Monday, November 6

Wawekezaji waahidi ARV zinazozalishwa nchini mwezi huu


Takriban nusu ya Watanzania wanaoishi na virusi vya Ukimwi wataanza kunufaika na dawa za kufubaza ugonjwa huo (ARV) zitakazoanza kuzalishwa na kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries Limited (TPI)
Kiwanda hicho kilichojengwa jijini Arusha kwa ubia kati ya Serikali yenye asilimia 40 ya hisa na watu binafsi wanaomiliki asilimia 60, kinatarajia kuzalisha ARV 500,000 kwa mwezi. TPI inatarajia kuanza uzalishaji wa dawa hizo mwishoni mwa mwezi huu.
Ofisa mtendaji mkuu wa TPI, Ramadhani Madabida alisema ujenzi wa kiwanda hicho utakaogharimu Sh99 bilioni utasaidia kuokoa Sh806 bilioni kwa mwaka zinazotumika kuagizia dawa nje ya nchi.
Madabida alisema fedha za ujenzi wa kiwanda hicho zimetokana na ufadhili walioupata kutoka Umoja wa Ulaya (EU) ambapo zimetumika katika awamu tatu ambazo ni ukarabati wa majengo, utengenezaji wa mashine na upanuzi.
Alisema wao kama wawekezaji wa ndani wameamua kuunga mkono kaulimbiu ya Rais John Magufuli kuhusu Tanzania ya viwanda na hivyo wamejipanga kutoa ajira kwa vijana 200 kwa awamu ya kwanza.
“Mheshimiwa Rais Magufuli ametutia moyo na tuna imani ametupa msukumo, sisi tutaendelea na uzalishaji na si dawa tu pia tutazalisha malighafi,” alisema Madabida
Mtendaji huyo aliwaambia wanahabari kwamba mbali na ujenzi wa kiwanda hicho, pia wanatarajia kujenga maabara ya kisasa ya utafiti na maendeleo kwa ajili ya kuboresha utengenezaji wa dawa bora na kukifanya kiwe kitovu cha kutoa taaluma kwa wanataaluma mbalimbali.
Alisema kwamba mashine za kiwanda hicho zitaendeshwa kwa mfumo wa kompyuta na pia kitazalisha dawa za kutibu kifua, malaria, tumbo na dawa nyingine zilizo katika orodha ya dawa muhimu nchini.
Mkazi wa Kwa Mollel jijini hapa, Geophrey Stephen alisema anatarajia kuona baadhi ya watu wanaoishi na VVU wanapata dawa za kufubaza virusi na kupunguza makali ya ugonjwa huo kwa urahisi zaidi.

No comments:

Post a Comment