Nairobi, Kenya. Katika kile kinachoweza kutafsiriwa kuwa siasa si uadui, ‘mahasimu’ watatu wa uchaguzi uliofanyika mara mbili nchini Kenya wamekutanishwa na kanisa, lakini hawakupata fursa ya kuzungumza hadharani.
‘Mahasimu’ hao walikutana jana katika hafla ya kuadhimisha karne moja ya Kanisa la Anglikana iliyofanyika mjini hapa.
Rais Uhuru Kenyatta, kiongozi wa muungano wa Nasa, Raila Odinga na Jaji Mkuu, David Maraga ambao wamegeuka kuwa ‘mahasimu’ walikutana katika hafla ya ibada iliyoongozwa na kiongozi wa Anglikana duniani, Askofu wa Canterbury, Justin Welby kwenye kanisa kuu la Nairobi.
Kwa pamoja, viongozi hao ambao wametikisa siasa za Kenya kuanzia mwezi Agosti, walikutana na kusimama pamoja mstari katika hafla hiyo iliyohutubiwa na Askofu Welby aliyewataka Wakenya kuwa na maridhiano.
Kenyatta alisimama kulia kwa Askofu Welby wakati Odinga alisimama kushoto wakati kiongozi huyo wa kanisa alipokuwa akitoa baraka nje ya kanisa.
Wanasiasa hao wamekuwa na uhasama wa kisiasa kufuatia uchaguzi wa Agosti 8 ambapo Jaji Mkuu Maraga akiwa kiongozi wa jopo la majaji wa Mahakama ya Juu lililofikia uamuzi wa kutengua ushindi alioupata Kenyatta na kuamuru uchaguzi urudiwe.
Kufuatia uamuzi huo, Kenyatta ambaye pia ni kiongozi wa Jubilee alimshutumu Jaji Maraga na majaji wenzake waliofikia uamuzi huo kuwa hawakumtendea haki. Pia alimlaumu Odinga kwa kutumia ‘mbeleko’ ya mahakama ili kubebwa kisiasa.
Hata hivyo, Maraga na Odinga mara zote wamekuwa wakisema ushindi wa Kenyatta ambaye pia alishinda uchaguzi wa marudio Oktoba 26 uliosusiwa na Odinga, kuwa ulikiuka sheria na taratibu za uchaguzi.
Askofu alilia maridhiano
Akizungumza katika hafla hiyo ya kuadhimisha miaka 100 ya kanisa hilo akiwa na wanasiasa hao na Jaji Maraga waliokutana mara ya kwanza tangu kumalizika kwa uchaguzi huo, Askofu Welby alisema maridhiano ni jambo muhimu kwa Wakenya na kwamba tangu walipopata Uhuru wametunza amani na utulivu nchini mwao, hivyo hawapaswi kuviacha viondoke.
“Tangu uhuru, Kenya imekuwa mfano Afrika. Ndiyo, pamoja na matatizo na majaribu lakini kwa sehemu kubwa mmeitunza amani. Tunahitaji mfano wa maridhiano si tu katika nchi hii, lakini katika eneo lote ambalo (Kenya) ni kiongozi,” alisema.
Hii ni mara ya kwanza Odinga kukutana ana kwa ana na Kenyatta tangu kumalizika uchaguzi wa Agosti 8 na Oktoba 26, lakini ni mara ya pili Kenyatta kukutana na Jaji Maraga.
Kenyatta na Maraga walikutana Oktoba 20 katika maadhimisho ya Mashujaa kwenye viwanja vya Uhuru jijini Nairobi, sherehe ambazo Odinga alisherehekea Bondo na Kisumu alikofanya harambee kuwachangia walioathiriwa na vurugu za baada ya uchaguzi.
Kwa Askofu Welby hii ni mara ya pili kuitembelea Kenya. Februari 2017 alikuwa nchini humo katika uzinduzi wa sherehe hizo za kuadhimisha miaka 100.
No comments:
Post a Comment