Monday, August 14

Mbowe akomaa na Rais Magufuli


Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, amemtaka Rais John Magufuli kurejesha nyumba za Serikali alizouza wakati wa utawala wa Benjamin Mkapa.
Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, alisema kama kweli Rais Magufuli anachukia ufisadi, arejeshe nyumba hizo.
Alipoulizwa kuhusu madai hayo, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa alisema hajamsikia Mbowe. Hata hivyo, alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa sababu hayo ni mambo ya kisiasa.
Mbunge huyo wa Hai, alitoa kauli hiyo jana na juzi katika mikutano ya hadhara aliyoifanya katika vijiji vya Kakavu Chini na Nronga katika jimbo hilo, ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake.
Mbowe alisema kwa muda mrefu, walikuwa wanaiambia Serikali ya CCM kuwa kuna ufisadi ulifanyika katika ubinafsishaji viwanda, mashamba makubwa, mashirika ya umma na uuzaji nyumba za Serikali.
“Wakati tukipiga kelele hii, Magufuli alikuwa kwenye Baraza la Mawaziri. Magufuli amekuwa waziri kwa miaka 20. Niliingia bungeni mara ya kwanza tuliingia na Magufuli,” alisema Mbowe.
“Kwa hiyo amekuwa katika Baraza la Mawaziri ambalo lilifanya mikataba yote ya kupitisha kuuza madini, kubinafsisha viwanda na mashirika ya umma,” alisema na kuongeza:
“Tena akiwa waziri alihusika namba moja kuuza nyumba zote za Serikali. Tunamwambia Magufuli kama wewe hupendi ufisadi tunataka na nyumba za Serikali ambazo uliziuza wakati wa Mkapa. Karejeshe nyumba za wananchi zitumike na viongozi wa Serikali wa leo ambao wanahitaji nyumba. Leo kuna viongozi wa Serikali wanaishi hotelini kwa sababu nyumba zote ziliuzwa.
“Lakini kitu kimoja ambacho tunalia na Magufuli ni namna Rais anavyozuia uhuru wa Watanzania.”
Mbowe alisema ingawa Tanzania inaongozwa na Katiba ya mwaka 1977 ambayo ndiyo sheria mama, lakini bado kumekuwa na ukandamizaji wa uhuru wa kujieleza ambao ni takwa la kikatiba.
“Katiba ndiyo inaelekeza nini ni haki na nini si haki katika nchi. Kwa lugha ya Kiingereza ni mkataba wa kikatiba wanauita social contract kati ya watawala na watawaliwa.
“Huo ni mkataba. Mwaka 1992 tulikubaliana kuanza mfumo wa vyama vingi vya siasa. Tunamwambia acha vyama vya siasa vichuane. Kila kimoja kionyeshe sera zake za kuwaletea wananchi maendeleo.
“Wananchi wapewe uhuru wa kuamua kwenda Chadema sawa wakiamua kwenda CCM sawa, wakiamua kwenda CUF ni sawa. Vyama vishindanishe sera wananchi wapate chaguo.
“Kama vile ambavyo Taifa letu lina uhuru wa kuabudu, vilevile Taifa letu lina uhuru wa kila mmoja kuwa kwenye chama cha siasa anachokipenda na kufanya mikutano ya kisiasa ya hadhara.
“Lakini nchini mwetu Rais anageuza vyama vingi ni uadui na ni uhasama. Unapokuwa Rais wa nchi unakuwa Rais wa wote.”
Katika mikutano hiyo, Mbowe alifuatana na viongozi mbalimbali wa Chadema akiwamo katibu wa Mkoa Kilimanjaro, Basil Lema na Mbunge wa Viti Maalumu, Grace Kiwelu.
Bana amshauri Mbowe
Alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu kauli ya Mbowe, Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Benson Bana alisema uuzaji wa nyumba za Serikali ni sera mbaya lakini haikuwa uamuzi wa Rais Magufuli kwani yeye alikuwa waziri tu.
‘‘Ninachoweza kumshauri Mbowe ni kwamba aende bungeni apeleke hoja binafsi kuhusu hizo nyumba ili ziweze kurudishwa kwa sababu wengi waliouzwa wameshapangisha na wengine wameuza,” alisema Profesa Bana.
Alisema hakuna sababu ya kumlaumu Rais Magufuli kwa sababu alikuwa kwenye Baraza la Mawaziri na kwa mujibu wa sheria, baraza la mawaziri linamshauri Rais tu.
‘‘Hivyo ninamshauri rafiki yangu Mbowe aende na hoja binafsi bungeni kwa mujibu wa sheria ili zile nyumba zirudishwe lakini siyo kumrushia lawama Rais Magufuli,’’ alisema.
Akizungumza na wananchi, Kiwelu aliwataka kupuuza propaganda zinazoenezwa na baadhi ya viongozi wa CCM, kuwa Mbowe amewatelekeza mara tu baada ya kumchagua.
Alisema wananchi wa Jimbo hilo wana bahati ya kumchagua mbunge ambaye amekuja kukabidhiwa majukumu ya kitaifa ya kuwa kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni.
Alisema pamoja na kuwa ni kiongozi wa kitaifa, bado ameendelea kushirikiana na wananchi wa jimbo hilo kuwaletea maendeleo huku akisema watarajie mambo makubwa zaidi katika maendeleo.
Katika ziara hizo, Mbowe anayefuatana pia na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Hai, Helga Mchomvu, alitembelea miradi mbalimbali ya maendeleo katika vitongoji vya jimbo hilo na kushiriki katika shughuli za kijamii.

No comments:

Post a Comment