KATIKA siku za karibuni kumekuwapo na malalamiko mengi ya mihimili ya dola kuumbuana au kuingiliana katika mambo kadha wa kadha.
Hali hiyo imesababisha kuwapo malalamiko, kuwa mihimili hiyo imeshindwa kutambua mipaka yake iliyonayo kikatiba na kisheria.
Leo tumelazimika kusema haya, baada ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), kutangaza rasmi kumwandikia barua Spika wa Bunge, Job Ndugai juu ya kitendo cha Jeshi la Polisi kumkamata na kumhoji kwa zaidi ya saa tatu Mwandishi wa Habari wa Gazeti la Nipashe, Augusta Njoji.
Kamati hiyo, imesema bila kumung’unya maneno kuwa mhimili wa Bunge umeingiliwa na mamlaka nyingine kinyume na utaratibu wake.
Kamati hiyo imesema, Spika Ndugai anapaswa kulipa mwongozo kuhusu jambo ambalo linaonekana wazi kufedhehesha mhimili huo kisha atoe tamko.
Tunaamini uamuzi wa kamati hii, ni sahihi kwa sababu ni mhimili ambao umekuwa ukifanya kazi zake kwa uhuru bila kuingiliwa na chombo chochote, sasa inakuwaje polisi wanapoguswa kwenye jambo ambalo wanamaslahi nalo wanakuwa wakali.
Haiingii akilini, kama kweli jeshi hili limekumbwa na kashfa nzito ya aina hii eti wananchi wasijulishwe kupitia vyombo vya habari.
Haiwezekani kuwapo utata wa mkataba wa ununuzi wa magari 770 ya maji ya kuwasha, maarufu kama washawasha na taarifa hizi zimekaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG).
Tunasema hii ni mbinu chafu ya kutaka maovu yasiibuliwe kwenye jeshi hili ambao hata Rais Dk. John Magufuli amepata kulionya juu ya tuhuma mbalimbali zinazolikabili, zikiwamo ununuzi wa sare, ujenzi wa majengo na mengi.
Tunaamini kutaka kunyamazisha waandishi wa habari ni kukusudia kuficha uovu ambao umetafuna fedha za walipa kodi wa nchi hii.
Tunakubaliana na Mwenyekiti wa PAC, Naghejwa Kaboyoka kwamba, jeshi hilo halina mamlaka ya kumkamata mwandishi wa habari eti kisa ameandika kashfa hiyo.
Pia tunaona hii ni njia moja wapo ambayo kwa namna moja au nyingine inakusudia kulinyamazisha Bunge au kamati ambavyo tunaamini ndiyo chombo chenye mamlaka ya kujadili madudu yanayoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ili Watanzania waelewe nini kinachoendelea kwenye taasisi za Serikali.
Tunaelewa vizuri msimano wa Spika Ndugai, ni matarajio yetu kwamba atatumia kanuni na uwezo wake ili kuhoji uhalali wa jeshi hilo kufanya kitendo hicho ambacho si cha ungwana.
Tunajiuliza maswali mengi, hivi imefikia hatua polisi wanataka kufanya kazi za kamati za Bunge?
Tunashangaa kwanini polisi mkoani Dodoma wamemsumbua mwandishi huyo wa habari, wakati aliripoti taarifa rasmi iliyotolewa na Kamati ya Bunge ambayo ilitokana na ripoti ya CAG?
Kwa msingi huo, kitendo cha kutaka habari zao zisiandikwe kama kuna upungufu na idara yoyote na Serikali ni kitendo cha kuonyesha wanataka kuzima taarifa hizi zisiendelee kufichuliwa kwa sababu wanajua madudu yanayofanyika.
Umefika wakati sasa Jeshi la Polisi lianze kujitafakari katika utendaji kazi wa kila siku. Haiwezekani kila kukicha wao ndiyo watu wa kulaumiwa kila kona.
Tunasema hivyo, kwa sababu tunaamini jeshi hili kuanzia IGP Simon Sirro mpaka chini wanaongozwa na sheria, taratibu na kanuni za kazi.
Iweje kila siku wawe wao tu, hapa umefika muda wa kuangalia wapi wamejikwaa. Kwa kuwa jambo hili linakwenda kwa Spika, tunategemea majibu ya msingi yatakayotolewa yatafungua ukurasa mpya wa uhusiano mzuri kati ya polisi na wanahabari.
No comments:
Post a Comment