Tuesday, November 14

Wananchi Mwanga wanavyochangia maji na mifugo


Kata za Mgagao na Jipe zipo katika Wilaya ya Mwanga mkoani
Kilimanjaro. Wananchi wanaoishi katika kata hizo wamekuwa wakikubaliana na changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama.
Kutokana na changamoto hiyo, wananchi wa vijiji vya Jipe na Kiverenge wanalazimika kutumia maji ambayo siyo safi na salama ili waweze kukidhi mahitaji yao.
Unaweza kuona matatizo yako ni makubwa lakini ukiyasikiliza ya mwenzako utaona ya kwako yana unafuu kidogo na hivi ndivyo ilivyo katika vijiji hivyo.
Vijiji hivyo ni kati ya vijiji vilivyopitiwa na mradi wa visima ambavyo havifanyi kazi kutokana na sababu mbalimbali za kiufundi.
Hali ilivyo kijiji cha Kiverenge
Katika Kijiji cha Kiverenge ambapo wanaishi jamii wa Wamasai wanakabiliana na adha ya maji safi na salama, huku wakitumia maji ya mvua yaliyotuama katika bwawa ambalo wananchi hao wanasema lilichimbwa na aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, David Cleopa Msuya.
Wananchi hao na wa kijiji cha jirani cha Pangaro wanalazimika kutumia maji ya bwawa kwa matumizi ya nyumbani na mifugo.
Akizungumza kijijini hapo, Diwani wa Kata ya Mgagao, Longoviro Kipuyo anasema bwawa hilo linatumiwa na mifugo na watu kutokana na maji safi na salama kupatikana umbali mrefu.
Anasema, kuna kisima kimoja ambacho kinatoa maji safi, lakini kipo mbali hali inayosababisha wanachi kutumia maji ya mvua yaliyotuama kwenye madimbwi.
Kipuyo anasema maisha ya wananchi wa vijiji hivyo yako hatarini kwasababu wanatumia maji machafu ambayo pia yanatumiwa na mifugo yao.
Anasema licha ya maji hayo kutokuwa salama kwa matumizi ya binadamu, bado wanahakikisha kuwa bwawa hilo halipungukiwi maji ili waweze kuyatumia yaliyopo.
Hata hivyo, anasema bwawa hilo kwa sasa limejaa tope na lipo hatarini kutoweka kama halitafanyiwa usafi kwa wakati.
Akizungumza wakati akichota maji ndani ya bwawa hilo, Agnes Moleli anasema licha ya maji hayo kuwa machafu lakini yamekuwa mkombozi kwao.
“Hatuna namna nyingine ya kupata maji safi na salama hivyo lazima tutumie haya, tunakunywa, tunapikia na mifugo pia inatumia maji haya haya” anasema Molel.
Anasema kuwa kuna wakati hutembea takribani kilomita saba hadi 10 kwenda kufuata maji kwenye mabwawa katika kijiji jirani.
Marufuku kuoga katika bwawa
Jitihada za kulinda afya zao wanazifanya wao wenyewe kwa kuwa wamepiga marufuku mtu kuoga ndani ya bwawa hilo.
Diwani huyo anasema atakayekutwa anaoga kwenye bwawa hilo anachukuliwa hatua kali kwa kuwa wanajitahidi kulinda usalama wa maji hayo.
Anasema wametenga eneo la pembeni kwa ajili ya kufulia nguo na kwamba siyo rahisi kuizuia mifugo kunywa maji katika bwawa hilo kwa kuwa ni mingi.
“Inabidi wakati mifugo ikitaka kunywa maji, watu waipishe na baada ya hapo shughuli nyingine ziendelee,” anasema diwani Kipuyo.
Naye Taitas Laizer aliyekutwa akinyweshea mifugo bwawani, anasema hakuna sehemu maalumu ya mifugo kunywa maji kwenye bwawa hilo.
Laizer anasema wangepata sehemu nyingine mbadala ya kupata maji safi, wangeacha bwawa hilo litumiwe na mifugo pekee.
Kijiji cha Jipe
Wakati nikiwa njiani kuelekea Kijiji cha Jipe kata ya Jipe hali inaoneka kuwa haina utofauti na maeneo mengine ya Mwanga kwakuwa wananchi wanatembea umbali mrefu kuyasaka maji kwa matumizi yao.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Abdala Hatibu anaeleza adha wanayoipata wananchi wa kijiji hicho ni kuwa wapo hatarini kukumbwa na magonjwa kutokana na matumizi ya maji ya Ziwa Jipe.
Licha ya kuwa wako jirani kabisa na ziwa hilo, lakini hakuna namna yoyote wanayoweza kufanya ili wakayatumia maji hayo katika hali ya usafi na salama.
Hatibu anasema kutokana na ukosefu wa maji safi na salama, wanalazimika kutumia maji ya ziwa ambayo hutumiwa kwa kila shughuli za kibinadamu na zisizo za kibinadamu.
Anasema: “Katika ziwa hilo, mifugo wanakunywa hapo, wavuvi nao wanafanya kila aina ya uchafu huko ziwani halafu hapohapo tunachota maji, tunakunywa na kupikia,” anasema.
Wanunua ndoo ya maji kwa Sh500
Hatibu anasema kuwa wakitaka kupata maji ya kunywa wanalazimika kwenda kununua katika kijiji cha jirani kwa bei ya Sh500 kila ndoo.
“Kwa mtu mwenye uwezo mdogo, angalau anaweza kwenda kununua maji hayo kwa ajili ya kunywa, lakini wale wasio na uwezo kabisa wanatumia maji yaliyopo ambayo siyo salama,” anaeleza.
Kwa upande wake, mwanakijiji Nanzia Msofe, anasema kuwa wanatumia maji hayo kwakuwa hana namna nyingine.
Mkazi huyo aliyekutwa akichota maji huku ng’ombe wakiwa wanakunywa, anasema hiyo ndiyo hali halisi ya upatikanaji wa maji katika kijiji chao.
Anaiomba Serikali na wadau kuwaletea maji yanayotiririka kutoka mlimani kwani wana hofu zaidi ya afya zao.
Nasoro Mwanagiko ni mtendaji wa Kijiji cha Butu kilichopo Kata ya Jipe, anakiri kuwa kijiji hicho cha jirani kina tatizo kubwa la upatikanaji wa maji safi na salama.
“Hapa Kijiji cha Jipe vilichimbwa visima vitano ambavyo baadhi vilitoa maji mwezi mmoja na vingine havikutoa maji kabisa,” anasema.
Anasema zipo sababu mbalimbali zilizofanya visima hivyo visitoe maji mojawapo ikiwa ni miundombinu ya kiufundi kuwa mibovu.
Hata hivyo, anasema kadhia ya kukosa kabisa maji safi na salama wanakumbana nayo wakati wa kiangazi kwa kuwa maji kutoka mlimani hukatika kabisa.

No comments:

Post a Comment