Monday, August 14

Odinga awataka wafuasi wake wasiende kazini kesho,kutoa msimamo mkali




Aliyekuwa mgombea wa Nasa, Raila Odinga amewataka wananchi wa Kenya wanaomuunga mkono wasiende kazini kesho mpaka pale atakapotangaza msimamo wake kuhusu kile alichodai uwepo wa  wizi wa kura kipindi cha uchaguzi.
Akizungumza na wafuasi hao waliojitokeza kwa wingi katika eneo la Kibera Odinga alisema siku Jumanne  ndiyo atatoa msimamo wake.
Odinga aliwakilisha muungano wa Nasa katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Agosti 8 nchini Kenya, lakini alishindwa kufurukuta baada ya Uhuru Kenyatta kutetea kiti chake kwa kupata ushindi wa asilimia 54.
Odinga aliwaeleza wafuasi wake kuwa walitambua fika kuwa uchaguzi huo ungegubikwa na wizi wa kura na hivyo ndivyo ilivyokuwa.
“Tulitabiri wangeiba kura na hicho ndicho kilichotokea.Hatujamaliza bado. Hatutakata tamaa. Subiri hatua inayofuata nitatoa msimamo Jumanne,”
“Ni wazi kuwa mamlaka husika zimeshindwa kuchukua hatua stahiki na badala yake wanaua watu. Kura zimeibiwa hakuna cha kuficha hapo
“Ila ninachoweza kuwaambia kwa sasa kesho   msiende kazini,”alisema Odinga
Wakazi wa Kibera walifurika kwa wingi kumsikiliza Odinga ambaye aliongea kwa mara ya kwanza katika eneo hilo tangu Kenyatta atangazwe kuwa mshindi kwenye kinyang’anyiro hicho.
Huenda agizo hilo la Odinga likaungwa mkono katika maeneo ambayo muungano huo una wafuasi wengi kama Magharibi mwa Kenya na mitaa ya Kibera na Mathare iliyopo mjini Nairobi.
Kauli hiyo ya Odinga imekuja muda mfupi baada jumuiya za kimataifa kumtaka awatulize wafuasi wake.
Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan, ambaye alikuwa mpatanishi mkuu baada ya mzozo wa kisiasa nchini Kenya uliotokana na ghasia za uchaguzi uliofanyika mwaka 2007, alimtaka Odinga kutumia mifumo ya kisheria kutafuta haki kuhusu matokeo ya uchaguzi wa urais.
 "Namshukuru kiongozi wa upinzani Raila Odinga kwa kampeni ya uchaguzi ya amani aliyoiendesha. Amekuwa mtetezi jasiri wa demokrasia," alisema Dkt Annan kupitia taarifa.
"Kwa hivyo, namhimiza sasa afuatilie malalamiko yake kupitia mifumo ya kisheria iliyowekwa na aweke maslahi ya taifa mbele, kama alivyofanya kwa uzalendo mara nyingi awali."
Mwaka 2007, watu zaidi ya 1,000 walifariki na wengine 600,000 walihama makazi yao wakati wa ghasia za kikabila zilizozuka baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa.
Hali ya sintofahamu imeendele kuwamo nchini Kenya tangu yalipotangazwa matokeo ambayo yalipingwa na wapinzani na kusababisha kuibuka kwa vurugu.
Hadi sasa watu 16 wamepoteza maisha kufuatia vurugu hizo huku wapinza wakiwatuhumu polisi kwa kutumia nguvu kubwa kupambana na raia.

No comments:

Post a Comment