Msekwa ambaye pia amewahi kuwa Spika wa Bunge, amesema utaratibu wa kumchagua mwenyekiti wa Taifa kupitia mkutano mkuu maalumu unakigharimu chama hicho, badala yake uwekwe utaratibu wa kikatiba utakaoruhusu mtu anayechaguliwa kuwa rais kupitia CCM moja kwa moja awe mwenyekiti wa chama.
Kwa muda mrefu CCM imekuwa ikifanya mkutano mkuu maalumu kwa ajili ya kumsimika mwenyekiti mpya Taifa, mkutano ambao unadaiwa kutumia fedha nyingi zinazofikia takriban Sh1 bilioni.
Katika mwendelezo huo, chama hicho Julai 23, 2016 kilifanya mkutano mkuu maalumu na kumchagua Rais John Magufuli kupokea kijiti kutoka kwa mtangulizi wake, Jakaya Kikwete.
Lakini, Msekwa katika makala yake ya miaka miwili ya uongozi wa Rais Magufuli katika chama hicho, anasema “Ingewezekana kabisa kupunguza gharama hizo kwa kuondoa haja ya kuitisha mkutano mkuu wa chama, kwa njia rahisi tu ya kurasimisha utamaduni huo kwa kuuingiza kwenye katiba ya chama.”
Akitoa mfano, Msekwa anasema CCM inaweza kuongeza ibara ndogo katika ibara ya 118 ya Katiba ya CCM, itakayosomeka, “Wakati wote ambapo chama kitakuwa madarakani, Rais wa Jamhuri ya Muungano anayetokana na CCM atakuwa pia ndiye mwenyekiti wa Taifa wa CCM, na atakuwa katika nafasi hiyo kwa muda wote atakapokuwa Rais.”
Anafafanua kuwa matokeo ya marekebisho hayo ya Katiba yatakuwa ni kwamba, Rais mpya anayetokana na CCM akisha kuapishwa, basi moja kwa moja anakuwa pia ni mwenyekiti wa Taifa wa CCM, bila haja ya kuitisha mkutano mkuu maalumu wa kumpigia kura na kwa hiyo kuondoa gharama zake.
“Ni wazo linalopendekezwa kwa ajili ya kufikiriwa, tuliangalie hili,” alisisitiza Msekwa.
Msekwa anasema wanachama wa CCM wanauelewa vizuri utamaduni wa chama chao kwamba mtu anayechaguliwa kuwa Rais kutokana na CCM, ndiye vilevile anakuwa mwenyekiti wa CCM.
Utaratibu ulivyoanza
Alisema miaka ya nyuma enzi za Tanu, utaratibu ulikuwa ni kwamba wakati wa uchaguzi unapofika, mwenyekiti wa CCM ndiye aliyekuwa akiteuliwa kuwa mgombea wa nafasi ya urais.
“Utaratibu huo ulijulikana kwa jina la ‘Kofia mbili za uongozi’. Mwalimu Nyerere alipoamua kustaafu urais mwaka 1985, kulikuwa na wasiwasi mkubwa miongoni mwa jamii, kwamba bila Mwalimu kuwapo katika uongozi, nchi yetu ingeyumba.
“Ili kudhibiti wasiwasi huo, chama kilifanya uamuzi kwamba, Mwalimu aendelee kuwa mwenyekiti wa Taifa wa CCM kwa kipindi kitakachoivusha nchi kutoka kwenye wasiwasi huo. Mwalimu Nyerere alikubali kuendelea na wadhifa huo, hadi alipokabidhi kijiti kwa Rais Mwinyi mwaka 1990. Wakati huo Mwinyi alikuwa anachaguliwa kwa kipindi cha pili.
Hata hivyo, Msekwa anasema kwa kuwa mwaka 1990 haukuwa wa uchaguzi wa kawaida wa viongozi wa CCM, ilibidi ufanyike uchaguzi mdogo wa kumchagua Rais Mwinyi kuwa Mwenyekiti wa CCM ili kuendeleza utamaduni huo wa ‘kofia mbili za uongozi’ katika ngazi hiyo.
Kuanzia wakati huo hadi sasa, rais aliyepo madarakani amekuwa akichaguliwa kuwa mwenyekiti wa CCM kwa njia ya uchaguzi mdogo, ambapo inabidi kuitisha mkutano mkuu maalumu wa chama hicho kwa ajili hiyo.
“Hapo ndipo suala la gharama linapojitokeza, inabidi kuwa na wazo la kupunguza gharama hizo,” anaongeza Msekwa.
No comments:
Post a Comment