Tuesday, November 14

Wananchi Mwanga wanavyochangia maji na mifugo


Kata za Mgagao na Jipe zipo katika Wilaya ya Mwanga mkoani
Kilimanjaro. Wananchi wanaoishi katika kata hizo wamekuwa wakikubaliana na changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama.
Kutokana na changamoto hiyo, wananchi wa vijiji vya Jipe na Kiverenge wanalazimika kutumia maji ambayo siyo safi na salama ili waweze kukidhi mahitaji yao.
Unaweza kuona matatizo yako ni makubwa lakini ukiyasikiliza ya mwenzako utaona ya kwako yana unafuu kidogo na hivi ndivyo ilivyo katika vijiji hivyo.
Vijiji hivyo ni kati ya vijiji vilivyopitiwa na mradi wa visima ambavyo havifanyi kazi kutokana na sababu mbalimbali za kiufundi.
Hali ilivyo kijiji cha Kiverenge
Katika Kijiji cha Kiverenge ambapo wanaishi jamii wa Wamasai wanakabiliana na adha ya maji safi na salama, huku wakitumia maji ya mvua yaliyotuama katika bwawa ambalo wananchi hao wanasema lilichimbwa na aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, David Cleopa Msuya.
Wananchi hao na wa kijiji cha jirani cha Pangaro wanalazimika kutumia maji ya bwawa kwa matumizi ya nyumbani na mifugo.
Akizungumza kijijini hapo, Diwani wa Kata ya Mgagao, Longoviro Kipuyo anasema bwawa hilo linatumiwa na mifugo na watu kutokana na maji safi na salama kupatikana umbali mrefu.
Anasema, kuna kisima kimoja ambacho kinatoa maji safi, lakini kipo mbali hali inayosababisha wanachi kutumia maji ya mvua yaliyotuama kwenye madimbwi.
Kipuyo anasema maisha ya wananchi wa vijiji hivyo yako hatarini kwasababu wanatumia maji machafu ambayo pia yanatumiwa na mifugo yao.
Anasema licha ya maji hayo kutokuwa salama kwa matumizi ya binadamu, bado wanahakikisha kuwa bwawa hilo halipungukiwi maji ili waweze kuyatumia yaliyopo.
Hata hivyo, anasema bwawa hilo kwa sasa limejaa tope na lipo hatarini kutoweka kama halitafanyiwa usafi kwa wakati.
Akizungumza wakati akichota maji ndani ya bwawa hilo, Agnes Moleli anasema licha ya maji hayo kuwa machafu lakini yamekuwa mkombozi kwao.
“Hatuna namna nyingine ya kupata maji safi na salama hivyo lazima tutumie haya, tunakunywa, tunapikia na mifugo pia inatumia maji haya haya” anasema Molel.
Anasema kuwa kuna wakati hutembea takribani kilomita saba hadi 10 kwenda kufuata maji kwenye mabwawa katika kijiji jirani.
Marufuku kuoga katika bwawa
Jitihada za kulinda afya zao wanazifanya wao wenyewe kwa kuwa wamepiga marufuku mtu kuoga ndani ya bwawa hilo.
Diwani huyo anasema atakayekutwa anaoga kwenye bwawa hilo anachukuliwa hatua kali kwa kuwa wanajitahidi kulinda usalama wa maji hayo.
Anasema wametenga eneo la pembeni kwa ajili ya kufulia nguo na kwamba siyo rahisi kuizuia mifugo kunywa maji katika bwawa hilo kwa kuwa ni mingi.
“Inabidi wakati mifugo ikitaka kunywa maji, watu waipishe na baada ya hapo shughuli nyingine ziendelee,” anasema diwani Kipuyo.
Naye Taitas Laizer aliyekutwa akinyweshea mifugo bwawani, anasema hakuna sehemu maalumu ya mifugo kunywa maji kwenye bwawa hilo.
Laizer anasema wangepata sehemu nyingine mbadala ya kupata maji safi, wangeacha bwawa hilo litumiwe na mifugo pekee.
Kijiji cha Jipe
Wakati nikiwa njiani kuelekea Kijiji cha Jipe kata ya Jipe hali inaoneka kuwa haina utofauti na maeneo mengine ya Mwanga kwakuwa wananchi wanatembea umbali mrefu kuyasaka maji kwa matumizi yao.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Abdala Hatibu anaeleza adha wanayoipata wananchi wa kijiji hicho ni kuwa wapo hatarini kukumbwa na magonjwa kutokana na matumizi ya maji ya Ziwa Jipe.
Licha ya kuwa wako jirani kabisa na ziwa hilo, lakini hakuna namna yoyote wanayoweza kufanya ili wakayatumia maji hayo katika hali ya usafi na salama.
Hatibu anasema kutokana na ukosefu wa maji safi na salama, wanalazimika kutumia maji ya ziwa ambayo hutumiwa kwa kila shughuli za kibinadamu na zisizo za kibinadamu.
Anasema: “Katika ziwa hilo, mifugo wanakunywa hapo, wavuvi nao wanafanya kila aina ya uchafu huko ziwani halafu hapohapo tunachota maji, tunakunywa na kupikia,” anasema.
Wanunua ndoo ya maji kwa Sh500
Hatibu anasema kuwa wakitaka kupata maji ya kunywa wanalazimika kwenda kununua katika kijiji cha jirani kwa bei ya Sh500 kila ndoo.
“Kwa mtu mwenye uwezo mdogo, angalau anaweza kwenda kununua maji hayo kwa ajili ya kunywa, lakini wale wasio na uwezo kabisa wanatumia maji yaliyopo ambayo siyo salama,” anaeleza.
Kwa upande wake, mwanakijiji Nanzia Msofe, anasema kuwa wanatumia maji hayo kwakuwa hana namna nyingine.
Mkazi huyo aliyekutwa akichota maji huku ng’ombe wakiwa wanakunywa, anasema hiyo ndiyo hali halisi ya upatikanaji wa maji katika kijiji chao.
Anaiomba Serikali na wadau kuwaletea maji yanayotiririka kutoka mlimani kwani wana hofu zaidi ya afya zao.
Nasoro Mwanagiko ni mtendaji wa Kijiji cha Butu kilichopo Kata ya Jipe, anakiri kuwa kijiji hicho cha jirani kina tatizo kubwa la upatikanaji wa maji safi na salama.
“Hapa Kijiji cha Jipe vilichimbwa visima vitano ambavyo baadhi vilitoa maji mwezi mmoja na vingine havikutoa maji kabisa,” anasema.
Anasema zipo sababu mbalimbali zilizofanya visima hivyo visitoe maji mojawapo ikiwa ni miundombinu ya kiufundi kuwa mibovu.
Hata hivyo, anasema kadhia ya kukosa kabisa maji safi na salama wanakumbana nayo wakati wa kiangazi kwa kuwa maji kutoka mlimani hukatika kabisa.

Uamuzi wa mbunge waibua mvutano Kibaha


Kibaha. Mvutano umeibuka kwenye Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha baada ya upande mmoja wa madiwani kukataa ombi la Mbunge wa Kibaha Vijijini, Hamoud Jumaa kutaka arudishiwe gari moja kati ya mawili ya kubebea wagonjwa aliyoyakabidhi hivi karibuni ili ampe rafiki yake aliyeyoko mkoani Tabora.
Upande mwingine wa madiwani uliunga mkono hoja hiyo kwa madai kuwa kwa vile Jumaa ndiye aliyeyanunua na kuikabidhi halmashauri hiyo basi pia ana uwezo wa kulichukua tena na kulipeleka popote anapotaka yeye na Kibaha isihoji.
Gari hilo linalohitajika kuchukuliwa na Jumaa na kulipeleka Tabora kwa rafikiye ni SM 11995 ambalo ni miongoni mwa magari matatu yaliyokabidhiwa Julai 24 na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kwemye mkutano wa hadhara uliofanyika Mlandizi mbapo kati yake mawili alinunua Jumaa na moja lilitolewa na Rais.
Kabla ya mvutano huo, mkurugenzi wa halmashauri hiyo Tatu Selemani aliwasilisha ajenda ya ombi la Jumaa ya kuliomba baraza hilo limkubalie achukue gari moja kati ya mawili ya wagonjwa aliyowakabidhi hivi karibuni kwa ajili wananchi wa jimbo hilo.
Baada ya kuwasilishwa hoja hiyo ndipo mjadala ulioendana na minong'ono ya chini chini ulipoanza hatua iliyosababisha Mwenyekiti wa Halmashauri, Mansour Kisebengo kila mara kuwataka madiwani wawe watulivu na kutoa mawazo yao kama apewe au asipewe na sio kutoka nje ya hoja.
Diwani Kata ya Magindu(Chadema), Issa Mkali ambapo amesema hatua ya Jumaa kutaka kuchukua gari alilokwisha wakabidhi wananchi wa jimbo lake ni sawa na kuwanyanganya pamoja na kucheza na maisha ya watu kwani bado upo uhitaji mkubwa wa magari ya wagonjwa.
Mkali amesema siku mbunge huyo alipokabidhi magari hayo ilifanyika sherehe kubwa iliyowakusanya wananchi wa wilaya hiyo na mgeni rasmi alikua Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu hakusema atalichukua baadaye.
“Mwenyekiti mbunge sasa analeta siasa wakati tumeshaambiwa tusubiri 2020, pia anacheza na maisha ya watu, hivi leo unatoa gari mbili tena unampa waziri akusaidie kuyakabidhi halafu baada ya miezi mitatu unakuja kusema unaliomba moja unalipekea mkoa mwingine kwa rafiki yako ana uhitaji mkubwa, kwa huyo sisi watu wafe kwa usiasa wenu huu hapana gari haitoki,"amesema Mkali.
Kwa upande wake Diwani Kata ya Kwala(CCM), Josephin Gunda alimshukuru mbunge kupambana mpaka akapata magari mawili na kuwakabidhi lakini suala la leo kuja na ombi la kuchukuliwa moja ili lipelekwe mkoa mwingine kwa rafiki yake haitawaingia masikioni wapigakura ambao siku ya kutolewa waliitwa wakayapokea.
Pia Gunda alionyesha hofu kuwa kama baraza hilo litaridhia gari hilo lichukuliwe upo uwezekano katika mgao ujao wa Serikali halmashauri hiyo ikakosa maana itaonekana hawana uhitaji mkubwa kwani walishakua na uwezo wa kugawa hata yake machache iliyonayo.
Diwani Viti Maalum, Mariam Shirima amesema mbunge huyo angefanya busara kwa kufanya mbinu zake atafute jingine na akilipata hana haja ya kulihusisha na Kibaha bali alipeleke moja kwa moja kwa rafiki yake huyo lakini sio kutumia jina la halmashauri yao anapoagiza halafu aje ampe mtu wa wilaya na mkoa mwingine.
"Mimi nashauri mbunge atoe maelezo kwa nini ameamua kulichukua hili gari maana sisi hatujui ana nini na isitoshe huyu huyu ndiye juzi juzi alituletea maboksi kibao ya vitabu, ameleta shehena ya madawa na vifaa tiba sidhani kama ana nia mbaya, embu tumsikilize na kama baraza turidhie alichukue tu,"amesema Chezeni Diwani kata ya Soga
Akihitimisha hoja hiyo Jumaa alisema sio kwamba amekurupuka kuomba kulichukua gari hilo bali ana maana yake ambayo hakuweka bayana zaidi ya kusema kuondoka gari hilo kwenda Tabora ni hatua moja wapo ya Kibaha kiendelea kupata misaada mingi zaidi ikiwemo magari mengine mbili za wagonjwa wakati wowote mwishoni mwa mwaka huu.
"Jamani mimi ndiye nimeleta magari mawili sijasaidiwa na mtu hata mmoja humu na pia hata ushuru hakuna aliyenisaidia si halmashauri wala ninyi madiwani mnaobishabisha humu, sasa basi nina akili timamu sio mpumbavu naombeni nipeni hilo gari najua ninachokifanya,"amesema Jumaa
"Nimpe rafiki yangu aliyeko Simbu Wilaya ya Manonga ana uhitaji zaidi hata ya sisi, watu kule wanakufa jamani nimeguswa nikaona nimsaidie maana hata yeye anaweza kuwa msaada kwetu pia huko mbele na pia hamuwezi kujua hata zile kontena za vitabu na madawa nilipatajepataje,"amesema Jumaa.
Baada ya michango hiyo mbalimbali, Mwenyekiti Kisebengo alihoji baraza hilo kama wameridhia na ndipo sauti za "apewe" zilisikika huku za apana zikiwa dhaifu na hivyo hoja hiyo kuitimishwa kwa kuliruhusu gari moja kuondoka kwenda Manonga.

Dk Mpango atumia dakika 40 kujibu makombora ya wabunge


Dodoma. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango jana Jumatatu jioni alitumia dakika 40 kujibu makombora ya wabunge kwa kutoa ufafanuzi wa kina wa deni la Taifa na kuyumba kwa sekta ya mabenki nchini.
Katika kujibu hoja za wabunge ambao walijadili mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa 2018/2019, Dk Mpango aliwataka wabunge kumkosoa kwa haki na hofu ya Mungu.
Dk Mpango alienda mbali na kuwaeleza kinagaubaga wabunge kuwa Serikali itaendelea kukopa mpaka kieleweke na akisema hakuna dhambi kukopa ikiwa fedha hizo zinakwenda kukuza uchumi.
Kuhusu hoja kuwa Deni la Taifa linakuwa kwa kasi kubwa wakati uchumi unakua kwa kasi ndogo, Dk Mpango alisema deni hilo ni himilivu akisema baadhi ya wabunge wanashindwa kukokotoa hesabu.
Alisema Deni la Taifa liliongezeka kutoka dola 22.3 bilioni za Marekani mwaka 2016 na kufikia dola 26 bilioni ilipofika mwezi Juni 2017 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 17.
“Deni hilo ni sawa na asilimia 31.2 ya GDP (Pato la Taifa) ikilinganishwa na ukomo wa uhimilivu wa asilimia 56. Uhimilivu wa Deni la Taifa hupimwa kwa kuzingatia uwezo wa nchi kulipa deni”
Dk Mpango alitoa takwimu za nchi za Afrika Mashariki za uhimilivu wa deni la taifa kwa nchi hizo akisema Tanzania bado iko vizuri na iko katika nafasi nzuri ya kukopesheka na wataendelea kukopa.
Alizitaja nchi hizo na uhimilivu wa deni lao kuwa ni Uganda ambayo ni asilimia 35.4, Rwanda asilimia 36.6, Burundi asilimia 43.4 na Kenya asilimia 50.4 akisema hali ni nzuri kulinganisha na nchi nyingine.
Alilinganisha nchi hizo na Zambia yenye uhimilivu wa asilimia 57.2, United Republic of Emirates asilimia 60.3, Marekani asilimia 73.8, Morocco asilimia 77 na Uingereza asilimia 92.2.
“Misri ni asilimia 92.6, Msumbiji asilimia100.3, Italia asilimia 132.5 na Ugiriki asilimia 181.6. Kwa takwimu hizi sisi bado tuna nafasi kubwa ya kukopa,”alisema Dk Mpango na kuongeza;
 “Tutaendelea kukopa kwa sababu moja tu kubwa. Kwamba ni kwa ajili ya ni kukuza uwezo wetu wa baadaye wa kumudu uendeshaji wa nchi yetu na kulinda uhuru na heshima ya nchi yetu,” alisema.
“Napenda nisisitize hakuna dhambi ya nchi kukopa ilimradi nchi husika itumie fedha hizo za mkopo kukuza uwezo wa kiuchumi na kuzalisha na kurejesha hiyo mikopo,”
“Kama Rais (John Magufuli) alivyosema alivyokuwa ziarani Kagera kwa kweli tutaendelea kukopa mpaka kieleweke ilimradi Deni la Taifa tuhakikishe linaendelea kuwa himilivu.”
Kuhusu benki za biashara nchini kuporomoka kwa kiasi kikubwa kwa mikopo binafsi, mikopo ya biashara na mikopo ya sekta za uzalishaji, alisema hilo limetokea nchi kadhaa.
“Katika miezi 12 iliyoishia Septemba 2017, wastani wa ongezeko la mikopo kwa sekta binafsi nchini Kenya ilikuwa asilimia 3.8, Tanzania asilimia 5.0, Uganda 5.2 na  Rwanda asilimia 10.3.
Dk Mpango alikuwa akijibu hoja za baadhi ya wabunge kuwa amekuwa na kiburi na hana ushirikiano wa wabunge na wakati mwingine hapokei simu za wabunge wanapomtafuta kumshauri.
Kuhusu ushiriki wa sekta binafsi, Dk Mpango alikiri kuwa ndio injini ya uchumi lakini akasema zipo changamoto kiuhalisia na kusema “akili za kuambiwa tuchanganye na za kwetu”
“Akili za kuambiwa mzee Kikwete alituambia lazima tuchanganye na za kwetu kabla ya kuamua kufikia hatua ya kuwa na sekta binafsi yenye nguvu,”
“Kweli natamani sana wawekezaji wa ndani na nje watatupunguzia huu mzigo. Sekta binafsi tuliyonayo bado inahitaji kulelewa ili iweze kubeba jukumu hili.”

Serikali yawataka wabunge kuanzia bungeni suala la pensheni


Dodoma. Serikali imewataka wabunge wanaotaka utaratibu wa kulipwa pensheni mara baada ya kumaliza kipindi cha ubunge urejeshwe, walipeleka jambo hilo kwanza kwenye  Tume ya Utumishi ya Bunge kabla ya kulifikisha serikalini.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira, Anthony Mavunde amesema leo Jumanne bungeni kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Vunjo (NCCR_Mageuzi), James Mbatia.
Mbatia amesema sheria ya mwaka 1981 ilikuwa inatambua pensheni kwa wabunge wanaomaliza muda wao na kuihoji Serikali inatamka nini kuhusu kulifufua suala hilo.
Akijibu swali hilo, Mavunde amesema kwa sababu swali la mbunge huyo ni kufufua sheria ya pensheni ni vyema lianzie kwao ( Tume ya Utumishi ya Bunge) ndio lifike serikalini.
Katika swali la msingi, Mbatia ametaka kufahamu Serikali haioni busara kuifanyia marekebisho Sheria ya Maslahi na Mafao ya Majaji namba 3 ya mwaka 2007 au vinginevyo ili majaji waweze kupatiwa huduma muhimu za matibabu wakati wanapostaafu.
Akijibu Mavunde amesema masharti ya kazi na stahili za majaji ya mwaka 2013 kwa maana majaji wa Mahakama Kuu yamefafanua kuwa majaji hao wamejumuishwa katika utaratibu wa matibabu kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHF)wawapo kazini.
Amesema gharama hizo hulipwa na Serikali na hata wanapostaafu wanaendelea kupata huduma hizo kupitia mfuko huo.
"Kwa wale waliostaafu kabla ya masharti hayo kuanza kutumika hawanufaiki na mfuko huo," amesema.
Kuhusu kuangalia kulifanya suala hilo la  kiutawala, Mavunde amesema kwa sababu ni suala la kisheria na sera wanalichukua na kulifanyia kazi.

Wabunge 40 wapanga kumng’oa Waziri Mkuu Uingereza


London, Uingereza. Wabunge wapatao 40 kutoka chama tawala cha Conservative inadaiwa wako tayari kutia saini barua ya kutokuwa na imani na kiongozi wao Waziri Mkuu Theresa May.
Gazeti la Independent limesema endapo wabunge wanane wataongezeka hivyo wakawa 48, idadi hiyo itakuwa inatosha kushinikiza kuanzishwa mchakato kamili wa kupiga kura ya kutokuwa na imani naye na hatimaye kuondolewa.
Gazeti la Metro limeripoti kwamba idadi hiyo iliongezeka katika wiki za hivi karibuni kutoka 35 baada ya May kutoa hotuba isiyoridhisha na chama kukabiliwa na ongezeko la kashfa tangu ulipoitishwa uchaguzi mkuu wa mapema Juni 8. Waziri Mkuu ameshuhudia mawaziri wawili, Michael Fallon na Priti Patel wakijiuzulu kipindi cha wiki moja.
Mbali ya kashfa ya ngono, mawaziri kujiuzulu na kosa lililofanywa na Waziri wa Mambo ya Nje Boris Johnson lililochangia mwanamke mwenye uraia wa Uingereza, Nazanin Zaghari-Ratcliffe kukabiliwa na kifungo kirefu zaidi nchini Iran, mvutano kuhusu Uingereza kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya (EU) maarufu kama Brexit ni miongoni mwa mambo yaliyoongeza hofu ndani ya chama katika kiwango ambacho May anashindwa kukidhibiti.
Watu wengi sasa wanaamini Waziri Mkuu ni hasara katika mchakato wa Brexit na wengine wanafikiri Conservatives wanahitaji kukaa kipindi kirefu kwenye upinzani ili wajiunge upya.
Waziri mmoja aliliambia gazeti la Independent: “Inatisha kuzungumzia jambo hili lakini nionavyo tunakaribia sana kwenye nukta ambayo tunapaswa kukaa muda wa kutosha kwenye upinzani ili kujirekebisha.”
Mwingine alisema: “Uvumilivu umepungua sana na katika namna fulani umekatika.”
Taarifa nyingine iliyochapishwa na gazeti la Sunday Mail imeelezea barua ya siri kutoka kwa Johnson na Waziri wa Mazingira, Michael Gove inayomtaka May kushinikiza mipango migumu ya Brexit.
''Ikiwa tunataka kukabiliana na wale wanaotaka kuuharibu mchakato huo, kuna njia za kusisitiza kuhusu namna ya kulitatua hilo,'' imesema barua hiyo na wamewambia May ''afafanue mawazo'' ya mawaziri walioko katika baraza lake la mawaziri ambao wanaunga mkono mipango mepesi katika mchakato wa Brexit.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, Johnson na Gove wametaka mipangilio ya kipindi cha mpito kwa ajili ya nchi hiyo kujiondoa katika Umoja wa Ulaya ikamilike Juni 20, mwaka 2021.
Mambo haya yamekuja baada ya washauri wa EU kutishia kuzuia mazungumzo ya biashara hadi Machi mwakani labda Uingereza ikubali viwango ilivyopangiwa katika mpango wa Brexit. Mshauri mkuu katika mazungumzo ya Brexit, Michel Bariner ameiongezea presha serikali baada ya kuipa muda wa wiki mbili tu.

Mtoto asimulia bomu lililoua wenzake shuleni


Ngara. Mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Kihinga, wilayani hapa mkoani Kagera, Domina Wabandi (10) amesema wakati wakiingia darasani, mwenzao Juliana Tarasisu (13) aliyefariki dunia alikuwa akiwaonyesha kitu kizito cha chuma chenye umbo la mviringo au kama nanasi.
Mtoto Wabandi ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Kihinga ni miongoni mwa majeruhi 42 katika tukio la kulipukiwa na bomu la kutupwa kwa mkono lilioua wanafunzi watano walipokuwa shuleni.
Wabandi alisema hayo juzi baada ya kuruhusiwa kutoka Hospitali ya Misheni ya Rulenge alikokuwa amelazwa.
Alisema siku hiyo ya Novemba 8, mwalimu wao alikuwa akiandika maneno ubaoni huku wao wakiwa wamejipanga foleni na kuingia mmoja mmoja darasani.
Wabandi alisema kuwa mwenzao Tarasis alikuwa kaficha bomu hilo (akidhani kitu cha kuchezea) kwenye mfuko wa daftari ili wenzake wasimuibie huku akieleza kuwa aliokota njiani.
Alisema ghafla kulitokea mlipuko na wanafunzi wengi kuanguka na yeye alijikuta akipata fahamu baada ya kufikishwa hospitali.
Wabandi alisema alipata kumbukumbu wakati akihudumiwa na wauguzi huku akihojiwa na watu mbalimbali chanzo cha kuumia kwake.
Katika tukio hilo mwanafunzi huyo aliumia vidole viwili vya mkono wa kushoto na alipata majeraha usoni.
Pia, ameumia jicho la kushoto na kumsababishia uoni hafifu na anadai kuwa licha ya kuruhusiwa hospitali anakabiliwa na maumivu ya mwili.
Akizungumzia tukio hilo, mwenyekiti wa kijiji cha Kihinga, kata ya Kibogora, Hassan Mohamed alisema: “Umri wa aliyefariki dunia na darasa alilokuwa anasoma, ni wazi alikuwa hana utambuzi wa elimu kwamba chuma alichokuwa nacho kingekuwa ni hatari kwa maisha yake.”
Mmoja wa wazazi ambaye ni Kamanda wa Jeshi la Mgambo katika Kijiji cha Kihinga, (MG 370 152) Emanuel Kaloli alisema mwanafunzi aliyekuwa na bomu hilo aliliokota njiani asubuhi akitokea nyumbani kwenda shuleni.
Alisema bomu hilo aliliokota kandokando ya uwanja wa mpira ulio jirani na kituo cha kijiji cha Kihinga ambacho hutumiwa na wanafunzi na wanakijiji katika michezo ya aina mbalimbali.
Kaloli alisema huenda bomu hilo lilidondoshwa na majambazi ambao siku moja kabla ya tukio wamliteka mkazi wa kijiji cha Rwinyana, Josepha Francis na kumpora vitu mbalimbali na kuondoka kusikojulikana.
“Mama huyo alitusimulia kwamba walimtishia kwa visu na waliongea kwa lugha ya Kirundi kwamba akikataa kuwapa simu na namba ya siri watamlipua hivyo inawezekana liliwadondoka,” alisema Kaloli .
Mtaalamu wa kutegua mabomu kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kabote Mafimbo alisema katika uchunguzi bomu hilo lilikuwa ni la kutupwa kwa mkono na hutumika wakati wa vita.
Mafimbo alisema kwamba bomu hilo inawezekana lilitoka nchi jirani zenye vita kama Burundi au Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), hivyo wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari dhidi ya vitu vya namna hiyo.

Rais JPM awatumia salamu Nape, Bashe


Dodoma. Rais John Magufuli amewataka wabunge wawili wa CCM, Nape Nnauye na Hussein Bashe, ambao michango yao bungeni imekosoa uendeshaji uchumi, wampelekee majina ya wawekezaji wanaokwamishwa ili awape kazi.
Wabunge hao wa Mtama na Nzega Mjini waliikosoa Serikali wakati wa kujadili Mpango wa Taifa wa Maendeleo kwa mwaka 2018/2019.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango ambaye alishutumiwa na wabunge hao kumpotosha Rais, alisema wakati akihitimisha mjadala huo kuwa alipigiwa simu na mkuu wa nchi na kuelezwa hayo.
“Naomba ninong’one na Bunge lako tukufu. Mheshimiwa Rais Magufuli aliposikia huu mjadala, alinipigia simu na aliniambia hivi,” alisema Waziri Mpango.
“Waziri, mwambie ndugu yako mheshimiwa Nape na mheshimiwa Bashe kuwa nawataka sana hao wawekezaji kwenye ujenzi wa Standard Gauge Railway.
“Wawalete hata kesho niko tayari kuwapa reli ya kutoka Kaliua –Mpanda au Isaka-Mwanza au reli ya Mtwara-Mchuchuma hadi Liganga waijenge.
“Hayo ni maneno ya mheshimiwa Rais. Natumaini waheshimiwa husika will raise up to this challenge from his excellence the president (wataifanyia kazi changamoto ya mheshimiwa Rais.”
Akijibu hoja za wabunge hao na wengine, Dk Mpango alisema si kwamba Serikali imeiweka pembeni sekta binafsi bali bado haijakaa vizuri na wakati mwingine inakuja na mashart

Maelezo ya shahidi yaibua mvutano kortini

Watuhumiwa wa kesi ya mauaji ya Erasto Msuya
Watuhumiwa wa kesi ya mauaji ya Erasto Msuya wakiingia katika chumba cha Mahakama Kuu mjini Moshi jana huku mtuhumiwa mmoja akisaidiwa kutembea baada ya kuugua tumbo ghafla akiwa mahabusu. Picha na Dionis Nyato 
Moshi. Mvutano wa kisheria umeibuka katika Mahakama Kuu mjini hapa kuhusu nani anayetakiwa na nani asiyetakiwa kutoa nyaraka za shahidi wa 13 katika kesi ya mauaji ya bilionea Erasto Msuya.
Baada ya shahidi wa 13 Elirehema Msuya kumkubalia wakili wa utetezi Majura Magafu kukabidhi nyaraka za maelezo katika Mahakama hiyo kama ushahidi wake, upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili wa Serikali Kassim Nassir uliweka pingamizi kupinga maelezo hayo.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa shahidi huyo hakuiomba Mahakama kuchukua maelezo hayo kama ushahidi wake bali aliyeomba yapokewe kama kielelezo ni wakili Magafu.
Wakili Nassir ambaye anaiwakilisha Jamhuri alidai kuwa Magafu hana uwezo wa kutoa nyaraka mahakamani, badala yake anayepaswa kutoa nyaraka hizo ni shahidi pekee.
Baada ya pingamizi hilo, wakili Magafu aliiambia Mahakama kuwa pingamizi lililotolewa na upande wa mashtaka halina mantiki, hivyo litupiliwe mbali kwa sababu halina miguu ya kisheria na akaomba ushahidi huo upokewe.
Akitoa uamuzi, Jaji Salma Maghimbi anayesikiliza kesi hiyo alisema upande wa mashtaka hawakuwa wakimsikiliza wakili Magafu wakati akifanya mahojiano na shahidi huyo.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Sharifu Mohamed, Shaibu Jumanne, Musa Mangu, Jalila Zuberi, Karimu Kihundwa, Sadiki Mohamed na Ally Mussa.
Yafuatayo ni mahojiano ya shahidi wa 13, Elirehema Msuya yakiongozwa na wakili Kassim Nassir.
Wakili Nassir: Unafanya shughuli gani?
Shahidi: Udereva
Wakili Nassir: Unafanyia wapi?
Shahidi: SG Resort Lodge.
Wakili Nassir: Iko wapi?
Shahidi: Sakina.
Wakili Nassir: Tarehe 6/8/2013 ulikuwa wapi?
Shahidi: Hotelini.
Wakili Nassir: Siku hiyo ilikuwaje?
Shahidi: Baada ya kutoka mjini kwenye kufanya manunuzi ya hotelini, saa 4:30 asubuhi nilimkuta marehemu (Msuya) anaongea na simu.
Wakili Nassir: Yeye na nani?
Shahidi: Alikuwa kwenye swimming pool (bwawa la kuogelea) na mtu mmoja.
Wakili Nassir: Wewe ulikuwa unafanya nini wakati huo?
Shahidi: Nilikuwa nimesimama kwenye parking (eneo la kuegesha magari).
Wakili Nassir: Nini kiliendelea?
Shahidi: Waliendelea na maongezi na baada ya muda walielekea hotelini.
Wakili Nassir: Kabla ya kwenda hotelini aliongea na huyo mtu kwa muda gani?
Shahidi: Kama dakika 20.
Wakili Nassir: Kutokea ulipokuwa umesimama na pale walipokuwa wamekaa kulikuwa na umbali gani?
Shahidi: Sio mbali.
Wakili Nassir: Walikuwa wanasemaje?
Shahidi: Walikuwa wakitazamana.
Wakili Nassir: Baada ya kuelekea hotelini ilikuwaje?
Shahidi: Walipita pale parking (eneo la kuegesha magari) nilipokuwa nimesimama.
Wakili Nassir: Baada ya hapo?
Shahidi: Erasto Msuya aliniita uko wapi kaka? Nikamwambia niko huku parking (eneo la kuegesha magari). Aliniambia washa gari, nikamwambia langu au lako? Niliwasha gari langu nikasogea karibu na marehemu (Msuya).
Akaniambia nimpeleke mgeni wake stendi ya mabasi Arusha kisha nimpandishe Coaster (basi) za Moshi.
Wakili Nassir: Nini kiliendelea?
Shahidi: Marehemu (Msuya) alimwambia huyo mtu ahakikishe anamhimiza ndugu yake wamalize hiyo biashara asubuhi.
Wakili Nassir: Baada ya hapo ilikuwaje?
Shahidi: Alimwambia sawa brother (kaka).
Wakili Nassir: Wakati marehemu (Msuya) akiwa anamwambia maneno hayo wewe ulikuwa wapi?
Shahidi: Nilikuwa karibu yao.
Wakili Nassir: Baada ya hapo nini kiliendelea?
Shahidi: Aliingia kwenye gari, nilipofika stendi huyo rafiki yake akaniambia nimwache pale pale hakuna shida.
Wakili Nassir: Baada ya hapo ikawaje?
Shahidi: Nilirudi hotelini.
Wakili Nassir: Huyo mtu aliyekuwa na marehemu siku ile ukiambiwa umuonyeshe utamkumbuka?
Shahidi: ndiyo.
Wakili Nassir: Huyo mtu ana mwonekano gani?
Shahidi: Macho mekundu, uso mpana, alikuwa si mrefu wala mfupi na alikuwa mwembamba kidogo.
Wakili Nassir: Kabla ya tarehe 6/8/2013 ulishawahi kumwona?
Shahidi: Sikuwahi kumwona.
Wakili Nassir: Ulishawahi kuwa na ugomvi naye?
Shahidi: Hapana.
Wakili Nassir: Nini kiliendelea baada ya wewe kumpakiza kwenye gari yule aliyekuwa na marehemu siku ile.
Shahidi: Nilirudi hotelini, tarehe 7/8/2013 alinipigia simu akaniambia anataka Sh1 milioni hivyo nikaichukue kwa meneja kisha nitoke nje nitamkuta mtoto wake wa kike aliyemwagizia aje kuchukua kisha tukaelekea Philips na zile fedha.
Wakili Nassir: Baada ya maagizo hayo?
Shahidi: Nilimpa Sh1 milioni yule mtoto wake tulipofika pale Philips, kisha nikarudi hotelini muda kidogo marehemu aliingia.
Wakili Nassir: Nini kiliendelea?
Shahidi: Aliingia akapaki gari lake kisha akanipa simu, charger ya simu pamoja na kipimo cha kupimia mawe ya madini kisha akaingia uwani. Kabla hajatoka uwani alikuja mtoto wake akiwa na gari aina ya Range Rover akapaki na muda kidogo marehemu alitoka.
Wakili Nassir: Mtoto wake anaitwa nani?
Shahidi:Glory.
Wakili Nassir: Nini kiliendelea?
Shahidi: Alinipa funguo za gari akaniambia nimpe zile fedha Sh1 milioni, charger na kipimo cha madini.
Wakili Nassir: Ulifanyaje?
Shahidi: Nilimpa vitu vyote.
Wakili Nassir: Baada ya hapo nini kiliendelea?
Shahidi: Aliniambia anaenda KIA kufanya biashara.
Wakili Nassir: Ilikuwaje?
Shahidi: Aliondoka na ile Range Rover.
Wakili Nassir: Nini kilitokea mkiwa mjini?
Shahidi: Nilipigiwa simu na Rama kuwa Erasto Msuya amepigwa risasi huko KIA Mijohoroni.
Wakili Nassir: Baada ya huo ujumbe ulifanya nini?
Shahidi: Nilirudi hotelini nikakuta watu wanalia wanasema Erasto Msuya kapigwa risasi.
Wakili Nassir: Nini kiliendelea?
Shahidi: Meneja aliniambia tuwashe gari tuelekee KIA mimi na yule jamaa, tulipofika tukaambiwa twende Boma tulipofika kwenye hiyo zahanati tulikuta watu wamekusanyika wengi na marehemu (Msuya) akiwa ameshaingizwa ndani.
Wakili Nassir: Nini kiliendelea?
Shahidi: Tulikaa kidogo na kurudi hotelini.
Wakili Nassir: Baada ya mazishi nini kiliendelea?
Shahidi: Tuliendelea na kazi, baadaye kidogo nilipigiwa simu nahitajika Moshi mjini tarehe 7/10/2013.
Wakili Nassir: Uliambiwa unahitajika Moshi sehemu gani?
Shahidi: Kwa RCO (Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai)
Wakili Nassir: Sasa ikawaje baada ya kupata taarifa unahitajika Moshi?
Shahidi: Nilipofika Moshi niliambiwa nitamwona mtu ambaye nilimpeleka stendi tarehe 6/8/2013.
Wakili Nassir: Baada ya hapo?
Shahidi: Nilikuta watu wamepanga mistari.
Wakili Nassir: Je, ulimwona?
Shahidi: Ndiyo. Nilimshika bega, niliambiwa niandike maelezo yangu kuhusiana na huyo mtu.
Wakili Nassir: Je,ni yuleyule uliyemtambua mara ya kwanza?
Shahidi: Ni yuleyule.
Wakili Nassir: Yule bwana ulimpeleka stendi na gari gani?
Shahidi: Noah, nyeusi T108 BZC.
Wakili Nassir: Ulisema marehemu aliondoka na Range, unaweza kukumbuka namba za hiyo gari?
Shahidi: Ndio,T800 CKF.
(Mara baada ya kumaliza mahojiano hayo yalifuata mahojiano ya upande wa utetezi yakiongozwa na Wakili Hudson Ndusyepo)
Wakili Ndusyepo: Una elimu gani?
Shahidi: Kidato cha nne.
Wakili Ndusyepo: Shule gani?
Shahidi: Makumira Sekondari.
Wakili Ndusyepo: Ulimaliza mwaka gani?
Shahidi: 1992.
Wakili Ndusyepo: Ulianza kazi mwaka 2012 kweli si kweli?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili Ndusyepo: Kabla ya hapo ulikuwa unafanya nini?
Shahidi: Nilikuwa nachimba madini Mererani.
Wakili Ndusyepo: Uliajiriwa kama ndugu au mfanyakazi?
Shahidi: Mfanyakazi.
Wakili Ndusyepo: Kwenye parking (eneo la kuegesha magari) na swimming pool (bwawa la kuogelea) kuna umbali gani?
Shahidi: Siyo mbali sana.
Wakili Ndusyepo: Mbali na Erasto na huyo mgeni, kulikuwa na nani mwingine?
Shahidi: Hakuna.
Wakili Ndusyepo: Hapo swimming pool(bwawa la kuogelea) kulikuwa na nini?
Shahidi: Meza yenye mwavuli na viti viwili.
Wakili Ndusyepo: Unakumbuka hiyo siku huyo mgeni wake alikuwa amevaaje?
Shahidi: Kofia ya kapero.
Wakili Ndusyepo: Rangi yake alikuaje?
Shahidi: Mweusi.
Wakili Magafu: Ni mara ya ngapi kufika hapa mahakamani tangu kesi ianze?
Shahidi: Mara ya kwanza.
Wakili Magafu: Ulikuwa unazuiwa kuja hapa mahakamani toka kesi hii imeanza?
Shahidi: Sikuwahi kuzuiwa.
Wakili Magafu: Marehemu alikuwa bosi wako na ulikuwa unampenda? Kwanini hukuja mahakamani kesi ikiwa inaanza?
Shahidi: Shughuli zilikuwa nyingi.
Wakili Magafu: Siku ya tukio ulipata taarifa saa ngapi?
Shahidi: Kama saa saba hivi.

Fundi ujenzi alivyokatisha ndoto za Secelela

Msichana Secelela Juma akiwa amembeba mwanawe
Msichana Secelela Juma akiwa amembeba mwanawe aliyezaa ana mwanaume aliyekuwa na uhusiano nao wakati akisoma sekondari. Picha na Habel Chidawali 
“Sijawahi kuwaza kitu kingine zaidi ya kazi mbili hadi leo, moja ni udereva wa magari makubwa na kazi ya pili ni kuwa muuguzi katika hospitali zenye wagonjwa wengi kutoka vijijini, lakini ndiyo basi tena,”
Ni simulizi ndefu ya msichana Secelela Juma (17) binti ambaye anashuhudia ndoto yake ikiyeyuka kwa sasa, licha ya kujitia moyo kuwa suala la udereva anaweza kupambana hadi alifikie.
Secelela ambaye kwa sasa anaitwa mama John, anaanza kutaja sababu za kupotea kwa ndoto yake ni fundi ujenzi ambaye alikutana naye Julai 2015 wakati akiwahi shuleni. Alikuwa akisoma kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Ihala ya mjini Mpwapwa.
Anasema umbali wa shule ulimfanya apatiwe msaada wa usafiri wa pikipiki ili kumwahisha na ilifanyika hivyo lakini wakiwa njiani, mtoa msaada alibadil mazungumzo na kuanza kumtaka kimapenzi, huku akiahidi kuendelea kumpa lifti ya kuwahi shule wakati wowote.
“Siku ya kwanza nilipata ukakasi kidogo kumjibu, siku iliyofuata niliamua kumkubalia na siku hiyo hiyo jioni tulianza uhusiano wetu,” anasema.
Msichana huyo ni miongoni mwa wasichana waliotoa ushuhuda kwenye mafunzo ya kujitambua ambayo yaliendeshwa na shirika lisilo la kiserikali la Utu wa mtoto (CBF) kwa wasichana walioolewa au kuzaa chini ya umri. Alionyesha ujasiri mkubwa wa kuwafundisha wenzake 25 mbinu za kujikinga na wanaume wakware.
Katika simulizi yake anasema hakuwahi kuwaza kujifunza kitu kinachoitwa mapenzi na hakutarajia kufanya katika umri wake, lakini alijikuta akitumbukia kwa sababu ya lifti.
Nini kilitokea
Secelela anasema, alipomaliza masomo ya msingi, alichaguliwa kujiunga na shule ya sekondari Ihala wakati yeye akiishi kwa wazazi wake mtaa wa Igovu mjini Mpwapwa ambako ni mbali na shule aliyopangiwa.
Anasema umbali huo ulikuwa ni changamoto ya kumfanya akutane na vishawishi vingi kutoka kwa wavulana wa mtaani na hata watu wazima. Kila alipokwenda shule au aliporudi nyumbani, hakukosa kukutana na mtu aliyemweleza habari za uhusiano ya kimapenzi.
Kwa maelezo yake, alijitahidi kuwa mvumilivu na mtu mwenye misimamo lakini mwishoni akajikuta ametumbukia kwenye shimo ambalo liliharibu maisha yake kwa jumla.
Anaeleza kukutana na mvulana ambaye alizoea kumuona mtaani hapo, ingawa kwa sasa ana muda mrefu hajamwona zaidi ya kuwasiliana kwenye mitandao. Alianza kama mtu mwema kabla ya kumgeukia na kuwa mpenzi wake kwa muda mrefu.
Aacha shule
Secelela alikwenda shuleni hadi novemba Mwaka 2015 alipofanya mtihani wa taifa wa kidato cha pili na kisha wakafunga shule, huku wakingoja matokea ya kuingia kidato cha tatu.
Hata hivyo, hakuwahi kukanyaga kidato cha tatu kwani walipofungua shule, aliona aibu kwenda kuungana nao kwa kuwa alishakuwa na mimba kubwa.
“Yaani kabla hatujaitwa kwenda kupimwa shuleni, mimi nilikuwa wa kwanza kujiondoa mwenyewe ingawa matokeo nilisikia kuwa nilikuwa nimefaulu na kutakiwa niendelee na kidato cha tatu, ‘’ anasema na kuongeza:
“..nilivyoanza kuhudhuria kliniki nikawa nakutana na wenzangu wengi ambao tulikuwa darasa moja ama walikua na watoto au wana mimba .”
Maisha baada ya kuacha shule
Hali ilikuwa shubiri nyumbani baada ya wazazi wake kuanza kumsimanga kila wakati kuwa amewatia aibu akiwa ni mtoto wao wa mwisho kati ya watoto watano, jambo lililomfanya awaze hata kujidhuru kabla ya kutoroka nyumbani na kwenda kuishi kwa kwa ndugu.
Aliishi nje ya familia yao kwa miezi mitatu lakini mimba ilipofikia miezi 8 aliamua kurudi kwa wazazi wake na kuomba msamaha.
Mwisho wa ndoto yake
Secelela anasema giza nene katika maisha yake lilianzia hapo na kufifisha ndoto yake aliyoanza kuiwaza tangu shule ya msingi kwamba wakati mmoja aje kumiliki leseni ya kuendesha magari makubwa ndani na nje ya nchi.
Licha ya kujipa moyo kuhusu udereva kwamba anaweza kutumia elimu yake ya kidato cha pili na kujifunza, anasikitika kuwa pengine magari atakayoendesha ni ya ndani ya nchi na siyo nje ya nchi.
Kuhusu ndoto ya uuguzi, anasema: ‘’ Ndoto hiyo ni kama imekufa kifo cha aibu kwa kuwa siwezi tena kufikia hatua ya kuwa muuguzi katika zanahati zinazokusanya kinamama wa vijijini ambao nilitamani kuwahudumia. Sasa nawaza kumiliki mgahawa au duka la vyakula ambavyo vinahitaji mtaji.’’
Hatari kwa wasichana wadogo
Selelela anasema kuwa, wasichana kati ya miaka 15 hadi 17 ndiyo kundi linalodanganywa kwa sehemu kubwa na wanaume, kwani bado hawana uwezo mkubwa katika kujibu mashambulizi ya kuepuka vishawishi pale wanapodanganywa.
Sababu nyingine anatajwa ni kuwa wanaume hawaoni tabu kugharimia wasichana wadogo ambao kimsingi hawana mahitaji mengi. Ndiyo maana hata wavulana wadogo nao wamekuwa wakiwarubuni.
“Msichana anatamani chipsi, wakati mwingine kiwi ya viatu tu au nauli au nguo ambavyo wavulana wenye vipato vya chini pia wanaweza kumudu kuvipata,” anaeleza.

‘Bilionea’ nyumba za Lugumi pasua kichwa


Dar es Salaam. Wanasheria wametofautiana katika sakata la Dk Louis Shika kuhusu kosa gani amefanya na sheria gani itatumika kumchukulia hatua.
Wakati wanasheria wakitofautiana polisi wamesema kuwa wanaendelea kumshikilia na kuhoji Dk Shika kabla ya kumfikisha mahakamani.
Pia wameeleza kuwa wanawasiliana na vyombo vingine vya Serikali ili kuona kama anaweza kupimwa akili.
Dk Shika alipata umaarufu kwa muda mfupi baada ya kushiriki katika mnada wa nyumba tatu za kifahari jijini Dar es Salaam na kuibuka mshindi, akiwa ameweka dau la takriban Sh2 bilioni, lakini akashindwa kufanya malipo ya awali ya asilimia 25.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya mawakili walihoji sheria gani amevunja, huku wengine wakisema alivunja sheria ya mikataba. Wakili wa kujitegemea, John Mallya alisema, “hamna jambo la jinai hapo ni suala la madai tu labda tusubiri akifikishwa mahakamani tuone atafunguliwa kesi gani.”
“Unajua katika mnada unaposema utalipa asilimia 25 unakuwa hujui hasa ni kiasi gani kwani hakuna bei rasmi, unaweza kuwa umejiandaa asilimia ya Sh500 milioni.
“Lakini inapofika zaidi ya hapo ni tatizo na ndio maana naona ni kesi ya madai ambayo Yono watakuwa wanadai kuwa kaharibu mnada, kwamba mteja wa pili angeweza kununua ila sioni jinai hapo.”
Mallya anaungwa mkono na mhadhiri wa Sheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk James Jesse aliyesema, “sijui ni sheria gani ambayo ameivunja katika hilo labda kama ni kuharibu mnada, waulizwe hao walioendesha watakuwa wanajua.”
Wakili wa kujitegemea, Alex Mgongolwa alisema kilichojitokeza ni kuvunja sheria ya mikataba ambayo mteja awali alikubali kwa kufikia bei ya juu zadi ya wateja wengine. “Hakuna jinai pale na alitakiwa ndani ya saa 48 awe amefikishwa mahakakani baada ya kuwa amekamtwa au kuachiwa, lakini kama bado anashikiliwa labda kuna kitu nyuma ya pazia,” alisema Mgongolwa.
Mallya na Dk Jesse wanatofautiana na Profesa wa Sheria wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Cyriacus Binamungu aliyesema mara baada ya tukio hilo walikuwa na majadiliano na liliwaacha njia panda.
“Bado tunajiuliza hapo ni criminal case (kesi ya jinai) au ni nini. Mnada ni process inakuwa na taratibu zake, sasa mhusika anatakiwa kuwa aware na masharti yaliyowekwa,” alisema Profesa Binamungu
“Haitegemei mtu ashiriki kwa kuleta utani au kuvuga ili kuharibu shughuli hiyo na kama mtu anashiriki lazima afuate masharti yaliyowekwa na yule anayeendesha mnada huo.
“Haiwezekani mtu ashiriki mnada wa kwanza, pili na tatu halafu atakiwe kutoa asilimia 25 aseme hana hela. Hii nayo inatuchanganya kwani hata aliposema anaweza kufanya muamala kwa njia ya mtandao, hauwezi kuhamisha fedha Sh200 milioni, 300 au 700 kwa kutumia kadi, hapana lazima uwepo mwenyewe.”
Yono wadai alijua anachokifanya
Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya udalali ya Yono, Scholastika Kevela alisema, “Dk Shika alikuwa anajua anachokifanya na kwa lengo gani.”
Alipoulizwa kwa nini hawakushtuka na kumtaka kulipa kwanza asilimia 25 kwa nyumba ya kwanza, Scholastika alisema: “ Ukiangalia baada ya kumaliza mnada wa kwanza na kwa kuwa muda wa benki ulikuwa bado, aliwekwa chini ya ulinzi kwa kushirikiana na maofisa wa TRA.
“Tangu pale na ule mnada wa pili, ili kuhakikisha hakimbii na kwa kuwa alikuwa akijieleza vizuri na alitoa nyaraka pale katika mnada wa kwanza hatukuwa na hofu, ndio maana tulivyomaliza mnada wa pili na kuhamia Upanga alibebwa na gari la Serikali na sio ajabu bila ulinzi angekimbia.”
Akijibu swali la Mwananchi kwamba mwonekano wake haukuwashtua, alisema, “katika mnada huwezi ‘kumjaji’ mtu kwa kumwona, mavazi hayampimi mtu kuwa na uwezo, niseme tu kwamba alikuwa anajua anachokifanya na kwa kuwa yupo katika mikono ya Serikali basi hatua zitachukuliwa.”
Alipoulizwa kama tukio hilo limewahi kujitokeza huku nyuma, alisema: “Hili ni tukio la kwanza, sijawahi kuendesha mnada nikakutana na kitu kama hiki.”
Polisi yaendelea kumhoji
Kaimu kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Benedict Kitalika alisema bado wanamshikilia Dk Shika na wanaendelea na uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili.
Kitalika alisema mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani muda wowote baada ya uchunguzi kukamilika.
Alisema mpaka jana hakukuwa na ndugu yeyote wa mtuhumiwa huyo aliyejitokeza kushirikiana na polisi katika uchunguzi unaoendelea.
Kabla ya kumfikisha mahakamani, Kitalika alisema polisi inawasiliana na mamlaka nyingine za Serikali kuangalia kama kuna uwezekano wa kumpima matatizo ya akili.
“Bado tunamshikilia huyu mtu (Dk Shika) wakati tunaendelea na uchunguzi. Tunashauriana na taasisi nyingine za Serikali kuona kama tunaweza kumpima akili,” alisema Kitalika na kusisitiza kwamba hana uhakika ni lini mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani.