Tuesday, November 14

Uamuzi wa mbunge waibua mvutano Kibaha


Kibaha. Mvutano umeibuka kwenye Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha baada ya upande mmoja wa madiwani kukataa ombi la Mbunge wa Kibaha Vijijini, Hamoud Jumaa kutaka arudishiwe gari moja kati ya mawili ya kubebea wagonjwa aliyoyakabidhi hivi karibuni ili ampe rafiki yake aliyeyoko mkoani Tabora.
Upande mwingine wa madiwani uliunga mkono hoja hiyo kwa madai kuwa kwa vile Jumaa ndiye aliyeyanunua na kuikabidhi halmashauri hiyo basi pia ana uwezo wa kulichukua tena na kulipeleka popote anapotaka yeye na Kibaha isihoji.
Gari hilo linalohitajika kuchukuliwa na Jumaa na kulipeleka Tabora kwa rafikiye ni SM 11995 ambalo ni miongoni mwa magari matatu yaliyokabidhiwa Julai 24 na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kwemye mkutano wa hadhara uliofanyika Mlandizi mbapo kati yake mawili alinunua Jumaa na moja lilitolewa na Rais.
Kabla ya mvutano huo, mkurugenzi wa halmashauri hiyo Tatu Selemani aliwasilisha ajenda ya ombi la Jumaa ya kuliomba baraza hilo limkubalie achukue gari moja kati ya mawili ya wagonjwa aliyowakabidhi hivi karibuni kwa ajili wananchi wa jimbo hilo.
Baada ya kuwasilishwa hoja hiyo ndipo mjadala ulioendana na minong'ono ya chini chini ulipoanza hatua iliyosababisha Mwenyekiti wa Halmashauri, Mansour Kisebengo kila mara kuwataka madiwani wawe watulivu na kutoa mawazo yao kama apewe au asipewe na sio kutoka nje ya hoja.
Diwani Kata ya Magindu(Chadema), Issa Mkali ambapo amesema hatua ya Jumaa kutaka kuchukua gari alilokwisha wakabidhi wananchi wa jimbo lake ni sawa na kuwanyanganya pamoja na kucheza na maisha ya watu kwani bado upo uhitaji mkubwa wa magari ya wagonjwa.
Mkali amesema siku mbunge huyo alipokabidhi magari hayo ilifanyika sherehe kubwa iliyowakusanya wananchi wa wilaya hiyo na mgeni rasmi alikua Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu hakusema atalichukua baadaye.
“Mwenyekiti mbunge sasa analeta siasa wakati tumeshaambiwa tusubiri 2020, pia anacheza na maisha ya watu, hivi leo unatoa gari mbili tena unampa waziri akusaidie kuyakabidhi halafu baada ya miezi mitatu unakuja kusema unaliomba moja unalipekea mkoa mwingine kwa rafiki yako ana uhitaji mkubwa, kwa huyo sisi watu wafe kwa usiasa wenu huu hapana gari haitoki,"amesema Mkali.
Kwa upande wake Diwani Kata ya Kwala(CCM), Josephin Gunda alimshukuru mbunge kupambana mpaka akapata magari mawili na kuwakabidhi lakini suala la leo kuja na ombi la kuchukuliwa moja ili lipelekwe mkoa mwingine kwa rafiki yake haitawaingia masikioni wapigakura ambao siku ya kutolewa waliitwa wakayapokea.
Pia Gunda alionyesha hofu kuwa kama baraza hilo litaridhia gari hilo lichukuliwe upo uwezekano katika mgao ujao wa Serikali halmashauri hiyo ikakosa maana itaonekana hawana uhitaji mkubwa kwani walishakua na uwezo wa kugawa hata yake machache iliyonayo.
Diwani Viti Maalum, Mariam Shirima amesema mbunge huyo angefanya busara kwa kufanya mbinu zake atafute jingine na akilipata hana haja ya kulihusisha na Kibaha bali alipeleke moja kwa moja kwa rafiki yake huyo lakini sio kutumia jina la halmashauri yao anapoagiza halafu aje ampe mtu wa wilaya na mkoa mwingine.
"Mimi nashauri mbunge atoe maelezo kwa nini ameamua kulichukua hili gari maana sisi hatujui ana nini na isitoshe huyu huyu ndiye juzi juzi alituletea maboksi kibao ya vitabu, ameleta shehena ya madawa na vifaa tiba sidhani kama ana nia mbaya, embu tumsikilize na kama baraza turidhie alichukue tu,"amesema Chezeni Diwani kata ya Soga
Akihitimisha hoja hiyo Jumaa alisema sio kwamba amekurupuka kuomba kulichukua gari hilo bali ana maana yake ambayo hakuweka bayana zaidi ya kusema kuondoka gari hilo kwenda Tabora ni hatua moja wapo ya Kibaha kiendelea kupata misaada mingi zaidi ikiwemo magari mengine mbili za wagonjwa wakati wowote mwishoni mwa mwaka huu.
"Jamani mimi ndiye nimeleta magari mawili sijasaidiwa na mtu hata mmoja humu na pia hata ushuru hakuna aliyenisaidia si halmashauri wala ninyi madiwani mnaobishabisha humu, sasa basi nina akili timamu sio mpumbavu naombeni nipeni hilo gari najua ninachokifanya,"amesema Jumaa
"Nimpe rafiki yangu aliyeko Simbu Wilaya ya Manonga ana uhitaji zaidi hata ya sisi, watu kule wanakufa jamani nimeguswa nikaona nimsaidie maana hata yeye anaweza kuwa msaada kwetu pia huko mbele na pia hamuwezi kujua hata zile kontena za vitabu na madawa nilipatajepataje,"amesema Jumaa.
Baada ya michango hiyo mbalimbali, Mwenyekiti Kisebengo alihoji baraza hilo kama wameridhia na ndipo sauti za "apewe" zilisikika huku za apana zikiwa dhaifu na hivyo hoja hiyo kuitimishwa kwa kuliruhusu gari moja kuondoka kwenda Manonga.

No comments:

Post a Comment