Friday, October 13

Marekani yaitaka Uturuki kuwasilisha ushahidi wake dhidi ya raia wa Marekani.

Marekani inaitaka serikali ya Uturuki kuwasilisha ushahidi wa kutetea shutuma zake ilizotumia kuelezea kukamatwa kwa wafanyakazi wa ubalozi mdogo wa Marekani na raia kadhaa wa Marekani akiwemo mchungaji wa kimarekani aliyefungwa jela Andrew Brunson.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Heather Nauert aliwaambia waandishi wa habari kwamba Marekani haijaona ushahidi wowote kuhusiana na hilo na iliitaka Ankara kutekeleza ahadi yake ya kuwaruhusu watu waliokamatwa kuonana na mawakili wao.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Rex Tillerson.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Rex Tillerson.
Wakati huo huo waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson alizungumza na waziri wa mambo ya nje wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu na kumuelezea wasi wasi wa Washington juu ya kukamatwa kwa watu hao. Haya ni mazungumzo ya simu ya mara ya pili chini ya muda wa wiki moja kati ya wanadiplomasia hawa wawili wa cheo cha juu katika ushirika wa NATO.
Uhusiano kati ya Uturuki na Marekani umekuwa wa mashaka kufuatia kukamatwa wiki iliyopita mfanyakazi wa ubalozi mdogo wa Marekani huko Uturuki Metin Topuz kwa mashtaka ya ugaidi na uhaini katika uhusiano na jaribio lililoshindikana la mapinduzi la mwaka jana dhidi ya Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan.

No comments:

Post a Comment