Mahakama Kuu nchini Uganda imeamrisha kuwa kila mshukiwa wa mauaji ya aliyekuwa msemaji wa polisi Andrew Felix Kaweesi alipwe fidia ya Shilingi milioni 80 kutokana na uvunjifu wa haki zao za kibinadamu.
Jaji Margret Oguli Alhamisi ameitaka serikali ilipe shilingi milioni 80 na riba ya asilimia 20 kwa kila mshukiwa ambao ni watu 23 kwa sababu vyombo vya magereza vilihusika na uvunjifu wa haki zao kwa kuwatesa wakati wakiwa rumande.
“Wanaofikishwa mahakamani bado ni washukiwa mpaka pale watakapopatikana na makosa. Na ilikuwa ni wajibu wao kuwatendea haki bila ya kuwatesa,” amesema Jaji.
Kwa mujibu wa Jaji, kulikuwa na ushahidi wa kutosha kuonyesha kwamba vyombo vya magereza vilikuwa vinaficha kitu walipokataa washukiwa hao kupatiwa matibabu.
Hili linafuatia maombi yaliyoletwa na wakili wa washukiwa hao Ladislaus Rwakafuzi akiitaka mahakama iilazimishe serikali kuwapeleka wakapimwe hospitali ili kuthibitisha sababu zilizopelekea kuwa na majeraha.
Washukiwa hao waliiambia mahakama kuwa walikamatwa wakiwa majumbani mwao na kinyume cha sheria wakazuiliwa katika rumande ya kijeshi kabla hawajapelekwa kwenye kituo cha polisi cha Nalufenya, Wilaya ya Jinja kinachojulikana kwa mateso makali.
Pia washukiwa hao waliiambia mahakama kwamba hawakupatiwa huduma yoyote ya tiba kutokana na majeraha walioyapata wakati wa mateso hayo.
Kaweesi alipigwa risasi akiwa na mlinzi wake na dereva Machi 17 mwaka huu wakati akitoka nyumbani kwake katika eneo la Kulambiro.
Washambuliaji waliokuwa na bunduki waliondoka na bastola yake na ya mlinzi wake.
Washukiwa wengi walikamatwa na kuwekwa rumande lakini walipoletwa mahakamani wengi wao walikuwa na majeraha ambayo walidai yalisababishwa na mateso walioyapata kutoka kwa maafisa wa ulinzi.
No comments:
Post a Comment