Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani, Papa Francis, amewasili Myanmar (27.11.2017) wakati taifa hilo likikabiliwa na kipindi kigumu kutokana na ukosoaji mkubwa na jumuiya ya kimataifa kwa kuwatimua Rohingya.
Waumini wa kanisa Katoliki waliovalia nguo za kitamaduni walipererusha bendera na kucheza katika uwanja wa ndege wa mji mkuu Yaongon kumkaribisha kwa furaha papa Francis, anayefanya ziara ya kwanza kabisa nchini Myanmar kuwahi kufanywa na kiongozi wa kanisa hilo.
Ziara hiyo inakuja wakati jeshi la Myanmar likikabiliwa na ukosoaji kwa kuendesha kampeni ya mauaji dhidi ya Waislamu warohingya. Zaidi ya Warohingya 620,000 wamekimbia ukandamizaji na mauaji katika jimbo la kaskazini la Rhakhine na kutafuta hifadhi nchini Bangladesh katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.
Ziara ya siku nne ya papa Francis inaongeza shinikizo kwa Myanmar kuhusu jinsi inavyowatendea watu wa jamii ya wachache ya Rohingya ambao hawana uraia, kundi ambalo ameliita mara kwa mara "ndugu na dada" ili kupunguza makali ya madhila yanayowakabili.
Hotuba za kiongozi huyo mkuu wa kanisa Katoliki zitafuatiliwa kwa karibu na waumini wa madhehebu ya Budha wenye misimamo mikali iwapo neno Rohigya litatajwa, neno linalotumiwa katika nchi ambako kundi hilo la waislamu linadharauliwa na kutukwanwa na kuitwa Wabengali - wahamiaji wasio halali kutoka Bangladesh.
Matumaini ya amani
Wakimbizi wa jamii ya Rohignya katika kambi ya Kutupalong, kusini mwa Bangladesh wanasema wana matumaini makubwa ziara ya Papa Francis nchini Myanmar na Bangladesh itasaidia kuleta amani. Mohammed Nadir Hossain, mkimbizi kutoka mji wa Buthidaung nchini Myanmar, alisema, "Ataiona hali yetu ya kusikiisha na tuna matumaini ataelewa tutakachomueleza. Akitaka anaweza kuituliza serikali ya Myanmar na kuleta amani kwa kuzungumza nasi. Tunateseka sana kwa sasa. Tuna wasiwasi. Kwa hiyo tunashukuru sana kwamba anazuru nchini mwetu."
Senu Ara, ni mkimbizi kutoka Myanmar aliyekimbilia nchini Bangladesh mwezi Septemba mwaka huu, naye alisema, "Tunatumai kutakuwa na amani. Nadhani huenda akatusaidia kurejea nchini mwetu kwa amani. Anaweza kutusaidia kupata amani ambayo tunaitafuta kwa udi na uvumba. Hata tukibaki hapa, ataibadili hali yetu kuwa nzuri. Akiamua kuturudisha nyumbani, atafanya hivyo kwa njia ya amani."
Papa Francis atakutana na kiongozi wa Myanmar, Aung San Suu Kyi, mshindi wa zamani wa tuzo ya amani ya Nobel, ambaye heshima na hadhi yake imeshuka kwa sababu ya kushindwa kwake kuzungumzia hadharani kuwatetea Warohingya.
Baba Mtakatifu Francis pia atafanya mazungumzo na mkuu wa majeshi, Min Aung Hlang, mkutano kati ya kiongozi wa kidini ambaye amekuwa akitetea haki za wakimbizi na mtu ambaye anatuhumiwa kwa kusimamia kampeni ya kuwatimua Warohingya kutoka Myanmar.
Ziara ya Papa Francis ni fursa ya kihistoria kwa waumini wa kanisa Katoliki nchini Myanmar kumkaribia kiongozi wa kanisa lao. Waumini 700,000 wa kanisa hilo ni jumla ya asilimia moja ya wakazi milioni 51 wa Myanmar na wametawanyika katika pembe mbalimbali za taifa hilo, wengi wakikabiliwa na mizozo.
Takriban waumini 200,000 wa kanisa Katoliki wanamiminika mji mkuu Yangon kwa ndege, treni na magari kuhudhuria misa kubwa ya hadhara itakayofanyika siku ya Jumatano.
No comments:
Post a Comment