Ni vema kufahamu kwamba kukuza na kulea mkiwa wazazi wawili ni njia bora na yenye manufaa zaidi kuliko kuwa mzazi mmoja. Lakini kama kwa kuwa wazazi wawili wenye misuguano na ugomvi inaleta usumbufu ya akili na moyo kwa watoto basi ni bora kubaki mzazi mmoja kwa afya ya watoto kuliko mkawa wawili na kuleta uharibifu mkubwa kwa wengi.
Pamoja na kwamba kuwa wazazi wawili ni njema sana, mara nyingine inakuwa ngumu sana kubaki wawili. Unakuta mpo pamoja kama wazazi lakini majukumu yote yahusuyo watoto anayafanya mzazi mmoja na wala watoto hawaoni mchango wa mzazi mwingine, labda haonekani katika kipato wala uwepo wake nyumbani, na kuwepo kwake kunakuwa bora kutokuwepo kabisa. Katika nyakati kama hizi wasaidie watoto wako au mwanao kuwa mwenye heshima, kuheshimu watu na mazingira yao, wafundishe kuwa na upendo kwa wanaowazunguka, usikatishwe tamaa au kuhofu kubeba majukumu peke yako kwasababu mazingira yameshakulazimu, unaweza kuzipunguza athari kwa kuwaweka watoto mbali na mzazi mwingine mwenye uharibifu kwao kuliko kung’ang’ania kuwa wote pamoja na hatimaye ukawaharibia watoto picha ya maisha.
Imeonekana mara nyingi kwamba watoto wa familia za mzazi mmoja wanaweza kujifunza kujituma na kuchukua majukumu mapema zaidi kuliko watoto wa familia za wazazi wawili. Hii ni kukuonyesha kwamba sio mara zote athari ni lazima kuwa hasi tu pale ambapo mzazi analazimika kulea na kukuza watoto au mtoto akiwa pekeyake. Weka vipaumbele katika mambo yaliyo chanya na wafundishe watoto wako hayo, wafundishe pia kuwa na mitazamo chanya katika maisha ya kila siku, usisahau kuwa mzazi kioo “a good model” kwao ili katika kuyatengeneza maisha yao wakutazame wewe kama mfano kwao. Wasaidie kujua kwamba ziko nyakati wanaweza kufanya mambo mazuri pale ambapo dunia na mazingira yanawaletea mambo ya kuumiza.
Baadhi ya usumbufu unaowakumba
Pamoja na kwamba yapo kuna usumbufu mwingi, upo unayowasumbua wazazi hawa zaidi. Kwa mfano; ile hali ya kuhakikisha unafanya kila kitu peke yako bila ya wakumlaumu endapo kitu hicho hakitafanyika vile kilivyotakiwa kifanyike. Unakuta mzazi wa hali hii anafahamu kwamba kama anataka kitu au vitu fulani vinatakiwa kufanyika basi hakuna wakuvifanya isipokuwa yeye mwenyewe.
Hata kama maranyingine unawatu au marafiki wa kukusaidia, lakini wawezakujikuta unalazimika kufanya baadhi ya vitu wewe mwenyewe. Kukubaliana na kuchukuliana na hali hizi ni sehemu mojawapo ya muhimu sana katika kuwezana na changamoto hii kubwa. Siku utakayoshindwa kujifunza kutokana na mazingira yanayokuzunguka ndiyo siku utakayoanza kutoweka.
Baadhi ya faida kwa watoto wa familia za mzazi mmoja
Baadhi ya watoto wanaotoka katika familia hizi wameonyesha uwezo mkubwa katika kusaidia kazi za nyumbani na hata kuwajali au kuwahudumia wadogo zao. Hali hizi huwafanya kupevuka na kuyaelewa maisha kwa haraka zaidi kuliko wale wa familia zenye wazazi wawili ambao wanawafanyia karibu kila kitu.
Watoto wa familia za mzazi mmoja wameonekana kuweza kujitegemea mapema zaidi na kujisimamia wenyewe katika ufanyaji wa mambo, wamekuwa na uwezo zaidi kwenye utatuzi wa matatizo binafsi na hata katika kubeba majukumu. Wanaweza kujifunza pia kwamba maisha sio wakati wote yanakuwa rafiki ingawa bado yawapasa kujeuza hali kuwa njema kutoka katika hali tete wanazokutana nazo. Kama wazazi wataweka utaratibu mzuri wa watoto kuwa na muda na wazazi wote katika nyakati tofauti basi mara nyingine watoto wanaweza kuwa na wakati mzuri na bora na kila mzazi pekeyake tofauti na muda waliokuwa wanapata wakati wazazi hawa wakiwa pamoja.
No comments:
Post a Comment