Monday, August 14

Wanawake waitaka Serikali kuongeza bajeti ya kilimo


Wanawake wanaounda Jukwaa la wakulima wadogo nchini wameitaka serikali kuongeza bajeti kwenye sekta ya kilimo ili wakulima waweze kuzalisha kwa wingi na kulisha viwanda.
Wito huo umetolewa leo na Rais wa jukwaa hilo kanda ya Afrika, Eva Mageni kwenye kongamano la wakulima hao lililofanyika mjini hapa lililokuwa na lengo la kujadili changamoto mbalimbali wanazokutana nazo na jinsi ya kuzitatua katika sekta ya kilimo.
Mageni amesema kuwa kama serikali itaendelea kutenga kiasi kidogo cha fedha kwenye bajeti ya kilimo ni wazi kuwa azma ya serikali ya kufikia uchumi wa kati haitafikiwa kutokana na asilimia zaidi ya 70 ya watanzania kujiajiri kwenye sekta ya kilimo.
"Kama kweli serikali ina nia thabiti ya kufikia uchumi wa viwanda ni lazima iongeze bajeti yake ya kilimo kutoka asilimia 4.6 ya sasa hadi kufikia asilimia 10 ili kuwawezesha wakulima ambao ndiyo wazalishaji wakubwa wa malighafi za viwandani kuwa na vitendea kazi vya kutosha," amesema Mageni
Mbali na hilo ameitaka serikali kuajiri maofisa ugani ikibidi kwa kila kijiji ili waweze kuwasaidia wakulima kukabiliana na changamoto mbalimbali katika shughuli zao hasa mabadiliko ya tabia nchi.
Amesema idadi ya maofisa ugani iliyopo kwa sasa nchini haikidhi mahitaji ya wakulima kwa kuwa wapo mmoja mmoja kwa kila Kata hivyo wanashindwa kuwahudumia wakulima kama inavyotakiwa.

No comments:

Post a Comment