Mwenyekiti huyo mwenza wa Taasisi ya Bill Gates alitembelea Kijiji cha Kicheba wilayani Muheza kujionea jinsi kazi ya ugawaji dawa za matende na mabusha inavyofanyika nchini ikiwa ni mkakati wa kutokomeza magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele nchini ifikapo mwaka 2020.
Akiwa kijijini hapo, Bill Gates alitembea nyumba kwa nyumba akiwa na lengo la kujifunza namna ugawaji wa dawa hizo unavyofanyika.
Akisimulia ziara hiyo ya aina yake, Mratibu wa Magonjwa yasiyopewa kipaumbele, Dk Upendo Mwingira alisema Gates ambaye amekuwa akitoa msaada kwa Tanzania tangu mwaka 2000, alikuja nchini kuangalia ugawaji huo ili aweze kuchukua uamuzi sahihi kuhusu programu hiyo.
Alisema Gates amekuwa akitoa msaada wa Dola milioni 100 kila mwaka kwa Afrika na bara la Asia, kupitia mashirika mbalimbali kwa ajili ya tafiti mbalimbali za magonjwa, dawa na kutibu magonjwa yasiyopewa kipaumbele ikiwamo mabusha na matende.
“Ni mara ya kwanza amekuja kuangalia zoezi hili linakwendaje nchini, alipenda kutembelea maeneo husika ambako dawa zinagawiwa na alipita nyumba kwa nyumba akiangalia namna wanavyogawa dawa, wanavyopima urefu, wanatoa vidonge vingapi,” alisema.
Alisema wakati wa matembezi hayo, Gates alikuwa anauliza maswali yanayohusiana na ugawaji wa dawa na wapi wanakopata maji ya kunywea dawa hizo.
“Alikuwa anaangalia na mazingira. Alifurahi kuona kuna baadhi ya nyumba walikuwa wanatumia umeme, aliulizia vyoo akaona namna vyoo vya wakazi vilivyo na tulipoenda kwenye zahanati, akaangalia pia chanjo. Nilikuwa naye kwa muda wa saa moja na nusu,” alisema Dk Mwingira.
Alisema tajiri huyo aliulizia kuhusu takwimu za magonjwa yasiyopewa kipaumbele na kutaka kujua shughuli za wakazi wa Kicheba.
Mbali na kuangalia mchakato mzima wa ugawaji wa dawa hizo na kuangalia baadhi ya maeneo muhimu, Dk Mwingira alisema Gates alipenda kujua kuhusu huduma za fedha kupitia mitandao na alikutana na mwananchi mmoja ambaye akizungumza naye kuhusu suala hilo. “Bill Gates amekuwa msaada mkubwa kwetu hasa kwenye eneo la utafiti na sasa hivi anataka kuingia katika mradi huu wa usambazaji wa dawa,” alisema.
Magonjwa yasiyopewa kipaumbele
Kuna kundi la magonjwa takriban 18 yaliyokuwa hayapewi kipaumbele yaliyopo katika ukanda wa tropiki barani Afrika, Asia na Amerika Kusini, ambako pia kuna wadudu wanaoyaeneza na mazingira yanaruhusu maambukizi yake.
Dk Mwingira alisema magonjwa haya yana uhusiano mkubwa na umaskini na kunyanyapaliwa na jamii inayowazunguka.
Pamoja na kuwa hayasababishi vifo kwa haraka, magonjwa haya yanaleta usumbufu mkubwa kwani, wagonjwa huugua kwa muda mrefu, hivyo kutumia rasilimali chache zilizopo na hatimaye kuwaletea umaskini kwa kushindwa kushiriki katika shughuli zao za kila siku.
“Magonjwa haya ni kama usubi, minyoo ya tumbo, kichocho, trakoma (mtoto wa jicho), matende na mabusha.
Athari zinazoletwa na magonjwa haya ni maumivu ya muda mrefu na wakati mwingine ulemavu mkubwa, kudhoofisha ukuaji hasa kwa watoto wenye umri mdogo, kimwili na kiakili pamoja na utapiamlo kwa watoto. Lakini pia husababisha umaskini na kudumaza uchumi wa kaya na hatimaye Taifa.”
Dk Mwingira aliyataja madhara mengine ya magonjwa hayo kuwa ni utumbo kujisokota, upofu unaotokana na trakoma, saratani ya ini na kibofu cha mkojo kutokana kichocho na hatimaye kifo kama mgonjwa hatapata tiba ya mapema.
Alisema Tanzania imekuwa ikitekeleza mpango wa udhibiti wa magonjwa hayo katika halmashauri zote nchini.
“Lengo la mpango huu ni kudhibiti maambukizi ya magonjwa haya kulingana na azimio la nchi wanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO) No. 66.12 la mwaka 2013, tunao mpango mkakati ambao ni dira ya kudhibiti na kutokomeza magonjwa haya nchini,” alisema Dk Mwingira.
Alisema ni jambo la kujivunia kuwa jitihada hizo zinaonyesha matunda sasa ambako tathmini zinaonyesha kuwa kiwango cha maambukizi kimepungua katika halmashauri nyingi nchini.
“Mwaka huu, Serikali kwa kushirikiana na wadau tutaendelea kutoa dawa za kingatiba ya matende na usubi kwa wananchi milioni 15 kutoka halmashauri 47 na dawa za trakoma kwa wananchi takriban milioni 5.2 wa halmashauri 21. Ugawaji wa dawa za kingatiba za minyoo utaendelea kwa halmashauri zote 186 na kichocho katika halmashauri 126 zenye watoto takriban milioni 9.5 wa umri wa kwenda Shule.”
No comments:
Post a Comment