Tuesday, November 7

WB: Tanzania inaweza kufikia malengo yake



Mkurugenzi mkazi wa Benki ya Dunia, Bella Bird
Mkurugenzi mkazi wa Benki ya Dunia, Bella Bird 
Dar es Salaam. Ingawa kasi ya ukuaji wa uchumi imeshuka kidogo ikilinganishwa na makisio, Benki ya Dunia imesema Tanzania inaweza kuyafikia malengo yake ya kiuchumi endapo itaweka mikakati thabiti.
Kwa nusu ya kwanza ya mwaka huu, uchumi umekua kwa asilimia 6.8 tofauti na asilimia 7.7 za kipindi kama hicho mwaka jana. Makadirio ya benki hiyo yalionyesha uchumi ungekua kwa asilimia 6.9 kwenye nusu ya kwanza.
Pamoja na kutofikiwa kwa malengo yaliyowekwa, mchumi mkuu wa benki hiyo Kanda ya Afrika, Dk Albert Zeufack alisema Tanzania itaendelea kuwa miongoni mwana nchi zenye uchumi unaokua kwa kasi Afrika.
“Kufanikisha hilo, Tanzania inahitaji kuziimarisha taasisi zake, kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo na kuijengea uwezo sekta binafsi,” alisema Dk Zeufack.
Mambo mengine ya kuzingatia alisema ni kupambana na rushwa na kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji kwa kutunga sera zinazotabirika kwa wawekezaji.
Takwimu hizo zilitolewa jana kwenye uzinduzi wa Ripoti ya 10 ya Mwenendo wa Uchumi Tanzania ambayo pamoja na mambo mengine, imesisitiza usimamizi makini wa rasilimali za maji kwa maendeleo endelevu.
Ripoti hiyo, inapendekeza kuimarishwa kwa sekta binafsi ili kuongeza mchango wake kwenye Pato la Taifa (GDP) kwa kushughulikia changamoto inazozikabili.
Inabainisha changamoto hizo kuwa ni pamoja na kupungua kwa mikopo ya sekta binafsi hivyo kutochochea uwekezaji ambao utasaidia kuongeza ajira na kupunguza umaskini.
Nyingine ni kupungua kwa uwekezaji kutoka nje (FDI) na kuongezeka kwa mikopo isiyolipika. “Kwa miaka mitatu iliyopita, (2013 mpaka 2016), FDI imepungua kwa Dola 500 milioni za Marekani (zaidi ya Sh1.1 bilioni). Sekta binafsi ni muhimu kufanikisha utekelezaji wa mipango ya serikali,” alisema Dk Zeufack.
Mkurugenzi mkazi wa benki hiyo nchini, Bella Bird alisema Tanzania ina fursa za kufanikisha mipango yake kiuchumi endapo itasimamia vyema rasilimali ilizonazo.
“Mwaka 2015 mchango wa kodi kwenye Pato la Taifa ulikuwa asilimia 11 lakini hivi sasa ni asilimia 12.8. Ndani ya miaka hii miwili, Serikali imesimamia vyema ukusanyaji wa mapato na kudhibiti rushwa. Matumaini yanaonekana,” alisema Bird.
Alisema maboresho yanahitajika kwenye mfumo wa usimamizi wa kodi ili kuongeza vyanzo na uwazi, viwango vinavyolipika na iwe sawa kwa wote.
Kwa mabadiliko yaliyopo serikalini, mkurugenzi huyo alisema Tanzania inahitaji miaka minane ya kukuza uchumi wake kwa zaidi ya asilimia saba ili kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 na kuhitaji miaka 25 ya kasi hiyo ya ukuaji wa uchumi kumaliza umaskini nchini.
Kwa sasa, zaidi ya Watanzania milioni 12 wanaishi chini ya mstari wa umaskini wakitumia chini ya Dola moja kwa siku.
Pamoja na matumaini hayo, Bird alitahadharisha kwamba uwiano wa deni la Taifa haufiki asilimia 50 kwa miaka ya karibuni.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo alisema inawezekana kutekeleza na kufanikisha mambo mengi ambayo Serikali imepanga kwani Watanzania wapo tayari kushiriki.
“Kwa miezi sita niliyokaa wizarani nimejifunza kitu muhimu... miongoni mwa rasilimali adimu tulizonazo ni watumishi wa umma. Ni wavumilivu na wanajituma licha ya changamoto walizonazo,” alisema Profesa Mkumbo.

No comments:

Post a Comment