Wednesday, March 7

Serikali kukarabati shule za ufundi


 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Ave Semakafu amesema Serikali inakarabati shule za sekondari za ufundi ili kuwaandaa wasichana kuwa wabunifu wa teknolojia ya sayansi.
Semakafu amesema hayo leo Machi 7 kwenye kongamano la wabunifu lililoandaliwa na British Council kwa kushirikiana na Human Development Innovation Fund (HDIF) ikiwa ni maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wanawake duniani.
Amesema kufutwa kwa shule za sekondari za ufundi kulisababisha vijana kuanza kujifunza masuala ya ubunifu wa teknolojia baada ya kumaliza kidato cha nne.
“Vijana wanatakiwa kujifunza masuala hayo tangu wakiwa wadogo ili waweze kuwa wabunifu na kutoa mchango wao kwa taifa,” amesema na kuongeza serikali imeliona hilo na kuanza kuchukua hatua.
Akitoa mfano, Semakafu alisema kuna shule za sekondari ambazo zinakarabatiwa zikiwemo za Ifunda na Moshi na baadaye zitawekewa vifaa ili zianze kutoa mafunzo ya ufundi.
“Zipo shule nyingi zinakarabatiwa hivi sasa ambazo ni za ufundi zitaanza kutoa elimu,” amesema.
Amesema katika mwaka wa fedha 2018/19 shule za sekondari za ufundi zitaanza kutoa elimu.
“Hii itasaidia kwa kiasi kikubwa wasichana wabunifu kuanza kazi hiyo wakiwa bado na umri mdogo,” alisema.
Naibu Kiongozi wa Timu wa HDIF, Joseph Manirakiza alisema kongamano hilo limewaleta pamoja wabunifu wanawake ili waweze kushawishi wengine kuingia katika ubunifu.
Alisema taasisi hiyo imekuwa ikisaidia wanawake na wasichana ikiamini kwamba wanawake wakisaidiawa jamii nzima itanufaika.
Naibu Mkuu wa Idara ya Kimataifa ya Maendeleo ya Uingereza (DFID), Jane Miller alisema imekuwa ikisaidia wanawake wa Tanzania katika sekta elimu, afya hasa uzazi wa mpango.
Alisema wakati huu ambao yanafanyika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wanawake, Uingereza itaendelea kuwasaidia wanawake na wasichana ili waweze kusimama wenyewe na kujitegemea.
“Wanawake wanatakiwa kujiamini na kuona kuwa wanaweza kufanya jambo lolote hata kuwazidi wanaume,” amesema.

No comments:

Post a Comment