Friday, October 13

UTAFITI: WATOTO WAVIVU HUWA NA MIFUPA DHAIFU


NI wachache mno wasiojua umuhimu wa mazoezi kwa afya ya binadamu kwa vile ni suala linalozungumzwa na kuhimizwa mno na wataalamu wa afya.
Sababu ni faida nyingi zinazotokana na kufanya mazoezi au kwa maneno mengine kujishughulisha kimwili.
Yana umuhimu mkubwa hasa katika nyakati hizi, ambazo ujio wa sayansi na teknolojia umemrahisishia binadamu mambo mengi na hivyo kumsababishia uvivu unaoshuhudia kuibuka kwa maradhi mengi yanayotokana na staili hiyo mbaya ya maisha.
Mazoezi hupunguza lehemu isiyotakiwa mwilini, husaidia kupunguza uzito, huimarisha mifupa, hupunguza shinikizo la damu, huondoa sonona (depression).
Kadhalika mazoezi hupunguza makali ya ugonjwa wa pumu, kisukari, huboresha afya ya ubongo, kupunguza maradhi ya moyo, saratani, kuzuia kiharusi.
Hali kadhalika huboresha mfumo wa usingizi, uwezo wa kufanya tendo la ndoa, husaidia ukuaji wa mimba unaotakiwa kiafya na mengineyo mengi yanayoweza kujaza ukurasa nzima.
Ni kwa sababu hizo. mazoezi huhimizwa mno kwa watu mbalimbali hasa wenye umri wa utu uzima pamoja na wajawazito.
Kwa maana hiyo ni mara chache watoto kuhimizwa kwa kiwango sawa na watu wazima kufanya mazoezi au kujishughulisha.
Sababu ya unadra huo kwa watoto ni kutokana na wengi kutogundua bado au kukosa ufahamu kuhusu umuhimu wa mazoezi kwa watoto.
Lakini pia kuwahimiza watoto kuamka na kujijengea utamaduni wa kufanya mazoezi si kitu rahisi.
Lakini utafiti mpya umethibitisha kuna hitaji la kweli kwa watoto kuachana na simu zao za mikononi na kujishughulisha nje– na si tu kwa ajili ya kuzuia unene.
Vijana wana uwezekano mkubwa wa kuugua miteguko au mivunjiko ya mifupa iwapo hawatakuwa wakijishughulisha, wanasayaansi wanaonya.
Utafiti ulioendeshwa nchini Canada uligundua kuwa watoto waliokosa kiwango kinachokubalika cha kujishughulisha kila siku walikuwa na mifupa dhaifu kuliko wenzao walioendekeza ukakamavu.
Mwanasayansi Leigh Gabel kutoka Chuo Kikuu cha British Columbia nchini humo, anasema: “Tulibaini kuwa vijana ambao hawajishughulishi wana mifupa dhaifu.
“Hiyo inasikitisha mno kwa vile nguvu ya mifupa ni muhimu kuzuia utegukaji au uvunjikaji wao.
“Vitoto ambavyo vinakaa tu bila kujishughulisha haviikomazi mifupa ya miili yao kwa namna ambayo ingeimarisha nguvu ya mifupa yao hiyo.”
Watafiti walipima kujishughulisha kimwili na nguvu ya mifupa ya vijana wadogo 309 katika wakati muhimu wa makuzi yao.
Wavulana waliosimamiwa walikuwa wa miaka kati ya 12 na 16 wakati dirisha la miaka minne kwa wasichana lilianza wakati walipofikisha umri wa miaka 10.
Wakati huu wa maisha yao unahesabiwa kuwa muhimu kwa vile asilimia 36 ya mifupa ya binadamu huundwa katika kipindi hicho cha miaka minne.
Walitumia picha za xray za 3D X kulinganisha tofauti baina ya vijana ambao walifanya mazoezi na wale ambao waliendekeza uvivu.
Watoto ambao walikuwa na mazoea ya kila siku ya kujishughulisha kunakokubalika kwa dakika 60 kwa siku walilinganishwa na wale waliofanya kidogo chini ya nusu saa.
Wakati wavulana walionekana kuwa na mifupa mikubwa na yenye nguvu kipindi chote cha utafiti, jinsia zote zilikuwa na majibu sawa kuhusu umuhimu wa kujishughulisha kimwili.
Sote tunafahamu watoto huiga masuala ya kijamii kutoka kwa wazazi wao – maneno, imani na hata tabia ya sauti.
Lakini Januari mwaka huu, wataalamu wa afya walionya kuwa ni wazazi wachache waliokuwa na ufahamu namna mazoea yao ya kikakamavu yanavyochochea hamasa hiyo kwa kizazi cha vijana.
Watafiti wa Serikali ya Marekani walibaini kuwa watoto walifanya zaidi mazoezi iwapo wazazi wao walikuwa na utamaduni huo.
Nguvu ya mfupa ni muunganiko wa ukubwa wa mfupa, uzito (density) na muunganiko wa mifupa, watafiti waliandika katika Jarida la Mifupa na Utafiti wa Madini.
Mifupa dhaifu inajulikana kwa kuongeza hatari ya maradhi ya mifupa, ambayo kwa kitaalamu huitwa osteoporosis, hali ambayo huathiri watu wazima milioni tatu nchini Uingereza.
Professa Heather McKay, ambaye alishiriki katika utafiti huo anasema: “Ni muhimu kwa watoto na vijana kuondokana na mazoea ya kukaa kwenye skrini, sofa na kwenda kujishughulisha.
Hilo linakuja baada ya watafiti wa Hispania kukuta watoto ambao walikuwa na mazoezi chini ya saa moja kwa siku wakielekea kuwa na hatari ya kukumbwa na maradhi ya moyo kwa siku za usoni.
Utafiti wa mwaka 2013 ulionesha wale watoto walio na umri chini ya miaka 10 wakihitaji kufanya mazoezi kwa wastani kila siku kuwafanya mioyo yao kuwa na afya.
Januari mwaka huu, watafiti wa Norway walibaini watoto ambao wanashiriki katika mazoezi ya viungo walikuwa na nafasi nzuri ya kuwa na afya njema ya akili.
Vijana waliofanya mazoezi mara kwa mara wana uwezekano mdogo kukumbwa na maradhi ya akili kama ilivyo kwa watu wazima, wanasayansi walibaini.
Osteoporosis kwa ufupi?
Osteoporosis ni maradhi ya mifupa yanayotokana na kupungua kwa protini na madini kwenye mifupa.
Hali hii husababisha mifupa kuwa milaini na myepesi, ambapo inaweza kuvunjika kirahisi.
Kipindi cha utoto hadi kufikia umri wa miaka 30 ni muhimu ambacho mifupa hujijenga zaidi.
Dalili za maradhi hayo ni kuteguka hovyo, kukatika mifupa hovyo, maumivu makali ya mifupa na kadhalika.
Mbali ya kukosa mazoezi, upungufu wa vitamin kwa ujumla lishe duni inachangia kwa kiasi kikubwa katika udhaifu wa mifupa.
Ugonjwa huu pia unawapata wanawake zaidi kuliko wanaume. Utafiti unaonesha kuwa asilimia takribani 25 ya wanawake waliokwishafikia kukoma kwa hedhi wanapata matatizo ya udhaifu wa mifupa.
Ni muhimu kula mlo uliosheheni madini ya calcium, phosphorus, shaba pamoja na vitamini C, D, E na B12, kufanya mazoezi na inapobidi kupata ushauri wa tabibu.

MAZOEZI KWA WANAUME WENYE UMRI WA MIAKA 50

NI kawaida kwa watu wenye umri wa miaka 50 na kuendelea kuishi bila kufanya mazoezi yeyote. Katika utafiti uliofanyika nchi nzima mwaka 2012 (Tanzania STEPS survey), imebainika kwamba watu wengi walio katika kundi hili hawatimizi viwango vya mazoezi vinavyoshauriwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Tukiangalia upande wa wanaume tafiti na sayansi vinaonyesha kwamba, kiwango cha kichocheo kinachoitwa testosterone (homoni ya kiume) huwa kimepungua kwa kiasi kikubwa mtu anapofikia umri wa miaka 50. Kichocheo/homoni hii kwa kiasi kikubwa husaidia ufanyaji kazi wa mfumo wa uzazi na mifumo mingine kwa wanaume. Sambamba na kupungua kwa kiwango cha homoni hii, kunakuwa na ongezeko la kasi la kiasi cha mafuta katika sehemu za tumbo la mwanamume (abdominal obesity). Kwa pamoja hivi huchangia kusababisha magonjwa sugu yasiyoambukizi kama vile kisukari, kupanda kwa shinikizo la damu, matatizo ya moyo na baadhi ya saratani.
Mazoezi ni sehemu muhimu sana ya kukabiliana na hali hii – na nitathubutu kusema kwamba, kufanya mazoezi huenda kukawa muhimu zaidi katika zama hizo ukilinganisha na zama zilizopita. Lakini ni muhimu tufahamu aina ya mazoezi na vitu muhimu vya kuzingatia ili tusije kusababisha madhara zaidi ya faida.
1. Tahadhari
Ni dhahiri kwamba katika umri huu ki-baiolojia mwili wako ni tofauti sana na ulipokuwa na miaka 20, 30 au 40, jikubali. Kwa maana hiyo zingatia kuanza mazoezi taratibu na baada ya kupata ushauri kutoka kwa daktari wako. Ikiwezekana pata pia ushauri wa kitaalamu kutoka kwa mtaalamu wa mazoezi. Kumbuka kwamba moyo wako hauna uwezo mkubwa wa kukabiliana na mazoezi ya kasi kubwa sana hivyo ni muhimu kutozidisha viwango. Zingatia kupata mapumziko na lishe muafaka ya kutosha. Hakikisha unaupa mwili mapumziko kati ya zoezi moja na linalofuata. Hii itakusaidia kuepuka kuumia, kitu ambacho ni rahisi zaidi kutokea katika umri huu.
2. Mazoezi ya kusukuma, kuvuta au kunyanyua uzito ni msingi wa afya bora uzeeni
Napenda kurudia hili kutokana na ukweli kwamba aina hii ya mazoezi hupuuziwa sana. Kumbuka, misuli na mifupa, ambavyo hutoa mchango mkubwa katika kujongea, huimarishwa na aina hii ya mazoezi. Ikumbukwe pia, aina hii ya mazoezi husaidia kudumisha viwango bora vya testosterone mwilini. Zaidi ya hayo tunatakiwa kufahamu kwamba kiasi cha misuli hupungua kadiri umri unavyoongezeka, na kufanya mazoezi ya resistance husaidia kuzuia kuporomoka kwa misuli mwilini. Kuporomoka kwa misuli huchangia kudhoofisha uwezo wa mwili kutumia sukari, na kuweza kusababisha ugonjwa wa kisukari.
3. Mazoezi ya cardio/aerobics ni muhimu pia
Hili linafahamika zaidi. Nguvu na uwezo wa mapafu na moyo kufanya kazi hupungua kadiri umri unavyoongezeka. Kufanya mazoezi ya cardio au aerobics husaidia kuimarisha viungo hivi muhimu sana katika miili yetu. Kama hujawahi kabisa kufanya mazoezi anza na kutembea taratibu kasha haraka haraka. Kuogelea pia ni zoezi zuri sana maana huufanyisha mwili wote mazoezi na msukumo wa maji huzuia shinikizo linaloweza kusababisha madhara kwenye maungio (joits) wakati wa mazoezi. Unaweza pia kutumia mashine za kukimbilia (tread mills), baiskeli za mazoezi (stationary bicycles) na vifaa vingine chungu nzima.
4. Mazoezi ya kuimarisha kiwiliwili ni sehemu ya kanuni ya afya bora uzeeni
Kiwiliwili huusisha mgongo na tumbo. Kuketi kwa muda mrefu kazini na misukosuko mingi ya maisha husababisha maumivu sugu ya sehemu ya chini ya mgongo hata kwa wanaume. Hii huchangia pia kudhoofisha misuli ya tumbo. Kuwa na kiwiliwili dhaifu huchangia kusababisha matatizo ya uwiano au balance, na ni sababu mojawapo ya tatizo la kuanguka anguka ambako hutokea sana umri unapoongezeka.
Kiwiliwili dhaifu na maumivu ya mgongo huweza kukusababishia kukosa uwezo na ufanisi wa kufanya shughuli muhimu sana za maisha. Mazoezi kama vile planks ni rahisi kufanyika na husaidia kuimarisha misuli ya tumbo na ile ya mgongo kwa pamoja. Hakikisha unapata maelekezo sahihi ya jinsi ya kufanya planks, na anza leo kuzifanya.
Dk. Mashili ni mtaalamu wa Fisiolojia ya Mazoezi na Homoni. Pia ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS).0752255949 fredirick@gmail.com.

ROMANUS MWANGI’NGO: UZAGAAJI WA MAJITAKA UTAKUWA HISTORIA

SERIKALI kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji inaendelea kuboresha hali ya usafi wa mazingira kwa kuongeza uwezo wa mfumo wa ukusanyaji na usafishaji wa majitaka katika jiji la Dar es Salaam.
Maandalizi ya awamu ya kwanza ya mpango huo yameanza baada ya Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) kukabidhiwa eneo la Jangwani ambapo mtambo wa kwanza wa kisasa wa kusafisha
majitaka utajengwa.
Mradi huu ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuongeza uwezo wa mfumo wa ukusanyaji na usafishaji wa majitaka katika jiji la Dar es Salaam ambapo lengo ni kulaza kilometa 563 za mabomba ya ukubwa mbalimbali ya ukusanyaji majitaka yatakayokusanya majitaka na kuyamwaga katika mitambo mikubwa mitatu itakayojengwa Jangwani,
Kurasini na Mbezi.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Romanus Mwangi’ngo, anasema mitambo hiyo mipya itatumika kuzalisha gesi asilia na umeme kwa ajili ya kujiendesha, hivyo kupunguza matumizi na gharama
za umeme kwenye mradi huo.
Anasema maji yatakayokuwa yamesafishwa yatauzwa na kutumika katika shughuli mbalimbali kama vile kupozea mitambo na umwagiliaji na tope litakalobaki baada ya mchakato huo wa usafishaji litatumika kama mbolea kwa ajili ya kilimo.
Katika eneo la Jangwani, bustani ya kisasa itakayokuwa na miti ya kivuli, maua na viti vya kupumzikia itatengenezwa ili kuboresha taswira ya eneo hilo.
Mwangi’ngo anasema mradi huo unahusu ujenzi wa mtambo wa kusafisha majitaka eneo la Jangwani na utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kusafisha mita za ujazo 200,000 kwa siku.
Mfumo wa mabomba yenye urefu wa kilometa 376 yatakayolazwa kuanzia Ubungo hadi Jangwani, Kinondoni, Mwananyamala, Msasani, katikati ya jiji na Ilala utajengwa.
Awamu ya kwanza ya ujenzi itahusisha mtambo utakaoweza kusafisha mita za ujazo 25,000 za majitaka kwa siku na mabomba ya kilometa 17.43 yatakayojengwa katika mitaa ya eneo la Magomeni.
Katika awamu hii ya kwanza bomba linalomwaga majitaka baharini litaacha kutumika na badala yake majitaka hayo yatakwenda kusafishiwa katika mtambo huo.
Kuhusu mfumo wa majitaka Mbezi Beach, Mwang’ingo anasema mradi huo unahusu ujenzi wa mtambo wa kusafisha majitaka utakaojengwa eneo la Kilongawima ambapo ukikamilika utakuwa na uwezo wa kusafisha mita za ujazo 16,000 kwa siku na utajumuisha mfumo wenye urefu wa kilometa 97 utakaojengwa katika eneo la Mbezi Beach, Kawe, Kilongawima, Tegeta na maeneo mengine jirani.
Mradi huo utajengwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia kupitia mkopo wa masharti nafuu na unatarajiwa kugharimu dola za Marekani milioni 65.
Anasema utaratibu wa kumtafuta mkandarasi mshauri atakayefanya usanifu wa kusimamia ujenzi ulianza Februari mwaka huu na ujenzi unatarajiwa kuanza mapema mwakani.
Mradi mwingine ni ujenzi wa mfumo wa majitaka Kurasini utakaojengwa katika maeneo yalipo mabwawa ya kusafisha majitaka.
Anasema mradi huo utakuwa na mfumo wenye urefu wa kilometa 90 utakaolazwa katika maeneo ya Keko,
Chang’ombe, Kurasini, Temeke na Uwanjawa Taifa. Mtambo huu utakuwa na uwezo wakusafisha mita za ujazo 11,000 kwa siku.
Awali katika utafutaji wa eneo la Jangwani, mamlaka iliomba kutumia eneo hilo baada ya kupata kibali kutoka Manispaa ya Ilala.
Baada ya notisi kutolewa Agosti 16 mwaka huu, kazi ya usafishaji wa eneo hilo ilifanywa na manispaa na kulikabidhi
rasmi kwa mamlaka.
Meneja Uhusiano wa Jamii wa DAWASA, Neli Msuya, anasema mradi wa uboreshaji wa huduma zanugawaji na usambazaji maji unaendelea kutekelezwa kwa kasi katika maeneo mbalimbali jiji la Dar es salaam na katika miji ya Bagamoyo na Kibaha.
Mradi huo ulianza rasmi Machi mwaka 2016 na utakamilika Novemba 2017, ambapo kazi zinazofanyika chini ya mradi huu ni pamoja na ujenzi wa matanki tisa ya kuhifadhi na kusambaza maji yenye ukubwa wa kuhifadhi lita
milioni 3 hadi milioni 6, ujenzi wa vituo vinne vya kusukuma maji, ununuzi na ufungaji wa pampu kubwa za kusukuma maji 16.

Kazi zingine ni ununuzi wa transfoma na ufungaji njia za umeme wa msongo mkubwa, ununuzi na ulazaji wa mabomba makubwa ya ugawaji maji na ulazaji wa mabomba ya usambazaji maji mitaani yatakayokuwa na urefu wa kilometa 477.
“Maeneo yatakayonufaika na mradi huu ni Salasala, Bunju, Wazo, Makongo, Changanyikeni, Bagamoyo, Mpiji, Zinga, Kiromo, Kitopeni, Ukuni, Kerege, Buma, Mataya na Ukanda maalumu wa EPZA ambayo yanahudumiwa na mtambo wa Ruvu Chini,  Kiluvya, Kibamba, Mbezi, Msakuzi, Makabe, Malambamawili na Msigani,” anasema Msuya.

‘AWAMU YA TANO IMEANZA KUREJESHA MTIZAMO WA NYERERE’

NAIBU Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha, amesema Serikali ya awamu ya tano imeanza kurejea katika mtazamo wa Mwalimu Julius Nyerere juu ya uchumi wa viwanda aliouanzisha.
Akizindua Kongamano la Kumbukizi ya Kifo cha Mwalimu Nyerere lililofanyika katika  Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere  jijini Dar es Salaam juzi, Ole Nasha alisema Mwalimu Nyerere alijenga viwanda vingi hapa nchini.
Alivitaja viwanda ambavyo Mwalimu Nyerere alivijenga kuwa ni viwanda vya nguo kama Urafiki, Mbeya Tex, Mwatex, Mutex, viwanda vya ngozi, viwanda vya zana za kilimo, viwanda vya kutengeneza vipuli pamoja na viwanda vinavyotegemea malighafi za mazao yanayolimwa hapa nchini.
Alisema Taifa linahitaji viongozi wazalendo na waadilifu kama alivyo Rais Dk. John Magufuli ambaye ameonesha nia ya dhati ya kufuata nyendo za Mwalimu Nyerere kwa kuhimiza maendeleo ya kiuchumi yanayotegemea viwanda.
“Serikali ya awamu ya tano kwa muda wa miaka miwili iliyokaa madarakani, imejitahidi kurejea na kuweka kwenye vitendo dhana ya Mwalimu Nyerere ya uchumi wa viwanda, kwani kwa sasa  inatekeleza Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa, mwaka  2016/2017-2020/2021 unayojikita katika ujenzi wa viwanda kama njia ya maendeleo ya kiuchumi na maisha ya watu,”alisema Ole Nasha.
Alisema mtazamo wa Mwalimu Nyerere ulikuwa ni kutumia viwanda vya ndani kama njia ya kujinasua kutoka kwenye unyonyaji wa muda mrefu.
Kama Taifa huru kuna haja ya kuondoa tofauti za kisiasa na kuishi katika misingi ya usawa, umoja, ushirikiano ili kujiletea maendeleo ya uchumi kwa mtu mmoja na taifa kwa ujumla, ikiwemo kuhimiza uzalendo kwa kila mtanzania ili kujenga Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati ifikapo 2025.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Kumbumbuku ya Mwalimu Nyerere, Profesa Shadrack Mwakalila, alisema kuwa ili kufikia Tanzania ya viwanda taifa linahitaji viongozi wazalendo wenye uchu wa maendeleo na wasio na misingi ya ukabila wala udini.
“Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kuwa, ili tuendelee tunahitaji vitu vinne ambavyo ni watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora, hivyo ustawi wa uchumi wa viwanda  unahitaji viongozi na watendaji ambao ni wazalendo, watiifu na wenye kutanguliza mbele masilahi ya taifa,”alisema Profesa Mwakalila.
Kongamano la maadhimisho ya siku ya  Mwalimu Nyarere hufanyika kila mwaka ili kujadili busara, fikra na hekima zake katika kujenga usawa, maendeleo, umoja na ustawi wa uchumi wa taifa letu.
Maadhimisho ya mwaka huu ni ya 18, tangu Mwalimu Nyerere afariki mnamo Oktoba 14, 1999, ambapo kauli mbiu ya kongamano la mwaka huu inasema “Mtazamo wa Mwalimu Nyerere katika Uchumi wa Viwanda na Maendeleo ya Jamii”.
Maadhimisho hayo yatafanyika visiwani Zanzibar ambapo shughuli ya kuzima mwenge wa uhuru itafanyika.

FAMILIA YA LISSU: TUPO GIZANI

MWANASHERIA Alute Mughwai, ambaye ni kaka mkubwa wa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, amesema familia hiyo ipo gizani juu ya upelelezi wa tukio la ndugu yao kupigwa risasi, huku akieleza  kushangazwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, kutaka mjadala wa jambo hilo ufungwe.
Sirro alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akiwashangaa waandishi wa habari na watu wengine ambao wamekuwa wakimuuliza tukio la Lissu na kusema tukio hilo ni la kawaida kama yalivyo matukio mengine.
Akizungumza na MTANZANIA ofisini kwake jana, Mughwai alisema. “Familia iko gizani haijui kinachoendelea katika upelelezi sasa tunanyamaza vipi? Tuwe tunapata taarifa za hatua zilizofikiwa katika upelelezi ili tusipige kelele,” alisema.
Alisema kauli ya IGP Sirro  kuwa tukio la kushambuliwa kwa Lissu ni sawa sawa na matukio mengine ni ushahidi kuwa polisi imezidiwa  na ndiyo maana familia imeomba uchunguzi usaidiwe na vyombo kutoka nje.
“Ni kweli matukio ya kushambuliwa na kuumizwa hata kuuwawa watu kwa kutumia risasi  yapo mengi ndio maana sisi kama familia tunasema kama wamezidiwa na kazi kwa hili la ndugu yetu waruhusu wachunguzi kutoka nje ya nchi.
“Anapodai kuwa ni tukio la kawaida analinganisha na tukio lipi ambalo kiongozi wa umma alishambuliwa hadharani kama Lissu? Kama ni lile la RPC wa Mwanza (marehemu Liberatus Barlow), pamoja na kwamba alishambuliwa usiku, mbona waliohusika walikamatwa kesho yake na sasa wako mahakamani? Kwanini hili la mchana kweupe hatuambiwi kinachoendelea?
“Familia itanyamaza pale ambapo wahalifu waliokusudia kumuua Lissu na wale wote waliohusika kupanga njama hizo watakapotiwa mbaroni na kufikishwa mahakamani
“Sisi hatumfundishi kazi (Sirro) lakini Polisi ni chombo cha Serikali na Katiba yetu Ibara 8 (1) (c ) inaeleza serikali itakavyo wajibika kwa wananchi na sisi ni sehemu ya wananchi wa Tanzania” alieleza.
Mughwai alisema badala ya IGP Sirro kupuuza ushauri wa watu, yeye kama mtumishi wa umma angeupokea hata kama hatoufanyia kazi badala ya kukataza watu kusema kwa madai kuwa wanakifundisha kazi chombo hicho.
Alisema iwapo familia ingekuwa inapata taarifa za hatua zilizofikiwa katika upelelezi, kusingekuwa na malumbano yoyote na akashangaa polisi kutowajulisha waathirika wa tukio hilo hasa familia hatua iliyofikiwa mpaka sasa zaidi ya amri na makatazo ya IGP Sirro.
“Matarajio yetu badala ya kusema asifundishwe kazi angesema tu kwa unyenyekevu kuwa amepokea ushauri ataufanyia kazi au laa,” alisema Mughwai.
Alisema njia pekee ni kwa Sirro kuacha upelelezi wa kwenye vyombo vya habari na badala yake afanye kazi yake kwa weledi, haki na kwa haraka.
“Hatuwezi kukaa kimya kama familia, nasema sijui kama IGP alinukuliwa vizuri lakini hawezi kutunyamazisha kuhusu sula la kushambuliwa kwa Lissu.
“Njia pekee ni yeye kuacha malumbano ya kwenye vyombo vya habari kwa kufanya upelelezi unaojitosheleza, wenye matokeo yenye tija na kwa haraka,” alisema.
Majibu ya Barua ya AG
Kuhusu barua ambayo familia hiyo ilimuandikia Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kuomba upelelezi wa tukio la Lissu kupigwa risasi ufanywe na vyombo kutoka nje ya nchi, alisema mawasiliano kati yao na Serikali yanaendelea vizuri kiasi cha kuonyesha matumaini ya ndugu yao kupata haki.
Mughwai alikiri kupokea barua kutoka kwa AG yenye majibu ya barua yao ya awali yenye ujumbe wa familia kuhusu namna suala la kushambuliwa kwa ndugu yao linavyoshughulikiwa na vyombo vinavyohusika.
Alisema hivi sasa familia hiyo isingependa kuendelea na utaratibu wa kujibizana na Serikali kupitia vyombo vya habari na badala yake wameanza kutumia utaratibu wa kuwasiliana.
Huku akimwonesha mwandishi wa gazeti hili faili lenye barua ya AG na ambayo Spika wa Bunge, Job Ndugai, aliwaandikia akiomba kukutana nayo, Mughwai alisema kwa sasa familia inavipa nafasi vyombo vinavyohusika vifanye kazi.
“Ni kweli majibu ya barua yetu ambayo tulimwandikia AG tumeyapata na ieleweke sisi tuliandika barua tatu moja kwenda kwa mwanasheria mkuu, nyingine kwa waziri wa sheria na nyingine kwa Spika chombo ambacho ndugu yetu ni mtumishi akiwakilisha wananchi wa Singida Mashariki.
“Siwezi kukuruhusu ukasoma maudhui yote yaliyoko kwenye barua hizi, kama unavyo ona ina muhuri wa siri ni ‘confidential’. Hata barua ya Spika kutaka kuonana na familia hii hapa pia sisi hatukujipeleka kwenda kuonana nao, kwa ujumla familia inawapa nafasi ili Serikali iweze kufanyia kazi yale tuliyohoji kwenye barua yetu.
“Pamoja na kwamba hivi sasa ninapozungumza na wewe natumia chombo cha habari lakini tusingependa kuendelea na utaratibu huu wa kuzungumzia kinachoendelea katika mawasiliano yetu na Serikali mpaka hapo tutakapokwama kwa njia hii au hata tukifanikiwa tutawajulisha umma,” alisema.

Mahakama Uganda yaamrisha washukiwa 23 kulipwa fidia

Washukiwa wa Kesi ya mauaji ya Kaweesi wakiwa mahakamani
Mahakama Kuu nchini Uganda imeamrisha kuwa kila mshukiwa wa mauaji ya aliyekuwa msemaji wa polisi Andrew Felix Kaweesi alipwe fidia ya Shilingi milioni 80 kutokana na uvunjifu wa haki zao za kibinadamu.
Jaji Margret Oguli Alhamisi ameitaka serikali ilipe shilingi milioni 80 na riba ya asilimia 20 kwa kila mshukiwa ambao ni watu 23 kwa sababu vyombo vya magereza vilihusika na uvunjifu wa haki zao kwa kuwatesa wakati wakiwa rumande.
“Wanaofikishwa mahakamani bado ni washukiwa mpaka pale watakapopatikana na makosa. Na ilikuwa ni wajibu wao kuwatendea haki bila ya kuwatesa,” amesema Jaji.
Kwa mujibu wa Jaji, kulikuwa na ushahidi wa kutosha kuonyesha kwamba vyombo vya magereza vilikuwa vinaficha kitu walipokataa washukiwa hao kupatiwa matibabu.
Hili linafuatia maombi yaliyoletwa na wakili wa washukiwa hao Ladislaus Rwakafuzi akiitaka mahakama iilazimishe serikali kuwapeleka wakapimwe hospitali ili kuthibitisha sababu zilizopelekea kuwa na majeraha.
Washukiwa hao waliiambia mahakama kuwa walikamatwa wakiwa majumbani mwao na kinyume cha sheria wakazuiliwa katika rumande ya kijeshi kabla hawajapelekwa kwenye kituo cha polisi cha Nalufenya, Wilaya ya Jinja kinachojulikana kwa mateso makali.
Pia washukiwa hao waliiambia mahakama kwamba hawakupatiwa huduma yoyote ya tiba kutokana na majeraha walioyapata wakati wa mateso hayo.
Kaweesi alipigwa risasi akiwa na mlinzi wake na dereva Machi 17 mwaka huu wakati akitoka nyumbani kwake katika eneo la Kulambiro.
Washambuliaji waliokuwa na bunduki waliondoka na bastola yake na ya mlinzi wake.
Washukiwa wengi walikamatwa na kuwekwa rumande lakini walipoletwa mahakamani wengi wao walikuwa na majeraha ambayo walidai yalisababishwa na mateso walioyapata kutoka kwa maafisa wa ulinzi.

Maafisa wawili wa jeshi la Somalia wamejiuzulu wadhifa wao

Jeshi la Somalia.
Vyombo vya habari vya serikali ya Somalia vilitangaza Alhamis kwamba maafisa wawili wa vyeo vya juu wa jeshi la Somalia wamejiuzulu katika hatua ambayo itaweza kuwa ni pigo kubwa katika juhudi za nchi hiyo ya pembe ya Afrika kupambana na wanamgambo wa ki-Islam.
Radio Mugdisho inayomilikiwa na serikali ilitangaza Alhamis kuwa mkuu wa jeshi la ulinzi Ahmed Jimale Gedi alijiuzulu na waziri wa ulinzi Abdirashid Abdullah Mohamed aliyewasilisha barua yake ya kujiuzulu kwa baraza la mawaziri la Rais Mohamed Abdullahi Farmayo. Redio hiyo imeeleza kwamba baraza la mawaziri lilimteuwa Jenerali Abdiweli Jama Hussein baada ya Ahmed Jimale Gedi kujiuzulu.
Radio Muqdisho haikueleza sababu za kujiuzulu kwa maafisa hao na wala hakuna ofisa yeyote wa serikali au msemaji wake aliyeweza kutoa sababu zilizopelekea uwamuzi wao.

Marekani yaitaka Uturuki kuwasilisha ushahidi wake dhidi ya raia wa Marekani.

Marekani inaitaka serikali ya Uturuki kuwasilisha ushahidi wa kutetea shutuma zake ilizotumia kuelezea kukamatwa kwa wafanyakazi wa ubalozi mdogo wa Marekani na raia kadhaa wa Marekani akiwemo mchungaji wa kimarekani aliyefungwa jela Andrew Brunson.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Heather Nauert aliwaambia waandishi wa habari kwamba Marekani haijaona ushahidi wowote kuhusiana na hilo na iliitaka Ankara kutekeleza ahadi yake ya kuwaruhusu watu waliokamatwa kuonana na mawakili wao.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Rex Tillerson.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Rex Tillerson.
Wakati huo huo waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson alizungumza na waziri wa mambo ya nje wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu na kumuelezea wasi wasi wa Washington juu ya kukamatwa kwa watu hao. Haya ni mazungumzo ya simu ya mara ya pili chini ya muda wa wiki moja kati ya wanadiplomasia hawa wawili wa cheo cha juu katika ushirika wa NATO.
Uhusiano kati ya Uturuki na Marekani umekuwa wa mashaka kufuatia kukamatwa wiki iliyopita mfanyakazi wa ubalozi mdogo wa Marekani huko Uturuki Metin Topuz kwa mashtaka ya ugaidi na uhaini katika uhusiano na jaribio lililoshindikana la mapinduzi la mwaka jana dhidi ya Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan.

Ghana kuangalia upya sheria za wanyama pori kutokana na biashara haramu ya Kakakuona

Ghana italazimika kuangalia upya sheria zake za wanyamapori kutokana na biashara ya Kakakuona ambayo imekithiri mno. Hali hii imesababishwa na hofu ya kwamba nchi hiyo inatumiwa kuendesha biashara hiyo haramu.

Schuppentier - Manidae (picture-alliance/AP Photo/Firdia Lisnawati)
Wito umetolewa kwa taifa hilo kuangalia upya sheria zake juu ya uhalifu wa wanyamapori, kutokana na hofu ya kuwa nchi ya Ghana imekuwa ikitumiwa kama njia ya kusafirisha bidhaa kwajili ya biashara hiyo haramu ya kakakuona.
Zaidi ya kilo 31,000 ya magamba ya Kakakuona zimenaswa kote duniani mwaka huu, kulingana na shirika la kimataifa la ustawi wa wanyama, IFAW.
Mnamo mwezi Mei na Juni shehena mbili kubwa zilinaswa nchini Malaysia na angalau kilo 700 zilipatikana zikiwa zimesafirishwa kupitia Ghana. Shehena nyengine kubwa zilikamatwa pia nchini Uganda, Camerron na Ivory Coast.
Mark Hofberg kutoka shirika la IFAW amesema magamba mengi kutoka kwa mnyama huyo kutoka Afrika imeuzwa ili kufikia mahitaji yake katika bara la Asia, ambako hutumiwa katika dawa za jadi.
Kakakuona anapatikana sana katika nchi za Afrika na kusini mashariki mwa Asia.
Aina mbili kati ya nane ya mnyama huyo wameorodheshwa kuwa hatarini kwenye orodha nyekundu ya aina ya wanyama walio hatarini.
Kwa mujibu wa bwana Hofberg, kuongezeka kwa kamatakamata ya mizigo hiyo kunaweza kuwa ishara kuwa mamlaka husika zinalichukulia suala hili kwa uzito lakini amesema nchi nyingi hazina sheria kali za kuadhibu wafanyabiashara haramu.
"Kwa biashara hii kupungua kwa kiasi kikubwa, kunahitajika adhabu na hukumu kali," aliiambia shirika la habari la AFP.
Kakakuona ni mnyama aliyehifadhiwa nchini Ghana lakini mkuu wa tume ya Wanyamapori wa Ghana, Nana Kofi Adu-Nsiah, amesema sheria kali inahitajika.
Sheria zilizopo za ulinzi wa wanyamapori zilipitishwa katika miaka ya 1960 na tume hiyo inataka ziangaliwe upya ili kufikia viwango vya kimataifa.
Watu watatu walikamatwa nchini Ghana kuhusiana na mizigo iliyonaswa mwezi Juni nchini Malaysia.
Schuppentier - Manidae (picture-alliance/Photoshot)
Kakakuona
Viongozi wa Serikali wanaamini sheria mpya zitazuia Ghana kutumiwa kuwa hatua ya usafiri kwa wanyama hao wanaosafirishwa lakini pia kuna wasiwasi pia juu ya uwindaji wa ndani wa kakakuona.
Katika barabara kuu nyingi nchini Ghana, watu wanaonekana wakimuuza mnyama huyu, ambaye hushikwa juu chini, kutoka mkiani.
Wanyama hao ambao wana ukubwa wa sentimita 30 hadi 100 wanaweza kuuzwa kwa karibu dola 45 au euro 38. Na wale wawauzao kwa kawaida ni watu masikini. Maofisa wa Tume ya Wanyamapori wanamkamata mtu yeyote anayemuuza mnyama huyu lakini Bwana Adu-Nsiah alipendekeza suluhisho la kuwaokoa wanyama hao kwa njia ya kuwanunua wakiwa hai kutoka kwa wauzaji na kuwatengea makazi mbadala.
Haijulikani ni wangapi wanaoishi porini huko Ghana lakini makazi yao yameathiriwa na ukataji miti na maendeleo. Hali hiyo pia huwafanya wanyama hao kuwa mawindo rahisi na kusababisha kuwa wanyama wanaosafirishwa kwa wingi ulimwenguni.
"Sio wanyama ambao wanaweza kukimbia kwa haraka ili kujilinda," anasema bwana Abu-Nsiah.
Watafiti wamegundua kuwa kakakuona anatumika kwajili ya chakula na magamba yake yanatumiwa kwajili ya viungo. Jamii mbali mbali vijijini katika taifa la Ghana wanahamasishwa kuhusu umuhimu na uhifadhi wa Kakakuona ambaye yuko hatarini ya kuangamia na kupotea katika taifa hilo.

Uhispania yaadhimisha siku ya kitaifa na mgogoro unaendelea

Maelfu ya Wakatalani waonataka Catalonia ibaki ndani ya Uhispania wameadhimisha siku ya kitaifa. Kitisho cha kujitenga kwa jimbo hilo kimeitumbukiza nchi hiyo kwenye sintofahamu. 

Spanien Madrid Demonstration gegen Unabbhähigkeit Kataloniens (Getty Images/AFP/J. Soriano)
Katika mji mkuu wa Madrid, vikosi vya jeshi na polisi vilisimama katikam gwaride mbele ya Mfalme Felipe VI, aliyekuwa ameongozana na wanasiasa wa kitaifa pamoja na wa mikoa. Maelfu ya watu waliokuwa wamejipanga katika njia ya Paseo de la Castellana ya mjini Madrid kwa ajili ya kushuhudia gwaride la kijeshi, walipeperusha bendera za Uhispania.
Uhispania inasubiri majibu kutokana na ombi la serikali kwakiongozi wa Catalonia Carles Puigdemont juu ya ufafanuzi iwapo tayari ametangaza uhuru. Ikiwa hivyo, serikali kuu ya Uhispania inaonya kuwa inaweza kutumia kifungu cha 155 cha katiba yake ili kuchukua udhibiti wa jimbo la Catalonia kwa sehemu au kwa ukamilifu.
Rais wa mkoa wa Catalonia Carles Puigdemont alitangaza siku ya Jumanne kwamba atautumia ushindi wa kura ya maoni  iliyopigwa marufuku kuendelea mbele na kutangaza uhuru wa jimbo la Catalonia na kisha akasimamisha uamuzi huo kwa kipindi cha wiki moja ili kupisha mazungumzo na fursa ya kuweza kupatana na serikali kuu ya mjini Madrid.Lakini akizungumza katika bunge la taifa, Waziri Mkuu Mariano Rajoy alisema majibu ya Puigdemont kutokana na matendo yake yatakuwa muhimu katika kuamua matukio katika siku zijazo.
National-Feiertag in Spanien (picture-alliance/AP Photo/P. White)
Mfalme Felipe wa VI na malkia Letizia
Ni sikukuu gani hiyo?
Sikukuu ya leo nchini Uhispania  inajulikana kama Dia de la Hispanidad, kwa maana ya Siku ya Uhispania.  Nchi hiyo inakumbuka kuwasili nchini Marekani kwa Christopher Columbus na pia ni siku ya majeshi ya Uhispania. Viongozi wa Mikoa kwa kawaida hualikwa kuhudhuria gwaride mjini Madrid lakini kwa miaka mingi wawakilishi wa mikoa ya Basque na Catalonia wamesusa kuhudhuria maadhimisho hayo. Ofisi kadhaa za manispaa mjini Catalonia zimesema zitapuuza siku kuu hiyo na kuendelea kazi kama kawaida. Takriban raia milioni 2.3 wa Catalonia au asilimia 43 ya Wapiga kura katika jimbo hilo walipiga kura katika kura ya maoni ya kutafuta uhuru wa jimbo hilo. Asilimia 90 ya Wakatalonia waliunga mkono jimbo lao kujitenga na Uhispania.
Siku hiyo ilikumbwa na vurugu wakati polisi walipotumia nguvu pale walipojaribu kuzuia kufanyika kura hiyo ya maoni ambayo mahakama ilisema kuwa si halali. Ripoti ya shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch iliyotolewa siku ya Alhamisi ilisema polisi wa Uhispania walitumia nguvu nyingi wakati wa kuwakabili waandamanaji waliokuwa wakiandamana kwa amani siku hiyo. 
Jimbo la Catalonia lina wakazi milioni 7.5 na linachangia asilimia 20 katika uchumi wa Uhispania unaofikia Euro trilioni 1.1 sawa na Dola trilioni 1.3.

Yaya Toure aonya kuhusu kombe la dunia Urusi

Yaya Toure asema kombe la dunia la Urusi 2018 litafeli pakubwa iwapo litatawaliwa na ubaguzi wa rangi
Image captionYaya Toure asema kombe la dunia la Urusi 2018 litafeli pakubwa iwapo litatawaliwa na ubaguzi wa rangi
Kiungo wa kati wa Manchester City Yaya Toure anasema kuwa kombe la dunia la mwaka ujao litakuwa na ''litafeli pakubwa iwapo litatawaliwa na ubaguzi wa rangi'' .
Toure mwenye umri wa miaka 34 alikabiliwa na matamshi ya ubaguzi wa rangi wakati City ilipocheza dhidi ya CSKA Moscow katika kombe la vilabu bingwa nchini Urusi 2013.
Anataka kuisaidia Fifa na serikali ya Urusi kukabiliana na tatizo hilo kabla ya michuano hiyo kuanza rasmi.Lazima tuone mabadiliko kwa sababu hawalizungumzii swala hili na kuewa utatuzi, aliongezea.
Mwezi uliopita, Liverpool ililalamika kwa Uefa kuhusu madai ya matamshi ya ubaguzi wa rangi yaliomlenga winga Bobby Adekanye wakati wa mechi ya kombe la Uefa upande wa vijana katika uwanja wa Spartak Moscow.

Makamanda wa jeshi wamejiuzulu.

Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi FarmajoHaki miliki ya pichaGOOGLE
Image captionRais wa Somalia Mohamed Abdullahi Farmajo
Kwa mujibu wa taarifa za serikali, waziri wa ulinzi naye aliamua kujiuzulu wakati wa mkutano wa wiki wa baraza la mawaziri.
Katika tukio jingine Mkuu wa Jeshi Ahmed Jimale Irfiid naye alijiuzulu hapo jana mchana. Rais Farmajo hapo hapo akamteua Meja Jenerali Abdiweli Jama Gorod kuwa mkuu wa majeshi.
Hatua hiyo imekuja wakati ambao Somalia inakabiliwa na tishio la usalama kutoka kwa kundi la wapiganaji wa Al Shabab.
Nafasi ya Jenerali Mohamed Jima'le Irfid imechukuliwa na Jeneral Abdiweli Jama Hussein Gorod. Somalia kwa muda mrefu imekuwa ikikabiliwa na mashambulio kutoka kwa wapiganaji wa Al Shabab.

Mpango wa nyuklia wa Iran: Trump atarajiwa kujiondoa

Waandamanaji nje ya Ikulu ya Whitehouse wamemtaka rais Trump kuunga mkono makubaliano hayo.Haki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionWaandamanaji nje ya Ikulu ya Whitehouse wamemtaka rais Trump kuunga mkono makubaliano hayo.
Rais wa Marekani Donald Trump anatarajiwa kutounga mkono makubaliano ya kinyuklia na Iran Ijumaa na kuweka chini mkakati wa kukabiliana na mpango huo.
Hatua hiyo hautaiondoa Marekani katika makubaliano hayo lakini utalipatia uwezo bunge la Congress siku 60 kuamua iwapo itafanya hivyo kwa kuiwekea Iran Vikwazo.
Waziri wa maswala ya kigeni nchini Marekani Rex Tillerson amekuwa akijadiliana na wenzake kutoka Ulaya na China kulingana na maafisa.
Bwana Trump amekuwaa akishinikizwa nyumbani na ughaibuni kutofutilia mbali mpango huo.
Chini ya makubaliano hayo ya 2015 , Iran ilikubali kusitisha mpango wake wa kinyuklia kwa lengo la kuondolewa kwa muda baadhi ya vikwazo ilivyowekewa.
Rais Trump amekuwa mkoasoaji mkubwa wa makubaliano hayo na akaahidi kuufutilia mbali wakati wa kampeni .
Rais Trump na mwenzake wa Iran Hassan Rouhani
Image captionRais Trump ameutaja mkataba huo kuwa mbaya zaidi na kuonya kuufutilia mbali.
Bunge la Congress litamtaka rais kuthibitisha kila siku 90 kwamba Iran inatekeleza makubaliano hayo.
Rais Trump tayari amethibitisha mara mbili .
Uvumi kwamba rais Trump huenda akakataa kuthibitisha kwamba Iran inatekeleza makubaliano hayo umezua hofu miongoni mwa washirika wa Marekani pamoja na maafisa wa utawala wake.
Waziri wa Ulinzi James Mattis aliambia kikao cha bunge la Seneti mapema mwezi huu kwamba sio lengo la taifa la Marekani kusita kuunga mkono mkataba huo.
Rais Trump ameutaja mkataba huo kuwa mbaya zaidi na kuonya kuufutilia mbali.