Monday, August 14

Saa mbili za Bill Gates ndani ya Muheza


Kuna mambo ambayo katika hali ya kawaida unaweza usidhanie kama yanaweza kutokea na mojawapo ni hili la tajiri mkubwa duniani, Bill Gates kutumia muda wake kutembelea makazi ya watu wa hali ya chini Muheza na kushiriki nao katika chakula cha mchana.
Mwenyekiti huyo mwenza wa Taasisi ya Bill Gates alitembelea Kijiji cha Kicheba wilayani Muheza kujionea jinsi kazi ya ugawaji dawa za matende na mabusha inavyofanyika nchini ikiwa ni mkakati wa kutokomeza magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele nchini ifikapo mwaka 2020.
Akiwa kijijini hapo, Bill Gates alitembea nyumba kwa nyumba akiwa na lengo la kujifunza namna ugawaji wa dawa hizo unavyofanyika.
Akisimulia ziara hiyo ya aina yake, Mratibu wa Magonjwa yasiyopewa kipaumbele, Dk Upendo Mwingira alisema Gates ambaye amekuwa akitoa msaada kwa Tanzania tangu mwaka 2000, alikuja nchini kuangalia ugawaji huo ili aweze kuchukua uamuzi sahihi kuhusu programu hiyo.
Alisema Gates amekuwa akitoa msaada wa Dola milioni 100 kila mwaka kwa Afrika na bara la Asia, kupitia mashirika mbalimbali kwa ajili ya tafiti mbalimbali za magonjwa, dawa na kutibu magonjwa yasiyopewa kipaumbele ikiwamo mabusha na matende.
“Ni mara ya kwanza amekuja kuangalia zoezi hili linakwendaje nchini, alipenda kutembelea maeneo husika ambako dawa zinagawiwa na alipita nyumba kwa nyumba akiangalia namna wanavyogawa dawa, wanavyopima urefu, wanatoa vidonge vingapi,” alisema.
Alisema wakati wa matembezi hayo, Gates alikuwa anauliza maswali yanayohusiana na ugawaji wa dawa na wapi wanakopata maji ya kunywea dawa hizo.
“Alikuwa anaangalia na mazingira. Alifurahi kuona kuna baadhi ya nyumba walikuwa wanatumia umeme, aliulizia vyoo akaona namna vyoo vya wakazi vilivyo na tulipoenda kwenye zahanati, akaangalia pia chanjo. Nilikuwa naye kwa muda wa saa moja na nusu,” alisema Dk Mwingira.
Alisema tajiri huyo aliulizia kuhusu takwimu za magonjwa yasiyopewa kipaumbele na kutaka kujua shughuli za wakazi wa Kicheba.
Mbali na kuangalia mchakato mzima wa ugawaji wa dawa hizo na kuangalia baadhi ya maeneo muhimu, Dk Mwingira alisema Gates alipenda kujua kuhusu huduma za fedha kupitia mitandao na alikutana na mwananchi mmoja ambaye akizungumza naye kuhusu suala hilo. “Bill Gates amekuwa msaada mkubwa kwetu hasa kwenye eneo la utafiti na sasa hivi anataka kuingia katika mradi huu wa usambazaji wa dawa,” alisema.
Magonjwa yasiyopewa kipaumbele
Kuna kundi la magonjwa takriban 18 yaliyokuwa hayapewi kipaumbele yaliyopo katika ukanda wa tropiki barani Afrika, Asia na Amerika Kusini, ambako pia kuna wadudu wanaoyaeneza na mazingira yanaruhusu maambukizi yake.
Dk Mwingira alisema magonjwa haya yana uhusiano mkubwa na umaskini na kunyanyapaliwa na jamii inayowazunguka.
Pamoja na kuwa hayasababishi vifo kwa haraka, magonjwa haya yanaleta usumbufu mkubwa kwani, wagonjwa huugua kwa muda mrefu, hivyo kutumia rasilimali chache zilizopo na hatimaye kuwaletea umaskini kwa kushindwa kushiriki katika shughuli zao za kila siku.
“Magonjwa haya ni kama usubi, minyoo ya tumbo, kichocho, trakoma (mtoto wa jicho), matende na mabusha.
Athari zinazoletwa na magonjwa haya ni maumivu ya muda mrefu na wakati mwingine ulemavu mkubwa, kudhoofisha ukuaji hasa kwa watoto wenye umri mdogo, kimwili na kiakili pamoja na utapiamlo kwa watoto. Lakini pia husababisha umaskini na kudumaza uchumi wa kaya na hatimaye Taifa.”
Dk Mwingira aliyataja madhara mengine ya magonjwa hayo kuwa ni utumbo kujisokota, upofu unaotokana na trakoma, saratani ya ini na kibofu cha mkojo kutokana kichocho na hatimaye kifo kama mgonjwa hatapata tiba ya mapema.
Alisema Tanzania imekuwa ikitekeleza mpango wa udhibiti wa magonjwa hayo katika halmashauri zote nchini.
“Lengo la mpango huu ni kudhibiti maambukizi ya magonjwa haya kulingana na azimio la nchi wanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO) No. 66.12 la mwaka 2013, tunao mpango mkakati ambao ni dira ya kudhibiti na kutokomeza magonjwa haya nchini,” alisema Dk Mwingira.
Alisema ni jambo la kujivunia kuwa jitihada hizo zinaonyesha matunda sasa ambako tathmini zinaonyesha kuwa kiwango cha maambukizi kimepungua katika halmashauri nyingi nchini.
“Mwaka huu, Serikali kwa kushirikiana na wadau tutaendelea kutoa dawa za kingatiba ya matende na usubi kwa wananchi milioni 15 kutoka halmashauri 47 na dawa za trakoma kwa wananchi takriban milioni 5.2 wa halmashauri 21. Ugawaji wa dawa za kingatiba za minyoo utaendelea kwa halmashauri zote 186 na kichocho katika halmashauri 126 zenye watoto takriban milioni 9.5 wa umri wa kwenda Shule.”

Waziri Tizeba awa ‘mbogo’


Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba ametaka sheria iliyounda Bodi ya Kahawa (TCB) iangaliwe upya ili chombo hicho kibebe jukumu la kusimamia uzalishaji kahawa.
Dk Tizeba amemtaka mwanasheria wa TCB, Engerasia Mongi kwenda Dar es Salaam mara moja, ili kushirikiana na wanasheria wa wizara kuanza mchakato wa kubadili sheria hiyo.
Waziri Tizeba alionyesha kukerwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCB, Primus Kimaryo aliposema kwamba moja ya majukumu ya bodi hiyo ni kusimamia sekta ya kahawa na sio uzalishaji.
Katika mazungumzo hayo ilibainika kuwa jukumu la kusimamia uzalishaji wa kahawa limeachwa kwa halmashauri za wilaya, ambazo kwa maoni ya waziri, zina mazao mengi ya kusimamia.
“Haileti afya. Kuna vacuum (ombwe) kubwa namna hii! Nataka tukubaliane suala la uzalishaji wa kahawa nchini halina mwenyewe. Halmashauri haziwezi kwa sababu zina mazao mengi,” alisema.
“Kama kazi yako ni ku monitor (kusimamia) tu maana yake you are not responsible (huwajibiki). Lingekuwa ni jukumu la bodi kungekuwa na kitengo kabisa cha uzalishaji Kahawa,” alisema.
“Mwanasheria nenda wizarani kamtafute mkurugenzi wa maendeleo ya mazao, mlete muswada Septemba hii ili tuiongezee bodi jukumu la kusimamia uzalishaji wa kahawa. “Kumbe hata pesa nimewaachia nyingi za nini kama hamsimamii kuongezeka kwa uzalishaji wa kahawa nchini?
“Nilikuwa najiuliza kwa nini uzalishaji wa kahawa uko stagnant (umedorora) kumbe haina mwenyewe! Tutabadilisha majukumu yenu. Huwezi kusimamia kitu hakipo,” alisema.
Waziri Tizeba alisema katika marekebisho hayo ya sheria namba 23 ya mwaka 2001, kama ilivyorekebishwa na Sheria ya Mazao namba 20 ya mwaka 2009, jukumu la uzalishaji liwe la kwanza.
Katika mazungumzo hayo na wafanyanyakazi na menejimenti ya bodi hiyo, Katibu Tawala (RAS) wa Mkoa Kilimanjaro, Aisha Amour alipendekeza sheria yote iliyounda bodi ipitiwe upya.
Awali, Kimaryo alisema majukumu ya bodi ni kusimamia sekta ya kahawa na kuratibu majukumu shirikishi ya wadau wa kahawa ikiwamo uzalishaji kahawa.
Akitembelea eneo la ushughulikiaji sampuli za kahawa, Dk Tizeba aliitaka bodi hiyo kutafuta dawa ya kudumu kudhibiti uvushaji wa kahawa kimagendo kwenda nchi jirani na kuitaka kutafuta njia bora za kuvifanya vyama vya ushirika mkoani Kagera, kununua kahawa kwa bei ya juu kama ile inayotolewa na kampuni za Uganda.
Inadaiwa mwaka 2015, tani 12,000 za kahawa zilisafirishwa kimagendo kupitia Kagera.

Chadema wadhamiria kurejesha majimbo


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Serengeti kimeanza mikakati ya kurejesha majimbo waliyopoteza katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2015.
Majimbo yaliyochukuliwa na CCM katika kanda hiyo yenye Mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga ni pamoja na jimbo la Musoma mjini (Mara), Maswa, Meatu Mashariki na Magharibi yote ya Mkoa wa Simiyu.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kanda hiyo, John Heche katika kikao cha viongozi wa chadema kanda hiyo kilichofanyika jijini Mwanza jana.
Heche ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Tarime vijijini amesema katika kikao hicho wamewaagiza viongozi waende kwenye majimbo kukaa vikao vya ndani kuanzia ngazi ya msingi hadi kanda kuweka misingi itakayokiwezesha kushinda kwa kishindo uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2019 na Uchaguzi mkuu 2020.
“Tumetoka na maazimio kadhaa, kwanza viongozi wanapotoka hapa kuanzia ngazi za mashina wakafanye vikao vya ndani lengo ni kukomboa majimbo tuliyopokonywa, hiyo ni kwa ajili ya maendeleo kwa mfano ukiangalia halmashauri zinazoongozwa na Chadema zinaongoza kwa miradi ya maendeleo,” amesema Heche
Pia, amewataka wanachama kutokata tamaa kuhusiana na matukio ya kidhalimu yanayondelea ya kuwakamata na kuwaweka ndani viongozi wa chama hicho na kuzuia mikutano ya hadhara ambayo imeruhusiwa kikatiba, badala yake waendelee kupambana mpaka ushindi utapatikana.
Amesema kuna vitisho vingi vinavyotolewa dhidi ya viongozi vikilenga kufifisha demokrasia na nafasi ya watu kushindana kisiasa ili watu waamini CCM kwa nguvu, lakini watapambana navyo bila kuchoka hadi hatua ya mwisho.
“Kuanzia wenyeviti, madiwani na wabunge, wanaokamatwa na kutishwa, tutawalinda na kuendelea kuwapa ushirikiano msaada wowote kisheria hata wanachama wanaotishiwa na kushindwa kufanya kazi zao,” amesema Heche
Mbunge Viti Maalumu Mkoa wa Shinyanga, Salome Makamba amesema kadri serikali inavyozidi kutumia nguvu kubwa kudhibiti kuiminya demokrasia, ndivyo inavyozidi kuwapa nafasi ya kufanya maamuzi magumu na picha mbaya “sio tu kwamba chadema huwa hatushindi, tunashinda ila hatutangazwi.”
Mbunge viti Maalumu Mkoa wa Mara, Catherine Ruge amesema rasilimali kubwa waliyonayo ni nguvu ya umma hivyo watwalinda viongozi wote wanaofanyiwa vitendo vya uzalilishaji kwa kutumia pia msaada wa sheria.

Waziri Mkuu aagiza wananchi wasizuiwe kuonyesha mabango


Robert Kakwesi na Peter Elias, Mwananchi mwananchi@mwananchi.co.tz
Sikonge/Dar. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametaka mabango yanayoonyeshwa na wananchi kwa viongozi wa kitaifa wanapowatembelea yasiwe yanazuiwa kwa vile yanakuwa yanaelezea changamoto wanazokabiliana nazo.
Majaliwa alisema hayo baada ya kuona mabango yaliyoinuliwa na wananchi kwenye mkutano wake na wananchi mwishoni mwa juma lililopita mjini Sikonge mkoani Tabora huku wananchi hao wakitakiwa kuyashusha.
“Siku nyingine msirudie na kuanzia sasa waacheni wananchi waonyeshe mabango yao kwani ndiyo njia wanayotumia kuonyesha hisia zao kwa yale wanayokumbana nayo na kuwasababishia kero,” alisema Majaliwa.
Kutokana na hali hiyo, Waziri Mkuu aliwaagiza wasaidizi wake wayakusanye mabango yote wayaandike kisha wampelekee yaliyomo akiahidi kwamba atayafanyia kazi.
Alieleza kuwa malalamiko mengi kwenye mabango hayo yanahusu kero za vyama vya msingi vya ushirika na migogoro ya ardhi na kumtaka Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri kutenga siku kwa ajili ya kusikiliza kero za wananchi huku akiwa na wakuu wa idara mbalimbali.
Hiyo siyo mara ya kwanza kwa wananchi kuinua mabango kwa viongozi wa kitaifa. Julai 22 huko Kigoma wakati wa ziara ya Rais John Magufuli, wananchi waliinua mabango yao ili ayasome huku wakizuiwa na walinzi.
“Waacheni, waacheni tu jamani…jamani mtulie nitayasoma yote. Nimeyaona yote ndiyo maana nayapitia na wasaidizi wangu wanayapiga picha nyinyi msiwe na wasiwasi,” alisema Rais Magufuli wakati akihutubia katika Uwanja wa Lake Tanganyika huku wananchi wakikazana kumwonyesha mabango yao.
Hali kama hiyo ilijitokeza tena huko Tabora Julai 23, wakati Rais Magufuli akiwahutubia wananchi na kuwataka washushe mabango yao kwa sababu wananchi walikuwa wakipiga kelele, jambo lililokatisha hotuba yake.
“Naomba myashushe mabango yenu ili niendelee na hotuba yangu,” alisema Rais Magufuli lakini wananchi waliendelea kuyainua juu, jambo lililoonyesha kumkera, “Nimesema shusheni hayo mabango, la sivyo siyashughulikii. Ukitaka hata ukayatandike kwenye kitanda cha mke wako, siyasomi.”
Akitoa maoni yake kuhusu vitendo vya wananchi kuinua mabango yao kwa viongozi wa kitaifa, Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Benson Bana alisema hiyo inaonyesha kukua kwa demokrasia nchini.
Alisema wananchi wanatafuta namna ya kufikisha ujumbe kwa viongozi wa kitaifa juu ya mambo ambayo Serikali za mitaa au mkoa zimeshindwa kukabilaiana nazo au wameshindwa namna ya kuwafikia.
“Huko ndiko kupevuka kwenyewe na kukua kwa demokrasia. Viongozi kwenye maeneo hayo wameshindwa kutatua kero za wananchi ndiyo maana wananchi wanaona bora watumie fursa ya kueleza kero zao kupitia mabango,” alisema.
Mwanazuoni huyo alisisitiza kwamba kuna haja ya kuimarisha mifumo ya mawasiliano kati ya wananchi na viongozi wao wa Serikali za mitaa mpaka mkoa ili kumaliza changamoto zao bila kuzifikisha kwa viongozi wa kitaifa.
“Viongozi wa mikoa wawe na mawasiliano ya karibu na wananchi, wawe wanajibu meseji zao na kuwafikia katika maeneo yao. Hiyo itasaidia kupunguza mabango kwa viongozi, japo siyo jambo baya pia kuinua mabango,” alisema.
Katibu Mkuu wa Chama cha Kijamii (CCK), Renatus Muabhi alisema kitendo cha wananchi kuonyesha mabango kwa viongozi kinaonyesha udhaifu wa Serikali katika kukabiliana na changamoto za jamii husika.
Alisema mara nyingi askari wamekuwa wakiwazuia wananchi kupaza sauti zao ndiyo maana nao wameamua kuja na mtindo wa kutumia mabango kufikisha ujumbe kwa viongozi wao wa kitaifa. “Katiba yetu inaruhusu uhuru wa kutoa maoni bila kujali kwamba yatawafurahisha au kuwakera viongozi. Askari wasitumie nguvu kuwanyamazisha wananchi kwa sababu ni haki yao ya msingi,” alisema Muabhi.
Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu) alimpongeza Waziri Mkuu kwa kutambua umuhimu wa sauti ya umma na kusisitiza kwamba hiyo ni njia moja wapo ya kufikisha ujumbe kwa wananchi.
Alisema siyo jambo baya kwa wananchi kuinua mabango yao kwa viongozi kwa sababu wakati mwingine wanawakumbusha juu ya mambo ambayo wanatakiwa kuyafanyia kazi.

Mbowe akomaa na Rais Magufuli


Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, amemtaka Rais John Magufuli kurejesha nyumba za Serikali alizouza wakati wa utawala wa Benjamin Mkapa.
Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, alisema kama kweli Rais Magufuli anachukia ufisadi, arejeshe nyumba hizo.
Alipoulizwa kuhusu madai hayo, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa alisema hajamsikia Mbowe. Hata hivyo, alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa sababu hayo ni mambo ya kisiasa.
Mbunge huyo wa Hai, alitoa kauli hiyo jana na juzi katika mikutano ya hadhara aliyoifanya katika vijiji vya Kakavu Chini na Nronga katika jimbo hilo, ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake.
Mbowe alisema kwa muda mrefu, walikuwa wanaiambia Serikali ya CCM kuwa kuna ufisadi ulifanyika katika ubinafsishaji viwanda, mashamba makubwa, mashirika ya umma na uuzaji nyumba za Serikali.
“Wakati tukipiga kelele hii, Magufuli alikuwa kwenye Baraza la Mawaziri. Magufuli amekuwa waziri kwa miaka 20. Niliingia bungeni mara ya kwanza tuliingia na Magufuli,” alisema Mbowe.
“Kwa hiyo amekuwa katika Baraza la Mawaziri ambalo lilifanya mikataba yote ya kupitisha kuuza madini, kubinafsisha viwanda na mashirika ya umma,” alisema na kuongeza:
“Tena akiwa waziri alihusika namba moja kuuza nyumba zote za Serikali. Tunamwambia Magufuli kama wewe hupendi ufisadi tunataka na nyumba za Serikali ambazo uliziuza wakati wa Mkapa. Karejeshe nyumba za wananchi zitumike na viongozi wa Serikali wa leo ambao wanahitaji nyumba. Leo kuna viongozi wa Serikali wanaishi hotelini kwa sababu nyumba zote ziliuzwa.
“Lakini kitu kimoja ambacho tunalia na Magufuli ni namna Rais anavyozuia uhuru wa Watanzania.”
Mbowe alisema ingawa Tanzania inaongozwa na Katiba ya mwaka 1977 ambayo ndiyo sheria mama, lakini bado kumekuwa na ukandamizaji wa uhuru wa kujieleza ambao ni takwa la kikatiba.
“Katiba ndiyo inaelekeza nini ni haki na nini si haki katika nchi. Kwa lugha ya Kiingereza ni mkataba wa kikatiba wanauita social contract kati ya watawala na watawaliwa.
“Huo ni mkataba. Mwaka 1992 tulikubaliana kuanza mfumo wa vyama vingi vya siasa. Tunamwambia acha vyama vya siasa vichuane. Kila kimoja kionyeshe sera zake za kuwaletea wananchi maendeleo.
“Wananchi wapewe uhuru wa kuamua kwenda Chadema sawa wakiamua kwenda CCM sawa, wakiamua kwenda CUF ni sawa. Vyama vishindanishe sera wananchi wapate chaguo.
“Kama vile ambavyo Taifa letu lina uhuru wa kuabudu, vilevile Taifa letu lina uhuru wa kila mmoja kuwa kwenye chama cha siasa anachokipenda na kufanya mikutano ya kisiasa ya hadhara.
“Lakini nchini mwetu Rais anageuza vyama vingi ni uadui na ni uhasama. Unapokuwa Rais wa nchi unakuwa Rais wa wote.”
Katika mikutano hiyo, Mbowe alifuatana na viongozi mbalimbali wa Chadema akiwamo katibu wa Mkoa Kilimanjaro, Basil Lema na Mbunge wa Viti Maalumu, Grace Kiwelu.
Bana amshauri Mbowe
Alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu kauli ya Mbowe, Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Benson Bana alisema uuzaji wa nyumba za Serikali ni sera mbaya lakini haikuwa uamuzi wa Rais Magufuli kwani yeye alikuwa waziri tu.
‘‘Ninachoweza kumshauri Mbowe ni kwamba aende bungeni apeleke hoja binafsi kuhusu hizo nyumba ili ziweze kurudishwa kwa sababu wengi waliouzwa wameshapangisha na wengine wameuza,” alisema Profesa Bana.
Alisema hakuna sababu ya kumlaumu Rais Magufuli kwa sababu alikuwa kwenye Baraza la Mawaziri na kwa mujibu wa sheria, baraza la mawaziri linamshauri Rais tu.
‘‘Hivyo ninamshauri rafiki yangu Mbowe aende na hoja binafsi bungeni kwa mujibu wa sheria ili zile nyumba zirudishwe lakini siyo kumrushia lawama Rais Magufuli,’’ alisema.
Akizungumza na wananchi, Kiwelu aliwataka kupuuza propaganda zinazoenezwa na baadhi ya viongozi wa CCM, kuwa Mbowe amewatelekeza mara tu baada ya kumchagua.
Alisema wananchi wa Jimbo hilo wana bahati ya kumchagua mbunge ambaye amekuja kukabidhiwa majukumu ya kitaifa ya kuwa kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni.
Alisema pamoja na kuwa ni kiongozi wa kitaifa, bado ameendelea kushirikiana na wananchi wa jimbo hilo kuwaletea maendeleo huku akisema watarajie mambo makubwa zaidi katika maendeleo.
Katika ziara hizo, Mbowe anayefuatana pia na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Hai, Helga Mchomvu, alitembelea miradi mbalimbali ya maendeleo katika vitongoji vya jimbo hilo na kushiriki katika shughuli za kijamii.

Wanawake waitaka Serikali kuongeza bajeti ya kilimo


Wanawake wanaounda Jukwaa la wakulima wadogo nchini wameitaka serikali kuongeza bajeti kwenye sekta ya kilimo ili wakulima waweze kuzalisha kwa wingi na kulisha viwanda.
Wito huo umetolewa leo na Rais wa jukwaa hilo kanda ya Afrika, Eva Mageni kwenye kongamano la wakulima hao lililofanyika mjini hapa lililokuwa na lengo la kujadili changamoto mbalimbali wanazokutana nazo na jinsi ya kuzitatua katika sekta ya kilimo.
Mageni amesema kuwa kama serikali itaendelea kutenga kiasi kidogo cha fedha kwenye bajeti ya kilimo ni wazi kuwa azma ya serikali ya kufikia uchumi wa kati haitafikiwa kutokana na asilimia zaidi ya 70 ya watanzania kujiajiri kwenye sekta ya kilimo.
"Kama kweli serikali ina nia thabiti ya kufikia uchumi wa viwanda ni lazima iongeze bajeti yake ya kilimo kutoka asilimia 4.6 ya sasa hadi kufikia asilimia 10 ili kuwawezesha wakulima ambao ndiyo wazalishaji wakubwa wa malighafi za viwandani kuwa na vitendea kazi vya kutosha," amesema Mageni
Mbali na hilo ameitaka serikali kuajiri maofisa ugani ikibidi kwa kila kijiji ili waweze kuwasaidia wakulima kukabiliana na changamoto mbalimbali katika shughuli zao hasa mabadiliko ya tabia nchi.
Amesema idadi ya maofisa ugani iliyopo kwa sasa nchini haikidhi mahitaji ya wakulima kwa kuwa wapo mmoja mmoja kwa kila Kata hivyo wanashindwa kuwahudumia wakulima kama inavyotakiwa.

Mbunge alia na unyanyasaji


Mbunge wa Viti Maalumu wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Anatropia Theonest(Chadema) amesema watoto 244 wamefanyiwa vitendo vya unyanyasaji katika halmashauri hiyo kwa kipindi cha robo tatu ya mwaka huu. 
Akizungumza leo, Agosti 13 Mbunge huyo amesema takwimu zilitolewa na Idara ya Ustawi wa jamii kwenye baraza la Madiwani zimeonyesha kati yao 85 walibakwa, 74 wakitelekezwa na 20 walilawitiwa.
Amesema matukio hayo yameongezeka kutoka 107 mwaka 2006 huku mtoto wa kike akiwa kwenye hatari ya kukosa haki ya elimu kutokana na kupata mimba.
"Ni lazima tusimame kwa pamoja tuweze kupaza sauti kwasababu tukiacha vitendo hivi viendelee tutajenga kizazi cha aina gani? cha walemavu?,"alisema 
Aidha, amesema atawasilisha bungeni hoja binafsi ya kutaka marekebisho ya Sheria ya mwaka 1979 ili kuwapa haki watoto wanaopata mimba kupata haki ya kuendelea na masomo.

Iran yapitisha mswada wa kuboresha programu ya makombora

Sayyad-3 missiles on display at an undisclosed location in Iran, 22 July 2017

Haki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionIran yapitisha mswada wa kuboresha programu yake ya makombora
Bunge la Iran limepitisha mswada wa kutenga zaidi ya dola nusu bilioni zaidi, kwa ajili ya mradi wa makombora.
Iran inajibu vikwazo vya karibuni kabisa, vilivyowekwa na Marekani dhidi ya nchi hiyo.
Vyombo vya habari vya taifa, vinasema, fedha hizo zinakusudiwa kupambana na vile vilivoitwa, vitendo vya kigaidi vya Marekani katika Mashariki ya Kati.
Mswada huo utaweka vikwazo dhidi ya wanajeshi pamoja na maafisa wa ujasusi wa Marekani.
Mpatanishi mkuu wa Iran katika mazungumzo kuhusu mradi wake wa nuklia, Abbas Araqchi, amesema, mswada huo mpya, umeungwa mkono na wizara ya mashauri ya nchi za nje, na kwamba hauendi kinyume na makubaliano ya mwaka 2015, yaliyozuia mradi wa nuklia wa Iran.
Makubaliano kuhusu programu ya nuklia kati ya Iran na mataifa sita yenye nguvu duniani ikiwemo China, Urusi na Uingereza,, yanaonekana kwa kiwango kikubwa kama njia mwafaka ya kuizuia Iran kuunda zana za nuklia.
Makubaliano hayo yalisababisha vikwazo vibaya kwa uchumi wa Iran kuondolewa, ili nchi hiyo ipate kupunguza programu zake za nuklia.

Jeshi la Uganda lasema halina mpango wa kuingia Kenya

Pata usaidizi kuhusu Me la Uganda Jeshi la Uganda la UPDF limekanusha taarifa kuwa liko tayari kuingia nchini Kenya kusaidia kudhibiti hali ya usalama nchini humo baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa wiki iliyopita.
Rais Uhuru Kenyatta alitangazwa mshindi, huku mpinzani wake mkuu Raila Odinga akiyapinga matokeo hayo.
Waziri wa mawasiliano nchini humo Frank Tumwebaze amesema jeshi la Uganda haliwezi kutumwa nje kushiriki operesheni ya kijeshi kisiri.
Msemaji wa jeshi la Uganda Richard Karemire, kupitia taarifa, amesema Kenya ni nchi huru na usalama wake umo chini ya serikali ya nchi hiyo.
Aidha, amesema Uganda haijapokea ombi kutoka kwa Kenya kutuma majeshi yake nchini humo au kuomba usaidizi.
Mwandishi wa BBC Siraj Kalyango anaarifu zaidi.

Watu 17 wauawa katika shambulio mji wa Ouagadougou, Burkina Faso

Police are seen on a street following an attack by gunmen on a restaurant in Ouagadougou, Burkina Faso

Haki miliki ya pichaREUTERS
Image captionPolisi wakiwa na gari lisilopenya risasi walifika eneo hilo kukabiliana na washambuliaji
Watu 17 wameuawa na wengine wanane kujeruhiwa katika shambulio la kigaidi lililotekelezwa katikati ya mji mkuu wa Burkina Faso, Ouagadougou, serikali ya nchi hiyo imesema.
Watu walioshuhudia wamenukuliwa wakisema kwamba watu watatu waliokuwa na bunduki waliwafyatulia risasi wateja waliokuwa nje ya hoteli moja na mgahawa.
Eneo la katikati mwa jiji limezingirwa na maafisa wa jeshi na ubalozi wa Marekani mjini Ouagadougou umewatahadharisha raia wake wasiende eneo hilo.
Watu 30 waliuawa katika shambulio la kijihadi katika mgahawa mdogo ulio karibu na hapo Januari mwaka jana.
Kuna wasiwasi kwamba shambulio hilo huenda limetekelezwa na moja ya washirika wa mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda ambao bado wanaendesha shughuli zao katika eneo la Sahel, mwandishi wa BBC Alex Duval Smith amesema.
Waziri wa mawasiliano wa Burkina Faso Remis Dandjinou amesema haijabainika ni washambuliaji wangapi hasa waliohusika.
"Wamejibanza katika sehemu moja ya jumba waliloshambulia. Maafisa wa usalama wanaendesha oparesheni ya kuwafurusha," amesema kwenye televisheni.
Ufyatuaji wa risasi ulianza muda mfupi baada ya 21:00 (21:00 GMT) siku ya Jumapili katika barabara yenye shughuli nyingi ya Kwame Nkrumah.
Maeneo mawili, Hotel Bravia na Aziz Istanbul Restaurant, yanaonekana kulengwa na washambuliaji.
"Shambulio lilisababisha vifo vya watu 17, ambao uraia wake bado haujathibitishwa, na wanane wamejeruhiwa," taarifa ya serikali iliyonukuliwa na shirika la habari la AFP inasema.
Ouagadougou, Burkina FasoHaki miliki ya pichaREUTERS
Image captionMmoja wa waliojeruhiwa akiwa ameketi chini
Hospitali moja mjini humo ilisema mmoja wa waliouawa ni raia wa Uturuki.
Shambulio hilo linakaribiana sana na shambulio lililotekelezwa Januari 2016 ambapo watu wenye silaha walishambulia hoteli ya Splendid Hotel na mgahawa wa karibu wa Cappucino, pia katika barabara ya Kwame Nkrumah Avenue.
Watu zaidi ya 170 walishikwa mateka na 30 wakauawa.
Al-Qaeda walikiri kuhusika.
Burkina Faso inapatikana katika eneo la Sahel, ambalo linajumuisha pia nchi ya Mali ambapo makundi ya Kiislamu yamekuwa yakitekeleza mashambulio tangu mwaka 2012.
Map of West Africa


Uchaguzi Kenya

Raila Odinga awashauri wafuasi wa upinzani kususia kazi Jumatatu

Raila Odinga Kibera, Nairobi, Kenya Agosti 13, 2017Haki miliki ya pichaREUTERS
Image captionBw Odinga alikariri madai yake ya awali kwamba serikali ya Bw Kenyatta iliiba kura, ingawa waangalizi wa uchaguzi wamesema uchaguzi ulikuwa huru na wa haki
Kinara wa muungano upinzani nchini Kenya Raila Odinga, amewashauri wafuasi wake kususia kazi siku ya Jumatatu kama njia ya kupinga matokeo ya uchaguzi uliofanyika Jumanne iliyopita.
Akihutubia wafuasi wake mtaani Kibera, Nairobi kwa mara ya kwanza kabisa tangu kutangazwa matokeo, ambapo Rais Uhuru Kenyatta alitangazwa mshindi, Bw Odinga amedai kuwa serikali ilikiwa imepanga kuwaua wafuasi wa upinzani kabla ya kutangazwa matokeo.
Hii ni siku moja baada wa watu kadha kuripotiwa kuuawa maeneo tofauti ya mji wa Nairobi na Kisumu, wakati wafuasi wa upinzani walijitokeza kulalamikia matokeo ya uchaguzi
Wafuasi wa upinzani wakiandana mtaa wa Mathare NairobiHaki miliki ya pichaEPA
Image captionWafuasi wa upinzani wakiandana mtaa wa Mathare Nairobi
Aidha Odinga amesema kuwa siku ya Jumanne, mrengo wa Nasa utatangaza mwelekeo ambao utachukua.
Bw Odinga baadaye alizuru mtaa wa Mathare Kaskazini jijini Nairobi ambapo msichana wa miaka tisa alifariki baada ya kupigwa risasi wakati wa makabiliano kati ya polisi na waandamanaji.
Rais Uhuru Kenyatta alitangazwa mashindi kwa kura 8,203,290 huku naye Raia Odinga akipata kura 6,762,224.
Katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan, ambaye alikuwa mpatanishi mkuu baada ya mzozo wa kisiasa nchini Kenya miaka kumi iliyopita, alikuwa ametoa wito kwa Bw Odinga kutumia mifumo ya kisheria kutafuta haki kuhusu matokeo ya uchaguzi wa urais.
Raila OdingaHaki miliki ya pichaEPA
Image captionWafuasi wengi wa Bw Odinga walihudhuria mkutano huo uwanja wa Kamukunji mtaa wa Kibera, Nairobi
Polisi wa kupambana na ghasia mjini KisumuHaki miliki ya pichaREUTERS
Image captionPolisi wa kupambana na ghasia mjini Kisumu
Bw Annan alikuwa mpatanishi mkuu baada ya ghasia kuzuka baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 uliokumbwa na utata.
"Namshukuru kiongozi wa upinzani Raila Odinga kwa kampeni ya uchaguzi ya amani aliyoiendesha. Amekuwa mtetezi jasiri wa demokrasia," amesema Dkt Annan kupitia taarifa.
"Kwa hivyo, namhimiza sasa afuatilie malalamiko yake kupitia mifumo ya kisheria iliyowekwa na aweke maslahi ya taifa mbele, kama alivyofanya kwa uzalendo mara nyingi awali."
Mwaka 2007, watu zaidi ya 1,000 walifariki na wengine 600,000 wakafurushwa makwao wakati wa ghasia za kikabila zilizozuka baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa.