Wednesday, October 25

Wabunge walazwa kwa kuvuta hewa ya mabomu ya machozi


Kampala, Uganda. Wabunge wawili jana walilazwa katika kituo cha afya cha Lira baada ya kuzimia kutokana na kuvuta hewa yenye moshi wa mabomu ya machozi yaliyopigwa na polisi kutawanya mkutano wa mashaurino kuhusu ukomo wa umri wa rais uliofanyika wilaya ya Lira.
Waliolazwa ni wabunge wawakilishi wa wanawake Cecelia Ogwal Atim wa Dokolo na Sylvia Akello wa Otuke. Pia polisi walitumia risasi.
Wawili hao walishiriki mkutano huo ulioandaliwa na mbunge mwakilishi wa wanawake wa Lira Joy Atim Ongom katika uwanja wa michezo wa tarafa ya Adyel kumsaidia kuwashauri wapigakura wake juu ya muswada wa marekebisho ya katiba kwa lengo la kuondoa ibara ya 102 (b) iliyoweka ukomo wa umri kwamba usiwe chini ya miaka 35 wala zaidi ya miaka 75.
Ogwal na Akello walipanga pia kushirikiana katika mkutano mwingine wa mashauriano na wabunge wengine kutoka majimbo jirani ya uchaguzi.
Wabunge wengine walioungana nao katika mkutano huo walikuwa Charles Angiro wa Erute Kaskazini, Felix Okot Ogong na Jonathan Odur wa Erute Kusini.
Muda mfupi baada ya wabunge hao kuungana na Ongom kupanda jukwaani, polisi walianza kufyatua ovyo mabomu ya kutoa machozi. Wabunge wote walikuwa wamevaa utepe mwekundu mwekundu ambao kwa siku za hivi karibuni ni utambulisho wa wanasiasa wanaopinga kuondolewa kwa ukomo wa umri wa rais.
Hata hivyo, umati wa watu ulichachamaa na kuanza kuwarushia mawe polisi katika kambi ya Lira. Hadi wakati habari hii inachapishwa, maofisa wa polisi bado walikuwa wakikimbizana na wafuasi wa wabunge hao.

No comments:

Post a Comment