Wednesday, October 25

Lugola aagiza Nemc kuwasilisha taarifa kutovunjwa nyumba ya Rwakatare


Dodoma. Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Kangi Lugola ameagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc) kufikisha mezani kwake maelezo ni kwa nini nyumba ya mbunge wa Viti Maalumu, Mchungaji Getrude Rwakatare (CCM) haijabomolewa.
Lugola ametoa muda kwa Nemc hadi kesho Alhamisi Oktoba 26,2017 saa 10:00 jioni awe amepata taarifa ya maandishi ili aweze kutoa uamuzi iwapo ibomolewe au la.
Naibu waziri ametoa agizo hilo leo Jumatano Oktoba 25,2017 wakati Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira ilipokutana na watendaji wa Nemc.
Lugola amefikia uamuzi huo baada ya Nemc katika taarifa yake kueleza Serikali imeshindwa kuivunja nyumba hiyo kutokana na zuio lililopelekwa mahakamani na Mchungaji Rwakatare tangu mwaka 2012.
Nemc imesema kesi ikiisha na uamuzi kutolewa hakutakuwa na shaka wala kigugumizi katika kuivunja nyumba hiyo.
Ka kauli hiyo, Naibu Waziri Lugola amesema hakuna mtu aliye juu ya sheria na kwamba, hatima ya jengo hilo lazima ijulikane mapema ili kuondoa sitofahamu iliyopo.
“Rais Magufuli ameniteua kufanya kazi hii na anajua kwa nini alinichagua mimi. Naamini anajua uwezo wangu na utendaji kazi wangu, siko tayari mtu wa nafasi yoyote kuniangusha na kunifanya nishindwe kutimiza malengo yangu. Sitaki migongano ya aina yoyote inayoweza kuniangusha, hakuna jiwe litakaloachwa kusalia juu ya jiwe,” amesema.
Awali, wajumbe wa kamati walihoji uhalali wa nyumba hiyo kubaki bila kuguswa licha ya kujengwa eneo lisiloruhusiwa kisheria.
Nyumba hiyo ipo mtaa wa Mbezi Beach jijini Dar es Salaam ambayo iliamriwa kubomolewa lakini hilo halikufanyika kutokana na Rwakatare kuweka zuio mahakamani.
Akizungumzia suala hilo, mjumbe wa kamati, Khatibu Haji (Konde -CUF) amesema kumekuwa na hali ya kulindana katika jengo hilo, huku Serikali ikiendelea kuwaonea wanyonge.
“Tunashuhudia Watanzania wanyonge wengi wakipoteza makazi yao na kuishi kwa mahangaiko baada ya kuangushiwa nyumba zao, lakini hakuna kitu chochote kinachoendelea kuhusu nyumba ya Mchungaji Rwakatare na jambo hili linaibuliwa na kuzimwa kuna nini huko,” amehoji Khatibu.
Amesema haileti picha nzuri kwa Serikali kuonyesha inawaonea wanyonge na kuwatetea wenye uwezo jambo linalosababisha kuwagawa watu kwa matabaka.
Khatibu hakuwa peke yake, Martha Mlata (Viti Maalumu -CCM) alitaka hatua kali zichukuliwe kwa waliomruhusu Rwakatare kujenga katika eneo lisiloruhusiwa kisheria.
“Huu ni uonevu ambao haupaswi kuvumiliwa. Macho na masikio ya Watanzania yamechoka kusikia nyumba za wanyonge zikivunjwa lakini Serikali inaendelea kulinda hekalu la mtu mmoja ambalo limejengwa mahali pasipohusika. Haikubaliki hata kidogo, kuna nini katika nyumba ya Mchungaji Rwakatare,” amehoji Gimbi Masaba (Viti Maalumu -Chadema).

Waziri Mwakyembe ataka vyombo vya habari kutovuka mipaka


Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Harrison Mwakyembe amesema Serikali inatambua haki ya vyombo vya habari katika kukosoa, kujadili na kuchambua masuala mbalimbali.
Hata hivyo, amesema visivuke mipaka na kuhatarisha masilahi ya Taifa katika kufanya kazi zake.
Dk Mwakyembe amesema hayo leo Jumatano Oktoba 25,2017 ikiwa ni siku moja baada ya Serikali kulifungia gazeti la Tanzania Daima.
Amesema hayo katika mkutano na viongozi wa madhehebu ya dini uliojadili masuala ya amani na uzalendo kuelekea uchumi wa viwanda.
Dk Mwakyembe amesema Serikali inatambua uhuru wa vyombo vya habari lakini amewataka wamiliki wake na waandishi kwa jumla kufahamu sheria na vifungu vya Katiba ili kulinda masilahi ya Taifa katika utoaji wa taarifa.
Amesema ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inatoa haki ya uhuru wa mawazo lakini ibara ya 30 inaweka mipaka kwa haki na uhuru huo.
Waziri Mwakyembe amesema katika kufikia uchumi wa viwanda vyombo vya habari ni vya muhimu ili kufikisha taarifa.
Amewataka waandishi wa habari kuzingatia weledi ili Taifa liendelee katika sekta mbalimbali na kufikia uchumi wa kati.
Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum amesema Watanzania wanatakiwa kuwa wazalendo kwa kuipenda nchi yao na kukemea mambo yote ambayo yanahatarisha amani.
"Wasomi na viongozi ni wakati wao wa kukemea mambo maovu ikiwemo rushwa na ufisadi kwa kuwa kufanya hivyo ni njia mojawapo ya kuipenda nchi na kulinda amani," amesema.

Ucheleweshaji ajira watajwa kikwazo kwa ATCL


Dar es Salaam. Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) limesema ucheleweshaji wa vibali vya ajira unakwamisha mipango ya ushindani wake kibiashara.
Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi amesema hayo leo Jumatano Oktoba 25,2017 alipozungumza na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Atashasta Nditiye.
Matindi amesema, “Katika utoaji wa vibali vya ajira za ATCL inachukuliwa kama idara ya huduma na si kampuni ya kibiashara yenye malengo ya kiushindani.”
Amesema bodi ya wakurugenzi ya shirika hilo imekuwa ikitaka ajira za baadhi ya wataalamu lakini kuchelewa kwa vibali ni kikwazo.
“Tunakuomba utusaidie kuimaliza changamoto hii, nia ni kuifanya ATCL kupata mafanikio zaidi,” amesema.
Amesema shirika linakabiliwa na changamoto nyingine ambazo ni upungufu wa marubani na wahandisi kutokana na udogo wa mishahara.
“Hali hii inatufanya tushindwe kupata marubani kutoka kwenye soko licha ya  wengi wao kuwa na nia ya kujiunga na ATCL,” amesema.
Amesema madhara yake ni kushindwa katika mipango ya kuongeza safari za ndege.
Mhandisi Matindi amesema changamoto nyingine ni baadhi ya viwanja vya ndege kutokuwa na miundombinu ya kuwezesha ndege kutua usiku.
“Changamoto hii inapunguza idadi ya safari na matumizi ya ndege, hivyo kuchangia kupunguza mapato,” amesema.
Hata hivyo, amesema sasa shirika linamiliki asilimia 24 ya soko la ndani la usafirishaji wa abiria na mizigo.
Amesema tangu shirika lilipofufuliwa Oktoba 2016 hadi Juni 2017 wamebeba abiria 106,138  hali inayowafanya kumiliki asilimia 24 ya soko la ndani.
Mkurugenzi mkuu huyo amesema uongozi umedhibiti matumizi yasiyokuwa ya lazima na kuhakikisha gharama za uendeshaji zinakuwa chini.
Akizungumza baada ya kuelezwa changamoto hizo, Nditiye ambaye ni naibu waziri anayeshughulikia sekta za mawasiliano na uchukuzi, ameahidi kuzishughulikia ili shirika hilo lipigwe hatua.
Pia, amewataka wafanyakazi kufanya kazi kwa weledi ili kujiepusha na makosa ya zamani yaliyosababisha shirika hilo kupata hasara.
“Katika awamu hii wafanyakazi wabadhirifu hatutawavumilia, Watanzania wanataka kuliona shirika hili likipata mafanikio,” amesema.

Dk Mashinji aeleza kilichojiri ofisini kwa DCI



Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji ameeleza kilichojiri kati yake na ofisa katika ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI).
Dk Mashinji amesema alichotarajia kukikuta kimekuwa tofauti.
"Awali nilikuwa na shaka kwamba wameniitia nini lakini kumbe ilikuwa ni majadiliano ya kawaida kati yangu na ofisi ya DCI," amesema Dk Mashinji leo Jumatano Oktoba 25,2017.
Amesema, "Majadiliano yalilenga kuelezana hiki kinachoendelea cha kamatakamata na je? sisi tunawaonaje na wao wanatuonaje. Pia, mambo mengine mengi."
Dk Mashinji amesema wamezungumzia pia kuhusu kuendelea kushikiliwa kwa Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo wa Chadema, Kigaila Benson.
Katibu mkuu Mashinji amesema ofisa huyo ameahidi kulifuatilia suala hilo.
"Mimi nimemweleza alichozungumza Kigaila kiko wazi na wala hakina tatizo lolote," amesema Dk Mashinji.

ASKARI WALIOHUSIKA KUPIGA RAIA WACHUKULIWE HATUA ZA KINIDHAMU - DC MJEMA


MAKAMU WA RAIS MHE. SAMIA SULUHU HASSAN AZITAKA BENKI KUFUNGUA MATAWI ZAIDI

MAKAMU wa Rais Samia Suluhu Hassan amezitaka benki zote zilizopo hapa nchini kuhakikisha zinaanzisha matawi yake katika mikoa mbalimbali ili kuwawezesha wananchi hasa wanawake kupata huduma za kifedha kirahisi.
Samia ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa siku mbili wa kimataifa wa Wanawake na Fedha uliyoandaliwa na Shirika la Kimataifa la Women’s World Banking na Benki ya NMB kuwa mshirika mwenza katika mkutano huo.
Mkutano huo ambao kwa mara ya kwanza umefanyika barani Afrika, nchini Tanzania umewakutanisha pamoja wanawake viongozi katika fani mbalimbali zaidi ya 300, zikiwemo mabenki, teknolojia, wafanyabiashara, mashirika ya umma na binafsi.
Mama Samia alisema benki zinapaswa kwenda zaidi kwa wananchi kwa kuanzisha matawi yao huko mikoani kwani baadhi ya watanzania wapo nje kabisa na mifimo ya kibenki kutokana na kutofikiwa.
“Asilimia 70 ya watanzania wanatumia simu za mkononi na kama mnavyojua Tigopesa, Mpesa na zinginezo zimesambaa sana hapa nchini hii inayonyesha huduma za kifedha tumepiga hatua ingawa bado kuna mambo tunapaswa kurekebisha kwa mfano mabenki yetu yaendelee zaidi kwenda huko kwa wananchi kwa kufungua matawi mengi.
Lakini pia benki yetu ya Wanawake ambayo imeundwa kwa madhumuni hayo tunaitaka ijitahidi kusambaza matawi yake huko mikoani, hivyo mkutano huu utaangalia ni jinsi gani jamii inafikiwa zaidi na huduma za kifedha hasa wanawake walioko vijijini ili wapate huduma za fedha ambazo ndizo zinakuza uchumi wan chi,” alisema.
Aidha alisema Shirika la Kimataifa la Women’s World Banking wameamua kuja kufanya kongamano hilo kwa mara ya kwanza hapa nchini ili kuja kuangalia Tanzania inafanyaje katika kusaidia maendeleo ya wanawake.
Naye Mkurugenzi wa Wateja wadogo na wa Kati wa Benki ya NMB, Abdumajid Nsekela alisema mkutano huo uliowakutanisha watu mbalimbali utajikita zaidi kuangalia ni kwa jinsi gani wataweza kumuwezesha mwanamke kupata fursa ili aweze kujikwamua kwenye mitaji na uwekezaji.
Alisema Benki ya NMB imeshirikiana kwa karibu na shirika hilo la Women’s World Banking katika kuzalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo ya kuwawezesha wananchi kwa maana ya mkulima na wafanyakazi hasa wanawake kwa kutengeneza bidhaa ambazo zitawawezesha kupata mikopo nafuu pamoja na kufungua akaunti.
“Zaidi ya wadau 300 ambao wametoka katika nchi mbalimbali duniani wapo katika mkutano huu wanajadiliana ni jinsi gani watumie teknolojia kumfikia mtanzania kwa ukaribu zaidi, wanawake wengi waliopo vijijini ni wakulima na wanahitaji huduma za kifedha hivyo mkutano huu ni mahususi kujadiliana changamoto zinazokwamisha kuwafikia wanawake


Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan akifungua mkutano wa taasisi ya benki ya ulimwengu ya kusaidia maendeleo ya wanawake uliofanyika jijini Dar es Salaam na kudhaminiwa na Benki ya NMB. (Picha na Francis Dande).
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB, Ineke Bussemeker, akiongea baada ya Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan kufungua mkutano wa Kimataifa la Women’s World Banking uliofanyika jijini Dar es Salaam na kudhaminiwa na Benki ya NMB. 


Washiriki a mkutano wa kimataifa wa Women’s World Banking.

WAZIRI AKERWANA RUSHWA VITUO VYA MIZANI


SERIKALI imewaonya wafanyakazi wa mizani nchini   kuacha vitendo vya vitendo vya rushwa kuleta tija na ufanisi wa kazi zao katika usimamiaji na ulinzi wa barabara.
Imesema ikiwa watumishi hao watafanya kazi  kwa weledi na  uadilifu Serikali  itaendelea kunufaika na miundombinu yake ya barabara na mizani ambayo imegharimu mabilioni ya fedha.
Onyo hilo lilitolewa    na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sektaya Ujenzi), Elias Kwandikwa.
Alikuwa   akikagua  mzani wa Tinde na Mwendakulima ambako  alikemea vitendo vya rushwa  vinavyofanywa kati ya  watumishi  na madereva wa malori na basi za abiria.
Waziri aliwataka watumishi hao kufuata sheria na taratibu za kiutumishi  na kuwaajibisha madereva wanaozidisha uzito na si kuomba rushwa.
Kwandikwa alisema kama wizara imepokea taarifa ya vitendo vinavyofanyika katika mizani mbalimbali na imeamua kupita kwa lengo la kuwaonya na kuwakumbusha kufuata sheria na taratbu za kiutumishi vinginevyo watawajibishwa.
Pia alisema wanatambua changamoto zinazowakabili na wanajipanga kushirikiana kwa pamoja kukaa na madereva  kuweza kutafuta suluhisho katika usimamiz wa mizani.
“Watumishi na madereva shirikianeni kutokomeza vitendo vya rushwa, kamwe msijihusishe kutoa wala kupokea rushwa  kupata huduma za haraka.
“Tukikubaini tutakuchukulia hatua kali za sheria, mambo yote yanayofanyika vituo kama hivi tumeyapata, hivyo badilikeni kabla ya hatua kuchukuliwa,”alisema.
Hata hivyo alitoa wito kwa madereva wa magari ya mizigo wanaotakiwa kuwa na stika maalumu za usafirishaji wa mizigo yao kufuata utaratibu wa kuchukua stika hizo mahali husika  kuepusha usumbufu na msongamano wa katika vituo vya mizani.
Akiwa katika eneo la sehemu ya maegesho  na kulaza magari mjini Kahama, Kwandikwa, alitoa wito kwa viongozi wa halmashauri hiyo kuchukua hatua kali kwa madereva wanaoegesha  nje ya eneo hilo  kudhibiti uchafuzi wa mazingira.
Alitoa ushauri kwa uongozi wa halmashauri hiyo kuona namna ya kujenga maegesho mengine kama hayo kupata chanzo cha mapato na kusaidia kuujenga mji kuwa na taswira nzuri.
Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mkoa wa Shinyanga,   Mibala Ndilindi, alisema ni kweli vitendo vya  rushwa  vinafanyika katika vituo vya mizani.
Alisema  tayari hatua za sheria zimechukuliwa kwa watumishi watatu wa mizani ya Mwendakulima.

NI AIBU KWA JESHI LA POLISI KUENDELEA KULAUMIWA


KATIKA siku za karibuni kumekuwapo na malalamiko mengi ya mihimili ya dola kuumbuana au kuingiliana katika mambo kadha wa kadha.
Hali hiyo imesababisha kuwapo malalamiko, kuwa mihimili hiyo imeshindwa kutambua mipaka yake iliyonayo kikatiba na kisheria.
Leo tumelazimika kusema haya, baada ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), kutangaza rasmi kumwandikia barua Spika wa Bunge, Job Ndugai juu ya kitendo cha Jeshi la Polisi kumkamata na kumhoji kwa zaidi ya saa tatu Mwandishi wa Habari wa Gazeti la Nipashe, Augusta Njoji.
Kamati hiyo, imesema bila kumung’unya maneno kuwa  mhimili wa Bunge umeingiliwa na mamlaka nyingine kinyume na utaratibu wake.
Kamati hiyo imesema, Spika Ndugai anapaswa kulipa  mwongozo kuhusu jambo ambalo linaonekana wazi kufedhehesha mhimili huo kisha atoe tamko.
Tunaamini uamuzi wa kamati hii, ni sahihi kwa sababu ni mhimili ambao umekuwa ukifanya kazi zake kwa uhuru bila kuingiliwa na chombo chochote, sasa inakuwaje polisi wanapoguswa kwenye jambo ambalo wanamaslahi nalo wanakuwa wakali.
Haiingii akilini, kama kweli jeshi hili limekumbwa na kashfa nzito ya aina hii eti wananchi wasijulishwe kupitia vyombo vya habari.
Haiwezekani kuwapo utata wa mkataba wa ununuzi wa magari 770 ya maji ya kuwasha, maarufu kama washawasha na taarifa hizi zimekaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG).
Tunasema hii ni mbinu chafu ya kutaka maovu yasiibuliwe kwenye  jeshi hili ambao hata Rais Dk. John Magufuli amepata kulionya juu ya tuhuma mbalimbali zinazolikabili, zikiwamo ununuzi wa sare, ujenzi wa majengo  na mengi.
Tunaamini  kutaka kunyamazisha waandishi wa habari ni kukusudia kuficha uovu ambao umetafuna fedha za walipa kodi wa nchi hii.
Tunakubaliana na Mwenyekiti wa PAC, Naghejwa Kaboyoka kwamba, jeshi hilo halina mamlaka ya kumkamata mwandishi wa habari  eti kisa ameandika kashfa hiyo.
Pia tunaona hii ni njia moja wapo ambayo kwa namna moja au nyingine inakusudia kulinyamazisha Bunge au kamati ambavyo tunaamini ndiyo chombo chenye mamlaka ya kujadili madudu yanayoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ili Watanzania waelewe nini kinachoendelea kwenye taasisi za Serikali.
Tunaelewa vizuri msimano wa Spika Ndugai, ni matarajio yetu kwamba atatumia kanuni na uwezo wake ili kuhoji uhalali wa jeshi hilo kufanya kitendo hicho ambacho si cha ungwana.
Tunajiuliza maswali mengi, hivi imefikia hatua polisi wanataka kufanya kazi za kamati za Bunge?
Tunashangaa kwanini polisi mkoani Dodoma wamemsumbua mwandishi huyo wa habari, wakati aliripoti taarifa rasmi iliyotolewa na Kamati ya Bunge ambayo ilitokana na ripoti ya CAG?
Kwa msingi huo, kitendo cha kutaka habari zao zisiandikwe kama kuna upungufu na idara yoyote na Serikali ni kitendo cha kuonyesha  wanataka kuzima taarifa hizi zisiendelee kufichuliwa kwa sababu wanajua madudu yanayofanyika.
Umefika wakati sasa Jeshi la Polisi lianze kujitafakari katika utendaji kazi wa kila siku. Haiwezekani kila kukicha wao ndiyo watu wa kulaumiwa kila kona.
Tunasema hivyo, kwa sababu tunaamini jeshi hili kuanzia  IGP Simon Sirro mpaka chini wanaongozwa na sheria, taratibu na kanuni za kazi.
Iweje kila siku wawe wao tu, hapa umefika muda wa kuangalia wapi wamejikwaa. Kwa kuwa jambo hili linakwenda kwa Spika, tunategemea majibu ya msingi yatakayotolewa yatafungua ukurasa mpya wa uhusiano mzuri kati ya polisi na wanahabari.

PITIA VICHWA VYA HABARI KATIKA MAGAZETI YA LEO OKTOBA 25,2017

Idadi ya meli na mizigo yashuka bandarini


Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) imesema idadi ya meli zinazoingia nchini imeshuka kutoka 1,200 hadi 1,000 huku mapato yanayotokana na biashara hiyo yakiongezeka.
Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo Mhandisi Deusdedit Kakoko alisema kwamba hata mizigo inayoingia nchini pia imepungua.
Kakoko alilazimika kuyasema hayo wakati akijibu swali liloulizwa na Mbunge wa Kilindi, Omary Kigua ambaye alitaka kupata ufafanuzi wa kuhusu hali ikoje katika biashara ya bandari.
“Kuna speculation (minong’ono) kuwa idadi ya meli zinazoingia nchini zimepungua. Nilitaka kufahamu hali biashara ikoje?”alihoji Kigua.
Kakoko alisema hatua wanazochukua zinalenga ufanisi , tija, gharama wanazotoza na huduma kwa mteja na kwamba kwa kukamilisha mambo hayo kutawezesha meli nyingi kuingia nchini.
“Uchunguzi wetu umejionyesha kuwa unapochukua hatua matokeo yake yanakuwa mbele hizi hatua ambazo tunachukua zinazaa matunda.
Alitaja sababu nyingine ya kupungua kwa meli ni uwezo wa kutia nanga kwa meli ambao hutegemea kina cha maji na kwamba kuna meli nyingi ambazo zinasubiri nje ya gati.
Alisema kina cha maji kuna mahali ni mita saba wakati kwingine ni mita 10.5 na meli nyingi duniani ni kubwa hivyo nyingine kusababisha meli kutofika nchini.
“Kwa hiyo kuna meli zinasubiri siku saba na meli inatengeneza hela ikitembea ikisimama inatumia hela kwasababu ni kama gari, hiyo ndio sababu inayotuathiri lakini sasa tumeanza ujenzi wa kuchimba gati zetu,”alisema.
Alisema sababu nyingine za usalama ambapo kuna baadhi ya watu wamekuwa wakiibiwa hadi betri na kwamba nyingine ni usimamizi wa sera ambapo awali kulikuwa kuna baadhi ya watu wanaleta mizigo hawalipii.
Alisema pia kampeni za masoko zilienda chini licha ya miaka 1960 ilikuwa ni bandarini yenye nguvu.
Mbunge wa Magomeni, Jamal Kassim alisema hoja nyingi za ukaguzi kwa mamlaka hiyo zinatoka na mfumo mbuvu walionao taasisi hiyo.
“Mwenyekiti (Mwenyekiti wa Bodi ya Bandari Profesa Ignas Rubaratuka) ulituambia kuwa mmevuka malengo kutoka Shilingi 632 bilioni hadi 705 bilioni lakini kutokana na mfumo mbovu Serikali wharfag (fedha za mizigo) zikusanywe na TRA ( Mamlaka ya Mapato Nchini),”alisema.
“Mkurugenzi atuambie hizo fedha walizokusanya zinajumuisha pia fedha za wharfag na atumbie pia ukoje huo utaratibu?”alihoji.
Akijibu Mhandisi Kakoko alisema wamerejeshewa Sh 112bilioni ambazo ni mapato yanayotokana na mizigo ya kipindi cha Agostihadi Desemba mwaka jana na kwamba walishazitumia.
Hata hivyo, alisema wanadai Serikali Sh 183 bilioni ambazohazijarejeshwa katika mamlaka hiyo.
“Awali makubaliano kati ya TRA na mamlaka kuwa watakusanya mapato hayo ya mizigo lakini hili lilifutika baada ya sheria ya bandari kufanyiwa marekebisho na kutoa mamlaka kwa TRA kukusanya mapato hayo ya mizigo na kisha kurejeshwa kwa TPA,”alisema.
Akisoma maazimio ya kamati hiyo Mwenyekiti wa Kamati hiyo Kaboyoka aliagiza mamlaka kuwasilisha mpango kazi wa kusimika na kuanza kutumika kwa mfumo wa Tehama katika ofisi ya Katibu wa Bunge.
“Bodi ikamilishe zoezi la uthaminishaji wa mali katika mwaka wa fedha 2017/18,”alisema.

Wabunge walazwa kwa kuvuta hewa ya mabomu ya machozi


Kampala, Uganda. Wabunge wawili jana walilazwa katika kituo cha afya cha Lira baada ya kuzimia kutokana na kuvuta hewa yenye moshi wa mabomu ya machozi yaliyopigwa na polisi kutawanya mkutano wa mashaurino kuhusu ukomo wa umri wa rais uliofanyika wilaya ya Lira.
Waliolazwa ni wabunge wawakilishi wa wanawake Cecelia Ogwal Atim wa Dokolo na Sylvia Akello wa Otuke. Pia polisi walitumia risasi.
Wawili hao walishiriki mkutano huo ulioandaliwa na mbunge mwakilishi wa wanawake wa Lira Joy Atim Ongom katika uwanja wa michezo wa tarafa ya Adyel kumsaidia kuwashauri wapigakura wake juu ya muswada wa marekebisho ya katiba kwa lengo la kuondoa ibara ya 102 (b) iliyoweka ukomo wa umri kwamba usiwe chini ya miaka 35 wala zaidi ya miaka 75.
Ogwal na Akello walipanga pia kushirikiana katika mkutano mwingine wa mashauriano na wabunge wengine kutoka majimbo jirani ya uchaguzi.
Wabunge wengine walioungana nao katika mkutano huo walikuwa Charles Angiro wa Erute Kaskazini, Felix Okot Ogong na Jonathan Odur wa Erute Kusini.
Muda mfupi baada ya wabunge hao kuungana na Ongom kupanda jukwaani, polisi walianza kufyatua ovyo mabomu ya kutoa machozi. Wabunge wote walikuwa wamevaa utepe mwekundu mwekundu ambao kwa siku za hivi karibuni ni utambulisho wa wanasiasa wanaopinga kuondolewa kwa ukomo wa umri wa rais.
Hata hivyo, umati wa watu ulichachamaa na kuanza kuwarushia mawe polisi katika kambi ya Lira. Hadi wakati habari hii inachapishwa, maofisa wa polisi bado walikuwa wakikimbizana na wafuasi wa wabunge hao.