Madai mengine ni dhidi ya Coastal Union kwa wachezaji Baraka Jaffary, Omary Salum, Raizen Hafidh na Fred Lewis huku madai mengine ni kwa Kagera Sugar kwa wachezaji Omar Abdallah, Abdallah Mguhi na Vicent Ludovic na Alhaji Zege .

Madai mengine ni dhidi ya timu ya Kinondoni Municipality Council (KMC) ambayo imewasajili Halfan Twenye, Yussuf Abdul na Rehani Kibingu wakati Singida United inalalamikiwa kumsajili Miraji Adam ilihali Njombe Mji inadaiwa fidia kwa kumsajili mchezaji Salum Juma.

Malalamiko mengine ni ya Kisa Academy ya Kinondoni, Dar es Salaam dhidi ya timu za Mbeya City (Idd Seleman); Majimaji (Jafar Mohammed); Mbao (Ally Rashid); Stand United (Said Mbati) na Friends Rangers (Hassan Abubakar).

Madai mengine dhidi ya timu za Coastal Union (Abubakar Nyakarungi na Ahmed George); The Mighty Elephant (Maliki Hamad); Kagera Sugar (Hussein Idd) na Azam FC (Omary Maunda).

Saturday, August 19

WACHEZAJI WANAOWANIA TUZO YA FIFA 2017 WATAJWA

Shirikisho la mpira wa miguu Duniani (FIFA) limewataja wachezaji 24 wakiume watakaowania tuzo ya mchezaji bora wa FIFA na wachezi 10 kwa upande wa soka la wakike, huku zoezi hilo likiendeshwa na Makocha wa timu za mataifa mbalimbali Duniani, Manahodha, Waandishi wa habari pamoja na Washabiki wa soka. Zoezi la kupiga kura ili kumpata mwanandinga huyo bora wa FIFA linatarajiwa kuanza Jumatatu Agosti 21 na kufungwa Septemba 7, 2017.

wachezaji 24 waliotajwa kuwania tuzo ya Mwanasoka Bora wa FIFA 2017 kwa upande wa wanaume ni hawa hapa.




Hawa ndiyo wachezaji 10 waliotajwa kuwania tuzo ya Mwanasoka Bora wa FIFA 2017 kwa upande wa wanawake.