Baada ya kuingia madarakani, ziara yake ya kwanza ya kushtukiza ilikuwa Novemba 6, 2015 katika Wizara ya Fedha ambako alisisitiza masuala ya fedha na uchumi. Ziara ya pili ya kushtukiza aliifanya Novemba 9, 2015 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alikokutana idadi kubwa ya wagonjwa wakilala sakafuni kwa kukosa vitanda.
Mbali na uhaba wa vitanda vya wagonjwa pia alikuta mashine mbili za MRI na CT-Scan zikiwa mbovu na alitoa agizo zitengenezwe. Serikali ilitoa fedha za kukarabati mashine hizo, lakini kwa upande wa vitanda aliagiza kumegwa fedha za mchapalo wa kupongeza wabunge zigharamie upungufu huo.
Sh225 milioni zilipatikana kutoka kwenye fungu la hafla ya wabunge na kufanikisha kununuliwa vitanda 300 na magodoro yake, mashuka 600, baiskeli za kubebea wagonjwa na vifaa vingine.
Mbali na Muhimbili, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ameeleza mara kadhaa jitihada za Serikali katika kuboresha huduma kwenye hospitali, vituo vya afya na baadhi ya zahanati nchini ikiwamo kuongeza wodi za wagonjwa.
Ummy anasema Serikali ya Rais Magufuli ilitoa msaada wa vitanda vya wajawazito, vitanda vya wagonjwa, magodoro na mashuka kwa wilaya zote 183 nchini. Vifaa hivyo ni vitanda vya kawaida 3,660, magodoro 3,660, mashuka 9,150 na vitanda vya wajawazito 915.
Kwa idadi hiyo kila halmashauri itapata vitanda 20 na magodoro yake, vitanda vya kuzalishia vitano na mashuka 50.
Matibabu ya kibingwa
Kipindi cha miaka miwili ya JPM, amefanikiwa kuanzisha huduma mbalimbali za kibingwa ikiwamo kuboresha Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na Kitengo cha Mifupa (MOI) ambako huduma za kambi za upasuaji ziliendelezwa ikiwamo kukamilisha jengo jipya la kitengo hicho.
Pia, kilianzishwa kitengo cha upandikizaji vifaa vya usikivu ambacho kimeanza kutoa huduma ya upasuaji kwa watoto wasiosikia na kuwawekea vifaa vinavyowawezesha kusikia.
Awali gharama za kupandikiza kifaa cha usikivu kwa mtoto mmoja ilikuwa kati ya Sh80 milioni hadi Sh100 milioni nje ya nchi
Pia, kitengo cha huduma za upandikizwaji na usafishwaji wa figo katika hospitali ya Muhimbili kimekamilika kwa asilimia 100, huku wataalamu watakaotoa huduma wakiwa tayari wameanza mafunzo ya namna ya kutumia miundombinu iliyopo.
Kitengo hicho kinatarajiwa kuokoa zaidi ya Sh12.4 bilioni ambazo Serikali ingezitumia kwa kipindi cha miaka mitatu kwa kusafirisha wagonjwa wa figo 160 nje ya nchi kwa matibabu.
Kuanzishwa kwa kitengo hicho, kutaifanya hospitali hiyo kuwa na vitengo muhimu vinne, ikiwemo Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Kitengo cha Mifupa (MOI), figo na Kitengo cha upandikizaji wa vifaa vya usikivu.
Upatikanaji wa dawa nchini
Novemba 2015 Magufuli alitoa maagizo kwa Wizara ya Afya, kuhakikisha dawa na bidhaa nyinginezo kwa ajili ya hospitali za umma nchini zinanunuliwa moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji badala ya kupitia kwa mawakala.
Vilevile, alirudia maagizo hayo alipotimiza mwaka mmoja madarakani, akilenga kuipunguzia Serikali gharama na kuhakikisha dawa zenye ubora zinapatikana kwa bei nafuu na hivyo kupunguza mzigo kwa wananchi.
Kutekeleza agizo hilo, Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017 kupitia Bohari ya Dawa (MSD) ilianza kununua dawa na bidhaa nyinginezo moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji.
Hatua ya kununua dawa moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji imesaidia kupunguza gharama za kununua dawa kwa asilimia 15 hadi 80. Vituo vya afya vya kutolea huduma za afya pia vinaweza kuagiza mahitaji yao zaidi na kwa bei nafuu.
Unafuu huo wa bei kiuhalisia umeanza kuonekana kuanzia Julai Mosi 2017, ambapo wazalishaji walianza kuleta dawa nchini. MSD imeweza kukuza mtaji wake na kuendelea kuagiza dawa kutoka kwa wazalishaji, bei ya dawa itaendelea kupungua na halmashauri zitaweza kuagiza dawa zaidi na hivyo kutatua kwa kiasi kikubwa changamoto ya uhaba wa dawa vituoni.
Mpaka sasa MSD imeingia mikataba na jumla ya wazalishaji 110 na kati ya hao wazalishaji wa ndani ni 10 sawa na asilimia 9. Wazalishaji wa nje wanatoka nchi mbalimbali zikiwamo Kenya, Uganda, India, Denmark, Ufaransa, Ujerumani, China, Afrika Kusini, Nchi za Falme za Kiarabu na Bangladesh.
Kubadilisha vifungashio vya dawa
Kwa kipindi kirefu tangu kuanzishwa kwake, MSD ilikuwa inasambaza dawa hasa aina ya vidonge zikiwa kwenye makopo, kisha wagonjwa walifungashiwa kwenye vibahasha maalumu.
Kuanzia Mwaka wa Fedha 2017/2018, MSD imeanza kuagiza dawa kutoka kwa wazalishaji zikiwa zimefungashwa kwa mfumo wa blister pack ili kuendana na maelekezo ya Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA).
Hatua hii, imewawezesha watumiaji kutunza dawa katika hali ya usafi na salama zaidi kwa mujibu wa miongozo ya utunzaji inayokubalika kimataifa.
Mkurugenzi wa Bohari ya Dawa (MSD), Laurean Bwanakunu anasema hali ya upatikanaji wa dawa nchini imeendelea kuimarika ambapo kwa sasa ipo kati ya asilimia 80 na 85 kwa dawa muhimu 135, zinazohitajika katika vituo vya Serikali vya kutolea huduma za afya nchini.
Bwanakunu anasema katika kutekeleza kaulimbiu ya Tanzania ya Viwanda na kujenga uwezo wa wazalishaji wa ndani, MSD ilitangaza zabuni maalumu ya kununua dawa, vifaa na vifaa tiba ambayo iliwalenga wazalishaji wa ndani pekee kwa kufuata sheria na kanuni za ununuzi wa umma.
Anasema matokeo ya zabuni ya wazalishaji wa ndani imeiwezesha MSD kuingia mikataba ya ununuzi wa dawa na bidhaa nyinginezo kutoka kwa wazalishaji mbalimbali nchini.
Kuhusu bajeti ya dawa, Bwanakunu anasema katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Magufuli, kumetokea mabadiliko makubwa ambapo Serikali ilitenga bajeti ya kutosha kukidhi mahitaji ya dawa nchini ikilinganishwa na miaka iliyotangulia.
“Kwa mfano, Mwaka wa Fedha 2016/17 ilikuwa Sh251.5 bilioni na Mwaka wa Fedha 2017/18 bajeti iliyotengwa kwa ajili ya dawa na vifaa tiba ni Sh269 bilioni. Tofauti kubwa inaweza kuonekana kutoka Sh29 bilioni zilizotengwa mwaka 2015/16.
Anasema kufuatia upatikanaji wa dawa hospitalini, MSD imeanzisha maduka ya dawa kwenye baadhi ya hospitali za rufaa na mkoa. Hatua hiyo ni utekelezaji agizo la Rais.
“Maagizo hayo yalilenga kusogeza huduma ya dawa karibu na wananchi wa hali ya chini ambao hapo kabla walilazimika kununua dawa mitaani kwa bei kubwa.”
Maduka haya yapo ndani ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Sekou Toure ndani ya Hospitali ya Mkoa wa Mwanza, Mbeya (karibu na Hospitali ya Mkoa ya Mbeya), Mount Meru ndani ya Hospitali ya Mkoa wa Arusha, Chato (Hospitali ya Wilaya ya Chato) Mkoani Geita, Ruangwa ndani ya Hospitali ya Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi, Mpanda mkoani Katavi.
Hata hivyo, anasema MSD iko mbioni kufungua maduka ya aina hiyo mikoani Ruvuma na Shinyanga.
Ukiacha mabaduiliko hayo, kwa ujumla yapo mengine mengi ambayo yamefanyika katika Sekta ya afya, kama vile nidhamu ya watumishi, yanayoonyesha kwamba Dk Mafuguli ni championi ya mabadiliko kwenye sekta hiyo.
No comments:
Post a Comment