Tuesday, August 15

Wapigadebe Dar ‘wajinafasi’ vituoni


Dar es Salaam. Agizo lililotolewa na polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaamu mwishoni mwa wiki iliyopita kuwataka wapigadebe wa daladala wasionekane vituoni kuanzia jana, la sivyo watakamatwa, halijatekelezeka.
Mwishoni mwa wiki, Kaimu Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Lucas Mkondya alitangaza kuwa msako dhidi ya wapigadebe ambao watakaidi amri hiyo ungeanza jana baada ya kupokea malalamiko mengi ya wananchi waliodai kuporwa vitu vyao kwenye vituo vya daladala.
Hata hivyo, jana wapigadebe hao walikutwa wakiendelea na kazi yao kama kawaida kwenye vituo mbalimbali.
Waandishi wa habari hizi waliwashuhudia wapigadebe hao kwenye vituo vya Mnazi mmoja, Baridi, Ilala na Buguruni vilivyopo wilayani Ilala na Riverside, Stendi ya Mabasi Ubungo na Darajani vya Wilaya ya Ubungo.
Alipopigiwa simu kuulizwa kuhusu wapigadebe hao kuendeea kuwapo vituoni, Mkondya alisema hawawezi kumaliza suala hilo kwa siku moja.
Akizungumzia suala hilo, dereva wa Bajaj katika eneo la Ubungo, Charles Robert alisema litapunguza vitendo vya wizi na vurugu katika vituo vya mabasi ambavyo vimekuwa vya kawaida. “Naliomba Jeshi la Polisi kuhakikisha watu hawa wanaondolewa katika vituo, kwani bado wanaendelea kufanya kazi bila ya wasiwasi,” alisema.
Hussein Said anayeendesha daladala alisema iwapo polisi watawaondoa wapigadebe hao watakuwa wamesaidia kuwapunguzia gharama za kuwalipa fedha kutokana na kuwaitia abiria vituoni akidai kuwa hata wasipoita abiria baadhi ya wapigadebe hulazimisha walipwe.
Abiria aliyejitambulisha kwa jina la Mariam Hussein alitaja kero ya wapigadebe ni kuwalazimisha abiria kupanda magari hata wasiyoyataka.
Baadhi ya wapigadebe walisema juzi kuwa, siyo wote wanaojihusisha na wizi na ukwapuaji wa mali za abiria.
“Kaka mimi nina familia yangu, mke na watoto na hii ni kama kazi nyingine. Nachofanya hapa ni kutafuta riziki tu, kama ningekuwa mwizi hapa nisingekuwepo maana huwezi kunyea kambi halafu ukarudi kulala hapohapo,” alisema Masoud Issa anayepiga debe kituo cha Tandika wilayani Temeke.
Jacob Joel maarufu kwa jina la Joe anayepiga debe katika Kituo cha Daladala cha Karume wilayani Ilala alisema kuwa wanao utaratibu wa kuwafukuza wezi wanaokwenda kituoni hapo kwa kuwa hawataki kusikia vilio vya abiria.
Akizungumzia uamuzi wa jeshi hilo, Julius Nyakweele anayetumia usafiri wa daladala alisema wapigadebe wana faida na kasoro zao.
“Kama mtu ni mgeni akisikia wanaita abiria inamrahisishia kujua gari analopanda, pia wapo wapigadebe wezi wanaowafanya watu wapande mabasi wakiwa wameibiwa mali zao,” alisema.
Machi 2007, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Alfred Tibaigana aliagiza wapigadebe wote kuondoka katika vituo vya daladala, lakini agizo hilo halitekelezwa.

No comments:

Post a Comment