Kutokana na athari zake ambazo tayari zimeshaanza kujidhihirisha katika maeneo mengi duniani, jitihada mbalimbali zimechukuliwa kukabiliana nazo.
Athari hizo zimegawanywa katika makundi mawili ambayo ni pamoja na zinazosababishwa na nchi zilizoendelea kiviwanda zinazochangia kiasi kikubwa cha hewa ukaa angani kulinganisha na nchi zinazoendelea.
Kundi la pili ni la nchi zinazoendelea ambazo licha ya kuwa na mchango mdogo katika uharibifu, yanachangiwa na mbinu mbaya za kilimo na uharibifu wa misitu kama uvunaji holela wa miti, uchomaji holela wa mkaa, ongezeko kubwa la mifugo ambayo huharibu tabaka la juu la udongo hivyo kupoteza uwezo wa udongo kutunza hewa ukaa. Athari za mabadiliko ya tabia nchi zinaweza kuonekana moja kwa moja sasa au hata baadaye. Kulingana na mwenendo wa uharibifu wa mazingira, yapo baadhi ya maeneo nchini yameathiriwa na mabadiliko ya tabianchi kutokana na uharibifu wa maliasili na mazingira.
Miongoni mwa athari hizo ni pamoja na kuongezeka kwa ujazo wa maji katika bahari kutokana na kuyeyuka kwa barafu inayosababishwa na kuongezeka kwa joto duniani. Pia kuongezeka kwa joto.
Wadau wajitokeza
Kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, Chama cha Wanasheria Watetezi wa Mazingira (Leat) kupitia mradi wake wa “Ushiriki wa wananchi katika Usimamizi wa Maliasili’ kimetoa mafunzo ya visababishi vya mabadiliko ya tabia nchi kwa vijiji 32 katika Mkoa wa Iringa.
Wakizungumza katika mafunzo hayo, baadhi ya washiriki wanasema wamefaidika ikiwa pamoja na mapato yatokanayo na rasilimali za misitu.
Mwenyekiti wa timu ya ufuatiliaji wa uwajibikaji wa kijiji cha Idodi, Mwangosi Ngola anasema awali walijikita zaidi katika uharibifu wa misitu bila kupata faida, lakini sasa wanatunza misitu huku pia wakipata faida.
“Tatizo lilikuwa ni ukataji wa miti na uchomaji wa mkaa, lakini sasa umedhibitiwa na badala yake sasa wananchi wanatumia kuni kwenye maeneo yaliyoainishwa. Leat wamegawa mizinga 22 kwa kila kijiji, kwa hiyo wananchi wanafaidika kwa kuvuna asali inayowaingizia kipato,” anasema.
Anazungumzia pia suala la sheria za vijiji akisema wananchi wameshirikishwa katika uundwaji wake.
“Tumeshirikishwa katika uundwaji wa sheria ndogondogo za utunzaji wa mazingira ambazo zimeweka adhabu kwa wanaoharibu mazingira. Zimetusaidia kutenga maeneo kwa matumizi bora na uendelevu wa rasilimali za misitu. Zimesaidia pia kupunguza migogoro kati yetu na hifadhi ya Ruaha na kati ya wakulima na wafugaji,” anasema Ngola.
Naye Eunice Mpatule ambaye pia ni mjumbe wa timu ya ufuatiliaji na uwajibikaji wa kijiji cha Isimikinyi wilayani Mufindi, anasema awali hakukuwa na mpango wa matumizi ya rasilimali za misitu bali wananchi waliharibu misitu.
“Awali uelewa wetu katika mazingira ulikuwa chini, lakini sasa tunaona umuhimu. Hapa kijijini tuna misitu, mto na mawe ambayo ni kivutio cha utalii. Tumejifunza kutunza na kwa sasa tunapata watalii wanaokuja kutembelea na kutoa ada,” anasema Mpatule.
Hamza Chang’a mwenye kikundi cha kutunza mazingira katika kijiji cha Kiwere wilayani Mufindi mkoani humo anasema kwa sasa wameainisha rasilimali za misitu na kuziwekea ulinzi mkali.
“Awali tuliona ukataji wa misitu na kuchoma mapori ndiyo njia bora za kilimo, kumbe tulikuwa tukiharibu mazingira. Tumepata mafunzo mengi ikiwa pamoja na kujua haki za raia kwa Serikali za vijiji na jinsi ya kusimamia rasilimali za misitu,” anasema.
Anasema kwa sasa wameweka walinzi kwenye kila msitu ambao huwaripoti waharibifu kwenye kamati za usimamizi wa misitu ili wapewe adhabu.
Ofisa uhusiano wa Leat, Edna Tibaijuka anasema mafunzo hayo yalijikita katika kuwawezesha wananchi na serikali za vijiji kutambua umuhimu wa kutunza maliasili zao kwa faida ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo na kujikinga kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
“Vitendo vya ukataji miti kiholela, kuchoma mkaa na kuharibu vyanzo vya maji ni kati ya shughuli ambazo zinachangia kwa kiasi kikubwa mabadiliko ya tabianchi.
Katika kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi, Leat imesaidia mchakato kufanya marejeo na kupitisha sheria ndogo katika usimamizi wa misitu ya vijiji,’’ anasema na kuongeza:
“Upitishwaji wa sheria hizi ndogo ulikuwa na lengo la kusimamia ipasavyo rasilimali zilizomo ndani ya mipaka ya vijiji, zikiwamo misitu na wanyamapori ili kuhakikisha kuwa rasilimali hizi zinatumika kwa njia endelevu.’’
Tibaijuka anasema ili kupunguza utegemezi wa moja kwa moja wa maliasili katika vijiji vya mradi, Leat imewawezesha wanavijiji 704 (22 kila kijiji) kuanzisha mradi wa ufugaji nyuki kama njia mojawapo ya kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ya maliasili na kama njia ya kukabiliana na vichocheo vya mabadiliko ya tabianchi.
“Katika kufanikisha hili, Leat ilitoa mafunzo ya ufugaji nyuki kutokana na ukweli kwamba ufugaji nyuki hauna athari za kimazingira na pia ni njia mojawapo ya wanachi kujiongezea kipato kwa kutoa mizinga 700 kama mtaji kianzio wa mradi huo,” anasema na kuongeza”
“Leat inaamini wananchi wakipatiwa mafunzo juu ya usimamizi wa maliasili na kupata njia mbadala za vipato inaweza kuwa ni chachu ya kupunguza matumizi yasiyodumu ya maliasili kwa kuwa wataongeza jitihada za utunzaji wa rasilimali hizo.”
No comments:
Post a Comment