Wednesday, October 25

Ucheleweshaji ajira watajwa kikwazo kwa ATCL


Dar es Salaam. Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) limesema ucheleweshaji wa vibali vya ajira unakwamisha mipango ya ushindani wake kibiashara.
Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi amesema hayo leo Jumatano Oktoba 25,2017 alipozungumza na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Atashasta Nditiye.
Matindi amesema, “Katika utoaji wa vibali vya ajira za ATCL inachukuliwa kama idara ya huduma na si kampuni ya kibiashara yenye malengo ya kiushindani.”
Amesema bodi ya wakurugenzi ya shirika hilo imekuwa ikitaka ajira za baadhi ya wataalamu lakini kuchelewa kwa vibali ni kikwazo.
“Tunakuomba utusaidie kuimaliza changamoto hii, nia ni kuifanya ATCL kupata mafanikio zaidi,” amesema.
Amesema shirika linakabiliwa na changamoto nyingine ambazo ni upungufu wa marubani na wahandisi kutokana na udogo wa mishahara.
“Hali hii inatufanya tushindwe kupata marubani kutoka kwenye soko licha ya  wengi wao kuwa na nia ya kujiunga na ATCL,” amesema.
Amesema madhara yake ni kushindwa katika mipango ya kuongeza safari za ndege.
Mhandisi Matindi amesema changamoto nyingine ni baadhi ya viwanja vya ndege kutokuwa na miundombinu ya kuwezesha ndege kutua usiku.
“Changamoto hii inapunguza idadi ya safari na matumizi ya ndege, hivyo kuchangia kupunguza mapato,” amesema.
Hata hivyo, amesema sasa shirika linamiliki asilimia 24 ya soko la ndani la usafirishaji wa abiria na mizigo.
Amesema tangu shirika lilipofufuliwa Oktoba 2016 hadi Juni 2017 wamebeba abiria 106,138  hali inayowafanya kumiliki asilimia 24 ya soko la ndani.
Mkurugenzi mkuu huyo amesema uongozi umedhibiti matumizi yasiyokuwa ya lazima na kuhakikisha gharama za uendeshaji zinakuwa chini.
Akizungumza baada ya kuelezwa changamoto hizo, Nditiye ambaye ni naibu waziri anayeshughulikia sekta za mawasiliano na uchukuzi, ameahidi kuzishughulikia ili shirika hilo lipigwe hatua.
Pia, amewataka wafanyakazi kufanya kazi kwa weledi ili kujiepusha na makosa ya zamani yaliyosababisha shirika hilo kupata hasara.
“Katika awamu hii wafanyakazi wabadhirifu hatutawavumilia, Watanzania wanataka kuliona shirika hili likipata mafanikio,” amesema.

No comments:

Post a Comment