Tuesday, November 7

JICHO LA MWALIMU : Maandalizi yanavyombeba mwalimu




Joseph Chikaka
Joseph Chikaka 
Mara nyingi hutokea mwalimu anaingia darasani na kugundua kuwa kuna kitu amekisahau ama amekiacha ofisini, hivyo huchukua hatua ya kumtuma mwanafunzi akamchukulie.
Wakati mwingine hutokea mwalimu kunogewa kueleza kwa kina kulikopitiliza malengo ya mada husika na wengine kwa kuzunguka ili kujibu swali moja tu la mwanafunzi ambalo hakulitegemea.
Pia, wakati mwingine hutokea mwalimu kuwa mkali anapokuwa darasani na kukataa kabisa maswali hata yale yaliyohusisha mada aliyoifundisha mwenyewe.
Mwingine huweza kuingia na zana mbalimbali, lakini cha ajabu asizitumie kwa sababu hakuwa amejiandaa vema.
Matukio ya aina hii na mengineyo, hudhihirisha ni kwa jinsi gani mwalimu husika alivyo mweledi kitaaluma, anavyolimudu, anavyolipenda somo husika; na ni kwa kiwango gani amejiandaa kwa ajili ya somo na mada aliyopanga kuifundisha.
Kabla ya kufundisha, mwalimu bora huhitaji maandalizi ya kutosha. Ipo miongozo maalumu iliyoandaliwa ya kumuongoza.
Mwalimu hapaswi kujitungia tu jambo la kufundisha kwani  ipo miongozo. Kwa mfano, kuna  mtalaa, mihutasari ya masomo, vitabu vya kiada, vitabu vya mwanafunzi, viongozi vya mwalimu na vitabu vya rejea.
Zana za rejea siyo vitabu tu, pia huhusisha vitu kama vipindi vya redio au runinga, majarida, kanda za video, magazeti, vipeperushi, chati na makala mbalimbali za intaneti.
Lakini, wapo baadhi ya walimu wa siku hizi ambao wao huona kujiandaa kufundisha kuwa ni mzigo mkubwa kwao na ni upotevu wa muda.  Wanatamani waruhusiwe kufundisha tu pasipo kujali kama walifanya maandalizi ya somo ama hawakufanya.
Wakati mwingine pia hali ya walimu kutopenda kuandaa, hutokana na kiburi cha kutojali taaluma; kwamba mwalimu amefundisha kwa miaka mingi hivyo kuona kuwa anafahamu kila kitu, hivyo kuona kwamba hana haja ya kujiandaa.
Maandalizi ya ufundishaji na somo ni ule mchakato ambao huhusisha mwalimu kuandaa somo kuanzia pale anapoandaa azimio la kazi (mpango kazi) wa mwaka, miezi au kipindi fulani na kwa kutumia muhutasari wa somo.
Kutoka hapo, mwalimu huandaa notisi,  andalio la somo na zana za kufundishia na kujifunzia.
Faida za mwalimu kuandaa somo
Katika tendo la kufundisha na kujifunza zipo faida nyingi za mwalimu kuandaa somo lake kabla ya kwenda kufundisha. Baadhi ni kama hizi zifuatazo:
Kujenga umakini kwa sababu hufahamu vitendo vya ufundishaji na ujifunzaji kwa ufasaha; kumpa mwalimu ujasiri.
Somo lililoandaliwa vema huvutia wanafunzi na kisha huleta mtiririko mzuri wa mada kwa mwanafunzi; kufahamu malengo ya ufundishaji wa somo na mada husika katika muda aliopanga.
Kukuza ufahamu na udadisi kwa wanafunzi na mwalimu husika; kuokoa muda ambao ungepotea bure na kumpatia mwalimu moyo wa kujiamini na kufahamu na kuzitengeneza zana, vifaa au njia za kumsaidia katika ufundishaji na ujifunzaji.

Madhara ya kutoandaa somo
Mwalimu asiyeandaa somo, husababisha madhara kadhaa katika tendo zima la ufundishaji na ujifunzaji; baadhi ni kama haya yafuatayo:
Kushindwa kufikia malengo au lengo mahususi katika mada husika; somo kukosa mvuto kutokana na kutokuwa na mtiririko mzuri uliopangiliwa.
Kwa mfano, huweza kujikuta akirukia kipengele hiki na kile; kufundisha kwa kufuata sura za vitabu au kufuata mtiririko wa maswali katika mithani ya taifa na wanafunzi kushindwa kuelewa mada husika.
Pia, mwalimu hupoteza uwezo wa kujiamini mbele ya wanafunzi wake; mwalimu kuwa mkali na mwenye hasira pasipo sababu; kushindwa kuwajengea ujuzi au stadi zilizotarajiwa katika somo husika; kushindwa kuweka kumbukumbu za somo hasa mambo yaliyofundishwa na  wakati yalipofundishwa.
Madhara mengine ambayo husababishwa na mwalimu kutojiandaa ni mwanafunzi kulichukia somo; mwanafunzi kushindwa kufikia ndoto zake za maisha za fani anayoipenda kwa kukosa alama zitakazomruhusu kuendelea mbele.
 Mwanafunzi kuiga mtindo na tabia ya kufanya kazi kwa staili ya zima moto au bora liende pasipo  kuwa na mpango au maono; mwanafunzi kujikuta akitengenezewa mazingira ya kudharau walimu au kuwabagua kutokana na utendaji wao.
Wakati mwingine hutokea wale walimu wasiojiandaa kupendwa sana na wanafunzi kwa sababu ili kukwepa maswali husimulia ‘vihadithi’ na visa vingi vingi darasani ambavyo viko nje kabisa ya mada wakiwa na lengo la kupoteza muda.
Changamoto wanazokutana nazo walimu
Baadhi ya walimu wameeleza kuwa zipo changamoto zinazowakabili kama vile umbali wa mahali wanapoishi na shule; ukosefu wa nishati ya umeme kwa wakati wa usiku; uduni wa mazingira yao ya kazi; uhaba wa malighafi katika baadhi ya sehemu.
Umasikini, kukosa ubunifu; mazingira yasiyokuwa rafiki katika kuchochea tendo zima la ufundishaji na ujifunzaji; kutojiamini na kufanya kazi kwa mazoea.
Maandalizi sahihi na ya kina ya mwalimu humbeba, yaani humrahisishia kazi yake ya ufundishaji na tendo zima la ujifunzaji darasani ama nje ya darasa.
Ni wajibu wa wadhibiti ubora (zamani waliitwa wakaguzi wa elimu) wa ndani ya shule na wa nje kutimiza wajibu wao wa kukagua, kushauri, kuonya, kufuatilia namna walimu wanavyofanya kazi zao kwa weledi.
Pia, kushauri katika mamlaka husika vikwazo vya kimazingira, kimaslahi, kisera, kimfumo na kimuundo ambavyo wanaona pengine vikitatuliwa vitawawezesha walimu kutekeleza majukumu yao kwa wepesi na ufanisi mkubwa
Hivyo, ni vema walimu wakazingatia umuhimu wa kufanya maandalizi ya kina kila wanapotaka kufundisha ili kulinda heshima ya taaluma ya ualimu.
Kwa kufanya hivyo watakuwa wakitoa mchango wao mkubwa usio na kifani katika ujenzi wa taifa imara lenye kuwajibika.

No comments:

Post a Comment