Julai mwaka jana, Rais John Magufuli akiwa ametoka kukabidhiwa uenyekiti wa CCM na Mkutano Mkuu, alisisitia uamuzi wa kuzuia mikutano ya kisiasa na maandamano, akitoa sababu kwamba hataki kuongoza nchi ambayo watu wake muda wote wanafanya siasa.
Mkutano huo ulitanguliwa na wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) na Kamati Kuu (CC) ukiwa ni mchakato wa kumtawaza Rais Magufuli uenyekiti ili kumrithi Jakaya Kikwete.
Kabla ya tangazo hilo, kulikuwa na maagizo ya Jeshi la Polisi ya kuzuia shughuli za kisiasa ndani na nje. Nakumbuka Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), lilitishia kuzuia mikutano hiyo ya CCM likidai ni kuunga mkono tamko la polisi.
Baadaye vikao vya ndani vya vyama viliruhusiwa, lakini mikutano ya hadhara bado ni marufuku. Ukiacha mikutano ya kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani na Serikali za Mitaa Januari mwaka huu na hii ya sasa, hakuna mingine iliyofanyika tangu tangazo la Rais Magufuli.
Ukiwa umepita zaidi ya mwaka mmoja sasa tangu tangazo la Rais Magufuli kuzuia mikutano ya hadhara na matukio ya wazi, ni muda wa kujiuliza kama je, tangazo limepunguza kufanyika kwa harakati za kisiasa?
Katazo la shughuli za kisiasa lilielekeza kusubiri Uchaguzi Mkuu 2020, kwa maana ya wakati wa kampeni za kuwania dola. Chadema walitangaza kuandaa na kutekeleza operesheni waliyodai ya kupinga udikteta Tanzania, yaani Ukuta.
Hata hivyo, hawakutekeleza operesheni yao Septemba Mosi, 2016 baada ya kuzuiwa na polisi na wao kutangaza kuiahirisha na hadi sasa hakuna kilichofanyika.
Maswali yanaongezeka; umepita mwaka mmoja tangu Chadema waliposhindwa kutekeleza operesheni ya Ukuta kwa kuogopa mkwara wa Serikali, hasa baada ya Rais Magufuli kusema “wasimjaribu”, je, hata baada ya Ukuta kutofanyika, siasa zimedumaa?
Majibu ya maswali
Katika mwaka 2017, Tanzania imeshuhudiwa ikitanuka kwa kuwa na majukwaa mengi ya ufanyaji siasa kuliko miaka mingine yote iliyopita. Watu wenye kuzungumza siasa nchini ni wengi na mijadala inafanyika kwa ukaribu zaidi.
Hitaji la watu kuhudhuria mikutano ya hadhara ili kusikiliza sera na hoja za wanasiasa limepungua. Mwananchi anaweza kupokea neno au kushiriki mjadala wa kisiasa popote alipo. Akiwa nyumbani au ofisini kwake, anapokuwa kwenye chombo cha usafiri au hata hospitali amelala kitandani.
Hiyo imekuwa sababu ya kipindi ambacho wanasiasa wakiwa hawafanyi mikutano ya hadhara kama ilivyokuwa mwanzo, lakini siasa zimekuwa zikipata mwitikio mkubwa mno. Majukwaa ya mawasiliano ya umma yamesababisha sauti zipazwe na kusikika.
Nguvu ya majukwaa mapya ya kisiasa imeondoa urasimu kwa wanachama na mashabiki wa vyama vya siasa kusubiri matamko na hoja za viongozi wao, hivi sasa nao wanaweza kujenga hoja za ushawishi au kuzitetea taasisi zao.
Athari za ukuaji wa matumizi ya na mitandao ya kijamii duniani zimekuwa kubwa nchini, hivyo kufanya Facebook, Twitter, Instagram, YouTube na WhatsApp kuwa kiungo muhimu cha mawasiliano ya umma.
Akaunti za Twitter, YouTube na Instagram, kurasa za Facebook na makundi yake, na kwa nguvu zaidi WhatsApp kupitia makundi yake ya kijamii, siasa zimekuwa zikishamiri na kufanya watu wasahau habari za mikutano ya hadhara ya kisiasa.
Kiongozi wa kisiasa anapotaka kuzungumza jambo analiwasilisha kwenye ukurasa wake wa Facebook, akaunti zake za Twitter, YouTube na Instagram, kisha watu wanachukua na kusambaza kwenye makundi ya WhatsApp, ujumbe unaenea na kujadiliwa.
Tofauti na mikutano ya hadhara ambayo hufanya kiongozi awe mbali na hadhira yake, mitandao ya kijamii inawezesha majadiliano kuliko hotuba. Kwamba kiongozi anaweza kuzungumza jambo kisha hadhira ikachangia kwa kuunga mkono au kupinga. Vilevile hadhira huuliza maswali na kujibiwa.
Kimsingi mitandao ya kijamii inawezesha watu kuzungumza fikra zao kwenye siasa na masuala mengine yote ya kijamii. Hali hiyo ndiyo ambayo inafanya mijadala ya kisiasa ipate nafasi kubwa. Tukio kubwa kuhusu nchi likitokea linaibua mijadala kwenye mitandao ya kijamii.
Kiongozi akihutubia, vipande vya hotuba yake vinasambazwa kwenye mitandao ya kijamii na kujadiliwa kwa upana. Watu hawasubiri viongozi wa kisiasa wahutubie ili kuchambua hotuba ya kiongozi, bali wao wenyewe kwenye majukwaa yao wanajadili.
Haishangazi siku hizi Rais Magufuli kusikika akijibu hoja za mitandao ya kijamii ambayo huanzishwa hata na watu wasiofahamika. Imekuwa kawaida sasa kwa viongozi wa kisiasa kukopa mawazo ya watu wa mitandaoni na kuyatumia kujenga hoja, tofauti na hapo zamani.
Siasa na teknolojia
Kwa kuipima falsafa ya siasa na teknolojia katika dunia ya sasa, sehemu kubwa ya maudhui yake inabebwa na simu za mkononi. Inaonekana wanasiasa wengi nchini hawakujitayarisha kwa ajili ya mabadiliko hayo, isipokuwa wamezolewa tu na mkumbo wa mapinduzi ya kiteknolojia.
Teknolojia inarahisisha mipango ya kisiasa bila mikutano ya hadhara, kiasi kwamba Tundu Lissu akiwa kitandani hospitalini Nairobi, Kenya, anaweza kuzungumza na Taifa zima na ujumbe ukaenea kila mahali. Anajirekodi akiwa hospitali, sauti inaingizwa YouTube.
Watu wanachukua sauti yake YouTube na kuipeleka Facebook na makundi ya WhatsApp, vilevile inakatwa nusunusu na kuwekwa Twitter na Instagram. Sauti inafika kwa wapigakura wake na kila eneo, kisha inajadiliwa kwenye majukwaa mbalimbali.
Mpango wa mawasiliano ya moja kwa moja kupitia mitandao ya kijamii, Facebook Live, Instagram Live na YouTube Live, unawezesha kufanya mikutano si tena na waandishi wa habari, bali na ulimwengu mzima.
Ukiweka ‘live’, popote ulipo unaweza kumfikia yeyote mwenye kuipata akaunti yako. Haya ndiyo mapinduzi makubwa ya kiteknolojia ambayo kwa kiasi kikubwa yanafanya siasa za majukwaa ya kawaida zianze kupitwa na wakati.
Wanasiasa lazima wajiandae kuendana na wakati. Wajifunze kutengeneza maudhui yenye kufikika kupitia simu za mkononi. Hiki ni kipindi ambacho mfanyakazi hawezi kusema alipitwa na mkutano kwa sababu alikuwa kazini, kwani simu yake inakuruhusu umfikie wakati wowote na uzungumze naye.
Maandalizi hayo ni kuielewa teknolojia na kuyafahamu mahitaji yenye kutosheleza kubeba maudhui ya kiteknolojia. Kwamba mwanasiasa mjanja atachanua wakati wote hata kama kutakuwa na hali ya kuzibwa mdomo kwa vyombo vya habari vya kawaida (traditional media).
Wala si jambo la ajabu, kwani kulishakuwa na njia za upashanaji habari kwa mtindo wa kale (old media), hivyo lazima kujua mahitaji ya Zama za Taarifa (Information Age) ambazo zinatawala sasa na ni dhahiri sayari ya dunia inakwenda kubadilika kupitia mtindo wa kimaisha kwa wakazi wake.
No comments:
Post a Comment