Tuesday, August 15

Makonda alivyoipiga chenga timu ya MCT sakata la Clouds

Mmoja wa wajumbe wa timu ya uchunguzi wa ripoti

Mmoja wa wajumbe wa timu ya uchunguzi wa ripoti ya uvamizi wa Studio za Clouds Tv,  Wakili Juma Thomas akizungumza jijini Dar es Salaam jana kuhusu  ripoti ya uchunguzi   uliofanywa  na Baraza la Habari Tanzania (MCT), kuhususiana na  tukio la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuvamia Studio za Clouds Media Group (CMG). Kushoto ni  mweyekiti wa  kamati ya maadili ya Baraza hilo, Jaji mstaafu Juxon Mlay. Picha na Mpiga picha wetu 
Dar es Salaam. Ripoti ya uchunguzi uliofanywa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) kuhusiana na tukio la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuvamia studio za Clouds Media Group (CMG) imeonyesha jinsi kiongozi huyo alivyowapiga chenga timu ya uchunguzi hivyo kushindwa kupata upande wake.
Kama ilivyokuwa kwa kamati iliyoundwa na aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye kuchunguza sakata hilo lilipotokea, ndivyo ilivyokuwa kwa timu hii ambayo pia ilishindwa kuzungumza na Makonda.
Kiongozi wa timu hiyo mwanasheria Juma Thomas alisema mara tatu wajumbe wa timu hiyo walikwenda kwenye ofisi za Makonda lakini hawakufanikiwa kukutana naye.
“Suala la uchunguzi linahusisha pande zote. Tumeongea na wafanyakazi wa CMG, Kamanda wa Polisi Kinondoni, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu,maofisa wa mamlaka ya mawasiliano na waandishi wengine lakini hatukufanikiwa kumpata Makonda,”
“Timu ilimwandikia barua Makonda ikitoa sababu za umuhimu wake kukutana naye. Barua hiyo yenye kumbukumbu namba MCT/15/005/2017 iliandikwa Mei 2 na ilipokelewa na kugongwa mhuri wa mkuu wa mkoa lakini mpaka ripoti hii inaandikwa, barua hiyo haikuwa imeshughulikiwa,”
“Tulimpa nafasi ya kumsikiliza lakini alishindwa kuitumia fursa hiyo. Kila tulipokwenda ofisini kwake tuliambiwa yupo nje ya ofisi kwa shughuli za kikazi. Hatukuishia hapo tulipata namba zake za simu tulipopiga iliita bila kupokelewa.”
Hata hivyo Makonda mwenyewe akizungumza wiki iliyopita wakati wa mkutano wa waandishi wa habari ulioandaliwa na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) alidai kuwa ripoti iliyotolewa na kamati iliyoundwa na Nape haikusikiliza upande wake.
“Hukumu ilitolewa kwa kusikiliza upande mmoja, sikusikilizwa na mimi nikaelezea upande wangu,” alisema Makonda.
Kwa mujibu wa ripoti ya MCT, Makonda anatakiwa kuomba radhi waandishi wa habari na Watanzania kwa ujumla kwa kitendo hicho.
Hata hivyo Makonda alishasema kuwa hawezi kuomba radhi na katu hawezi kutoa neno samahani kwenye kinywa chake. “Hilo neno halitokuja litokee kwenye kinywa changu, sitaomba radhi narudia tena kwa herufi kubwa,” alisema Makonda kwenye mkutano wa TEF.
Kilichobainika kwenye uchunguzi
Timu ya MCT ilibaini kuwa ni kweli Makonda alivamia studio za Clouds akiwa na askari watano wenye silaha.
Mlinzi aliyehojiwa na timu hiyo alieleza kuwa haikuwa mara ya kwanza kwa Makonda kwenda CMG lakini siku hiyo alikwenda akiwa na mwonekano tofauti.
“Tulipomuuliza mlinzi wa zamu kwa nini hakumzuia kuingia alisema kuwa alishindwa kufanya hivyo kwa kuwahofia wale askari aliokuwa ameambatana nao Makonda,” alisema.
Somo kwa vyombo vya habari
Timu ya uchunguzi ilipendekeza kuwa licha ya kuwepo kwa uhusiano kati ya wanasiasa na mashirika ya kisiasa ipo haja ya kuweka mipaka ili kuzuia siasa kuingilia uhuru wa vyombo vya habari.
Timu hiyo ilionya wahariri na watendaji wengine kwenye vyombo vya habari kujiepusha na uhusiano wa karibu sana na wanasiasa kiasi cha kufanya kazi yao ya uandishi kuwa ngumu.
Hali ya vyombo vya habari
Katibu Mtendaji MCT, Kajubi Mukajanga alisema walifanya utafiti kuangalia hali ya vyombo vya habari katika nyanja za kiuchumi, masuala ya kisheria, usimamizi pamoja na changamoto zinazoikabili tasnia hiyo.
Akielezea utafiti huo kwa upande wa Tanzania Bara, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha SAUT, Dk Joyce Bazira alisema kwa ujumla hali ya vyombo vya habari haikuwa nzuri kutokana na kuminywa kwa uhuru wa habari kutokana na mabadiliko ya kisheria.
Alisema wadau wameeleza kuwa mabadiliko hayo ikiwamo Sheria ya Huduma za Habari iliyopitishwa mwaka jana imekuwa na athari kubwa tofauti na matarajio ya wengi.
Sheria nyingine ni ya haki ya kupata habari (Access to Information Act) pamoja na Sheria ya Mitandao (Cybercrime Act) ambazo zote zimekuwa na changamoto wakati wa utekelezaji wake.

No comments:

Post a Comment