Baada ya mtu mmoja mwenye umri wa miaka 29 kuua watu wanane na kujeruhi makumi alipoendesha lori katikati ya umati mjini Manhattan katika tukio baya la kigaidi tangu Septemba 11, wakazi wamesema walikataa kutishwa.
Polisi jijini New York, mbali ya kutoa taarifa ya kukamatwa kwa dereva wake, wamesema kuwa gari hilo lilivamia watu lilipoendeshwa kwenye njia ya baiskeli na kusababisha vifo vya watu 8 na wegine 11 wakijeruhiwa.
Gari hilo liliwagonga waendesha baiskeli na watembea kwa miguu waliokuwa kwenye njia hiyo saa 9:00 mchana Jumanne. Pia polisi wanashuku kwamba tukio hilo lilikusudiwa na wanachunguza kisa hicho kama shambulio la kigaidi.
Vilevile, polisi wamesema mkononi dereva alibeba kile kilichoonekana kuwa bunduki baada ya kutoka ndani ya gari hilo na maofisa walimfyatulia risasi na kumkabili kwenye eneo la tukio.
Shirika la habari la ABC News na mashirika mengine ya habari yamesema mwanamume huyo ni mhamiaji kutoka Uzbekistan na wakati akikamatwa alipaza sauti akisema "Mungu ni Mkubwa" kwa lugha ya Kiarabu.
Saa kadhaa baada ya shambulio hilo, familia ziliendelea na sherehe zao za kitamaduni huku kukiwa na ulinzi wa polisi wenye silaha wakati maofisa wengine wa polisi wakiendelea kufanya uchunguzi wa tukio lile.
"Hiki ni kitendo cha kigaidi, na kwa upekee ni kitendo cha woga,” alisema meya wa New York Bill de Blasio. "Tukio hili liliwalenga raia wasio na hatia, watu wanaoishi maisha ya kawaida ambao hawakuwa wanajua kama walikuwa wamekusudiwa."
Maofisa wawili wa polisi wamethibitisha kwamba mtuhumiwa ametambuliwa kuwa ni Sayfullo Habibullaevic Saipov. Aliendesha gari alilokodi kwenye mtaa wenye shughuli nyingi wa watembea kwa baiskeli katika na jengo la World Trade Center akaligongesha kwenye basi la shule kisha akatoka akitishia kwa bunduki. Polisi mmoja alimtwanga risasi tumboni na akapelekwa hospitalini alikofanyiwa operesheni.
No comments:
Post a Comment