Wabunge wa Uingereza wameiomba serikali ya Misri iwape ruhusa ya kumtembelea kwa lengo la kumwona rais wa zamani Mohamed Morsi aliyeko jela huku kukiwa na taarifa juu ya kuzorota kwa afya yake.
Morsi anashikiliwa katika chumba cha peke yake katika gereza la Tora na familia yake imeruhusiwa kumtembelea mara mbili tu tangu alipofungwa baada ya kupinduliwa na jeshi mwaka 2013.
Morsi alishinda urais katika uchaguzi uliofanywa kufuatia maandamano yaliyoung’oa utawala wa miaka 30 wa Hosni Mubarak, na alitawala kwa mwaka mmoja kabla ya kufungwa.
Alihukumiwa baada ya kutiwa hatiani kutokana na mlolongo wa mashtaka yakiwemo ya kuhatarisha usalama wa taifa kwa kuvujisha nyaraka za siri kwa Qatar na kuhamasisha vurugu za kundi la Udugu wa Kiislamu (Muslim Brotherhood).
Kumekuwa na ripoti kwamba amenyimwa haki ya kupewa matibabu ya maana akiwa jela. Maombi ya kumtembelea yametumwa kwa Balozi wa Misri nchini Uingereza na yanatokana na maombi ya familia ya Morsi kwa wabunge wa Uingereza.
Wabunge na wanasheria wa kimataifa wanaotaka ruhusa ni pamoja na mwenyekiti wa zamani wa Kamati Maalum ya Mambo ya Nje Sir Crispin Blunt. Watu wengine wanaotaka mapitio ya kuwekwa kwake kizuizini ni pamoja na Lord Faulks, waziri wa zamani wa Sheria na Paul Williams, mwanachama wa kamati ya chama cha wafanyakazi kuhusu afya. Tim Moloney QC na mshauri wa kisheria wa kikundi.
Blunt amesema: "Kuna wasiwasi wa kuaminika kwamba hali ambamo Dk Morsi anashikiliwa inaweza kuwa haijafikia viwango vya kimataifa na Misri kwenyewe. Tunawasilisha ombi hili kwa mamlaka za Misri ili turuhusiwe kuona na kutathmini wenyewe mazingira ambamo Dk Morsi anazuiliwa.”
No comments:
Post a Comment