Monday, November 6

Shamba la mke wa Sumaye lapangiwa utaratibu wa mgawo


Serikali imeeleza utaratibu utakaotumika kuligawa shamba la eka 326 lililokuwa likimilikiwa na mke wa Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye.
Agosti, mwaka huu Serikali ilibatilisha umiliki wa eka zaidi ya 14,000 za mashambapori mkoani Morogoro ambapo eka zaidi ya 3,000 zipo wilayani Mvomero. Miongoni mwa mashamba yaliyobatilishwa ni lile lililokuwa likimilikiwa na mke wa Sumaye, Esther.
Akizungumza na Mwananchi, mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, Florent Kyombo alisema halmashauri inategemea kugawa viwanja vya makazi katika shamba hilo.
“Lile shamba lililokuwa la mke wa Sumaye lipo eneo la mji, hivyo halitagawanywa kama shamba. Pale tutapima viwanja na utaratibu wake utatolewa baada ya upimaji,” alifafanua Kyombo.
“Tukikamilisha upimaji tutatoa tangazo kuwa yeyote anayehitaji ardhi katika wilaya yetu atume maombi kwa mkurugenzi wa halmashauri na ndipo ugawaji utakapoanza.”
Kauli hiyo ya mkurugenzi wa halmashauri hiyo imekuja baada ya kuwapo kwa malalamiko ya wananchi juu ya ukimya wa Serikali kuhusu ugawaji wa mashambapori yaliyofutiwa umiliki wilayani humo.
Kyombo alisema kwamba wananchi hawapaswi kuwa na hofu kwa kuwa ugawaji utafanyika kwa uwazi na kwa kufuata taratibu zote za kiserikali.
“Kwanza tunafanya uthamini wa kiasi cha uendelezaji uliofanyika katika mashamba haya ili tuweze kuwafidia wamiliki wake kwa kuwa sheria inatutaka kufanya hivyo,” alisema.
Mkurugenzi huyo alisema katika fidia hiyo haimaanishi kwamba wananchi hao watapewa fedha, bali watapatiwa maeneo yanayolingana na yale waliyoyaendeleza.
Alisema taratibu za awali za uthamini zikishafanyika wananchi watatangaziwa ili waombe mashamba hayo ambayo yatauzwa kwa Sh100,000 kwa eka.
“Tutagawa mashamba kwa ajili ya kilimo na pia kuna maeneo tutapima viwanja kwa ajili ya makazi na maeneo mengine yatakuwa ya viwanda,” alisema.
Hivi karibuni wananchi wilayani humo walilalamikia kutoshirikishwa katika ugawaji wa mashambapori yaliyotaifishwa na Serikali.

No comments:

Post a Comment