Monday, November 27

Mgombea wa Chadema aeleza kilichosababisha awekwe chini ya ulinzi


Morogoro. Mgombea udiwani kwa tiketi ya Chadema katika Kata ya Sofi wilayani Malinyi mkoani Morogoro, Riko Venance ambaye aliwekwa chini ya ulinzi kwa takribani saa moja amesema polisi walifanya hivyo baada ya kuhoji sababu za mwananchi mmoja kuzuiliwa kupiga kura.
Alizungumza na Mwananchi leo Jumapili baada ya kuachiwa amesema alipofika katika kituo cha kupigia kura cha Shule ya Msingi Mission alipata malalamiko toka kwa mmoja wa wapiga kura aliyejulikana kwa jina moja la Akwilina kwamba amezuiliwa kupiga kura.
“Nilikuwa nahoji kwa nini Akwilina azuiliwe kupiga kura na ndipo nilipoambiwa nasababisha vurugu na kuwekwa chini ya ulinzi," amesema Venance.
Amesema mpiga kura huyo alipoulizwa jina alisema anaitwa Akwilino wakati kwenye kadi imeandikwa Akwilina na hapo ndipo utata ulipoanzia, hata hivyo baadaye aliruhusiwa kupiga kura.
Mgombea huyo ambaye anaendelea kutembelea vituo tayari ameshatembelea vituo 10 kati ya vituo 21 vya kupigia kura vilivyopo katika kata hiyo.

No comments:

Post a Comment