Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira, Anthony Mavunde amesema leo Jumanne bungeni kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Vunjo (NCCR_Mageuzi), James Mbatia.
Mbatia amesema sheria ya mwaka 1981 ilikuwa inatambua pensheni kwa wabunge wanaomaliza muda wao na kuihoji Serikali inatamka nini kuhusu kulifufua suala hilo.
Akijibu swali hilo, Mavunde amesema kwa sababu swali la mbunge huyo ni kufufua sheria ya pensheni ni vyema lianzie kwao ( Tume ya Utumishi ya Bunge) ndio lifike serikalini.
Katika swali la msingi, Mbatia ametaka kufahamu Serikali haioni busara kuifanyia marekebisho Sheria ya Maslahi na Mafao ya Majaji namba 3 ya mwaka 2007 au vinginevyo ili majaji waweze kupatiwa huduma muhimu za matibabu wakati wanapostaafu.
Akijibu Mavunde amesema masharti ya kazi na stahili za majaji ya mwaka 2013 kwa maana majaji wa Mahakama Kuu yamefafanua kuwa majaji hao wamejumuishwa katika utaratibu wa matibabu kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHF)wawapo kazini.
Amesema gharama hizo hulipwa na Serikali na hata wanapostaafu wanaendelea kupata huduma hizo kupitia mfuko huo.
"Kwa wale waliostaafu kabla ya masharti hayo kuanza kutumika hawanufaiki na mfuko huo," amesema.
Kuhusu kuangalia kulifanya suala hilo la kiutawala, Mavunde amesema kwa sababu ni suala la kisheria na sera wanalichukua na kulifanyia kazi.
No comments:
Post a Comment