Monday, August 14

Mkakati wa changamoto za ardhi waiva


Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ‘kesho’ anatarajiwa kupokea rasimu ya mkakati wa kukabiliana na changamoto za matumizi bora ya ardhi nchini, iliyoanisha mapendekezo katika uandaaji, utekelezaji na usimamizi.
Rasimu hiyo yenye changamoto 17 pia imeainisha mkakati wa kutatua na mpango kazi wa kupatia suluhisho changamoto hizo na kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa na wadau kuhusu mipango ya matumizi bora ya ardhi nchini.
Akizungumza wakati wa mkutano na wadau mbalimbali wakati wa kukamilisha rasimu hiyo Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Dk Stephen Nindi alisema rasimu hiyo imeelezea namna ya kusimamia na kutekeleza programu mbalimbali za matumizi ya ardhi nchini.
Amesema rasimu hiyo imeandaliwa kwa kushirikiana kati ya Tume, idara mbalimbali za serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali ikiwemo Care International, Oxfam na Ujamaa Community Trust Fund.
“Kikosi kazi hiki kiliundwa Agosti 4-5 mwaka jana hapa Morogoro na tumefanya kazi kuanzia wakati ule kuandaa rasimu ambayo kwa sasa ipo tayari kuiwasilisha kwa waziri kesho na tutamweleza wazi changamoto  gani zipo tunazokabiliana nazo kwa pamoja,” amesema na kuongeza;
“Tumebaini changamoto mbalimbali na namna ya kukabiliana nazo, tunataka kupeleka kwake aione na kuijua na baadaye ikipitishwa uwe mkakati kamili kwa ajili ya kupambana na changamoto mbalimbali za upangaji, utekelezaji na usimamizi wa mipango ya matumizi ya ardhi nchini.”

No comments:

Post a Comment