Friday, October 13

Ghana kuangalia upya sheria za wanyama pori kutokana na biashara haramu ya Kakakuona

Ghana italazimika kuangalia upya sheria zake za wanyamapori kutokana na biashara ya Kakakuona ambayo imekithiri mno. Hali hii imesababishwa na hofu ya kwamba nchi hiyo inatumiwa kuendesha biashara hiyo haramu.

Schuppentier - Manidae (picture-alliance/AP Photo/Firdia Lisnawati)
Wito umetolewa kwa taifa hilo kuangalia upya sheria zake juu ya uhalifu wa wanyamapori, kutokana na hofu ya kuwa nchi ya Ghana imekuwa ikitumiwa kama njia ya kusafirisha bidhaa kwajili ya biashara hiyo haramu ya kakakuona.
Zaidi ya kilo 31,000 ya magamba ya Kakakuona zimenaswa kote duniani mwaka huu, kulingana na shirika la kimataifa la ustawi wa wanyama, IFAW.
Mnamo mwezi Mei na Juni shehena mbili kubwa zilinaswa nchini Malaysia na angalau kilo 700 zilipatikana zikiwa zimesafirishwa kupitia Ghana. Shehena nyengine kubwa zilikamatwa pia nchini Uganda, Camerron na Ivory Coast.
Mark Hofberg kutoka shirika la IFAW amesema magamba mengi kutoka kwa mnyama huyo kutoka Afrika imeuzwa ili kufikia mahitaji yake katika bara la Asia, ambako hutumiwa katika dawa za jadi.
Kakakuona anapatikana sana katika nchi za Afrika na kusini mashariki mwa Asia.
Aina mbili kati ya nane ya mnyama huyo wameorodheshwa kuwa hatarini kwenye orodha nyekundu ya aina ya wanyama walio hatarini.
Kwa mujibu wa bwana Hofberg, kuongezeka kwa kamatakamata ya mizigo hiyo kunaweza kuwa ishara kuwa mamlaka husika zinalichukulia suala hili kwa uzito lakini amesema nchi nyingi hazina sheria kali za kuadhibu wafanyabiashara haramu.
"Kwa biashara hii kupungua kwa kiasi kikubwa, kunahitajika adhabu na hukumu kali," aliiambia shirika la habari la AFP.
Kakakuona ni mnyama aliyehifadhiwa nchini Ghana lakini mkuu wa tume ya Wanyamapori wa Ghana, Nana Kofi Adu-Nsiah, amesema sheria kali inahitajika.
Sheria zilizopo za ulinzi wa wanyamapori zilipitishwa katika miaka ya 1960 na tume hiyo inataka ziangaliwe upya ili kufikia viwango vya kimataifa.
Watu watatu walikamatwa nchini Ghana kuhusiana na mizigo iliyonaswa mwezi Juni nchini Malaysia.
Schuppentier - Manidae (picture-alliance/Photoshot)
Kakakuona
Viongozi wa Serikali wanaamini sheria mpya zitazuia Ghana kutumiwa kuwa hatua ya usafiri kwa wanyama hao wanaosafirishwa lakini pia kuna wasiwasi pia juu ya uwindaji wa ndani wa kakakuona.
Katika barabara kuu nyingi nchini Ghana, watu wanaonekana wakimuuza mnyama huyu, ambaye hushikwa juu chini, kutoka mkiani.
Wanyama hao ambao wana ukubwa wa sentimita 30 hadi 100 wanaweza kuuzwa kwa karibu dola 45 au euro 38. Na wale wawauzao kwa kawaida ni watu masikini. Maofisa wa Tume ya Wanyamapori wanamkamata mtu yeyote anayemuuza mnyama huyu lakini Bwana Adu-Nsiah alipendekeza suluhisho la kuwaokoa wanyama hao kwa njia ya kuwanunua wakiwa hai kutoka kwa wauzaji na kuwatengea makazi mbadala.
Haijulikani ni wangapi wanaoishi porini huko Ghana lakini makazi yao yameathiriwa na ukataji miti na maendeleo. Hali hiyo pia huwafanya wanyama hao kuwa mawindo rahisi na kusababisha kuwa wanyama wanaosafirishwa kwa wingi ulimwenguni.
"Sio wanyama ambao wanaweza kukimbia kwa haraka ili kujilinda," anasema bwana Abu-Nsiah.
Watafiti wamegundua kuwa kakakuona anatumika kwajili ya chakula na magamba yake yanatumiwa kwajili ya viungo. Jamii mbali mbali vijijini katika taifa la Ghana wanahamasishwa kuhusu umuhimu na uhifadhi wa Kakakuona ambaye yuko hatarini ya kuangamia na kupotea katika taifa hilo.

No comments:

Post a Comment