Nyumba hiyo ipo kwenye shamba linalomilikiwa na familia ya Mkapa lililopo eneo la Mbezi kwa Msuguri, maarufu kwa jina la Kituo cha Zamani.
Nyumba zilizojengwa eneo la kuanzia Kimara hadi Kiluvya ambazo ziko ndani ya mita 121 kutoka katikati ya barabara hiyo kuu inayounganisha jiji la Dar es Salaam na mikoa mingine, zitabomolewa kwa ajili ya kupisha upanuzi.
Ingawa kijana aliyekuwepo hakuwa tayari kutoa maelezo, nyumba hiyo imezungushiwa ukuta na ina lango lililopakwa rangi nyeusi na ina duka ambalo muuzaji amewekwa na msimamizi wa mali hiyo.
Katika moja ya sehemu za ukuta wa nyumba hiyo kumeandikwa “hatubomoi hadi tulipwe”, lakini mtu aliyedai kuwa ndugu wa mama huyo alisema familia haihusiki na maandishi hayo, akituhumu watoto kuwa ndio walioandika hivyo.
Waandishi wa Mwananchi walifika katika nyumba hiyo ya Mama Anna Mkapa jana saa 5:00 asubuhi na kumkuta mmoja wa watu aliyedai ni ndugu wa mke wa rais huyo wa zamani.
“Ni kweli hapa ndiyo nyumbani kwa mama Anna Mkapa, lakini mimi siwezi kuzungumza chochote kwa sababu si mhusika. Hapa ni kama mwangalizi wa nyumba tu,” alisema.
Huku akigoma kutaja jina lake, mtu huyo alishauri atafutwe mmiliki wa nyumba hiyo kwa ajili ya maelezo zaidi.
“Naomba mtafute mama (Anna Mkapa) mwenyewe. Nendeni ofisini kwake. Mimi hapa ameniachia tu kama mwangalizi wa nyumba yake, kwa hilo mtanisamehe siwezi kuzungumza,” alisema .
Hata hivyo, mmoja wa wafanyakazi wa ndugu wa mke huyo wa Rais wa zamani ambaye alikuwa akiuza duka lililoko nje ya nyumba hiyo, alisema atafutwe mtu mmoja aliyemtaja kuwa ni “babu mmoja kipofu”.
“Naomba mkamuone babu mmoja kipofu na yeye nyumba yake imewekewa alama ya “X” anaweza kuwa na taarifa juu ya nyumba hii kwani nimekuwa nikimsikia akizungumza,” alisema.
Mmoja wa watoto waliokuwa eneo hilo aliwapeleka waandishi kwa babu huyo.
“Karibuni hapa ndipo nyumbani kwa babu,” alitukaribisha mtoto huyo.
“Karibuni nyinyi ni akina nani? Aliuliza babu,” na alipojibiwa kuwa ni waandishi alionekana kukubali.
“Ah. Nyie ndiyo waandishi wa Mwananchi mmekuwa mkiandika sana kuhusu bomoabomoa na leo mmeandika kuhusu waumini waliokimbia kanisa kwa sababu ya bomoabomoa,” alisema.
Baadaye alijitambulisha kuwa anaitwa James Shirinde (80) na alianza kueleza jinsi alivyonunua eneo hilo ambalo kwa sasa linamilikiwa na familia ya Mkapa.
“Nilinunua eneo hilo mwaka 1975 wakati huo nikiwa mfanyakazi wa Shirika la Reli ambalo kwa wakati huo lilijulikana kama TRC na huku kulikuwa ni mashamba tu,” alisema.
“Mwaka 1980, mke wa rais mstaafu alikuja akanunua shamba na akajenga nyumba ambayo mpaka sasa anaishi mdogo wake, Rose Silayo.”
Shirinde, ambaye kwa sasa anaishi peke yake baada ya mkewe kufariki na watoto wake kumtelekeza, alisema wakati wananunua eneo na kujenga, Wakala wa Barabara (Tanroads) walikuwa hawajaweka mawe
“Haya mawe waliyoyaweka sasa yametukuta baada ya kutungwa sheria mpya ya Hifadhi ya Barabara ya mita 121.5 mwaka 2007 na 2009. Wakati huo mke wa Mkapa naye alikuwa amejenga nyumba yake na mumewe pia alikuwa amenunua shamba huku la ekari tano,” alisema.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mji Mpya, Daniel Majige alisema shamba hilo ni mali ya Mkapa na nyumba ni ya mkewe.
“Ni kweli najua kuna shamba la Mkapa ambalo litamegwa nusu na Tanroads ili kupisha utanuzi wa barabara ya Morogoro, lakini kuhusu nyumba ya mke wake hiyo sijapata taarifa labda niifuatilie,” alisema.
Majige alisema shamba hilo ni la muda mrefu na moja ya mashamba ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na wananchi kutokana na kutelekezwa na hivyo kuwa pori.
“Tumekuwa tukiwaambia mara nyingi kuhusu shamba lao kuwa tatizo, lakini wanachofanya wanakuja wanafyeka kisha wanaliacha tena na tumeshaomba sana hilo shamba tupewe Serikali ya kijiji ili tuliendeleze kwa kujenga kituo cha polisi lakini hatujawahi kujibiwa chochote,” alisema.
Injinia wa Tanroads, Johnson Letechura alipoulizwa kuhusu alama ya bomoa katika nyumba hiyo, alijibu kwa kuuliza: “Unataka kujua kama ni nyumba yake ili iweje? Acheni kuandika habari za nonsense (zisizo na maana),”alisema.
Lutechura alisema nyumba ya mtu yeyote iliyoko kwenye hifadhi ya barabara itabomolewa, na baadaye akakata simu.
Imeandikwa na Jackline Masinde, Asna Kaniki na Hidaya Nyanga, Mwananchi
No comments:
Post a Comment