Monday, November 27

SINTOFAHAMU UCHAGUZI WA MADIWANI


*Chadema yasusia Arumeru Mashariki, *CCM yashinda kat zote Arusha, *NEC yasema dosari hazikuathiri uchaguzi

NI uchaguzi wa vurugu. Ndivyo unaweza kusema baada ya kuripotiwa baadhi ya matukio ya fujo yaliyotekelezwa na watu wasiojulikana huku mawakala wa vyama vya upinzani wakitolewa kwenye baadhi ya vituo vya kupigia kura.
Maeneo yaliyoripotiwa kukumbwa na vurugu wakati wa uchaguzi mengi yako Mkoa wa Arusha ambako Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuliwataka wagombea wake wa udiwani katika kata zote za Wilaya ya Arumeru kujitoa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema Chadema kinajitoa kwenye uchaguzi wa kata Tano za Jimbo la Arumeru Mashariki huku kikieleza macho kwenye kata 38 zilizobaki.
Mbowe alidai uchaguzi huo wa marudio ulikuwa na matukio ya ukatili na mashambulizi waliyofanyiwa baadhi ya viongozi na wanachama wa Chadema.
Aliwataka vijana wa chama hicho kujitetea wanaposhambuliwa na polisi badala ya kusubiri tamko la chama.
Mbowe alizitaja kata zilizojitoa kuwa ni Ngabobo, Leguruki, Makiba, Maroroni na Mbureni.
“Nimewasiliana na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhani Kailima ameniambia yuko Tunduru, mambo haya viwango vinatofautiana. Katika hatua ya sasa tumejitoa katika kata tano hizi na tutaendelea kuangalia katika kata nyingine 38 zilizobaki, lakini tunafuatilia kwa karibu matukio haya.
“Kuna matukio mengi ya polisi kuumiza watu na sisi tunachelea kuruhusu vijana wetu kutoka kupiga watu kwa sababu hatuna sababu ya kupiga raia wetu wanapokwenda kutekeleza wajibu wao.
“Lakini tunapenda kuwaambia vijana wetu popote walipo wasikunje uso wanapoendelea kupigwa au wanapofanyiwa mashambulizi basi wajitetee, watafute utaratibu wa kujitetea wasisubiri tamko la chama, wajitetee kunusuru maisha yao,” amesema Mbowe.
Mbowe alisema mambo hayo yana mwisho wa uvumilivu kwa sababu vyombo vya dola vinatumika vibaya huku polisi wakishuhudia.
“Kamanda Mkumbo (Charles Mkumbo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa arusha) anajua yote haya, kama hajui hastahili kuwa ofisini lakini vijana wake ndiyo wanaongoza vijana wa ‘green guard,’ wanapiga watu, wanaumiza, wanakata mapanga, wanateka watu wanateka vuongozi.
“Arumeru hakuna uchaguzi kuna upumbavu na upuuzi ni fujo tu na zimasimamiwa na vyombo vya dola. Sisi kwa hali hii inayoendelea Arumeru tunawaagiza viongozi wetu wa chama na madiwani wetu haraka sana wajitoe.
“Mawakala wetu ambao wamekuja vituoni mchana huu waondoke wote waachanae na uchaguzi huu wa kikatili, tuwaachie wao waendelee na viongozi wote Chadema wasiende kwenye majumuisho ya kura hizi ambazo haziakisi maamuzi ya wanachi ama utashi wa wananchi,” alisema Mbowe.

Mgombea ageuka wakala

Mgombea udiwani wa Kata ya Mamba Wilaya ya Lushoto, Jafari Ngede (Chadema),  alilazimika kuwa wakala mwenyewe baada ya mawakala kutolewa katika vituo 13.
“Mimi Mgombea Udiwani Jafary Ndege, Kata ya Mamba Mawakala wangu wote katika vituo 13 vyote wameondolewa na kupelekwa Polisi mida ya saa 4:00 asubuhi.
“…na imenibidi nikae katika kituo kimoja wapo kama wakala na polisi wamekuja kunitishia hapa kuwa niache kiherehere,” alisema Ndege.

MKOA WA SONGWE
Mwandishi wetu Eliud Ndondo anaripoti kutoka Songwe kuwa, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Momba, Methew Kikoti (CCM) na Mbunge wa Momba, David Silinde (Chadema), jana walitunishiana misuli.
Tukio hilo lilitokea jana katika kituo cha kupigia kura cha Shule ya Msingi Kakozi, Kata ya Ndalambo wakati wa uchaguzi mdogo wa udiwani.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, mzozo ulianza baada ya Silinde kumuona Kikoti akitoka kwenye chumba kimoja cha kupigia kura na kuingia chumba cha pili.

Ilielezwa kuwa Silinde alimuuliza mwenyekiti huyo kwanini aliingia kwenye chumba cha kupigia kura wakati hairuhusiwi.
Kwamba baada ya swali hilo walianza kurushiana maneno ya kejeli na kashfa.
Majibishano baina ya Silinde na Kikoti yalikuwa hivi;
Silinde: Wewe Kikoti nani kakuruhusu kuingia kwenye chumba cha kupigia kura?
Kikoti: Nimeingia ili kuwaona mawakala wangu hivyo sina kosa lolote.
Silinde: Hujui kuwa ni kosa kuingia kwenye chumba cha kupigia kura wakati wewe siyo mhusika?
Kikoti: Mimi ndiye Mwenyekiti wa Halmashauri, ninapaswa kuangalia zoezi linavyofanyika na siyo vinginevyo.
Silinde: Mimi ndiye niliyechanguliwa na wananchi wa jimbo hili, lakini siruhusiwi kuingia, kwanini wewe uliyechaguliwa na madiwani uingie ndani ya chumba cha uchaguzi?
Kikoti: Waliopaswa kuniuliza maswali hayo ni wasimamizi siyo wewe ambaye ni sawa na mimi.
Silinde: Ndiyo maana mwenyekiti mzima hujui kusoma hata taratibu za uchaguzi huzifahamu.
Kikoti: Uliyesoma ungekuwa na busara hata ya kumuuliza mwenzako na siyo kuropoka maneno yasiyokuwa na maana kwenye uchaguzi.
Pamoja na majibizano hayo, Silinde aliwaagiza mawakala wa chama chake kuhakikisha wanajaza fomu za Kikoti kuingilia mwenendo wa uchaguzi.
Wakati huo huo, mgombea wa CCM, Flovian Sichzyan, alitangazwa mshindi kwa kupata kura 1402 dhidi ya Mgombea wa Chadema, Michael Kuyange, aliyepata kura 1298.
IRINGA
Mkoani Iringa katika Kata ya Kimara, wanachama kadhaa wa Chadema akiwamo Katibu wa Baraza la Wanawake wa chama hicho (Bawacha), Grace Tendega, walikamatwa na Jeshi la Polisi.
Wengine waliokamatwa ni  Diwani wa Kata ya Ikula, Raymond Francis aliyedaiwa kufanya kampeni kinyume cha taratibu, Frank Nyarusi ambaye ni Mwenyekiti wa madiwani wa Chadema Mkoa wa Iringa, na madiwani wengine watatu na viongozi wanne wa Chadema ambao majina hayakupatikana.
Tendega na wenzake walikamatiwa katika Kijiji cha Muhanga waliokuwa wameweka kambi yao.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Diwani wa Kata ya Nyalumbu, David Mfugwa (Chadema), alisema wanachama wenzake hao walikamatwa jana majira ya saa sita mchana na kupelekwa katika Kituo cha Polisi Kilolo kwa madai kwamba gari lao lilikwaruza gari la CCM, aina ya Land Cruiser.
“Inasemekana baada ya dereva wetu kukwaruza gari la CCM, alikimbia akaenda kujificha katika kambi yetu iliyokuwa na viongozi hao. Kwa hiyo, polisi walipofika ili kumkamata deerva huyo, aliwakamata na wengine waliokutwa mahali hapo,” alisema Mfungwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Julius Mjengi, alipozungumza na MTANZANIA kwa simu yake ya kiganjani alisema hana taarifa za kukamatwa kwa viongozi hao na kuahidi kufuatilia.

MOROGORO

Mkoani Morogoro katika Kata ya Sofi, Wilaya ya Malinyi, watu 11 wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Chadema, walimakatwa akiwamo mgombea udiwani wa chama hicho, Riko Venance.
Akizungumza na MTANZANIA kwa simu jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Urlich Matei, alisema watu hao walikamatwa jana asubuhi wakati wakijindaa kufanya vurugu katika vituo vya kupigia kura.
“Kwa hiyo bado tunaendelea kuwahoji na watakapobainika kuwa na makosa basi tutawafikisha katika vyombo vya sheria.
Katibu wa Chadema Mkoa wa Morogoro, Samuel Kitwika, aliliambia MTANZANIA kuwa waliokamatwa walikuwa wakikagua vituo vya kupigia kura na mawakala wao.
“Kwa mfano, Mgombea Riko Venance alikamatwa wakati akitembelea vituo kuona uwepo wa mawakala wake na mwenendo mzima wa uchaguzi,” alisema .

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Sudi Mpili, alisema uchaguzi katika Kata ya Kiloka, ulifanyika kwa utulivu na kukamilika saa 10: 28.

Alisema, awali kulitokea malalamiko katika baadhi ya vituo ambako mawakala walibadilishwa na kusababisha hali ya kutoelewana kwa vyama vilivyokuwa na wagombea.

“Lakini, baadaye kasoro hizo zilitatuliwa kwa mawakala wengine kuapishwa na uchaguzi ukaendelea kama kawaida,” alisema Mpili.

MKOA WA MBEYA

Mkoani Mbeya katika Kata ya Ibigi, wilayani
Rungwe, uchaguzi huo ulifanyika katika hali ya amani na utulivu

Katika kata hiyo, baadhi ya wabunge wa Chadema akiwamo Joseph Mbilinyi maarufu kwa jina la Sugu na Mbunge wa Viti Maalum, Sofia Mwakagenda waliweka kambi katika kata hiyo kuangalia mwenendo wa uchaguzi.

Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Rungwe, Sam Mwakapala hakupatikana kuzungumzia uchaguzi huo baada ya simu yake kuita bila kujibiwa.

Kata ya Ibighi
Katika Kata ya Ibighi wilayani Rungwe, Chadema imefanikiwa kutetea kiti chake babada ya mgombea wake, Goffrey Mwakajoka kupata kura 1436 dhidi ya 1205 za mpinzani wake, Suma Fyandomo wa CCM.

KILIMANJARO

Wilayani Hai, Mkoa wa Kilimanjaro katika Kata ya Machame Magharibi  iliripotiwa kuwa uchaguzi ulifanyika katika hali ya utulivu.

Hata hivyo taarifa zilisema katika vituo vya kupigia kura kulikuwa na wapiga kura wachache tofauti na ilivyotarajiwa.

Matokeo yaliyofikia MTANZANIA jana kutoka Kata ya Machame yalionyesha kuwa mgombea wa CCM, Martine Munisi alishinda kwa kura 1058 dhidi ya Mgombea wa Chadema, Elibariki Lema aliyepata kura 590.

Katika Kata ya Weluwelu, Swalehe Msengesi wa CCM alitangazwa mshindi kwa kupata kura 1454 dhidi ya kura 716 alizopata Mgombea wa Chadema, Moses Kalaghe.

Kata za Mnadani na Bomang’ombe, Manispaa ya Moshi,  hadi tunakwenda mitamboni matokeo yalikuwa hayajatangazwa ingawa wagombea wa CCM waliripotiwa kuongoza.

MKOA WA SINGIDA

Taarifa zinasema uchaguzi ulifanyika katika Kata ya Siuyu, Jimbo la Singida Mashariki katika hali ya amani na utulivu.

Hadi tunakwenda mitamboni taarifa zilieleza kuwa wagombea wa CCM na Chadema walikuwa wakichuana kwa karibu.

MKOA WA TANGA

Katika Kata ya Majengo wilayani Korogwe, Msimaizi wa Uchaguzi, Jumanne Shauri, alimtangaza Mgombea wa CCM, Mustafa Shengwatu kuwa mshindi baada ya kupata kura 583 dhidi ya kura 22 alizopata Mgombea wa Chadema, Abas Chomboka.

Mwandishi wetu kutoka mkoani Tanga anaripoti kuwa katika Kata ya Mamba Jimbo la Bumbuli, mgombea wa CCM alishinda kwa kupata kura 1373 dhidi ya kura 700 alizopata mgombea wa Chadema.

MKOA WA MTWARA

Mwandishi wetu kutoka Mtwara anaripoti kuwa katika Kata ya Milongodi wilayani Tandahimba mgombea CCM, Manzi Livedo alipata kura 827 dhidi ya kura 819 za mgombea wa CUF, Juma Mgawa huku Selemani Likome wa ACT akiambulia kura 2.

Taarifa zilizopatikana kutoka Masasi, Kata ya Chanikanguo zilieleza kuwa mgombea wa CCM alishinda kuwa kupata kura 928, CUF 36 huku mpinzani wake wa ACT Wazalendo kura 10.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Masasi, Mkoa wa Mtwara, Gimbana Ntavyo zaidi ya watu  3316  walijiandikisha lakini hadi majira ya mchana waliokuwa wamejitokeza kupiga kura ni 1727.

Taarifa hiyo ilieleza kuwepo kwa changamoto kadhaa  ikiwemo ya mawakala wa vyama vya siasa kutopewa utaratibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kusababisha watake kufanyakazi za wasimamizi walioandaliwa na Tume.

Matokeo ya awali yaliyolifikia MTANZANIA kutoka Kituo cha Mailisita yalionyesha mgombea wa Chadema alipata  kura 155, CCM 89, na CUF 03 na ACT haikuambulia kitu.

MKOA WA DODOMA

Taarifa kutoka Mpwapwa katika Kata Chipogoro zilionyesha  kuwa matokeo ya awali kwenye Kituo cha Zahanati namba 3 , Hosea Fweda wa CCM alipata kura 129 huku Jafari Simba wa Chadema akiwa na kura 103.
Kituo cha Zahanati namba 2, Hosea Fweda wa CCM alipata kura 131 na  Jafari Simba  wa Chadema alipata 91 na kituo cha Zahanati namba moja, mgombea huyo wa CCM alikuwa akiongeza kwa kura 109 dhidi ya 94 za yule wa Chadema.
Wakati huo huo, mwandishi NORA DAMIAN anaripoti akiwa Dar es Salaam kuwa  Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), jana ilieleza kuwa licha ya kuwapo kwa changamoto ndogondogo katika maeneo mengi uchaguzi umefanyika kwa amani.
Akizungumza jana na MTANZANIA, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhan Kailima alisema kasoro chache zilijitokeza mkoani Arusha na kusababisha kuondolewa kwa baadhi ya mawakala katika kata tatu.

“Changamoto haziwezi kukosekana hali iko vizuri ukiondoa kasoro chache zilizojitokeza Arusha, hata kwenye familia kama una watoto lazima watatokea wawili watakosana.

“Arusha wabunge waliwaondoa baadhi ya mawakala kwenye kata tatu lakini walikuwa wanaendelea na uchaguzi,” alisema Kailima.

Alifafanua kuwa kiutaratibu kila wakala lazima awe na barua ya chama, fomu ya kiapo namba sita barua ya msimamizi ya kumtambulisha kuwa wakala.

“Kama Bumbuli (Tanga) kuna watu waliapishwa kama mawakala lakini leo asubuhi (jana) wamekwenda watu wengine,” alisema Kailima.
Mkurugenzi huyo pia alikiri kutokea kwa vurugu katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Mwanza na kutadharisha kuwa watu wasikimbilie kufanya fujo na kama kuna mambo yamekiukwa wafuate taratibu za kisheria.
“Tuanze kujihurumia na kuihurumia nchi yetu, tujiulize tunafanya vurugu kwa faida ya nani? alihoji Kailima.

Papa Francis afanya ziara nchini Myanmar

Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani, Papa Francis, amewasili Myanmar (27.11.2017) wakati taifa hilo likikabiliwa na kipindi kigumu kutokana na ukosoaji mkubwa na jumuiya ya kimataifa kwa kuwatimua Rohingya.

Myanmar Ankunft Papst Franziskus (Reuters/M. Rossi)
Waumini wa kanisa Katoliki waliovalia nguo za kitamaduni walipererusha bendera na kucheza katika uwanja wa ndege wa mji mkuu Yaongon kumkaribisha kwa furaha papa Francis, anayefanya ziara ya kwanza kabisa nchini Myanmar kuwahi kufanywa na kiongozi wa kanisa hilo.
Ziara hiyo inakuja wakati jeshi la Myanmar likikabiliwa na ukosoaji kwa kuendesha kampeni ya mauaji dhidi ya Waislamu warohingya. Zaidi ya Warohingya 620,000 wamekimbia ukandamizaji na mauaji katika jimbo la kaskazini la Rhakhine na kutafuta hifadhi nchini Bangladesh katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.
Ziara ya siku nne ya papa Francis inaongeza shinikizo kwa Myanmar kuhusu jinsi inavyowatendea watu wa jamii ya wachache ya Rohingya ambao hawana uraia, kundi ambalo ameliita mara kwa mara "ndugu na dada" ili kupunguza makali ya madhila yanayowakabili.
Hotuba za kiongozi huyo mkuu wa kanisa Katoliki zitafuatiliwa kwa karibu na waumini wa madhehebu ya Budha wenye misimamo mikali iwapo neno Rohigya litatajwa, neno linalotumiwa katika nchi ambako kundi hilo la waislamu linadharauliwa na kutukwanwa na kuitwa Wabengali - wahamiaji wasio halali kutoka Bangladesh.
Matumaini ya amani
Wakimbizi wa jamii ya Rohignya katika kambi ya Kutupalong, kusini mwa Bangladesh wanasema wana matumaini makubwa ziara ya Papa Francis nchini Myanmar na Bangladesh itasaidia kuleta amani. Mohammed Nadir Hossain, mkimbizi kutoka mji wa Buthidaung nchini Myanmar, alisema, "Ataiona hali yetu ya kusikiisha na tuna matumaini ataelewa tutakachomueleza. Akitaka anaweza kuituliza serikali ya Myanmar na kuleta amani kwa kuzungumza nasi. Tunateseka sana kwa sasa. Tuna wasiwasi. Kwa hiyo tunashukuru sana kwamba anazuru nchini mwetu."
Senu Ara, ni mkimbizi kutoka Myanmar aliyekimbilia nchini Bangladesh mwezi Septemba mwaka huu, naye alisema, "Tunatumai kutakuwa na amani. Nadhani huenda akatusaidia kurejea nchini mwetu kwa amani. Anaweza kutusaidia kupata amani ambayo tunaitafuta kwa udi na uvumba. Hata tukibaki hapa, ataibadili hali yetu kuwa nzuri. Akiamua kuturudisha nyumbani, atafanya hivyo kwa njia ya amani." 
Myanmar Ankunft Papst Franziskus (Reuters/M. Rossi)
Papa Francis atakutana na kiongozi wa Myanmar, Aung San Suu Kyi, mshindi wa zamani wa tuzo ya amani ya Nobel, ambaye heshima na hadhi yake imeshuka kwa sababu ya kushindwa kwake kuzungumzia hadharani kuwatetea Warohingya.
Baba Mtakatifu Francis pia atafanya mazungumzo na mkuu wa majeshi, Min Aung Hlang, mkutano kati ya kiongozi wa kidini ambaye amekuwa akitetea haki za wakimbizi na mtu ambaye anatuhumiwa kwa kusimamia kampeni ya kuwatimua Warohingya kutoka Myanmar. 
Ziara ya Papa Francis ni fursa ya kihistoria kwa waumini wa kanisa Katoliki nchini Myanmar kumkaribia kiongozi wa kanisa lao. Waumini 700,000 wa kanisa hilo ni jumla ya asilimia moja ya wakazi milioni 51 wa Myanmar na wametawanyika katika pembe mbalimbali za taifa hilo, wengi wakikabiliwa na mizozo.
Takriban waumini 200,000 wa kanisa Katoliki wanamiminika mji mkuu Yangon kwa ndege, treni na magari kuhudhuria misa kubwa ya hadhara itakayofanyika siku ya Jumatano.

MIMBA ZA UTOTONI TISHIO WILAYANI MPANDA

MIMBA za utotoni bado ni tishio kubwa  katika Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi ambako wasichana  624 walio na umri wa chini ya miaka 18, wamejifungua   katika  vituo vya  afya  vilivyopo katika  manispaa hiyo.
Hayo yalisemwa  hapo  jana  na Mkuu wa  Mkoa wa  Katavi, Meja Jenerali  mstaafu, Raphael  Muhuga, wakati wa  uzinduzi  wa kampeni  ya  siku  16 za kupinga ukatili  wa  kijinsia   zilizofanyika  viwanja  vya Sabasaba  Kabungu  wilayani  Tanganyika.
Meja Jenerali Muhuga alisema  taarifa   kutoka  katika  vituo vya  afya  vya Manispaa ya  Mpanda  ya kipindi cha mwaka jana inaonyesha wasichana 624 wenye  umri wa chini ya  miaka 18 walijifungua  katika  vituo   vya afya vilivyopo  katika  manispaa  hiyo na kwamba kiwango hicho ni kikubwa na ni tishio.
Alisema  utafiti  wa  afya  ya uzazi  na  mtoto  na  viashiria  vya  maralia   wa mwaka   2015/16 uliofanywa  na Ofisi ya  Taifa ya Takwimu (NBS)  kwa  kushirikiana  na   Wizara  ya  Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na  Watoto umeonyesha  Mkoa wa  Katavi  unaongoza kitaifa kwa tatizo hilo.
Alisema utafiti  huo umeonyesha  kitaifa kuwa  asilimia 27 ya  wasichana  wa   miaka   15   hadi 19 wameishaanza  uzazi, huku asilimia 21 wakiwa wamezaa  mtoto hai angalau mmoja, huku  Mkoa wa   Katavi asilimia  45 ya   wasichana   wenye umri wa   miaka 15   hadi  19  tayari ni wazazi.
Kuhusu unyanyasaji wa  kijinsia, alisema kesi  1,178 ziliripotiwa  katika vituo  vya kutolea  huduma  za   afya mkoani humo na maofisa ustawi wa jamii mwaka   2016.
Alisema kati ya kesi hizo, kesi 401 zilihusu ukatili wa  kimwili , 66 zilihusu  ukatili wa  kingono, 264 zilihusu  ukatili  wa  kisaikolojia  na  447 zilihusu kutelekezwa watoto na familia zao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya  Mpanda, Liliani Matinga,   aliwataka wanawake ambao  wana tabia ya kupiga waume zao  waache  tabia hiyo mara moja kwa kuwa inawaaibisha wanawake wote nchini.
Naye Kamanda wa Polisi wa  Mkoa  wa Katavi, Damas  Nyanda, alisema licha ya jitihada zinazochukuliwa  na  Serikali  kwa kushirikiana  na  makundi  mbalimbali  ya kijamii, takwimu  bado  zinaonyesha  ongezeko  la ukatili  wa kijinsia.
Alisema ongezeko hilo linachangiwa  na changamoto zifuatazo  ambazo ni  imani za kishirikina, mila  na desturi  za  baadhi ya makabila, umasikini,  elimu na ukosefu wa  nyumba  salama, ambapo  baadhi ya wazazi  wamekuwa wakiwalaza wageni wao na  watoto wao na kusababisha  wageni hao kuwafanyia vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia.

Mgombea wa Chadema aeleza kilichosababisha awekwe chini ya ulinzi


Morogoro. Mgombea udiwani kwa tiketi ya Chadema katika Kata ya Sofi wilayani Malinyi mkoani Morogoro, Riko Venance ambaye aliwekwa chini ya ulinzi kwa takribani saa moja amesema polisi walifanya hivyo baada ya kuhoji sababu za mwananchi mmoja kuzuiliwa kupiga kura.
Alizungumza na Mwananchi leo Jumapili baada ya kuachiwa amesema alipofika katika kituo cha kupigia kura cha Shule ya Msingi Mission alipata malalamiko toka kwa mmoja wa wapiga kura aliyejulikana kwa jina moja la Akwilina kwamba amezuiliwa kupiga kura.
“Nilikuwa nahoji kwa nini Akwilina azuiliwe kupiga kura na ndipo nilipoambiwa nasababisha vurugu na kuwekwa chini ya ulinzi," amesema Venance.
Amesema mpiga kura huyo alipoulizwa jina alisema anaitwa Akwilino wakati kwenye kadi imeandikwa Akwilina na hapo ndipo utata ulipoanzia, hata hivyo baadaye aliruhusiwa kupiga kura.
Mgombea huyo ambaye anaendelea kutembelea vituo tayari ameshatembelea vituo 10 kati ya vituo 21 vya kupigia kura vilivyopo katika kata hiyo.

CHUO CHA USIMAMIZI WA WANYAMAPORI-MWEKA KUANZA KUTOA MAFUNZO MAALUM KWA WATOA HUDUMA ZA UTALII NCHINI

Katika kutimiza azma ya Serikali kuboresha huduma za ukarimu kwenye sekta ya utalii nchini, Wizara ya Maliasili na Utalii imekichagua Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka kilichopo mkoani Kilimanjaro kwa ajili kutoa mafunzo maalum kwa waongoza watalii nchini. 
Mafunzo hayo ambayo yanatarajiwa kuanza kesho (Jumatatu) chuoni hapo yatakuwa kwenye mfumo wa kujiendeleza na yamelenga kuwawezesha watoa huduma katika sekta hiyo kupata sifa za kusajiliwa na kupewa leseni ya kuendelea kutoa huduma hiyo kwa mujibu ya sheria ya utalii Na. 11 ya mwaka 2008 kifungu cha 48.
Hayo yamesemwa jana na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga katika mahafali ya 53 ya kuwatunuku vyeti wahitimu 224 wa chuo hicho katika kozi mbalimbali ikiwemo Shahada, Stashahada na Astashada kwenye Usimamizi wa Wanyamapori na Utalii.
"Katika kutambua utaalamu na uzoefu wa chuo chenu, Wizara yangu imeichagua Mweka kutoa mafunzo yatakayowawezesha waongoza watalii nchini kupata sifa ya kusajiliwa (cheti) na kupewa leseni," alisema Naibu Waziri Hasunga.
"Nimefurahi kusikia kuwa  mmeshajipanga tayari kuanza kutoa mafunzo hayo baada ya kufanya tathmini ya mahitaji ya mafunzo na kuainisha mapungufu kwenye taaluma, ujuzi na mitazamo pamoja na kuandaa mtaala wa mafunzo hayo.

"Nitoe wito kwa waongoza watalii  nchini wajisaji ili wapate mafunzo haya muhimu kwakua katika miaka michache ijayo hawataruhusiwa kutoa huduma hiyo bila kutimiza masharti haya ya kisheria,” alisema Hasunga.

Alisema tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa watalii wengi wanaokuja nchini hupata taarifa kutoka kwa wenzao waliotembelea Tanzania ambao muda wao mwingi wanakuwa na waongoza watalii kwenye maeneo ya vivutio.

"Hivyo ni muhimu wapewe mafunzo  maalum waweze kutoa huduma bora zaidi zitakazowafanya watalii wafurahie ukarimu wao waweze kuwa mabalozi wazuri wa kuutangaza utalii wetu watakaporudi nchini kwao" alisema  Hasunga. 

Alisema licha ya Sekta ya utalii nchini kuchangia asilimia 17 ya pato la taifa na asilimia 25 ya fedha za kigeni (watalii milioni 1.28 na bilioni 2 mwaka 2016), mchango wake unaweza kukua zaidi kupitia mikakati mbalimbali inayowekwa  na wizara yake ikiwemo hiyo ya mafunzo ambayo imelenga kuongeza idadi ya watalii kufikia milioni mbili mwaka 2020 na watalii milioni 8 mwaka 2025 pamoja na mapato ya dola za kimarekani bilioni 20 mwaka 2025.
Akizungumzia kuhusu mafunzo ya jeshi usu chuoni hapo, Naibu Waziri Hasunga aliuagiza uongozi wa chuo hicho kuendesha mafunzo hayo muda wote wa masomo tofauti na ilivyo hivi sasa ambapo hutolewa kwa wiki mbili katika kila 'semister'.
"Mafunzo haya yasiishie tu kwa muda wa wiki mbili, ni matarajio yangu kuona yanaendeshwa katika kipindi chote cha mafunzo ikiwemo wanafunzi kuvaa sare za heshima za jeshi usu, kuwa na nidhamu ya kijeshi na muhimu zaidi kuonyesha utayari na uwezo wa kukabiliana na wahalifu ikiwemo majangili," alisema Hasunga.
Aidha, alizitaka taasisi zilizopo chini ya Wizara yake kuajiri wananfunzi wanaomaliza chuoni hapo ikiwa ni pamoja na kutumia fursa ya chuo hicho mahiri kuwaongezea ujuzi wafanyakazi waliopo makazini.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Jafari Kideghesho alimueleza Naibu Waziri Hasunga kuwa Chuo chake kimeshafanya maandalizi yote ya kuanza kutoa mafunzo kwa waongoza watalii nchini kama ilivyoagizwa na wizara yake ambapo tathmini ya mahitaji ya mafunzo hayo imeshafanywa kwa kuainishwa mapungu katika taaluma, ujuzi na mitazamo. 

"Tumeshaandaa pia mitaala ya mafunzo ambayo imezingatia kuondoa mapungufu tuliyoyabaini, na tunatarajia kuanza mafunzo yetu ya kwanza kwa wapagazi 100 kwa muda wiki tatu kuanzia jumatatu ijayo (leo)," alisema Prof. Kideghesho.
Alisema ili kufanikisha mafunzo hayo chuo chake kimepokea msaada wa Shilingi milioni 110 kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa wapagazi wanaotoa huduma katika mlima Kilimanjaro, fedha ambazo zitatumika kwa ajili ya mafunzo na tafiti mbalimbali.
Mahafali hayo ya 53 yalihudhuriwa pia na Balozi wa Nigeria nchini,  Balozi Sahabi Dada, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Chuo hicho, Prof. Faustin Bee, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kippi Warioba, Mkuu wa Wilaya ya Same, Harun Mbogo, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Nebo Mwina, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo na baadhi ya wawakilishi wa Mamlaka ya Wanyamapori ya Uganda.
Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka kilianzishwa mwaka 1963 baada ya azimio la Arusha mwaka 1961 ambalo lilitaka uwepo wa watu waliopewa mafunzo kwa ajili ya kulinda na kusimamia urithi wa rasilimali za Afrika. 
Chuo hicho ambacho huendesha mafunzo yake kwa vitendo kwa zaidi ya asilimia 60 kimepata ongezeko la wanafunzi kutoka 25 mwaka 1963/1964 hadi zaidi ya wanafunzi 550 mwaka 2016/2017 kutoka nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Malawi na Cameroon.
Aidha, katika kipindi cha miaka 54 iliyopita chuo hicho kimeweza kufundisha zaidi ya mameneja wa wanyamapori 8,000 kutoka nchi zaidi ya 50 duniani.

Chuo hicho pia kimepewa tuzo na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kama Kituo cha Ubora wa Taaluma ya Usimamizi wa Wanyamapori (Centre of Excellence).
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (wa tatu kulia) akipata maelezo kutoka kwa Mwanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori-Mweka, Brightone Mbilinyi kuhusu mafunzo ya silaha yanavyotolewa chuoni hapo katika mahafali ya 53 ya chuo hicho yaliyofanyika jana katika wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro. Zaidi ya asilimia 60 ya mafunzo chuoni hapo hutolewa kwa vitendo. Wengine Pichani ni Balozi wa Nigeria nchini, Mhe. Sahabi Dada (wa pili kushoto) na Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Jafari Kideghesho (wa nne kulia).
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (wa pili kushoto) akipata maelezo kutoka kwa mmoja ya Mwanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka, Leonard Mgamba kuhusu mafunzo ya taaluma ya wanyamapori yanavyofanywa kwa vitendo chuoni hapo. Wengine pichani ni Balozi wa Nigeria nchini, Sahabi Dada (wa tatu kushoto), Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Harun Mbogo (kushoto) na Mtenaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu, Prof. Dos Santos Silayo.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) akiwa ndani ya handaki linalotumika kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo katika Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori-Mweka muda mfupi kabla ya kuwatunuku vyeti wahitimu 224 wa kozi mbalimbali chuoni hapo.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) akikagua gwaride la wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori-Mweka muda mfupi kabla ya kuwatunuku vyeti wahitimu 224 wa kozi mbalimbali ikiwemo Shahada, Astashahada na Stashada katika taaluma za usimamizi wa wanyamapori na utalii katika mahafali ya 53 yaliyofanyika chuoni hapo jana katika Wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro. Zaidi ya asilimia 60 ya mafunzo chuoni hapo hutolewa kwa vitendo na wahitimu 224 wa kozi mbalimbali walitunukiwa vyeti.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) akisalimiana na baadhi ya viongozi wa Mamlaka ya Wanyamapori ya Uganda ambao walishiriki kwenye mahafali ya 53 ya Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori-Mweka jana.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka, Prof. Faustin Bee (kulia), Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Mhe. Kippi Warioba (katikati) na Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Harun Mbogo (kushoto) wakiteta jambo wakati wa mahafali ya 53 ya chuo hichao ambayo yalifanyika jana mkoani Kilimanjaro.
Mkuu wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka, Prof. Jafari Kideghesho (kulia) akiwasilisha taarifa fupi kuhusu chuo hicho kwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kushoto) wakati wa mahafali ya 53 ya chuo hicho ambayo yamefanyika jana mkoani Kiliamanjaro. Wengine ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Chuo hicho, Prof. Faustin Bee (wa pili kushoto) na Balozi wa Nigeria nchini, Mhe. Sahabi Dada.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kushoto) akizungumza na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori-Mweka, Prof. Faustin Bee (kulia), Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Mhe. Kippi Warioba (wa pili kulia) na Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Harun Mgogo wakati wa mahafali ya 53 ya chuo hicho ambayo yamefanyika jana mkoani Kilimanjaro. 
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) na Balozi wa Nigeria nchini, Mhe. Sahabi Dada.
Mkuu wa Chuo chaUsimamizi wa Wanyamapori Mweka, Prof. Jafari Kideghesho (kulia) akiteta jambo na Balozi wa Nigeria nchini, Mhe. Sahabi Dada.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Mwanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka, Ebenezer Mollel kuhusu mafunzo ya taaluma ya wanyamapori yanavyofanywa kwa vitendo chuoni hapo. Wengine pichani ni Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Jafari Kideghesho (wa pili kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Mhe. Kippi Warioba.
Sehemu ya taswira ya Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga akipanda mti wa kumbukumbu chuoni hao.
Baadhi ya wanafunzi wa chuo cha Usimamizi ya Wanyamapori Mweka, pembeni yao ni mifupa ya miguu ya tembo katika chumba maalum cha mafunzo ya wanyamapori.
Sehemu ya wananfunzi 224 waliopewa vyeti vya kuhitimu mafunzo mbalimbali katika Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori-Mweka wakiwasili katika viwanja kwa ajili ya mahafali ya 53 yachuo hicho yaliyofanyika jana katika viwanja vya chuo hicho wilayani Moshi Mkoa wa Kiliamanjaro. Vyeti hivyo vilitpolewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga. 
Gwaride la wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka wakitoa heshma mbele ya mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (hayuko pichani)

Naibu Waziri wa Maliasi na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (wa pili kulia) akimtunuku cheti Mhitimu wa Shahada ya Usimamizi wa Wanyamapori, katika Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori-Mweka, Valentina Fiasco ambaye ni raia wa Italia katika mahafali ya 53 yaliyofanyika jana chuoni hapo katika wilaya ya Moshi mkoani Kiliamanjaro. Kulia ni Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Jafari Kideghesho. Jumla ya wahitimu 224 wa kozi mbalimbali walitunukiwa vyeti.
Naibu Waziri wa Maliasi na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (wa pili kulia) akimtunuku cheti mmoja ya wahitimu wa Shahada ya Usimamizi wa Wanyamapori, katika Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori-Mweka wakati wa mahafali ya 53 yaliyofanyika jana chuoni hapo katika Wilaya ya Moshi Mkoani Kiliamanjaro. Kulia ni Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Jafari Kideghesho. Jumla ya wahitimu 224 wa kozi mbalimbali walitunukiwa vyeti. 
 Naibu Waziri wa Maliasi na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (wa pili kulia) akitoa tamko la kuwatunuku kozi mbalimbali wananfunzi 224 wa chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka katika mahafali ya 53 ya chuo hicho ambacho yamefanyika jana mkoani Kilimanjaro. Kulia ni Mkuu wa chuo hicho, Prof. Jafari Kideghesho, Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo hicho, Prof. Faustin Bee (wa tatu kulia) na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Mhe. Kippi Warioba.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo (mwenye tai) na washiriki wengine katika mahafali hayo.

Chui milia auawa kwa kuzurura mjini Paris

Tiger - archive pic
Image captionHaijulikani alitoroka vipi kutoka kwenye sarakasi
Chui milia alitoroka sarakasi na kuzunguka mjini Paris kuisni mwa jengo la Eiffel kabla ya maafisa wanaomshughulikia kumpiga risasi na kumuua.
Polisi walituma ujumbe kwenye twitter kwamba kulikuwa na chui milia anayezurura lakini 'hatari imeondolewa'.
Hakuna aliyejeruhiwa na chui milia huyo mwenye uzito wa kilo 200, kwa mujibu wa taarifa kutoka eneo hilo.
Usafiri wa treni ulisitishwa katika eneo hilo. Wakaazi wakaita maafisa wa huduma za dharura walipomuona mnyama huyo akikimbia mwendo wa saa kumi na mbili jioni kwa saa za huko.
"Alikuwa mkubwa," mwanamume mmoja kwa jina Ralph ameuambia mtandao wa Le Parisien. "Tulisikia milio miwili au mitatu ya risasi na tukaona polisi wakielekea kwenye barabara ya chini."
Aliuawa kichochoroni, msemaji mmoja wa zima moto alieleza.
Mmiliki wake aliyemuua chui milia huyo anazuiwa na polisi shirika la habari la AFP linaripoti kwa kunukuu duru na kuongeza kuwa polisi wameanzisha uchunguzi.
Chui milia huyo alipigwa risasi na mmiliki wakeHaki miliki ya pichaAFP
Image captionChui milia huyo alipigwa risasi na mmiliki wake

Polisi Tanzania yasema miili iliyookotwa bado kutambuliwa

IGP Simon Sirro
Jeshi la polisi nchini Tanzania linaendelea kupeleleza tukio la kuokotwa kwa miili kadhaa katika maeneo mbalimbali, hususan katika jiji la Dar es Salaam.
“Kimsingi bado hakuna mwili hata mmoja uliotambuliwa wala ambaye amefika kutambua," alisema Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Simon Sirro.
Kamanda Sirro amesema hadi sasa hakuna watu waliojitokeza kutambua au kulalamika kwamba wamepoteza ndugu zao.
Taarifa ya jeshi hilo imesema kuwa baada ya watu kujitokeza utaratibu mwingine utaweza kufuatwa ikiwemo upelelezi wa vinasaba (DNA).
Hii inafuatia idadi kubwa ya miili inayookotwa maeneo mbalimbali.
Kwa mujibu wa jeshi la polisi miili hiyo ilikuwa iko kwenye viroba na mingine ikiwa imefungwa mawe makubwa na kamba.
Mkuu wa Jeshi hilo ameeleza changamoto ni kuwapata watu wanaothibitisha kupotelewa na ndugu zao.
Jeshi hilo tayari limetoa taarifa za kuokotwa kwa miili hiyo katika maeneo mbalimbali, hususani katika jiji la Dar es Salaam

"NATO ya Waislam" yazinduliwa Saudi Arabia

Mrithi wa Ufalme Mohammed bin Salman
Ushirika wa majeshi ya Waislam unaongozwa na Saudi Arabia, ambao kamanda wake ni mkuu wa majeshi ya Pakistan mstaafu umeanzishwa rasmi Jumapili huko mjini Riyadh ambapo mawaziri wa ulizindi wa nchi hizo wanakutana katika ufunguzi huo.
Wakati wanaounga mkono ushirika huo wameupa jina la “NATO ya Waislam,” lakini wadadisi pamoja na wale walioko Pakistan, wameendelea kuhoji malengo ya umoja huo na kuangalia kama ni kikundi kilichojikita katika madhehebu dhidi ya wapinzani wao -Mashia wa Iran, Syria na Iraq.
Mrithi wa Ufalme Mohammed bin Salman, ambaye pia ni waziri wa ulinzi wa Saudi Arabia, amefungua mkutano huo wa Umoja wa Majeshi ya Kiislam yanayopambana na ugaidi au kifupi chake IMCTC.
Tamko rasmi limeeleza kuwa “umoja huo wa nchi za Kiislam” ambazo ni 41 za madhehebu ya Kisuni zitaratibu na kugawana majukumu yao mmoja mmoja katika vita vya dunia dhidi ya ugaidi na uvunjifu wa amani uliopitiliza mipaka.
“Mkutano huo [unaofanyika mji mkuu wa Saudia unatimiza ahadi ya kuanzishwa rasmi kwa IMCTC na kuupa nguvu ushirikiano huo na muungano wa nchi wanachama katika ushirika huo,” taarifa hiyo imesema.
Maafisa wa Saudi Arabia walitangaza kuundwa kwa umoja huo mwaka 2015, wenye makao yake makuu Riyadh, ukiwa na lengo la kupambana na ugaidi, na hasa kukabiliana na tishio la kikundi cha Islamic State.
Lakini Tehran imepinga hatua hiyo kutokea mwanzoni kabisa, na imeendelea kuupinga katika duru mbalimbali, ikiamini kuwa lengo la ushirika huo wa Kisuni ni Saudi Arabia kupanua himaya yake katika eneo la Mashariki ya Kati.
Kuundwa kwa ushirika huo umekuwa ukiangazwa katika majadiliano yanayoendelea hasa Pakistan baada ya aliyekuwa mkuu wa majeshi wa Pakistani Raheel Sharif kuchaguliwa kuongoza taasisi hiyo ya IMCTC.
Wanaopinga hatua hiyo wamesema kuwa kushiriki kwa Islamabad katika ushirika huo unaweza kuwakasirisha jamii ya waliowachache wa madhehebu ya Kishia nchini humo na kuharibu mahusiano na Iran, ambayo inashirikiana katika mpaka wa kilomita 1,000 na Pakistan.
Baraza la Seneti la Pakistan lilishuhudia malumbano makali juu ya suala hili wiki iliyopita ambapo upinzani ulisisitiza kuwa serikali isishiriki katika shughuli za mkutano wa Jumapili Riyadh bila ya kupata idhini ya bunge.

Maandamano Islamabad : Jeshi la Pakistan lasema liko tayari kusaidia

Watu 200 walijeruhiwa katika mapigano ya JumamosiHaki miliki ya pichaEPA
Image captionWatu 200 walijeruhiwa katika mapigano ya Jumamosi
Jeshi la Pakistan linasema "liko tayari" kuisaidia serikali kuwatawanya waandamanaji wenye itikadi kali za kiislamu walioifunga barabara kuu wa Islamabad.
Serikali ililiomba jeshi liisaidie kurudisha utulivu baada ya polisi kushindwa kuwatawanya waandamanaji Jumamosi.
Hatahivyo taarifa ya jeshi inaonekana kuishutumu serikali kwa namna ilivyoshughulikia hali, ikieleza kuwa maafisa wa polisi hawakutumiwa vizuri.
Inaaminika kuwa takriban watu 6 wameuawa.
Wengine takriban 200 wamejeruhiwa.
Jeshi limeomba ufafanuzi zaidi kabla ya kuagiza kutumwa kwa wanajeshi.
Wengi ya waliojeruhiwa ni maafisa wa usalamaHaki miliki ya pichaREUTERS
Image captionWengi ya waliojeruhiwa ni maafisa wa usalama
Waandamanaji wamefunga barabara kwa wiki kadhaa wakitaka waziri wa sheria Zahid Hamid, afutwe kwa kazi kwa makosa ya kukufuru.
Maandamano yamesambaa hadi katika miji mingine ukiwemo Lahore na bandari ya kusini Karachi.
Siku ya Jumamosi, serikali ilifunga kwa muda vituo vya kibinfasi vya habari na kufunga baadhi ya mitandao ya kijamii ukiwemo Facebook, Twitter na Instagram - kutokana na wasiwasi kwamba matangazo ya moja kwa moja ya hatua ya polisi huenda yakachochea hisia kali za kidini.
Vyombo vya habari nchini vinasema vimesalia kufungwa siku ya Jumapili.

Sugu, Mwakagenda wamtaka DC Rungwe atoke ndani ya kituo cha kujumlishia kura

Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbiliny (Sugu)
Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbiliny (Sugu) akichukua matukio kwa  kutumia simu yake, wakati wakisubiri kutangaziwa matokeo ya uchaguzi Kata ya Ibighi Wilaya ya Rungwe, Mbeya. Matokeo yanatangaziwa Ofisi ya Mtendaji Kata ya Ibighi. Picha na Godfrey Kahango. 
Rungwe. Mbunge wa Mbeya Mjini(Chadema), Joseph Mbilinyi na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mbeya, Sophia Mwakagenda wamemkomalia Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Julius Chalya asikae ndani ya chumba za kujumlishia kura kwa madai kwamba hahusikii na zoezi hilo.
Chalya amefika muda mfupi leo Jumapili jioni baada wasimamizi kutoka vituo vyote vya kupigia kupeleka maboksi ya kura katika Ofisi ya Kata ya Ibighi kwa ajili ya kujumlishia kura.
Baada ya kuingia ndani Chalya ndipo  Sugu na Mwakagenda nao wakaingia ndani ambapo wametolewa nje na Mkuu wa Kituo cha Polisi(OCD) Rungwe kwa madai hawahusiki na wanaohusika ni wagombea na mawakala wao.
Sugu na Mwakagenda wakaibua hoja kwamba mkuu huyo wa Wilaya kwamba naye anatakiwa kutoka na si vinginevyo.
“Sawa tunatoka lakini na huyo Mkuu wa Wilaya anatafuta nini ndani?  Naye atoke ili turidhike wote," amesema Sugu.
Baada ya kauli hiyo, OCD amesema 'isiwe shida naye anatoka tu'. Kweli Chalya ametii hilo na kutoka nje taratibu.

Matokeo ya awali ya uchaguzi mdogo wa udiwani yaanza kumiminika


Dar\Mikoani. Matokeo ya awali ya uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata 43 yameanza kutolewa kukiwa na mchuano kati ya CCM na Chadema.
Jijini Mwanza matokeo ya awali kituo cha Sokoni A Kata ya Mhandu ni kama ifuatavyo, Amiri Barahila (ACT) kura  0, Sima Costantine (CCM) kura 103, Godfrey Faustine (Chadema) kura 55,  Vaileth John (Chaumma) kura 0, Masalu Sebastian (CUF) kura 0, na Beatus Bujiku (DP) kura 1.
Matokeo kituo cha Sokoni B Kata ya Mhandu,  Sima Costantine (CCM) kura 106, Barahila Kassim (ACT) kura 0, Godfrey Faustine (Chadema) kura 38, Vaileth John (Chaumma) kura 0, Masalu Sebastian (CUF) kura 4 na Beatus Bujiku (DP) kura 0.
Matokeo Sokoni B -2 Kata ya Mhandu, Amir Barahila (ACT) kura 0, Sima Costantine (CCM) kura 74, Godfrey Faustine (Chadema) kura 42, Vaileth John (Chaumma) kura 0, Masalu Sebastian (CUF) kura 2 na Beatus Bujiku (DP) kura 0.
Kata ya Makiba wilayani Arumeru mkoani Arusha matokeo ya awali kituo cha Patanumbe namba moja, CCM kura 140, Chadema 89 na ACT Wazalendo 2
Kituo cha afya Meta namba mbili CCM kura 158, Chadema 52 na ACT Wazalendo 0

Ofisi ya kata namba mbili CCM kura 163,  Chadema 80 na ACT Wazalendo 1.
Katika kata tano amesema chadema amechoka na kunyanyaswa kwani tangu kampeni hadi sasa vituo vya polisi vimejaa wanachama wa chadema
Katika Kituo cha Kanisa la Lutheran namba mbili CCM kura 85, Chadema 76 na ACT Wazalendo 2
Kituo cha Kanisa la Lutheran namba mbili CCM kura 83,  Chadema 66 na ACT Wazalendo 0.
Katika Kata ya Senga wilayani Geita Kituo cha Msilale namba mbili, CCM kura 72, Chadema 1 na CUF 8.
Kituo cha Msilale namba moja, CCM 76.   Chadema 3 na CUF 6.
Kwenye Kituo cha Shule ya Msingi Buligi CCM kura  138, CUF   13 na  Chadema 1.