Monday, November 6

Mbunge CCM aonyesha hofu kuidadisi Serikali


Mbunge wa Mpendae (CCM), Salim Hassan Turky ameeleza hofu waliyonayo baadhi ya wabunge ya kuhojiwa wanapoonekana kuihoji au kuidadisi Serikali.
Turky alitoa kauli hiyo jana mjini Dodoma wakati wa semina ya wabunge kuhusu jukumu la Bunge katika kufuatilia kikamilifu matumizi ya Serikali ambayo ilishirikisha kamati sita za Bunge.
Kamati hizo ni Bajeti; Kilimo, Mifugo na Maji; Viwanda, Biashara na Mazingira; Huduma na Maendeleo ya Jamii; Utawala na Serikali za Mitaa; na Hesabu za Serikali za Mitaa (Laac). Pia, watumishi wa Bunge walishiriki.
Turky akichangia katika semina hiyo alisema kuna jambo ambalo linamsumbua bungeni, “Unapoanza kuhoji na kudadisi unaitwa kuhojiwa. Utachangiaje wakati ukizungumza kitu au ukidadisi unaitwa na kuhojiwa?” alihoji.
Ingawa Turky hakusema wanakoitwa kuhojiwa kama ni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Jeshi la Polisi, CCM au kamati za Bunge, kumekuwa na matukio ya hivi karibuni ya baadhi ya wabunge kuhojiwa kutokana na kauli zao.
Tukio la karibuni ni la Polisi kumhoji kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe.
Tayari Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Mjini leo ataripoti Kituo cha Polisi cha Chang’ombe jijini Dar es Salaam na kesho atakwenda kitengo cha upelelezi wa masuala ya uhalifu wa makosa ya kifedha ambako anakabiliwa na makosa matatu.
Anatuhumiwa kutoa lugha za kichochezi katika mkutano wa kampeni za udiwani Kata ya Kijichi Oktoba 29 na alihojiwa Kituo cha Polisi Chang’ombe Novemba 2, siku ambayo pia alihojiwa na kitengo cha upelelezi wa makosa ya uhalifu wa kifedha kwa makosa mawili ya kukiuka sheria ya mitandao na ya takwimu.
Sakata hilo limechukua sura mpya baada ya chama hicho kusema jana kwamba wajumbe wote wa Kamati Kuu ya ACT- Wazalendo wametakiwa kwenda kitengo hicho.
Hata hivyo, kaimu mwenyekiti wa chama hicho, Yeremia Maganja aliwaambia waandishi wa habari kwamba, “Ni vigumu kuwakusanya wajumbe wote na kuwapeleka polisi, tutawawakilisha mimi na kiongozi wa chama (Zitto).”
Mbali ya Zitto, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) ameshahojiwa mara kadhaa na Jeshi la Polisi kutokana na kauli zake ambazo zimekuwa zikielezwa kuwa ni za uchochezi. Amefunguliwa kesi mahakamani na zingine upelelezi wake unaendelea.
Akichangia mada katika semina hiyo, Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini alisema tatizo sio uwezo wa wabunge katika kuchangia na kuisimamia Serikali, bali ukosefu wa fedha ambao ungewawezesha wabunge kuwa na watafiti wa kuwasaidia katika mambo ya kuzungumza bungeni ambayo wananchi wanayataka.
“Tukitaka kuimarisha Bunge, ni lazima mfuko wa Bunge ambao tumeupigia kelele kwa muda mrefu uwepo. Yaani Bunge lisipate fedha kwa hisani ya Serikali, kwa hisani ya Hazina. Na ndiyo maana wabunge tunatakiwa kufanya kamati wiki mbili lakini tunashuhudia wiki moja kwa sababu fedha hamna,” alisema Selasini.
Alisema jambo jingine linalowafanya wabunge kutosema yale wanayoyataka wananchi ni siasa kuingia bungeni tofauti na mabunge yaliyotangulia ambayo alisema wabunge walikuwa wakiacha siasa lango kuu la kuingilia bungeni.
Selasini alisema jambo hilo linaweza kusababishwa na viongozi wa Bunge au Serikali ambao hoja zenye manufaa zinaweza kupelekwa bungeni lakini wakaamua kuziua.
Kwa mtazamo wake, Mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Suleiman Bungara ‘Bwege’ alisema imefika mahali wabunge wanaosema hapana katika hoja bungeni Spika anataka wanyimwe maendeleo katika majimbo yao.
“Imefikia mahali wabunge wanaogopa kuikosoa Serikali kutokana na hali iliyopo sasa,” alisema.
Akijibu hoja, mtoa mada Deogratius Kirama kutoka Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali (NAOT), alisema Katiba imewapa mamlaka yote wabunge na kwamba inawezekana hawajaitumia vyema.
“Sijafanya utafiti kuhusu hili lakini Katiba imewapa mamlaka yote wabunge inawezekana hamjaitumia. Kama kuna uhitaji wa kanuni kuboreshwa ili kuongeza kinga hilo liko chini ya mamlaka yenu. Mpira uko kwenu,” alisema.
Kamati zajaa mapengo
Bunge linaanza vikao vyake huku likiwa na mapengo katika baadhi ya kamati kutokana na wenyeviti, makamu na mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Bunge nafasi zao kuwa wazi kutokana na waliokuwepo kuteuliwa katika Baraza la Mawaziri.

No comments:

Post a Comment