Tuesday, November 7

ELIMU NA MALEZI : Tabia tano za kusisitiza kwa watoto wanaoanza shule



Christian Bwaya
Christian Bwaya 
Kwa wiki kadhaa nimekuwa nikieleza kwa nini mafanikio ya mtoto hayategemei uwezo anaouonyesha darasani pekee.
Nimejaribu kueleza japo kwa ufupi namna gani matarajio ya kitaaluma tuliyonayo wazazi na walimu yanavyoweza kuathiri maisha ya mtoto.
Tumeona mathalani, tunapomweka mtoto mdogo kwenye shinikizo kubwa la kufaulu masomo, tunamfanya awe mshindani. Ushindani unaweza kuwa kikwazo cha mafanikio ya mtu baada ya maisha ya shule.
Pia, nilionyesha gharama ya kuthamini kupita kiasi uwezo wa mtoto kiakili darasani. Tunapoamini uwezo wa mtoto ni ule unaoonekana kupitia matokeo ya mitihani, iko hatari ya kudumaza maeneo mengine muhimu ya ukuaji.
Katika makala ya leo, tunaangazia tabia muhimu kusisitizwa katika miaka ya mwanzo ya maisha ya mtoto shuleni ili sio tu kuongeza uwezekano wa mtoto kufanya vizuri darasani, lakini pia kufanikiwa hata anapokuwa nje ya darasa.
Ujasiri na kujiamini
Mtoto jasiri ana uthubutu wa kufanya vitu vipya bila hofu ya kukosolewa. Kinyume cha ujasiri, ni woga na unyonge unaotokana na mtoto kukosa imani na uwezo alionao.
Ili mtoto awe jasiri lazima kwanza ajenge mtazamo chanya kuhusu maisha. Bila mtazamo chanya, mtoto hatojiamini na ni dhahiri atakosa ujasiri wa kujaribu kutafuta majibu mapya kwa changamoto alizonazo.
Wazazi wana nafasi muhimu katika hili. Kwa mfano, kupitia kumshirikisha mtoto kwenye shughuli ndogondogo zinazolingana na umri wake na pia kumpa mtoto nafasi ya kujaribu kufanya vitu bila kukosolewa, wazazi wanakuza hali ya mtoto kujiamini.
Walimu nao kwa upande mwingine, lazima waangalie namna gani wanamfundisha mtoto. Je, kazi wanazowapa watoto darasani zinawajengea kujiamini? Vipi watoto wanapokosea? Vipi watoto wasiofanya vizuri darasani? Je, wanawasaidia kujikosoa bila kuwafanya wakose imani na uwezo wao?
Udadisi
Udadisi ni uwezo wa kuibua maswali yanayochochea kiu ya kuelewa mambo kwa upana. Mtoto mdadisi kwa kawaida, haridhishwi na maelezo mepesi kwa jambo linalomtatiza.
Mtu mdadisi huwa na akili inayochemka muda wote. Huchunguza mazingira yake na mara zote hufikiria namna tofauti zinazoweza kutumika kuleta ufumbuzi wa tatizo.
Mzazi lazima ajenge mazingira ya kuchochea udadisi kwa mwanawe. Vifaa vinavyosisimua ufahamu wake sambamba na kumuuliza maswali yanayomtaka aelezee uzoefu wake, ni baadhi ya mambo yanayoweza kujenga kiu ya kutafuta majibu.
Walimu nao kwa nafasi yao, wana kazi kubwa ya kuligeuza darasa kuwa mahali panapoibua maswali yanayohitaji kutafutiwa majibu. Pia, walimu wanapowapa watoto fursa ya kuuliza na kujenga imani kwamba hakuna mtu anayemiliki majibu sahihi, wanawasaidia watoto kuwa na kiu ya kujifunza.
Ushirikiano
Mtoto anayejua umuhimu wa kufanya kazi na wenzake, kwa kawaida ana uwezo wa kujua mahitaji ya wengine na anaelewa namna gani mahitaji yake yanaathiri mahitaji ya watu wanaomzunguka.
Mtoto mwenye ushirikiano kwa mfano, hana tabia ya kutanguliza matakwa yake mbele ya matakwa ya wenzake. Mtoto huyu huwapenda wenzake, si mnyimi, huthamini hisia zao na pia ana uwezo wa kuelewa maumivu waliyonayo.
Kwa kiasi kikubwa, mafanikio ya mtoto ndani na nje ya darasa yanategemea namna anavyoweza kushirikiana na watu. Malezi na ufundishaji vina nafasi kubwa katika kukuza tabia hii.
Kwa mfano, ni muhimu walimu wasisitize wanafunzi wa madarasa ya awali kufanya kazi pamoja. Kazi za ujifunzaji zinapowalazimu watoto kusaidiana badala ya kushindana zinawafanya watoto wathamini urafiki, undugu na upendo kati yao.
Nyumbani, wazazi nao wana kazi ya kuwafundisha watoto kushirikiana na wenzao kwa kuonyesha mfano mwema kupitia maisha wanayoishi wao wenyewe.
Mawasiliano
Mawasiliano ni uwezo wa mtu kusoma mawazo na hisia zake kwa wengine. Ili iwe rahisi kuwasiliana na watu, mtoto anahitaji si tu kujiamini, lakini pia uwezo wa kuwaamini na kuheshimu hisia za wenzake.
Mafanikio katika maisha yanategemea pia uwezo wa kuwasiliana. Tunafahamu kwa mfano, bila ujuzi wa kuwasiliana, mtu anaweza kuwa na uwezo mkubwa wa kiakili lakini bado akapata shida kubwa kufanikiwa.
Malezi yanayojali hisia za mtoto, yanayomfanya mtoto aamini wazazi wanamwelewa na kumsikiliza, yana nafasi kubwa ya kukuza uwezo huu wa mtoto kuwasiliana na wenzake.
Mwalimu naye kwa upande wake, ana kazi kubwa ya kuchochea utamaduni wa mtoto kusoma hisia na mawazo yake pasipo woga wa kukosolewa wala kudhalilika.
Kujizuia
Kujizuia ni nidhamu inayomsukuma mtu kujisimamia bila kutegemea msukumo wa nje. Mtoto anayejizuia ana uwezo wa kusema hapana kwa kile kinachokwenda kinyume na dhamira yake.
Upo ushahidi mwingi wa kiutafiti unaohusianisha nidhamu ya mtu na mafanikio anayoweza kuyapata. Tunafahamu kwa mfano, malengo yoyote hayafikiwi bila nidhamu.
Malezi na mfumo wa ufundishaji vitakuwa na manufaa kwa mtoto ikiwa vitalenga kukuza nidhamu.
Wazazi na walimu kwa nafasi zao, wanawajibika kukuza tabia ya kujizuia kwa watoto kwa kuwasaidia kujenga misingi imara inayoongoza maamuzi yao ya kila siku.
Misingi hii ni pamoja na kujua kutofautisha mambo ya msingi na yale yasiyo ya msingi na namna bora ya kufuatilia na kufikia kile kilicho muhimu.
Aidha, adhabu zisizodhalilisha utu wa mtoto zinapotolewa kwa upendo, nazo zina nafasi yake katika kumkumbusha mtoto kipi anachoweza kufanya na kipi hana sababu ya kukifanya.
Daniel Goleman, katika kitabu chake cha ‘Emotional Intelligence’ anasema; “Mtoto asiyeweza kuwa na uzingativu, mwenye hofu badala ya kuwaamini watu, mwenye huzuni au hasira badala ya matumaini, asiyejifurahia wala kuwafurahia wenzake; mtoto kama huyu ana fursa finyu ya kufanikiwa shuleni na kwenye maisha yake kwa jumla.”
Wazazi na walimu kwa pamoja, tuna kazi ya kuhakikisha malezi na ufundishaji katika miaka ya mwanzo vinalenga kukuza tabia hizi ambazo kwa hakika mtoto anazihitaji ili kufanikiwa ndani na nje ya darasa.

No comments:

Post a Comment