Kama kawaida, Kenya inaendelea kuingia kwenye shimo la sintofahamu baada ya kukamilika uchaguzi na Uhuru Kenyatta kutangazwa mshindi.
Uchaguzi ulifanyika kama ulivyopangwa Oktoba 26 kama ilivyoamriwa na Mahakama ya Juu ikitarajiwa kwamba uchaguzi huo wa marudio ungekuwa dawa ya kuepusha maradhi ya chuki, kutoaminiana na unafiki miongoni mwa Wakenya na viongozi wao.
Ni wazi kwamba uchaguzi huo haukuleta nafuu. Lakini, hatimaye baadhi ya Wakenya wanafurahi kwamba, uchaguzi huo umewapa kisogo na wanaweza kuendelea na maisha yao na biashara zinazoendelea kudorora kila kukicha kwa sababu ya siasa zilizojaa chuki na ukabila.
Kwa wale waliofikiria maisha yatakwenda sawa baada ya uchaguzi, nina ujumbe kwao; mbele si sawa. Kwa nini? Kwa sababu kama ilivyokuwa baada ya uchaguzi wa Agosti 8, masuala yaliyoibuka bado hayajatatuliwa kulingana na madai ya kiongozi wa upinzani, Raila Odinga na viongozi wenza wa Muungano wa National Super Alliance (Nasa).
Rais Kenyatta alishinda uchaguzi wa juzi kama alivyoshinda ile ya Agosti 8. Ushindi wake umekumbwa na upinzani mkali kutoka kwa Nasa na mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo sasa wanadai Kenyatta analazimisha kuwaongoza Wakenya.
Kikundi hiki cha Wakenya kinadai mazingara ambayo uchaguzi ulifanywa hayangeweza kuhakikisha matokeo bora. Yafaa kukumbukwa kwamba Odinga aliyekuwa akipigania urais kwa tiketi ya Nasa alijiondoa akidai Tume ya Uchaguzi (IEBC) ilikataa kutekeleza mabadiliko na kurekebisha dosari zilizokuwa zimesheeni uchaguzi wa Agosti na kulazimisha mahakama kuufutilia mbali baada ya Nasa kwenda mahakamani kupinga ushindi wa Kenyatta.
Kiini cha upinzani kupinga matokeo ya uchaguzi ni madai kwamba, asilimia 27 pekee ya wapiga kura walifika katika vituo vya kupigia kura Oktoba 26. Nasa pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali yanahoji kwa nini Kenyatta atangazwe mshindi ilhali mamilioni mwa Wakenya hawakupiga kura? Pia, wanadai kwamba vikosi vya usalama kama vile polisi walitumiwa kuwadhalilisha wafuasi wa Nasa kwa kuitikia wito wa Raila wa kususia uchaguzi.
Takwimu za mashirika ya haki za kibinadamu kama vile Human Rights Watch (HRW) na Transparency International (TI) yanadai Wakenya wapatao 40 waliuawa kwa risasi au kuumizwa na polisi katika ngome za Nasa. Maeneo yaliyoathiriwa mno na ghasia na vifo ni majimbo ya Kisumu, Homa Bay, Siaya, Migori Bungoma na Kakamega.
Katika jiji kuu la Nairobi, maeneo ya Kibera, Mathare na Kawangware yalikumbwa na ghasia baada ya polisi kukabiliana na wafuasi wa Nasa kabla na baada ya uchaguzi hivi majuzi.
Licha ya HRW kuchapisha majina ya waliouawa kwenye ghasia hizo, Serikali imepinga vikali ripoti hiyo ikisema si ya kweli. Nasa inauliza kwa nini vijana walimiminiwa risasi na kuuawa ilhali walikuwa wamejihami na mawe.
Wakazi wa maeneo hayo walikabiliana vibaya na polisi huku wakifunga barabara na kurushiana mawe na walinda usalama katika juhudi za kuzuia kwa kila namna zoezi hilo kufanyika.
Wabunge wa maeneo hayo wamelaani “unyama wa polisi” wakisema kuna njia mbadala ambazo zingetumiwa na maofisa hao kuzima maandamano hayo.
Nasa inasisitiza kwamba vifo vingi vilivyoripotiwa katika ngome zao ni uthibitisho kwamba Serikali ya Jubilee inaendeleza sera zake za chuki kwa jamii zinazoegemea upande wa upinzani.
Raila ameapa kupigana na Serikali ya Kenyatta hadi mwisho akisema utawala wa Jubilee unafaa kuondolewa kwa sababu ya “wizi wa kura”, uongozi wa kidhalimu na ufisadi uliokithiri.
Lakini, Kenyatta anasema kwamba ushindi wake ni halali na kamwe chama chake cha Jubilee hakijatumiwa kwa njia yoyote ile katika wizi wa kura. Rais anasema ingawa kulikuwa na ghasia za hapa na pale, Wakenya walijitokeza kumchagua kama walivyofanya katika kura ya Agosti 8.
Wadadisi wa siasa wanasema Rais Kenyatta alitangazwa mshindi ilhali mamilioni ya Wakenya hawakupiga kura jambo linalofanya uchaguzi huo kuwa batili.
Raila anasema Kenyatta hana haki ya kuongoza Kenya kwa sababu kwa sababu asilimia 76 ya waliojiandikisha kupiga kura hawakujitokeza. Anaongeza kwamba, Wakenya waliitikia wito wake wa kususia na kwamba viongozi wa Jubilee wameshindwa kupunguza viwango vya umaskini nchini.
Oktoba 31, Raila na kiongozi mwenza wa Nasa, Musalia Mudavadi walitangaza kwamba tawi la muungano huo la kupambana na utawala mbaya (National Resistance Movement) litaanza kutekeleza wajibu wake wa kuleta haki kwa wote nchini na kutoa nafasi kwa Wakenya kuwa na uchaguzi wa huru na haki kwa kutumia mifumo ya amani kama ilivyokubalika katika Katiba ya Kenya kushinikiza uongozi bora na siasa zilizokomaa.
Nasa imewahimiza wafuasi wake na Wakenya wengine wanaoamini ndoto yao ya kuwa na Kenya wenye haki, wajitokeze kwa wingi kwa kutoa sauti zao zisikike ili Kenya iwe nchi yenye kukuza ndoto za Wakenya wote bila kujali misingi yao ya kikabila au kisiasa.
Raila anasema tawi hilo, kinyume na fikra za wengi, halitajihusisha na mapambano ya kujihami kwa silaha bali litaendesha kampeni kwa amani, lakini Rais Kenyetta na Naibu wake William Ruto wanasema Nasa wanataka kuleta uhasama Kenya kwa kutumia uhalifu kujitafutia makuu uongozini.
Vilevile, Nasa inajiandaa kwenda mahakamani kupinga kile wanachoita uchaguzi haramu wa hivi majuzi.
Awali walikuwa wamesema hawataenda kortini kwa sababu Jubilee imeweka mikakati kulemaza taasisi hiyo muhimu. Wiki tatu zilizopita, wabunge wa Jubilee walipitisha hoja ambayo itampa Rais uwezo kisheria kupunguza nguvu za mahakama na taasisi zingine kama vile IEBC.
Wakati hayo yakiendelea wafanyabiashara wanalalamika kuwa migogoro inayokumba nchi inaathiri biashara zao na wanataka suluhu ipatikane haraka kuokoa biashara zao.
Vilevile, viongozi wa dini wanapendekeza kuwa nafasi za waziri mkuu na naibu wawili zibuniwe haraka iwezekanavyo ili viongozi wa upinzani wapewe mamlaka katika Serikali ili kutuliza hali ya hewa.
Kabla ya hatua hiyo, wanataka Rais Kenyatta awe na mkutano na Raila wajadiliane jinsi ya kumaliza au kupunguza mizozo za kisiasa ili kupata suluhu kamili ya matatizo yanayosumbua nchi.
Pendekezo hilo limepingwa na viongozi wengine wa dini waliosema Kenyatta asimpe Raila nafasi ya majadiliano kwa sababu kiongozi huyo wa upinzani alijiondoa mwenyewe kwenye kinyang’anyiro hicho na kwa hivyo hana haki ya kuletwa kwenye meza ya mjadala.
Alipokuwa akitangazwa mshindi wa urais hivi majuzi, Kenyatta alisema hawezi kuzungumza na Raila hadi kiongozi huyo wa upinzani atafute suluhisho la madai yake katika mahakama na taasisi nyingine.
Raila naye ametoa masharti yake yatakayofungua mlango wa maongezi na Kenyatta. Anasema, atafanya hivyo tu ikiwa Kenyatta atakubali kung’atuka mamlakani na kukubali uchaguzi mwingine ufanyike ufanyike baada ya siku 90 kuanzia sasa.
No comments:
Post a Comment