Monday, November 6

JPM alivyorejesha nidhamu ya maisha, wafanyabishara walalama hali ngumu


Rais John Magufuli anatimiza miaka miwili madarakani tangu aapishwe Novemba 5, 2015 huku akionekana kupata mafanikio na changamoto katika maeneo kadhaa.
Magufuli aliapishwa baada ya kuibuka mshindi katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka 2015 ulioshirikisha wagombea wengine saba wa vyama vya upinzani, akiwamo Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, aliyegombea kupitia Chadema.
Katika kipindi hicho Rais Magufuli amefanya mambo kadhaa ambayo yameonekana kuwa na tija, moja ikiwa ni suala la udhibiti wa matumizi.
Tangu Rais Magufuli alipoingia madarakani, amekuwa akihubiri kuwa “mtu asiyefanya kazi na asile” na kuhimiza kila mwananchi kuchapa kazi kwa bidii kujipatia kipato ambacho kitamwezesha kulipa kodi halali.
Rais amepambana na ufisadi, amefuatilia wakwepa kodi, amefuta posho na mikutano ya Serikali hotelini, amedhibiti safari za ndani na nje ya nchi zisizo muhimu na ameagiza fedha zote za mashirika na taasisi zake zihifadhiwe Benki Kuu ya Tanzania (BoT) badala ya benki za biashara.
Kutokana na hali hiyo yamekuwapo malalamiko kuwa fedha zimepotea, biashara haziendi, benki zinayumba, baadhi ya viwanda vinapunguza wafanyakazi, kupungua mizigo bandarini na wenye mikopo kushindwa kufanya marejesho.
Pamoja na hilo uamuzi wa Serikali yake kupunguza matumizi yasiyo ya lazima kama kufuta shamrashamra za baadhi ya sherehe za kitaifa, mikutano/makongamano ya gharama kubwa pia inaelezwa kurejesha nidhamu kwa watumishi ambao baadhi yao waliitumia mianya hiyo kama njia ya kujipatia kipato isivyo halali.
Udhibiti huo wa fedha, ndio unaotajwa kuielekeza Serikali yake kufanya uhakiki wa watumishi wake na kugundua uwapo wa watumishi hewa zaidi ya 17,500 na hivyo kudai kuokoa kiasi cha Sh19 bilioni.
Si hilo tu, kubana kwingine matumizi kunatajwa kutokana na uamuzi wa Serikali kupanga kulipa mishahara ya juu kabisa isiyozidi shilingi milioni 15 kutoka milioni 30 hadi milioni 45.
Katika hilo, Aprili mwaka juzi Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Juliet Kairuki ambaye alitajwa kukataa mshahara wake tangu mwaka 2013 kwa madai kuwa ni mdogo.
Hata hivyo, aliyekuwa Waziri Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Nauye aliwatoa hofu wananchi akieleza kuwa ukame wa fedha uliopo mitaani si bahati mbaya, bali ni mkakati wa Serikali kuweka nidhamu ya fedha itakayowezesha kukuza uchumi.
“Hatutaacha wananchi waumie sana, baada ya muda tutaachia fedha mitaani lakini si kwa wapiga dili, bali kwa wanaofanya biashara na kazi za halali,” alikaririwa Nape bila kueleza ni kipindi gani hasa fedha hizo zingeachiwa.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Uhusiano wa Kimataifa, Kanali mstaafu Ngemela Lubinga anasema kwa sasa watumishi wa Serikali wamekuwa na nidhamu ya hali ya juu katika kazi huku visingizio visivyo na kichwa wala miguu vikipungua.
“Sasa watumishi wanawahi kazini na wanakaa hadi muda sahihi wa kutoka, unaona hata majaji na mahakimu wako makini katika kutimiza malengo.
“Najua tunaumia kwa sasa kwa sababu ya mazoea lakini tukubali utendaji wake utaliweka Taifa sehemu nzuri ya vizazi vyetu kuishi,” anasisitiza Lubinga.
Katika eneo hilo la nidhamu na maadili, Rais Magufuli anaelezwa kutekeleza ahadi yake ya kuanzisha Mahakama ya Mafisadi itakayoendesha kesi za rushwa na wahujumu uchumi baada ya majaji wake 14 kupatiwa mafunzo Lushoto mkoani Tanga.
Wafanyabiashara walalama
Hata hivyo, pamoja na Rais Magufuli kusifu Serikali yake kwa kukusanya mapato na kudhibiti fedha, baadhi ya wafanyabiasha wamekuwa wakilalamikia makali ya maisha kutokana na mzunguko mdogo wa fedha.
Juma Likote mfanyabishara wa duka la nguo katika soko la Kariakoo anasema hali kwa sasa imebadilika na kusababisha kipato chake kushuka kwa kiasi kikubwa huku Serikali ikiwa imewarundikia mzigo wa kodi.
“Hali ya kibiashara sasa imekuwa ngumu, lakini tunaelewa imesababishwa na mipango au utaratibu uliokuwa umezoeleka siku za nyuma, baadhi walikuwa hawalipi kodi, inawezekana mambo yakaja kuwa mazuri,” anasema Likote.
Hata hivyo, mfanyabiashara mwingine wa kuuza vifaa vya magari eneo mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam, Japhet Msangi anasema kwa sasa maisha ya kulalamikia ugumu wa hali ya maisha hayana budi kufikia kikomo kwani Serikali imeshaamua kubana matumizi na wananchi hawana budi kwenda sawia na matakwa yake.
Msangi anawashauri Watanzania kubadilika na kuendana na hali halisi ilyopo na kuachana na mazoea ya kuwa na matumizi makubwa ya fedha ambazo hazionekani.
Hata hivyo, Msangi alitahadharisha Serikali kuwa makini na hali hiyo na kusema kuwa endapo haitarekebisha, maisha yatakuwa magumu zaidi, kampuni zitafungwa na hata zitakazobaki zitazalisha fedha za kujiendesha tu na Serikali haitapata kodi zitokanazo na wafanyakazi.”
Nidhamu ya matumizi
Kutokana na hali hiyo wengi wa Watanzania wameshaanza kubadilikana na kuishi kutokana na hali halisi tofauti na miaka miwili kabla ya utawala wa Rias Magufuli.
Grace Mwakalukwa ambaye alikuwa akiishi nyumba ya kupanga ya Sh700,000 kwa mwezi anasema amelazimika kuhama nyumba hiyo mara baada ya kodi yake kuisha na kuamia eneo la Kimara ambako amepata nyumba ya 250,000 kwa mwezi.
“Unajua tulizoea kupata fedha nyingi. Watu walitumia vibaya fedha za Serikali. Kwa hiyo hata ukifanya biashara ndogo faida inaonekana kwa sababu wateja wapo na hivyo hata kupanga nyumba ya Sh8,400,000 kwa mwaka kwangu ilikuwa inawezekana lakini sasa siwezi.
Anasema kutokana na hali iliyokuwapo hata nyumba za kupanga zilipandishwa kodi maradufu lakini kwa sasa wenye nyumba wamelazimika kupunguza na bado wateja wanashindwa kumudu.
“Aliyekuwa akiishi katika nyumba nzima sasa amehamia vyumba viwili na sebule, wale wa vyumba viili amehamia kimoja ili kupambana na hali zao.”
Anasema wasinchana wengi walikuwa wakilipiwa nyumba za kupanga na marafiki zao wa kiume lakini sasa wamewakimbia, hivyo kurudi katika hali zao halisi huku wengi wakirejea kwa ndugu na wengine kuishi pamoja ama wawili au watatu.
Upendo katika familia
Inaelezwa kuwa hali ngumu ya maisha imeongeza upendo baina ya wanandoa na familia kwa ujumla kutokana na muda mwingi kuwa pamoja huku waliokuwa wakichelewa kurejea nyumbani wakiacha tabia hiyo.
“Kwa kweli hali ya maisha imesababisha mume wangu kurudi nyumbani mapema na siku za mwisho wiki na nyakati za sikukuu tunakuwa pamoja na watoto jambo ambalo halikuwapo, maana alikuwa akirudi usiku tena akiwa amelewa,” anasema Edina Njiku.
Anasema kwa sasa wanaishi kwa upendo na mume wake na pindi mshahara unapotoka ushirikiana pamoja kupanga mambo ya msingi ya kufanya.
Anasema kwa sasa hulazimika kutumia gari moja kwenda na kurudi kazini na mara chache sana kila mmoja hutumia usafiri wake, jambo ambalo anasema linazidisha upendo katika familia yao.
“Awali nilikuwa nikishiriki kuchangia harusi na ‘kichen part’ kila wiki na kununua nguo mpya kila wakati kwa ajili ya shughuli hizo lakini sasa naangalia zile za muhimu,” anasisitiza

No comments:

Post a Comment