Tuesday, August 15

MAZUNGUMZO YA PAMOJA SERIKALI YA MUUNGANO NA MISRI





Rais wa Misri Abdel Fattah El-Sisi katikati na Ujumbe aliofuatana nao wakiwa katika mazungumzo na Viongozi was Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wakiongozwa na Rais Dkt.John Pombe magufuli leo alipokuwa katika ziara ya siku mbili mazungumzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa Ikulu ya Jijini Dar es Salaam


 
Mazungumzo ya Viongozi baina ya Ujumbe wa Rais wa Misri Abdel Fattah El-Sisi (kulia) na Viongozi wa Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yaliyofanyika leo katika ukumbi wa Ikulu Jijini Dar es Salaam,Rais Abdel Sisi na Ujumbe wake wakiwa nchini kwa ziara ya siku mbili, [Picha na Ikulu).14/08/2017.

MOROGORO

WAZIRI LUKUVI APOKEA RASIMU YA MKAKATI WA KUKABILIANA NA CHANGAMOTO ZA MATUMIZI BORA YA ARDHI NCHINI, MJINI MOROGORO

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mh. William Lukuvi amepokea rarmi Rasimu ya Mkakati wa kukabiliana na Changamoto za Matumizi bora ya Ardhi Nchini na kutaja Teknolojia kuwa ni changamoto inayokabili mpango wa matumizi bora ya ardhi inayopelekea kulegalega kwa upangaji, upimaji na umikilishaji wa Ardhi.


Waziri Lukuvi ameyasema hayo mjini Morogoro wakati alipokuwa akipokea rasimu ya mkakati wa kukabiliana na changamoto za matumizi bora ya ardhi nchini, iliyoonesha na kuainisha mapendekezo katika uandaaji,usimamizi na utekelezaji.

“Tunahitaji teknolojia rahisi ambayo hata ninyi mkondoka serikali inaweza kuhimili, hatupendi mtuambukize teknolojia ambayo itakuwa ni ngumu kwetu, kwakuwa serikali inapopanga gharama kubwa zinajitokeza kwenye picha za anga na zile za chini,” alisema Lukuvi.

Lukuvi alisema kuwa kuhusu fedha si tatizo lakini ukosefu wa teknolojia ndio tatizo kubwa zaidi,hivyo ni vizuri kuyatazama haya mashirika yasiyo ya kiserikali tushirikiane nayo ili yaweze kuangalia ni teknolojia gani rahisi itakayoweza kupunguza gharama za upimaji na upangaji wa ardhi vijijini baada ya kusubiri ndege za anga ambazo ni gharama kubwa.

Aliongeza kuwa Serikali inapenda kuwa na uratibu wa haraka, ulio rahisi ambao wananchi wanaweza kupanga maeneo yao na kuongeza, lakini pia kuondokana na migogoro ya Ardhi.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mh. William Lukuvi akifungua rasmi mkutano kwa ajili ya kusikiliza na kupokea Rasimu ya Mkakati wa Kukabiliana na Changamoto za Matumizi Bora ya Ardhi Nchini, mjini Morogoro.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mh. Stephen Kebwe akitoa maelezo juu ya mkutano huo na kuonesha namna gani itakavyoweza kumaliza migogoro ya Ardhi Nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi Dkt. Stephen Nindi akitoa Mhtasari wa mkutano huo wa kuwasilisha Rasimu ya Mkakati wa Kukabiliana na Changamoto za Matumizi Bora ya Ardhi Nchini.
Bw. Gerald Mwakipesile Afisa Mipango wa Tume ya Mipango na Matumizi ya Ardhi akiwasilisha kwa Mh. Lukuvi Rasimu ya Mkakati wa kukabiliana na Changamoto za Matumizi Bora ya Ardhi Nchini.
Waziri wa Ardhi Mh. Lukuvi pamoja na wajumbe wakifuatilia kwa makini uwasilishwaji wa Rasimu ya mkakati wa kukabiliana na changamoto za matumizi bora ya ardhi nchini.
Bw. Emmanuel Msofe kutoka Idara ya Maliasili na Utalii akichangia jambo na ushiriki wao katika mkakati wa kukabiliana na changamoto za matumizi bora ya Ardhi.
Bw. Victor Mwita kutoka Wizara ya Kilimo na Ufugaji akichangia jambo ni namna gani watakavyo shirikiana katika kuhakikisha changamoto za Ardhi nchini zinakwisha.
Bi. Bertha Luzabiko Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Morogoro akieleza namna wanavyofanya kazi zao na kushirikiana na watu wa ardhi pia ushiriki wao wa kukabiliana na Changamoto za Matumizi bora ya Ardhi Nchini.
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Kimataifa la Care Nchini Tanzania Bw. Waleed Rauf akielezea namna ya wanavyoshirikiana vizuri na Serikali kuhakikisha jinsi gani matumizi bora ya Ardhi yanaenda sawa na kuongeza kuwa malengo yao pia ni kuona umasikini unapungua kwa kiasi kikubwa katika jamii zetu.
Mratibu wa Miradi ya Ardhi kutoka Oxfam Naomi Shadrack akichangia jambo kuwa kupitia rasimu hiyo wadau wamefanya kazi kwa pamoja kuhakikisha sekta ya ardhi ambayo inatambuliwa na wengi wakiwemo wakulima na wafugaji wadogo wadogo inafanyiwa kazi.
Bw. Anthony Temu, Meneja wa Ukasimishaji Rasilimali Ardhi Vijijini kupitia Mpango wa Kukasirimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania(MKURABITA) akichangia jambo wakati wa mkutano huo.
Bw. Jamboi Baramayegu Kutoka Ujamaa-CORT akichangia juu ya maswala ya ufugaji na kuomba mkakati huu wa kukabiliana na changamoto za matumizi bora ya Ardhi Nchini utambue maeneo ya kulishia mifuko vipindi vyote wakati wa kifukwe na kaingazi pia.
Kamishna wa Ardhi Nchini Bi. Mary Makondo akichangia jambo na kuelezea mambo mbalimbali yanayohusiana na ardhi na kusisitiza ushirikiano wa sekta zote katika kuhakikisha Mkakati wa kukabiliana na changamoto za matumizi bora ya ardhi unaenda vizuri.
Mwenyekiti mpya wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi Bw. Fidelis Mutakyamilwa akitoa neno la Shukurani kwa Mh. William Lukuvi (MB) , Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi baada ya kusikiliza uwasilishwaji wa Rasimu ya Mkakati wa Kukabiliana na Changamoto za Matumizi Bora ya ardhi na namna Tume itakavyofanya kazi na wadau ili kuhakikisha Mchakato Unafanyika kwa haraka.
Waziri wa Ardhi Mh. Lukuvi (Kulia) Akikabidhiwa rasmi Rasimu ya Mkakati wa Kukabiliana na Changamoto za matumizi Bora ya Ardhi Nchini kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi Bw. Fidelis Mutakyamilwa(Kushoto)
Waziri wa Ardhi Mh. Lukuvi (wa kwanza kulia) akimkabidhi Kamishna wa Ardhi Nchini Bi. Mary Makondo(wakatikati) Rasimu ya Mkakati wa Kukabiliana na Changamoto za matumizi Bora ya Ardhi Nchini, wa tatu kutoka kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi Dkt. Stephen Nindi.
Picha ya pamoja baada ya Waziri wa Ardhi Mh. Lukuvi kupokea rasmi Rasimu ya Mkakati wa Kukabiliana na Changamoto za matumizi Bora ya Ardhi Nchini



Wadau wakiendelea kufuatilia Mkutano huo 
Mkutano ukiwa unaendelea.


Picha ya Pamoja

Mjane aliyemlilia Rais Magufuli afikishwa mahakamani


Tanga. Swabaha Shoshi,  anayejulikana kwa jina maarufu kama mjane aliyemlilia Rais John Magufuli,  amefikishwa mahakamani jijini hapa na kusomewa shitaka la kuingia bila kibali katika  eneo la Chongoleani lililotengwa  kwa ajili ya mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Uganda.
Swabaha alifikishwa mbele ya Hakimu Hasna Majani wa Mahakama ya Mwanzo ya Usambara Mjini mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mwendesha mashtaka wa polisi, Koplo Rajabu alidai mahakamani hapo kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo Agosti 4 mwaka huu saa 8:00 mchana baada ya kuingia eneo hilo na kujenga vibanda vya biashara ya chakula.
Koplo Rajabu alidai kuwa eneo hilo limetengwa kwa ajili ya mradi wa bomba la mafuta ghafi unaounganisha Tanzania na Uganda, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria za nchi.
Hata hivyo, Swabaha alikana shitaka hilo na aliachiwa kwa dhamana na kesi hiyo itasikilizwa tena Agosti  18.
Swabaha  alikamatwa Chongoleani Agosti 4 mwaka huu na kukaa rumande hadi alipofikishwa mahakamani mwishoni mwa wiki.
Swabaha alijipatia umaarufu wakati alipojitokeza mbele ya Rais Magufuli Machi mwaka huu wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Sheria iliyofanyika kitaifa katika viwanja vya Diamond Jubilee.
Siku hiyo, mwanamke huyo alifanya harakati hadi Rais alipomuona na kutaka aruhusiwe atoe yake ya moyoni na akaeleza madai ya kudhulumiwa mali za urithi.

Wapigadebe Dar ‘wajinafasi’ vituoni


Dar es Salaam. Agizo lililotolewa na polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaamu mwishoni mwa wiki iliyopita kuwataka wapigadebe wa daladala wasionekane vituoni kuanzia jana, la sivyo watakamatwa, halijatekelezeka.
Mwishoni mwa wiki, Kaimu Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Lucas Mkondya alitangaza kuwa msako dhidi ya wapigadebe ambao watakaidi amri hiyo ungeanza jana baada ya kupokea malalamiko mengi ya wananchi waliodai kuporwa vitu vyao kwenye vituo vya daladala.
Hata hivyo, jana wapigadebe hao walikutwa wakiendelea na kazi yao kama kawaida kwenye vituo mbalimbali.
Waandishi wa habari hizi waliwashuhudia wapigadebe hao kwenye vituo vya Mnazi mmoja, Baridi, Ilala na Buguruni vilivyopo wilayani Ilala na Riverside, Stendi ya Mabasi Ubungo na Darajani vya Wilaya ya Ubungo.
Alipopigiwa simu kuulizwa kuhusu wapigadebe hao kuendeea kuwapo vituoni, Mkondya alisema hawawezi kumaliza suala hilo kwa siku moja.
Akizungumzia suala hilo, dereva wa Bajaj katika eneo la Ubungo, Charles Robert alisema litapunguza vitendo vya wizi na vurugu katika vituo vya mabasi ambavyo vimekuwa vya kawaida. “Naliomba Jeshi la Polisi kuhakikisha watu hawa wanaondolewa katika vituo, kwani bado wanaendelea kufanya kazi bila ya wasiwasi,” alisema.
Hussein Said anayeendesha daladala alisema iwapo polisi watawaondoa wapigadebe hao watakuwa wamesaidia kuwapunguzia gharama za kuwalipa fedha kutokana na kuwaitia abiria vituoni akidai kuwa hata wasipoita abiria baadhi ya wapigadebe hulazimisha walipwe.
Abiria aliyejitambulisha kwa jina la Mariam Hussein alitaja kero ya wapigadebe ni kuwalazimisha abiria kupanda magari hata wasiyoyataka.
Baadhi ya wapigadebe walisema juzi kuwa, siyo wote wanaojihusisha na wizi na ukwapuaji wa mali za abiria.
“Kaka mimi nina familia yangu, mke na watoto na hii ni kama kazi nyingine. Nachofanya hapa ni kutafuta riziki tu, kama ningekuwa mwizi hapa nisingekuwepo maana huwezi kunyea kambi halafu ukarudi kulala hapohapo,” alisema Masoud Issa anayepiga debe kituo cha Tandika wilayani Temeke.
Jacob Joel maarufu kwa jina la Joe anayepiga debe katika Kituo cha Daladala cha Karume wilayani Ilala alisema kuwa wanao utaratibu wa kuwafukuza wezi wanaokwenda kituoni hapo kwa kuwa hawataki kusikia vilio vya abiria.
Akizungumzia uamuzi wa jeshi hilo, Julius Nyakweele anayetumia usafiri wa daladala alisema wapigadebe wana faida na kasoro zao.
“Kama mtu ni mgeni akisikia wanaita abiria inamrahisishia kujua gari analopanda, pia wapo wapigadebe wezi wanaowafanya watu wapande mabasi wakiwa wameibiwa mali zao,” alisema.
Machi 2007, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Alfred Tibaigana aliagiza wapigadebe wote kuondoka katika vituo vya daladala, lakini agizo hilo halitekelezwa.

Bomoabomoa Dar yaipitia nyumba ya Mama Mkapa

Nyumba inayosadikiwa ya Anna Mkapa ,mke wa Rais

Nyumba inayosadikiwa ya Anna Mkapa ,mke wa Rais mstaafu wa awamu ya tatu Mzee Benjamini Mkapa ikiwa imewekewa alama ya X katika eneo la Mbezi kwa Msuguli inatarajia kubomolewa kupisha upanuzi wa barabara ya Morogoro jijini Dar es Salaam.Picha na Said Khamis 
Dar es Salaam. Nyumba ya Anna Mkapa, mke wa Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Benjamin Mkapa imekumbwa na bomoabomoa inayoendelea pembeni mwa Barabara ya Morogoro baada ya kuwekewa alama ya “X”.
Nyumba hiyo ipo kwenye shamba linalomilikiwa na familia ya Mkapa lililopo eneo la Mbezi kwa Msuguri, maarufu kwa jina la Kituo cha Zamani.
Nyumba zilizojengwa eneo la kuanzia Kimara hadi Kiluvya ambazo ziko ndani ya mita 121 kutoka katikati ya barabara hiyo kuu inayounganisha jiji la Dar es Salaam na mikoa mingine, zitabomolewa kwa ajili ya kupisha upanuzi.
Ingawa kijana aliyekuwepo hakuwa tayari kutoa maelezo, nyumba hiyo imezungushiwa ukuta na ina lango lililopakwa rangi nyeusi na ina duka ambalo muuzaji amewekwa na msimamizi wa mali hiyo.
Katika moja ya sehemu za ukuta wa nyumba hiyo kumeandikwa “hatubomoi hadi tulipwe”, lakini mtu aliyedai kuwa ndugu wa mama huyo alisema familia haihusiki na maandishi hayo, akituhumu watoto kuwa ndio walioandika hivyo.
Waandishi wa Mwananchi walifika katika nyumba hiyo ya Mama Anna Mkapa jana saa 5:00 asubuhi na kumkuta mmoja wa watu aliyedai ni ndugu wa mke wa rais huyo wa zamani.
“Ni kweli hapa ndiyo nyumbani kwa mama Anna Mkapa, lakini mimi siwezi kuzungumza chochote kwa sababu si mhusika. Hapa ni kama mwangalizi wa nyumba tu,” alisema.
Huku akigoma kutaja jina lake, mtu huyo alishauri atafutwe mmiliki wa nyumba hiyo kwa ajili ya maelezo zaidi.
“Naomba mtafute mama (Anna Mkapa) mwenyewe. Nendeni ofisini kwake. Mimi hapa ameniachia tu kama mwangalizi wa nyumba yake, kwa hilo mtanisamehe siwezi kuzungumza,” alisema .
Hata hivyo, mmoja wa wafanyakazi wa ndugu wa mke huyo wa Rais wa zamani ambaye alikuwa akiuza duka lililoko nje ya nyumba hiyo, alisema atafutwe mtu mmoja aliyemtaja kuwa ni “babu mmoja kipofu”.
“Naomba mkamuone babu mmoja kipofu na yeye nyumba yake imewekewa alama ya “X” anaweza kuwa na taarifa juu ya nyumba hii kwani nimekuwa nikimsikia akizungumza,” alisema.
Mmoja wa watoto waliokuwa eneo hilo aliwapeleka waandishi kwa babu huyo.
“Karibuni hapa ndipo nyumbani kwa babu,” alitukaribisha mtoto huyo.
“Karibuni nyinyi ni akina nani? Aliuliza babu,” na alipojibiwa kuwa ni waandishi alionekana kukubali.
“Ah. Nyie ndiyo waandishi wa Mwananchi mmekuwa mkiandika sana kuhusu bomoabomoa na leo mmeandika kuhusu waumini waliokimbia kanisa kwa sababu ya bomoabomoa,” alisema.
Baadaye alijitambulisha kuwa anaitwa James Shirinde (80) na alianza kueleza jinsi alivyonunua eneo hilo ambalo kwa sasa linamilikiwa na familia ya Mkapa.
“Nilinunua eneo hilo mwaka 1975 wakati huo nikiwa mfanyakazi wa Shirika la Reli ambalo kwa wakati huo lilijulikana kama TRC na huku kulikuwa ni mashamba tu,” alisema.
“Mwaka 1980, mke wa rais mstaafu alikuja akanunua shamba na akajenga nyumba ambayo mpaka sasa anaishi mdogo wake, Rose Silayo.”
Shirinde, ambaye kwa sasa anaishi peke yake baada ya mkewe kufariki na watoto wake kumtelekeza, alisema wakati wananunua eneo na kujenga, Wakala wa Barabara (Tanroads) walikuwa hawajaweka mawe
“Haya mawe waliyoyaweka sasa yametukuta baada ya kutungwa sheria mpya ya Hifadhi ya Barabara ya mita 121.5 mwaka 2007 na 2009. Wakati huo mke wa Mkapa naye alikuwa amejenga nyumba yake na mumewe pia alikuwa amenunua shamba huku la ekari tano,” alisema.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mji Mpya, Daniel Majige alisema shamba hilo ni mali ya Mkapa na nyumba ni ya mkewe.
“Ni kweli najua kuna shamba la Mkapa ambalo litamegwa nusu na Tanroads ili kupisha utanuzi wa barabara ya Morogoro, lakini kuhusu nyumba ya mke wake hiyo sijapata taarifa labda niifuatilie,” alisema.
Majige alisema shamba hilo ni la muda mrefu na moja ya mashamba ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na wananchi kutokana na kutelekezwa na hivyo kuwa pori.
“Tumekuwa tukiwaambia mara nyingi kuhusu shamba lao kuwa tatizo, lakini wanachofanya wanakuja wanafyeka kisha wanaliacha tena na tumeshaomba sana hilo shamba tupewe Serikali ya kijiji ili tuliendeleze kwa kujenga kituo cha polisi lakini hatujawahi kujibiwa chochote,” alisema.
Injinia wa Tanroads, Johnson Letechura alipoulizwa kuhusu alama ya bomoa katika nyumba hiyo, alijibu kwa kuuliza: “Unataka kujua kama ni nyumba yake ili iweje? Acheni kuandika habari za nonsense (zisizo na maana),”alisema.
Lutechura alisema nyumba ya mtu yeyote iliyoko kwenye hifadhi ya barabara itabomolewa, na baadaye akakata simu.
Imeandikwa na Jackline Masinde, Asna Kaniki na Hidaya Nyanga, Mwananchi

Makonda alivyoipiga chenga timu ya MCT sakata la Clouds

Mmoja wa wajumbe wa timu ya uchunguzi wa ripoti

Mmoja wa wajumbe wa timu ya uchunguzi wa ripoti ya uvamizi wa Studio za Clouds Tv,  Wakili Juma Thomas akizungumza jijini Dar es Salaam jana kuhusu  ripoti ya uchunguzi   uliofanywa  na Baraza la Habari Tanzania (MCT), kuhususiana na  tukio la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuvamia Studio za Clouds Media Group (CMG). Kushoto ni  mweyekiti wa  kamati ya maadili ya Baraza hilo, Jaji mstaafu Juxon Mlay. Picha na Mpiga picha wetu 
Dar es Salaam. Ripoti ya uchunguzi uliofanywa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) kuhusiana na tukio la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuvamia studio za Clouds Media Group (CMG) imeonyesha jinsi kiongozi huyo alivyowapiga chenga timu ya uchunguzi hivyo kushindwa kupata upande wake.
Kama ilivyokuwa kwa kamati iliyoundwa na aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye kuchunguza sakata hilo lilipotokea, ndivyo ilivyokuwa kwa timu hii ambayo pia ilishindwa kuzungumza na Makonda.
Kiongozi wa timu hiyo mwanasheria Juma Thomas alisema mara tatu wajumbe wa timu hiyo walikwenda kwenye ofisi za Makonda lakini hawakufanikiwa kukutana naye.
“Suala la uchunguzi linahusisha pande zote. Tumeongea na wafanyakazi wa CMG, Kamanda wa Polisi Kinondoni, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu,maofisa wa mamlaka ya mawasiliano na waandishi wengine lakini hatukufanikiwa kumpata Makonda,”
“Timu ilimwandikia barua Makonda ikitoa sababu za umuhimu wake kukutana naye. Barua hiyo yenye kumbukumbu namba MCT/15/005/2017 iliandikwa Mei 2 na ilipokelewa na kugongwa mhuri wa mkuu wa mkoa lakini mpaka ripoti hii inaandikwa, barua hiyo haikuwa imeshughulikiwa,”
“Tulimpa nafasi ya kumsikiliza lakini alishindwa kuitumia fursa hiyo. Kila tulipokwenda ofisini kwake tuliambiwa yupo nje ya ofisi kwa shughuli za kikazi. Hatukuishia hapo tulipata namba zake za simu tulipopiga iliita bila kupokelewa.”
Hata hivyo Makonda mwenyewe akizungumza wiki iliyopita wakati wa mkutano wa waandishi wa habari ulioandaliwa na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) alidai kuwa ripoti iliyotolewa na kamati iliyoundwa na Nape haikusikiliza upande wake.
“Hukumu ilitolewa kwa kusikiliza upande mmoja, sikusikilizwa na mimi nikaelezea upande wangu,” alisema Makonda.
Kwa mujibu wa ripoti ya MCT, Makonda anatakiwa kuomba radhi waandishi wa habari na Watanzania kwa ujumla kwa kitendo hicho.
Hata hivyo Makonda alishasema kuwa hawezi kuomba radhi na katu hawezi kutoa neno samahani kwenye kinywa chake. “Hilo neno halitokuja litokee kwenye kinywa changu, sitaomba radhi narudia tena kwa herufi kubwa,” alisema Makonda kwenye mkutano wa TEF.
Kilichobainika kwenye uchunguzi
Timu ya MCT ilibaini kuwa ni kweli Makonda alivamia studio za Clouds akiwa na askari watano wenye silaha.
Mlinzi aliyehojiwa na timu hiyo alieleza kuwa haikuwa mara ya kwanza kwa Makonda kwenda CMG lakini siku hiyo alikwenda akiwa na mwonekano tofauti.
“Tulipomuuliza mlinzi wa zamu kwa nini hakumzuia kuingia alisema kuwa alishindwa kufanya hivyo kwa kuwahofia wale askari aliokuwa ameambatana nao Makonda,” alisema.
Somo kwa vyombo vya habari
Timu ya uchunguzi ilipendekeza kuwa licha ya kuwepo kwa uhusiano kati ya wanasiasa na mashirika ya kisiasa ipo haja ya kuweka mipaka ili kuzuia siasa kuingilia uhuru wa vyombo vya habari.
Timu hiyo ilionya wahariri na watendaji wengine kwenye vyombo vya habari kujiepusha na uhusiano wa karibu sana na wanasiasa kiasi cha kufanya kazi yao ya uandishi kuwa ngumu.
Hali ya vyombo vya habari
Katibu Mtendaji MCT, Kajubi Mukajanga alisema walifanya utafiti kuangalia hali ya vyombo vya habari katika nyanja za kiuchumi, masuala ya kisheria, usimamizi pamoja na changamoto zinazoikabili tasnia hiyo.
Akielezea utafiti huo kwa upande wa Tanzania Bara, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha SAUT, Dk Joyce Bazira alisema kwa ujumla hali ya vyombo vya habari haikuwa nzuri kutokana na kuminywa kwa uhuru wa habari kutokana na mabadiliko ya kisheria.
Alisema wadau wameeleza kuwa mabadiliko hayo ikiwamo Sheria ya Huduma za Habari iliyopitishwa mwaka jana imekuwa na athari kubwa tofauti na matarajio ya wengi.
Sheria nyingine ni ya haki ya kupata habari (Access to Information Act) pamoja na Sheria ya Mitandao (Cybercrime Act) ambazo zote zimekuwa na changamoto wakati wa utekelezaji wake.

Mrema amshukuru Magufuli kanisani


Dar es Saalam. Mwenyekiti wa Bodi ya Msamaha kwa Wafungwa (Parole), Augustine Mrema ametoa shukrani zake kwa Rais John Magufuli kwa kumsaidia kupata matibabu nchini India na kufanikiwa kupona ugonjwa wa kansa.
Mrema alisema kwa sasa utendaji wake wa kazi utaimarika kwa kuwa ameshapona ugonjwa uliokuwa ukimsumbua na kushindwa kutumikia wananchi na Taifa.
Akizungumza mbele ya waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Mama Mwokozi jijini Dar es Salaam, alisema kuanzia sasa atamsaidia vizuri Rais katika nafasi yake ya kuwatetea wafungwa kupitia msamaha wa Bodi ya Parole.
Alisema amefikia hatua ya kutoa shukrani kwa sababu ya muujiza aliopata kutoka kwa viongozi wa Serikali na dini waliomuombea.
Paroko Kiongozi wa kanisa hilo, Cathbert Magaga aliwataka waumini wengine kuiga mfano wa Mrema wa kutoa shukrani na siyo kunyamaza kwa kuwa Mungu atawasaidia.

Uhuru aruhusu maandamano

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta akitoa ujumbe kwa

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta akitoa ujumbe kwa wagombea wote walioshindwa. Picha na Daily Nation 
Nairobi, Kenya. Rais Uhuru Kenyatta huenda akaingia katika vitabu vya kumbukumbu na historia kwa marais wa Afrika kwa kuamua kuruhusu maandamano ya amani kupinga ushindi wake alioupata katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 8.
Kenyatta amewataka polisi kujizuia kutumia nguvu kubwa na badala yake wawape ulinzi wakati wa maandamano hayo ya amani na yanayoruhusiwa kisheria kwa watu ambao hawafurahii matokeo ya uchaguzi uliopita.
Rais Kenyatta alisema hayo jana alipokuwa akitoa ujumbe kwa wagombea walioshindwa katika uchaguzi huo uliofanyika Jumanne iliyopita. Kenyatta alisema hayo akiwa Jengo la Harambee alikokwenda kukutana na Kamati ya Maandalizi ya Hafla ya kuapishwa kwake.
Katika ujumbe huo uliomlenga zaidi Raila Odinga aliyekuwa mgombea urais kupitia muungano wa Nasa, Kenyatta aliwataka wagombea wote ambao hawakuridhishwa na matokeo ya uchaguzi wachukue hatua zilizobainishwa na Katiba ili kupata wanachotaka.
“Marafiki zetu ambao hawataki kukubaliana na matokeo ... tumenyosha mkono wetu wa udugu kwao ... watumie njia zozote zilizobainishwa katika katiba kuelezea kutoridhishwa kwao,” alisema.
“Wale wanaotaka kushawishi wengi wagome wanaweza kufanya hivyo, lakini kwa kuzingatia vifungu vya sheria. Mwishoni mwa siku sisi sote ni Wakenya. Hakuna haja ya kudhuriana. Hakuna haja ya kuharibiana mali...tunawashukuru polisi kwa kazi nzuri lakini waendelee kujizuia.”
“Polisi wako tayari kuwalinda wakati mnafanya maandamano na wale waliochukia waelewe kwamba hawahitaji kibali changu wala cha Jubilee kufanya maandamano ya amani.”
Hata hivyo, alitoa onyo kali kwamba serikali haitavumilia maandamano yatakayosababisha vifo na uharibifu wa mali za watu kutokana na vurugu.
Vilevile alitoa onyo dhidi ya waporaji na waharibifu wa mali katika baadhi ya maeneo ya nchi, ambako yameripotiwa maandamano baada ya uchaguzi.
“Wakenya wengi wamesema uchaguzi umepita na wamerejea kazini. Hawataki maandamano ya ghasia. Msivuruge maisha ya watu wengine. Kama serikali hatutaruhusu uharibifu wa mali wala upotevu wa maisha na uporaji.”
Nasa wapinga
Rais Uhuru alitoa kauli hiyo baada ya viongozi wa muungano wa Nasa kuhamasisha wafuasi wao kukataa matokeo yaliyompa ushindi Uhuru na makamu wake, William Ruto. Baada ya kazi ya kuhesabu kura kukamilika, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilimtangaza Kenyatta kuwa mshindi kwa kura 8,203,290 sawa na asilimia 54.27.
IEBC ilisema mgombea urais kwa muungano wa Nasa, Raila Odinga alipata kura 6,762,224 sawa na asilimia 44.74 matokeo ambayo wanayapinga.
Wakiitikia wito wa viongozi wao kati ya Jumatano na Jumamosi maeneo, ambayo ni ngome ya upinzani ya Kisumu, Kibera, Homabay na Migori yalikumbwa na vurugu na soko la Garissa lilichomwa moto.
Nasa walidai kwamba, kwa mujibu wa vyanzo vyao kutoka ndani ya IEBC Raila alishinda kwa kura milioni nane akifuatiwa na Uhuru. Walidai wizi huo ulifanikishwa kwa kudukua kompyuta iliyokuwa inahifadhi matokeo na kumbukumbu nyingine.
Juzi, akizungumza na wafuasi wake waliojitokeza kwa wingi katika eneo la Kibera, Raila aliwataka wafuasi wake wote kususia kazi jana ili kuomboleza vifo vya waliouawa katika makabiliano na polisi.
Pia, alisema atatoa msimamo leo wa nini cha kufanya. Hapo awali Nasa walisema mwaka huu hawatakwenda Mahakama ya Juu kupinga matokeo hayo bali watatumia njia nyingine ambayo hawakuitaja.
Katika mkutano wa juzi, Raila aliwaeleza wafuasi wake kuwa walitambua fika kwamba uchaguzi huo ungegubikwa na wizi wa kura na hivyo ndivyo ilivyokuwa. “Tulitabiri wangeiba kura na hicho ndicho kilichotokea. Hatujamaliza bado. Hatutakata tamaa. Subirini hatua inayofuata, nitatoa msimamo Jumanne (leo),” alisema.
“Ni wazi kuwa mamlaka husika zimeshindwa kuchukua hatua stahiki na badala yake wanaua watu. Kura zimeibwa hakuna cha kuficha hapo. Ila ninachoweza kuwaambia kwa sasa kesho (leo) msiende kazini.”
Annan amsihi Raila
Wakati Raila akihamasisha wafuasi wake, jumuiya za kimataifa imemtaka awatulize. Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Mataifa (UN), Kofi Annan ambaye alikuwa katika timu ya upatanishi ulipoibuka mzozo wa kisiasa baada ya uchaguzi mwaka 2007, alimtaka Raila kutumia mifumo ya sheria kutafuta haki kuhusu matokeo ya uchaguzi huo.
“Namshukuru kiongozi wa upinzani Raila Odinga kwa kampeni za amani alizoendesha. Amekuwa mtetezi jasiri wa demokrasia,” alisema Annan.
“Kwa hivyo, natoa wito (Odinga) sasa afuatilie malalamiko yake kupitia mifumo ya kisheria iliyowekwa na aweke masilahi ya Taifa mbele kama alivyofanya kwa uzalendo kipindi kilichopita.”
Mwaka 2007 zaidi ya watu 1,000 walipoteza maisha na wengine 600,000 wakihama makazi yao wakati wa ghasia za kikabila zilizozuka baada ya matokeo kutangazwa.
Warejea kazini
Katika kile kinachoonekana kuwa ni kutii wito wa serikali, watu walionekana kupuuza wito wa Raila wa kususia kazi kuomboleza watu waliouawa katika makabiliano kati ya polisi na waandamanaji waliokuwa wanapinga matokeo ya uchaguzi wa urais.
Wengi walionekana barabarani wakirejea kwenye shughuli zao jana na kuendelea na maisha ya kawaida.

anzania yalenga makubwa Misri

Rais John Magufuli akisalimiana na mgeni wake,

Rais John Magufuli akisalimiana na mgeni wake, Abdel Fattah el-Sisi wa Misri Ikulu jijini Dar es Salaam jana. Picha na Ikulu. 
Dar es Salaam. Tanzania ina malengo ya kimkakati ya kuboresha uhusiano wake na Misri, Rais John Magufuli alisema jana mbele ya mgeni wake, Rais Abdel Fattah El-Sisi jijini Dar es Salaam jana.
Viongozi hao wawili walikubaliana kushirikiana katika masuala mbalimbali ya kiuchumi na kijamii baada ya kiongozi huyo wa taifa la Kiarabu kufanya mazungumzo na Rais Magufuli jana Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais John Magufuli aliwaambia wanahabari kuwa wamekubaliana na El-Sisi kukuza biashara kwa Serikali ya Misri kuanzisha kiwanda cha nyama hapa nchini.
“Tanzania ni ya pili kwa kuwa na mifugo mingi na Misri wana shida na nyama. Kiwanda kikianzishwa hapa nyama zitakuwa zinasafarishwa kutoka Tanzania hadi Misri na nchi nyingine,” alisema Rais Magufuli.
“Hatua hii itasaidia Serikali kupata mapato sanjari na wafugaji kupata soko la mifugo yao.”
Mbali na hilo, Rais Magufuli alisema wamekubaliana na mgeni wake kuwa Misri isaidie Tanzania katika sekta ya afya, akisema nchi hiyo itatoa fedha kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Alisema hatua hiyo itasaidia Muhimbili kutoa huduma ya operesheni ya figo na masuala mengine.
Pia alisema Serikali ya Misri ipo tayari kuisadia Tanzania katika teknolojia ya umwagiliaji kwa kuwa wapo juu katika suala hilo.
Kuhusu utalii, Rais Magufuli alisema Misri ipo tayari pia kubadilishana uzoefu na Tanzania katika masuala ya utalii pamoja na mashirika ya usafiri wa anga ya nchi hizi mbili.
“Tanzania ukimjulisha na Zanzibar tunapata watalii wasiozidi milioni mbili kwa mwaka. Wakati wenzetu wanapata milioni kumi. Kwa hiyo tutabadilishana ili watusaidie katika jambo hili ili tuongeze idadi ya utalii,” alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli alisema kupitia uhusiano ulipo kati ya Tanzania na Misri, hivi sasa kuna Watanzania 115 wanasoma katika vyuo mbalimbali nchini humo na kwamba serikali hiyo imeamua kuongeza idadi ya wanafunzi katika programu tofauti.
“Tutakuwa tukibadilisha walimu katika programu mbalimbali na nipo tayari kutoa walimu wa Kiswahili ili waende kufundisha vyuo vikuu vya Misri na wao wamesema watatoa wataalamu wa teknolojia na habari (IT) na walimu wa lugha ya kiarabu watakaofundisha hapa nchini,” alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli alitumia nafasi hiyo kumshukuru rais huyo wa Misri na kwa upendo alionao kwa Watanzania na kwamba wamejifunza mambo mengi kutoka Misri na wanaithamini ziara yake.
Alisema rais wa Misri ni mwanajeshi aliyefikia cheo cha Field Marshal ambaye anataka kazi ifanyike, kitu ambacho kinaendana na falsafa yake ya “hapa kazi tu”, hivyo kuwataka mawaziri wa nchi hizo mbili kujipanga ipasavyo kuendana kasi hiyo.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Rais El-Sisi alisisitiza umuhimu wa kukuza biashara hasa katika sekta ya madini na madawa.
Alisema uhusiano baina ya mataifa hayo utaimarishwa zaidi na biashara.
Alisema nchi yake itaongeza uwekezaji hapa nchini katika sekta za ujenzi, uhandisi na miundombinu. Pia aliongeza kuwa nchi hizo zitaongeza ushirikiano katika kubadilishana wataalamu katika nyanja mbalimbali.
Kuhusu suala la amani, Rais El-Sisi alisema nchi yake itaendelea kushirikiana kwa ajili ya amani ya bara la Afrika na maendeleo ya bara hili.
“Napongeza jitihada za Tanzania katika kuleta amani eneo la maziwa makuu ikiwa ni jitihada za (Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin) Mkapa, pia kupokea wakimbizi katika ukanda huu,” alisema El-Sisi.
El-Sisi alimpongeza Rais Magufuli kwa kupambana na ufisadi na kuwekeza kwenye maendeleo na kusema kwamba ziara yake itarudisha uhusiano baina ya Tanzania na Misri.

Viongozi, wanachama 51 wa Chadema waanza kutoka kwa mafungu


Chato. Viongozi na wanachama wa Chadema 51 waliokuwa wakisota rumande wakidaiwa kufanya mkusanyiko bila kibali Julai 7, wameanza kupata dhamana kwa mafungu baada ya polisi kupeleka gari Gereza la Biharamulo lililowafikisha kituo cha polisi cha Chato.
Viongozi na wanachama hao waliopata dhamana tangu Julai 26 waliendelea kukaa rumande baada ya polisi kusema hawakuwa na gari la kuwafikisha mahakamani kukamilisha taratibu.
Fungu la kwanza la watu 14 lilifikishwa mahabusu ya kituo cha polisi Chato kusubiri wadhamini wao wanaotarajiwa kufika mahakamani leo kukamilisha taratibu za dhamana.
Katibu wa Chadema Kanda ya Ziwa, Rehema James alisema washtakiwa hao walifikishwa wachache licha ya gari walilopewa kuwa na uwezo wa kubeba washtakiwa 40.
“Tumeelezwa wapo washtakiwa wengine wanaohitaji kuletwa mahakamani wapate dhamana na wapo zaidi ya mwezi mzima hivyo hawawezi kuleta wa Chadema pekee kwa kuwa mahitaji ni mengi na wengi hawafikishwi mahakamani kutokana na kukosa gari,” alisema Rehema
Alisema polisi wamewaelekeza kuwa gari hilo litaendelea kufanya kazi ya kuwaleta watu mahakamani kwa wiki nzima lakini si kwa ajili ya washtakiwa wa Chadema hivyo kutojua hatma ya waliobaki watatoka lini.
Miongoni mwa waliotoka ni wanawake sita na wanaume saba ambao ni wanachama na kiongozi mmoja Mange Sayi, ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Chato.
Viongozi na wafuasi 51 wa Chadema walikamatwa Julai 7 kwenye Ukumbi wa Manzagata Kata ya Muganza wilayani Chato wakiwa kwenye kikao cha ndani na kushtakiwa kwa kosa la kufanya mkusanyiko bila kibali.
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Chato, Jovis Kato aliwaachia kwa dhamana Julai 26, baada ya kupitia hoja za pande zote mbili kati ya mashitaka na washitakiwa huku upande wa mashitaka ukiomba mahakama iwanyime dhamana washtakiwa hao ili waendelee na upelelezi.
Kato alisema baada ya kuzipitia hoja zote kwa kina, mahakama imekubali ombi la upande wa utetezi kuwa kifungu namba 148(5) kilichowekwa na upande wa mashtaka cha kuzuia dhamana za washitakiwa hakiendani na zuio hilo. Alisema kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 13(6)(b) inatamka wazi kuwa ni marufuku kwa mtu aliyeshitakiwa kwa kosa la jinai kutendewa kama mtu mwenye kosa hilo mpaka itakapothibitika kuwa anayo hatia ya kutenda kosa hilo.
Aliweka dhamana za washtakiwa hao 51 wazi tangu Julai 26 ambazo walitimiza masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili waliosaini hati ya Sh500,000 kila mmoja lakini hadi sasa bado wapo magereza.