Tuesday, August 15

Mjane aliyemlilia Rais Magufuli afikishwa mahakamani


Tanga. Swabaha Shoshi,  anayejulikana kwa jina maarufu kama mjane aliyemlilia Rais John Magufuli,  amefikishwa mahakamani jijini hapa na kusomewa shitaka la kuingia bila kibali katika  eneo la Chongoleani lililotengwa  kwa ajili ya mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Uganda.
Swabaha alifikishwa mbele ya Hakimu Hasna Majani wa Mahakama ya Mwanzo ya Usambara Mjini mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mwendesha mashtaka wa polisi, Koplo Rajabu alidai mahakamani hapo kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo Agosti 4 mwaka huu saa 8:00 mchana baada ya kuingia eneo hilo na kujenga vibanda vya biashara ya chakula.
Koplo Rajabu alidai kuwa eneo hilo limetengwa kwa ajili ya mradi wa bomba la mafuta ghafi unaounganisha Tanzania na Uganda, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria za nchi.
Hata hivyo, Swabaha alikana shitaka hilo na aliachiwa kwa dhamana na kesi hiyo itasikilizwa tena Agosti  18.
Swabaha  alikamatwa Chongoleani Agosti 4 mwaka huu na kukaa rumande hadi alipofikishwa mahakamani mwishoni mwa wiki.
Swabaha alijipatia umaarufu wakati alipojitokeza mbele ya Rais Magufuli Machi mwaka huu wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Sheria iliyofanyika kitaifa katika viwanja vya Diamond Jubilee.
Siku hiyo, mwanamke huyo alifanya harakati hadi Rais alipomuona na kutaka aruhusiwe atoe yake ya moyoni na akaeleza madai ya kudhulumiwa mali za urithi.

No comments:

Post a Comment