Sunday, November 5

PROFESA MBARAWA AWEKA JIWE LA MSINGI LA UJENZI WA UWANJA WA NDEGE WA MKOA WA GEITA


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akisalimia wananchi wakati wa sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa mkoa wa Geita unaojengwa wilayani humo kwenye sherehe zilizofanyika leo Jumamosi Novemba 4, 2017. Uwanja huo ambao utakuwa na njia yenye urefu wa kilomita 3, unajengwa na makandarasi wazalendo.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akiwa na Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani ambaye ni Mbunge wa Chato wakifunua kitambaa kuashiria  uwekaji wa jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa mkoa wa Geita unaojengwa wilayani humo kwenye sherehe zilizofanyika leo Jumamosi Novemba 4, 2017. Uwanja huo ambao utakuwa na njia yenye urefu wa kilomita 3, unajengwa na makandarasi wazalendo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akiwa na Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani ambaye ni Mbunge wa Chato wakifunua kitambaa kuashiria  uwekaji wa jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa mkoa wa Geita unaojengwa wilayani humo kwenye sherehe zilizofanyika leo Jumamosi Novemba 4, 2017. Uwanja huo ambao utakuwa na njia yenye urefu wa kilomita 3, unajengwa na makandarasi wazalendo.

Wabunge wa Mkoa wa Geita wakipanda mti wakati wa sherehe za   uwekaji wa jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa mkoa wa Geita unaojengwa wilayani humo kwenye sherehe zilizofanyika leo Jumamosi Novemba 4, 2017. Uwanja huo ambao utakuwa na njia yenye urefu wa kilomita 3, unajengwa na makandarasi wazalendo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akiwa na Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani ambaye ni Mbunge wa Chato pamoja na viongozi waandamizi wa Wizara na mkoa wakikata utepe kuashiria  uwekaji wa jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa mkoa wa Geita unaojengwa wilayani humo kwenye sherehe zilizofanyika leo Jumamosi Novemba 4, 2017. Uwanja huo ambao utakuwa na njia yenye urefu wa kilomita 3, unajengwa na makandarasi wazalendo.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mhandisi Patrick Mfugale (kushoto) akipata maelezo wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa mkoa wa Geita unaojengwa wilayani Chato. Uwanja huo ambao utakuwa na njia yenye urefu wa kilomita 3, unajengwa na makandarasi wazalendo.

WANAFUNZI WATAKIWA KUTUMIA MITANDAO KUPATA MAARIFA

Wanafunzi wa Chuo cha Kodi (ITA) jijini Dar es Salaam, wametakiwa kutumia vyema teknolojia ya mawasiliano hususan mitandao ya kijamii kujifunza ili kupata maarifa badala ya kuitumia kwa mambo ambayo hayatawasaidia katika masomo.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Chuo cha Kodi Prof. Isaya Jairo wakati akiwakaribisha wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na chuo hicho kwa mwaka wa masomo 2017/18.Amesema vijana wengi wanatumia mitandao ya kijamii kwa masuala ya kijamii kwa kiwango kikubwa kuliko kuitumia kujifunza na kupata maarifa kwa mambo ambayo yatawasaidia kukuza kiwango cha elimu.

“Elimu ipo kila mahali siku hizi: katika vitabu, mitandao na tuna mambo mengi ambayo yanasaidia sana kujifunza tofauti na ilvyokuwa miaka 30 iliyopita. Ni wajibu wa wanafunzi kuitumia vyema mitandao hususan simu kujifunza na kupata maarifa”, alisema Prof. Jairo.

Mkuu huyo wa chuo amesema kwamba chuo cha kodi kinatumia mfumo wa kujenga umahiri kwa mwanafunzi ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi wa hali ya juu na ambao umelenga kumuwezesha mwanafunzi kujifunza badala ya kufundishwa. Ameongeza kwamba mfumo huo ndio utaratibu unaotumika ulimwenguni ili mwanafunzi anapohitimu awe na uwezo wa kujua nini cha kufanya katika fani yake na kwa Chuo cha Kodi ajue jinsi ya kukusanya kodi.

“Msije mkakaa mkategemea mtafundishwa tu na mtakaa na kumsikiliza mwalimu, hapana, tunawatarajia mjifunze kwa kutumia nyenzo mbalimbali zilizopo”, amesema Prof. Jairo na kuongeza kwamba huo ndio utaratibu unaotumika katika mfumo wa kujenga umahiri kwa mwanafunzi.

Katika hatua nyingine amewataka wanafunzi hao wa Astashahada ya Uwakala wa Forodha ya Afrika Mashariki, Shahada ya Usimamizi wa Forodha na Kodi na Stashada ya Uzamili ya Kodi, kuzingatia masomo kwani ndio lengo lao kuu la kuomba kujiunga na chuo cha kodi na kwa upande wake chuo cha Kodi kitatimiza wajibu wake kuhakikisha wanapata elimu wanayostahili na katika mazingira bora.

Aidha amewahakikishia wanafunzi hao kwamba wale watakaofaulu vizuri watapata ajira kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania kwani TRA huchukua wanafunzi waliofaulu kwa kiwango cha juu.Kuhusu maisha katika Chuo cha Kodi, Prof. Jairo amewataka wanafunzi hao kuishi kwa mujibu wa sheria za nchi pamoja na kufuata sheria ndogo ndogo na taratibu za chuo.

Pamoja na Mkuu wa Chuo cha Kodi, katika kuwakaribisha wanafunzi hao, pia walikuwepo Kaimu Naibu Mkuu wa Chuo Taaluma Justin Musa, Kaimu Mkuu wa Chuo, Utawala Emmanuel Masalu, Mkuu wa Huduma za Fedha Emmanuel Foya, Makamu wa Rais wa Serikali ya wanafunzi wa Chuo cha Kodi (ITASO) Darafu Abdalah, Wakuu wa vitengo mbalimbali pamoja na walimu.
Wanafunzi wapya katika Chuo cha Kodi wakifuatilia kwa makini maelezo ya Mkuu wa Chuo cha Kodi Prof. Isaya Jairo 
Mkuu wa Chuo cha Kodi (ITA) Prof. Isaya Jairo (aliyesimama) akizungumza na wanafunzi wapya waliojiunga na Chuo hicho kwa muhula wa masomo wa kuanzia 2017/18. Wengine kutoka kushoto ni Mkuu wa Huduma za Fedha Emmanuel Foya na Kaimu Naibu Mkuu wa Chuo Utawala, Fedha na Mipango Emmanuel Masalu. (Imeandaliwa na Robert Okanda Blogs) 
Wanafunzi wapya katika Chuo cha Kodi wakifuatilia kwa makini maelezo ya Mkuu wa Chuo cha Kodi Prof. Isaya Jairo 
Mkuu wa Chuo cha Kodi (ITA) Prof. Isaya Jairo akisisitiza jambo kwa wanafunzi wapya waliojiunga na Chuo hicho kwa muhula wa masomo unaoanza 2017/18. Kushoto kwake ni Kaimu Naibu Mkuu wa Chuo Utawala, Fedha na Mipango Emmanuel Masalu na Kaimu Naibu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri Justin Musa. 
Mmoja wa wananfunzi akiuliza swali wakati wa tujio la kuwakaribisha wanafunzi wapya katika Chuo cha Kodi (ITA) 
Kaimu Naibu Mkuu wa Chuo Utawala, Fedha na Mipango Emmanuel Masalu (Aliyesimama) akiwaeleza wanafunzi wapya katika Chuo cha Kodi masuala ya Utawala katika chuo hicho. Pamoja naye kutoka kulia ni Kaimu Naibu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri Justin Musa, Mkuu wa masuala ya Fedha Emmanuel Foya na Makamu Mwenyekiti wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo cha Kodi (ITASO) Darafu Abdalal .

Msekwa: Utaratibu wa kumkabidhi ‘kijiti’ mwenyekiti CCM utazamwe upya


Dar es Salaam. Makamu mwenyekiti wa CCM mstaafu, Pius Msekwa ameshauri utaratibu wa kupokezana vijiti katika uongozi wa juu wa CCM uangaliwe upya kwa kuwa unakiongezea gharama chama hicho.
Msekwa ambaye pia amewahi kuwa Spika wa Bunge, amesema utaratibu wa kumchagua mwenyekiti wa Taifa kupitia mkutano mkuu maalumu unakigharimu chama hicho, badala yake uwekwe utaratibu wa kikatiba utakaoruhusu mtu anayechaguliwa kuwa rais kupitia CCM moja kwa moja awe mwenyekiti wa chama.
Kwa muda mrefu CCM imekuwa ikifanya mkutano mkuu maalumu kwa ajili ya kumsimika mwenyekiti mpya Taifa, mkutano ambao unadaiwa kutumia fedha nyingi zinazofikia takriban Sh1 bilioni.
Katika mwendelezo huo, chama hicho Julai 23, 2016 kilifanya mkutano mkuu maalumu na kumchagua Rais John Magufuli kupokea kijiti kutoka kwa mtangulizi wake, Jakaya Kikwete.
Lakini, Msekwa katika makala yake ya miaka miwili ya uongozi wa Rais Magufuli katika chama hicho, anasema “Ingewezekana kabisa kupunguza gharama hizo kwa kuondoa haja ya kuitisha mkutano mkuu wa chama, kwa njia rahisi tu ya kurasimisha utamaduni huo kwa kuuingiza kwenye katiba ya chama.”
Akitoa mfano, Msekwa anasema CCM inaweza kuongeza ibara ndogo katika ibara ya 118 ya Katiba ya CCM, itakayosomeka, “Wakati wote ambapo chama kitakuwa madarakani, Rais wa Jamhuri ya Muungano anayetokana na CCM atakuwa pia ndiye mwenyekiti wa Taifa wa CCM, na atakuwa katika nafasi hiyo kwa muda wote atakapokuwa Rais.”
Anafafanua kuwa matokeo ya marekebisho hayo ya Katiba yatakuwa ni kwamba, Rais mpya anayetokana na CCM akisha kuapishwa, basi moja kwa moja anakuwa pia ni mwenyekiti wa Taifa wa CCM, bila haja ya kuitisha mkutano mkuu maalumu wa kumpigia kura na kwa hiyo kuondoa gharama zake.
“Ni wazo linalopendekezwa kwa ajili ya kufikiriwa, tuliangalie hili,” alisisitiza Msekwa.
Msekwa anasema wanachama wa CCM wanauelewa vizuri utamaduni wa chama chao kwamba mtu anayechaguliwa kuwa Rais kutokana na CCM, ndiye vilevile anakuwa mwenyekiti wa CCM.
Utaratibu ulivyoanza
Alisema miaka ya nyuma enzi za Tanu, utaratibu ulikuwa ni kwamba wakati wa uchaguzi unapofika, mwenyekiti wa CCM ndiye aliyekuwa akiteuliwa kuwa mgombea wa nafasi ya urais.
“Utaratibu huo ulijulikana kwa jina la ‘Kofia mbili za uongozi’. Mwalimu Nyerere alipoamua kustaafu urais mwaka 1985, kulikuwa na wasiwasi mkubwa miongoni mwa jamii, kwamba bila Mwalimu kuwapo katika uongozi, nchi yetu ingeyumba.
“Ili kudhibiti wasiwasi huo, chama kilifanya uamuzi kwamba, Mwalimu aendelee kuwa mwenyekiti wa Taifa wa CCM kwa kipindi kitakachoivusha nchi kutoka kwenye wasiwasi huo. Mwalimu Nyerere alikubali kuendelea na wadhifa huo, hadi alipokabidhi kijiti kwa Rais Mwinyi mwaka 1990. Wakati huo Mwinyi alikuwa anachaguliwa kwa kipindi cha pili.
Hata hivyo, Msekwa anasema kwa kuwa mwaka 1990 haukuwa wa uchaguzi wa kawaida wa viongozi wa CCM, ilibidi ufanyike uchaguzi mdogo wa kumchagua Rais Mwinyi kuwa Mwenyekiti wa CCM ili kuendeleza utamaduni huo wa ‘kofia mbili za uongozi’ katika ngazi hiyo.
Kuanzia wakati huo hadi sasa, rais aliyepo madarakani amekuwa akichaguliwa kuwa mwenyekiti wa CCM kwa njia ya uchaguzi mdogo, ambapo inabidi kuitisha mkutano mkuu maalumu wa chama hicho kwa ajili hiyo.
“Hapo ndipo suala la gharama linapojitokeza, inabidi kuwa na wazo la kupunguza gharama hizo,” anaongeza Msekwa.

Teknolojia imelizidi nguvu zuio la mikutano ya kisiasa nchini


Julai mwaka jana, Rais John Magufuli akiwa ametoka kukabidhiwa uenyekiti wa CCM na Mkutano Mkuu, alisisitia uamuzi wa kuzuia mikutano ya kisiasa na maandamano, akitoa sababu kwamba hataki kuongoza nchi ambayo watu wake muda wote wanafanya siasa.
Mkutano huo ulitanguliwa na wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) na Kamati Kuu (CC) ukiwa ni mchakato wa kumtawaza Rais Magufuli uenyekiti ili kumrithi Jakaya Kikwete.
Kabla ya tangazo hilo, kulikuwa na maagizo ya Jeshi la Polisi ya kuzuia shughuli za kisiasa ndani na nje. Nakumbuka Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), lilitishia kuzuia mikutano hiyo ya CCM likidai ni kuunga mkono tamko la polisi.
Baadaye vikao vya ndani vya vyama viliruhusiwa, lakini mikutano ya hadhara bado ni marufuku. Ukiacha mikutano ya kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani na Serikali za Mitaa Januari mwaka huu na hii ya sasa, hakuna mingine iliyofanyika tangu tangazo la Rais Magufuli.
Ukiwa umepita zaidi ya mwaka mmoja sasa tangu tangazo la Rais Magufuli kuzuia mikutano ya hadhara na matukio ya wazi, ni muda wa kujiuliza kama je, tangazo limepunguza kufanyika kwa harakati za kisiasa?
Katazo la shughuli za kisiasa lilielekeza kusubiri Uchaguzi Mkuu 2020, kwa maana ya wakati wa kampeni za kuwania dola. Chadema walitangaza kuandaa na kutekeleza operesheni waliyodai ya kupinga udikteta Tanzania, yaani Ukuta.
Hata hivyo, hawakutekeleza operesheni yao Septemba Mosi, 2016 baada ya kuzuiwa na polisi na wao kutangaza kuiahirisha na hadi sasa hakuna kilichofanyika.
Maswali yanaongezeka; umepita mwaka mmoja tangu Chadema waliposhindwa kutekeleza operesheni ya Ukuta kwa kuogopa mkwara wa Serikali, hasa baada ya Rais Magufuli kusema “wasimjaribu”, je, hata baada ya Ukuta kutofanyika, siasa zimedumaa?
Majibu ya maswali
Katika mwaka 2017, Tanzania imeshuhudiwa ikitanuka kwa kuwa na majukwaa mengi ya ufanyaji siasa kuliko miaka mingine yote iliyopita. Watu wenye kuzungumza siasa nchini ni wengi na mijadala inafanyika kwa ukaribu zaidi.
Hitaji la watu kuhudhuria mikutano ya hadhara ili kusikiliza sera na hoja za wanasiasa limepungua. Mwananchi anaweza kupokea neno au kushiriki mjadala wa kisiasa popote alipo. Akiwa nyumbani au ofisini kwake, anapokuwa kwenye chombo cha usafiri au hata hospitali amelala kitandani.
Hiyo imekuwa sababu ya kipindi ambacho wanasiasa wakiwa hawafanyi mikutano ya hadhara kama ilivyokuwa mwanzo, lakini siasa zimekuwa zikipata mwitikio mkubwa mno. Majukwaa ya mawasiliano ya umma yamesababisha sauti zipazwe na kusikika.
Nguvu ya majukwaa mapya ya kisiasa imeondoa urasimu kwa wanachama na mashabiki wa vyama vya siasa kusubiri matamko na hoja za viongozi wao, hivi sasa nao wanaweza kujenga hoja za ushawishi au kuzitetea taasisi zao.
Athari za ukuaji wa matumizi ya na mitandao ya kijamii duniani zimekuwa kubwa nchini, hivyo kufanya Facebook, Twitter, Instagram, YouTube na WhatsApp kuwa kiungo muhimu cha mawasiliano ya umma.
Akaunti za Twitter, YouTube na Instagram, kurasa za Facebook na makundi yake, na kwa nguvu zaidi WhatsApp kupitia makundi yake ya kijamii, siasa zimekuwa zikishamiri na kufanya watu wasahau habari za mikutano ya hadhara ya kisiasa.
Kiongozi wa kisiasa anapotaka kuzungumza jambo analiwasilisha kwenye ukurasa wake wa Facebook, akaunti zake za Twitter, YouTube na Instagram, kisha watu wanachukua na kusambaza kwenye makundi ya WhatsApp, ujumbe unaenea na kujadiliwa.
Tofauti na mikutano ya hadhara ambayo hufanya kiongozi awe mbali na hadhira yake, mitandao ya kijamii inawezesha majadiliano kuliko hotuba. Kwamba kiongozi anaweza kuzungumza jambo kisha hadhira ikachangia kwa kuunga mkono au kupinga. Vilevile hadhira huuliza maswali na kujibiwa.
Kimsingi mitandao ya kijamii inawezesha watu kuzungumza fikra zao kwenye siasa na masuala mengine yote ya kijamii. Hali hiyo ndiyo ambayo inafanya mijadala ya kisiasa ipate nafasi kubwa. Tukio kubwa kuhusu nchi likitokea linaibua mijadala kwenye mitandao ya kijamii.
Kiongozi akihutubia, vipande vya hotuba yake vinasambazwa kwenye mitandao ya kijamii na kujadiliwa kwa upana. Watu hawasubiri viongozi wa kisiasa wahutubie ili kuchambua hotuba ya kiongozi, bali wao wenyewe kwenye majukwaa yao wanajadili.
Haishangazi siku hizi Rais Magufuli kusikika akijibu hoja za mitandao ya kijamii ambayo huanzishwa hata na watu wasiofahamika. Imekuwa kawaida sasa kwa viongozi wa kisiasa kukopa mawazo ya watu wa mitandaoni na kuyatumia kujenga hoja, tofauti na hapo zamani.
Siasa na teknolojia
Kwa kuipima falsafa ya siasa na teknolojia katika dunia ya sasa, sehemu kubwa ya maudhui yake inabebwa na simu za mkononi. Inaonekana wanasiasa wengi nchini hawakujitayarisha kwa ajili ya mabadiliko hayo, isipokuwa wamezolewa tu na mkumbo wa mapinduzi ya kiteknolojia.
Teknolojia inarahisisha mipango ya kisiasa bila mikutano ya hadhara, kiasi kwamba Tundu Lissu akiwa kitandani hospitalini Nairobi, Kenya, anaweza kuzungumza na Taifa zima na ujumbe ukaenea kila mahali. Anajirekodi akiwa hospitali, sauti inaingizwa YouTube.
Watu wanachukua sauti yake YouTube na kuipeleka Facebook na makundi ya WhatsApp, vilevile inakatwa nusunusu na kuwekwa Twitter na Instagram. Sauti inafika kwa wapigakura wake na kila eneo, kisha inajadiliwa kwenye majukwaa mbalimbali.
Mpango wa mawasiliano ya moja kwa moja kupitia mitandao ya kijamii, Facebook Live, Instagram Live na YouTube Live, unawezesha kufanya mikutano si tena na waandishi wa habari, bali na ulimwengu mzima.
Ukiweka ‘live’, popote ulipo unaweza kumfikia yeyote mwenye kuipata akaunti yako. Haya ndiyo mapinduzi makubwa ya kiteknolojia ambayo kwa kiasi kikubwa yanafanya siasa za majukwaa ya kawaida zianze kupitwa na wakati.
Wanasiasa lazima wajiandae kuendana na wakati. Wajifunze kutengeneza maudhui yenye kufikika kupitia simu za mkononi. Hiki ni kipindi ambacho mfanyakazi hawezi kusema alipitwa na mkutano kwa sababu alikuwa kazini, kwani simu yake inakuruhusu umfikie wakati wowote na uzungumze naye.
Maandalizi hayo ni kuielewa teknolojia na kuyafahamu mahitaji yenye kutosheleza kubeba maudhui ya kiteknolojia. Kwamba mwanasiasa mjanja atachanua wakati wote hata kama kutakuwa na hali ya kuzibwa mdomo kwa vyombo vya habari vya kawaida (traditional media).
Wala si jambo la ajabu, kwani kulishakuwa na njia za upashanaji habari kwa mtindo wa kale (old media), hivyo lazima kujua mahitaji ya Zama za Taarifa (Information Age) ambazo zinatawala sasa na ni dhahiri sayari ya dunia inakwenda kubadilika kupitia mtindo wa kimaisha kwa wakazi wake.

Kenya bado inahitaji maombi kuvuka vikwazo


Kama kawaida, Kenya inaendelea kuingia kwenye shimo la sintofahamu baada ya kukamilika uchaguzi na Uhuru Kenyatta kutangazwa mshindi.
Uchaguzi ulifanyika kama ulivyopangwa Oktoba 26 kama ilivyoamriwa na Mahakama ya Juu ikitarajiwa kwamba uchaguzi huo wa marudio ungekuwa dawa ya kuepusha maradhi ya chuki, kutoaminiana na unafiki miongoni mwa Wakenya na viongozi wao.
Ni wazi kwamba uchaguzi huo haukuleta nafuu. Lakini, hatimaye baadhi ya Wakenya wanafurahi kwamba, uchaguzi huo umewapa kisogo na wanaweza kuendelea na maisha yao na biashara zinazoendelea kudorora kila kukicha kwa sababu ya siasa zilizojaa chuki na ukabila.
Kwa wale waliofikiria maisha yatakwenda sawa baada ya uchaguzi, nina ujumbe kwao; mbele si sawa. Kwa nini? Kwa sababu kama ilivyokuwa baada ya uchaguzi wa Agosti 8, masuala yaliyoibuka bado hayajatatuliwa kulingana na madai ya kiongozi wa upinzani, Raila Odinga na viongozi wenza wa Muungano wa National Super Alliance (Nasa).
Rais Kenyatta alishinda uchaguzi wa juzi kama alivyoshinda ile ya Agosti 8. Ushindi wake umekumbwa na upinzani mkali kutoka kwa Nasa na mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo sasa wanadai Kenyatta analazimisha kuwaongoza Wakenya.
Kikundi hiki cha Wakenya kinadai mazingara ambayo uchaguzi ulifanywa hayangeweza kuhakikisha matokeo bora. Yafaa kukumbukwa kwamba Odinga aliyekuwa akipigania urais kwa tiketi ya Nasa alijiondoa akidai Tume ya Uchaguzi (IEBC) ilikataa kutekeleza mabadiliko na kurekebisha dosari zilizokuwa zimesheeni uchaguzi wa Agosti na kulazimisha mahakama kuufutilia mbali baada ya Nasa kwenda mahakamani kupinga ushindi wa Kenyatta.
Kiini cha upinzani kupinga matokeo ya uchaguzi ni madai kwamba, asilimia 27 pekee ya wapiga kura walifika katika vituo vya kupigia kura Oktoba 26. Nasa pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali yanahoji kwa nini Kenyatta atangazwe mshindi ilhali mamilioni mwa Wakenya hawakupiga kura? Pia, wanadai kwamba vikosi vya usalama kama vile polisi walitumiwa kuwadhalilisha wafuasi wa Nasa kwa kuitikia wito wa Raila wa kususia uchaguzi.
Takwimu za mashirika ya haki za kibinadamu kama vile Human Rights Watch (HRW) na Transparency International (TI) yanadai Wakenya wapatao 40 waliuawa kwa risasi au kuumizwa na polisi katika ngome za Nasa. Maeneo yaliyoathiriwa mno na ghasia na vifo ni majimbo ya Kisumu, Homa Bay, Siaya, Migori Bungoma na Kakamega.
Katika jiji kuu la Nairobi, maeneo ya Kibera, Mathare na Kawangware yalikumbwa na ghasia baada ya polisi kukabiliana na wafuasi wa Nasa kabla na baada ya uchaguzi hivi majuzi.
Licha ya HRW kuchapisha majina ya waliouawa kwenye ghasia hizo, Serikali imepinga vikali ripoti hiyo ikisema si ya kweli. Nasa inauliza kwa nini vijana walimiminiwa risasi na kuuawa ilhali walikuwa wamejihami na mawe.
Wakazi wa maeneo hayo walikabiliana vibaya na polisi huku wakifunga barabara na kurushiana mawe na walinda usalama katika juhudi za kuzuia kwa kila namna zoezi hilo kufanyika.
Wabunge wa maeneo hayo wamelaani “unyama wa polisi” wakisema kuna njia mbadala ambazo zingetumiwa na maofisa hao kuzima maandamano hayo.
Nasa inasisitiza kwamba vifo vingi vilivyoripotiwa katika ngome zao ni uthibitisho kwamba Serikali ya Jubilee inaendeleza sera zake za chuki kwa jamii zinazoegemea upande wa upinzani.
Raila ameapa kupigana na Serikali ya Kenyatta hadi mwisho akisema utawala wa Jubilee unafaa kuondolewa kwa sababu ya “wizi wa kura”, uongozi wa kidhalimu na ufisadi uliokithiri.
Lakini, Kenyatta anasema kwamba ushindi wake ni halali na kamwe chama chake cha Jubilee hakijatumiwa kwa njia yoyote ile katika wizi wa kura. Rais anasema ingawa kulikuwa na ghasia za hapa na pale, Wakenya walijitokeza kumchagua kama walivyofanya katika kura ya Agosti 8.
Wadadisi wa siasa wanasema Rais Kenyatta alitangazwa mshindi ilhali mamilioni ya Wakenya hawakupiga kura jambo linalofanya uchaguzi huo kuwa batili.
Raila anasema Kenyatta hana haki ya kuongoza Kenya kwa sababu kwa sababu asilimia 76 ya waliojiandikisha kupiga kura hawakujitokeza. Anaongeza kwamba, Wakenya waliitikia wito wake wa kususia na kwamba viongozi wa Jubilee wameshindwa kupunguza viwango vya umaskini nchini.
Oktoba 31, Raila na kiongozi mwenza wa Nasa, Musalia Mudavadi walitangaza kwamba tawi la muungano huo la kupambana na utawala mbaya (National Resistance Movement) litaanza kutekeleza wajibu wake wa kuleta haki kwa wote nchini na kutoa nafasi kwa Wakenya kuwa na uchaguzi wa huru na haki kwa kutumia mifumo ya amani kama ilivyokubalika katika Katiba ya Kenya kushinikiza uongozi bora na siasa zilizokomaa.
Nasa imewahimiza wafuasi wake na Wakenya wengine wanaoamini ndoto yao ya kuwa na Kenya wenye haki, wajitokeze kwa wingi kwa kutoa sauti zao zisikike ili Kenya iwe nchi yenye kukuza ndoto za Wakenya wote bila kujali misingi yao ya kikabila au kisiasa.
Raila anasema tawi hilo, kinyume na fikra za wengi, halitajihusisha na mapambano ya kujihami kwa silaha bali litaendesha kampeni kwa amani, lakini Rais Kenyetta na Naibu wake William Ruto wanasema Nasa wanataka kuleta uhasama Kenya kwa kutumia uhalifu kujitafutia makuu uongozini.
Vilevile, Nasa inajiandaa kwenda mahakamani kupinga kile wanachoita uchaguzi haramu wa hivi majuzi.
Awali walikuwa wamesema hawataenda kortini kwa sababu Jubilee imeweka mikakati kulemaza taasisi hiyo muhimu. Wiki tatu zilizopita, wabunge wa Jubilee walipitisha hoja ambayo itampa Rais uwezo kisheria kupunguza nguvu za mahakama na taasisi zingine kama vile IEBC.
Wakati hayo yakiendelea wafanyabiashara wanalalamika kuwa migogoro inayokumba nchi inaathiri biashara zao na wanataka suluhu ipatikane haraka kuokoa biashara zao.
Vilevile, viongozi wa dini wanapendekeza kuwa nafasi za waziri mkuu na naibu wawili zibuniwe haraka iwezekanavyo ili viongozi wa upinzani wapewe mamlaka katika Serikali ili kutuliza hali ya hewa.
Kabla ya hatua hiyo, wanataka Rais Kenyatta awe na mkutano na Raila wajadiliane jinsi ya kumaliza au kupunguza mizozo za kisiasa ili kupata suluhu kamili ya matatizo yanayosumbua nchi.
Pendekezo hilo limepingwa na viongozi wengine wa dini waliosema Kenyatta asimpe Raila nafasi ya majadiliano kwa sababu kiongozi huyo wa upinzani alijiondoa mwenyewe kwenye kinyang’anyiro hicho na kwa hivyo hana haki ya kuletwa kwenye meza ya mjadala.
Alipokuwa akitangazwa mshindi wa urais hivi majuzi, Kenyatta alisema hawezi kuzungumza na Raila hadi kiongozi huyo wa upinzani atafute suluhisho la madai yake katika mahakama na taasisi nyingine.
Raila naye ametoa masharti yake yatakayofungua mlango wa maongezi na Kenyatta. Anasema, atafanya hivyo tu ikiwa Kenyatta atakubali kung’atuka mamlakani na kukubali uchaguzi mwingine ufanyike ufanyike baada ya siku 90 kuanzia sasa.

PITIA VICHWA VYA HABARI KATIKA MAGAZETI LEO NOVEMBA 5,2017