Wednesday, November 1

Hofu kubwa Kenya baada ya uchaguzi


Naionea huruma Kenya, nchi niliyoishi miaka sita ya maisha yangu nikiwa kijana (1971-1977), katika enzi ya Mwasisi wa taifa hilo, Jomo Kenyatta. Ni nchi iliyowekewa matumaini makubwa pale ilipopata uhuru mwaka 1963 toka ukoloni wa Mwingereza.
Ukombozi huo haujaja kwa urahisi kama vile wa nchi jirani za Tanganyika na Uganda. Damu nyingi ya Waafrika ilimwagika Kenya. Kama ilivyo kawaida katika harakati za ukombozi, pia Kenya kulikuwako Waafrika waliogeuka kuwa wahaini kwa kuwasaidia Waingereza. Lakini, makabila yote yalikubaliana kwamba kazi ya mwanzo na muhimu ni kumtimua mkoloni aliyewaibia ardhi yao. Mengine yangefuata baadaye.
Jaramogi Oginga Odinga (Baba yake Raila Odinga) alijitolea kupigania kutolewa kizuizini Jomo Kenyatta. Kaulimbiu ilikuwa: Kwanza Kenyatta awe huru, halafu Uhuru wa Kenya baadaye. Alishinda. Mwaka 1963 Kenyatta akawa waziri mkuu wa kwanza wa Kenya na baadaye akawa rais, mtu ambaye miaka michache kabla wakoloni wa Kiingereza walimuita kuwa ni kiongozi wa giza na machafuko. Odinga akawa makamo wake.
Haijapita muda taifa jipya la Kenya likashuhudia mvutano baina ya Kenyatta na Odinga. Mvutano huo ulichochewa zaidi na Vita Baridi wakati huo baina ya kambi za Mashariki (ikiongozwa na Urusi) na Magharibi (ikiongozwa na Marekani). Kenyatta alidaiwa amebadilika roho, akipokea amri kutoka Washington na London, huku akiwasahau Wakenya wanyonge waliomsaidia katika harakati za kupigania uhuru. Alituhumiwa “kuiuza” Kenya kwa wakoloni wa zamani kutokana na “uroho wake” wa kutaka kujitajirisha kwa haraka, yeye na jamaa zake.
Jaramogi Odinga alihisi Jomo Kenyatta ameisaliti ndoto ya Wakenya wengi kutaka kuwa huru “kikweli” na si kutosheka tu na kuishusha chini bendera ya kikoloni na kuipandisha juu ile ya taifa.
Kilio kikubwa cha Wakenya kilikuwa kutaka kumiliki ardhi, lakini baada ya uhuru ardhi iliyokuwa hapo kabla ikihodhiwa na Waingereza iliangukia mikononi mwa Waafrika wachache waliojigeuza kuwa mabwanyenye wapya. Cha kushangaza ni kwamba baadhi ya Wakikuyu walioshirikiana na Waingereza kuisaliti dhana ya ukombozi ndio waliokula matufaa ya uhuru, japokuwa si wao waliopanda mitufaa hiyo.
Nilipokuwa Kenya nilitambua jambo moja muhimu, nalo ni kwamba Wakenya walikwepa kuzungumzia hadharani tatizo ambalo walilijua kwamba wanalo: Ukabila. Viongozi wao walijitoa kimasomaso na kujidanganya ati kwamba ukabila hauko katika jamii yao. Walijifanya kusahau kwamba Kenya si taifa moja, ndani yake kuna mataifa kadhaa, mengine makubwa yenye mamilioni ya watu. Kuna Wakikuyu na wajomba zao-Waembu na Wameru – Waluhya, Wajaluo, Wakamba, Wasomali, wamijikenda, na wengineo.
Baada ya uhuru katika enzi ya Kenyatta aliuawa kiongozi kijana, tena mashuhuri na mwenye mvuto, Tom Mboya (Mjaluo). Pia, wakati wa utawala wa Rais Daniel arap Moi (Mkalenjini) aliuawa kwa njia ya ajabu kabisa aliyekuwa Waziri wa mambo ya kigeni wa Kenya, Dk Robert Ouko ambaye alikuwa mjaluo. Wajaluo hao wawili walikuwa wanasiasa waliong’ara wakati wao na walikuwa ni tishio kwa viongozi wa makabila mengine kwamba siku moja wangeweza kuvaa viatu vikubwa vya urais wa nchi.
Jomo Kenyatta alipokwenda Kisumu ilipo ngome ya familia ya Jaramogi Odinga. Kulitokea vurugu wakati Kenyatta alipotaka kuhutubia hadhara. Watu kadhaa waliuawa na polisi, ikisingiziwa kwamba kulikuwako jaribio la kutaka kumuua Kenyatta. Hadithi hiyo haikuwa kweli hata kidogo, lakini ilikusudia kuwatia dosari viongozi wa kijaluo akiwamo Jaramogi Odinga.
Tangu wakati huo siasa za Kenya zimezidi kuwa za kikabila, kinyume kabisa na ilivyo Tanzania. Nchini Kenya watu kwanza huagalia jina la mwisho la familia yako, wanataka kutambua wewe ni wa kabila lipi kabla ya kukupatia ajira au msaada wa kupata masomo ya juu. Ni sasa ambapo Wakenya wanazungumza hadharani kwamba saratani ya ukabila imesambaa karibu mwili mzima wa taifa lao. Chama cha Jubilee kinachotawala sasa na ambacho kiliundwa harakaharaka na rais wa sasa, Uhuru Kenyatta na makamo wake, William Ruto, ni ushirika wa watu hao wawili katika kukabiliana na kesi dhidi yao kutokana na machafuko ya uchaguzi wa 2007. Walifikishwa mbele ya Mahakama ya Jinai ya Kimataifa (ICC) iliyopo The Hague, Uholanzi. Ushirika huo pia ulikuwa na harufu ya kikabila baina ya makabila makuu mawili ya Kenya, Wakikuyu na Wakalenjini ili kuzuia tamaa ya Raila Odinga kutaka kuwa rais wa nchi. Naye Odinga alihisi kwamba kuufikia urais inambidi aunde ushirika na makabila mengine makubwa. Akampata Kalonzo Musyoka kuwa mgombea mwenza wake katika kinyanganyiro cha urais na pia Moses Wetangula na Musalia Mudavadi kuwa wandani wake. Huwezi kusonga mbele katika siasa nchini Kenya bila ya kutegemea kwanza kabila lako.
Kuna dhana iliyojengeka katika nchi hiyo kwamba rais akiwa wa kutoka kabila fulani basi watu wa kabila lake ndio watakaofaidika mwanzo kabisa na wasiokuwa wa kabila hilo watatoka patupu yanapokuja masuala ya nyadhifa serikalini na pia kugawanywa rasilimali za nchi.
Kenyatta ataendelea kuwa rais wa nchi, hasa baada ya kutangazwa mshindi na IEBC katika uchaguzi wa marudio wa Oktoba 26 baada ya matokeo ya uchaguzi wa Agosti 8 kufutwa.
Suala kubwa ni kama Uhuru Kenyatta ataweza kutawala vilivyo na kuwa na heshima ya kuwa kiongozi mwenye kuwaunganisha Wakenya wote? Kenya hivi sasa imegawanyika zaidi kikabila kuliko ilivyokuwa kabla ya Agosti 8, imegawanyika zaidi Oktoba 26 kuliko ilivyokuwa Agosti 8 na sasa imegawika zaidi kuliko pale ulipoondoshwa mfumo wa chama kimoja cha kisiasa.
Wapinzani sasa si tu wanaobisha uhalali wa Kenyatta, lakini hata ule wa dola. Wameona kwamba uchaguzi wa marudio ulikuwa ni mzaha, wakidai huo haujawa uchaguzi lakini ni uchafuzi, ilikuwa ni kura ya maoni ya Jubilee kama wanamtaka Kenyatta ama sivyo. Wanamlinganisha Kenyatta na watawala wengine duniani wanaong’ang’ania madaraka licha ya kwamba wananchi wengi hawawataki. Utamaduni wa kisiasa wa Kenya, ambao licha ya kuweko ufisadi na baadhi ya wakati matumizi ya nguvu, ulisifiwa, ikilinganishwa na baadhi ya nchi za jirani. Sasa sifa hiyo inaanza kupotea.
Wanaosema hawataki kugawana mkate wa kiutawala, hata nusu mkate, au hata silesi moja, wanakosea, hawaitakii mema Kenya. Na wale wanaoamini kwamba mustakabali wa Kenya utaamuliwa tu barabarani na kupitia fujo pia wanakosea.
Wakenya, wengi wao wasomi na walio na utajiri katika ardhi yao, wataitupa bahati waliyopewa na Mwenyezi Mungu ikiwa wataendelea kuwa wafungwa wa ukabila. Raila Odinga sasa ameubadilisha muungano wake wa Nasa kuwa vuguvugu la kuikaidi Serikali. Pia, kuna viongozi wa Jubileee waliomlinganisha Odinga sawa na al-Shabbab, magaidi wenye siasa kali za Kiislamu kutoka Somalia. Pia, kuna watu wengi wanaotaka sehemu zao zijitenge kutoka Kenya. Hizo ni dalili za kutisha huko mbele.
Lakini, tusikate tamaa kabisa. Inawezekana kukatokea maajabu. Usishangae baadaye Kenyatta akayameza matapishi yake mwenyewe na kumuingiza Odinga katika Serikali yake. Tukumbuke baada ya machafuko ya uchaguzi wa 2007 Rais Mwai Kibaki alikubali Odinga awe waziri mkuu katika Serikali yake ya Umoja wa Kitaifa. Kwa hivyo, sitostaajabu kuona Odinga akipewa nusu mkate tena mara hii huku watu wakifikiria namna gani Kenya itawaliwe siku za mbele.
Kwanini isiwe hivyo? Bora nusu ya shari kuliko shari kamili. Ikitokea hali hiyo, wanasiasa hao wote wawili wanaweza kudai kwamba wamefanya hivyo kwa masilahi ya taifa. Pindi ukabila ukishindwa huko Kenya - jambo ambalo tulitazamie labda bada ya miaka 100 ijayo, basi Kenya itaweza kuwa pepo ya Afrika.
Dawa? Kenya lazima iwe nchi ambapo raia wana imani kwa Serikali yao. Katiba mpya iliyopitishwa mwaka 2010, ambayo ni nzuri sana, inahitaji iboreshwe zaidi- madaraka yazidi kupelekwa mashinani (kwenye County).
Kwa ufupi, Kenya inahitaji Mapinduzi ya kisiasa na kiuadilifu, lakini ya amani, bila ya kujali kabisa nani sasa anatawala. Bado hamna mtu anayejua katika nchi hiyo namna ya kulifikia jambo hilo. Nadiriki kusema kwamba Wakenya waiweke nchi yao mwanzo, juu kabisa ya makabila na koo zao, juu kabisa hata ya nafsi zao.
Kenya, ikiwa na wakaazi karibu milioni 50, ni dola inayoongoza katika Afrika Mashariki. Mji mkuu wake, Nairobi, ni moja kati ya miji ya kisasa kabisa barani Afrika, na uchumi wa nchi hiyo ni mkubwa. Si tu inategemea kutengeneza bidhaa kutoka mali ghafi au kutegemea makampuni ya kiserikali, lakini harakati zake za kiufundi na teknolojia ya mawasiliano ni za kupigiwa mfano.
Tabaka la katikati la watu wa nchi hiyo limewekewa matarajio makubwa duniani kwamba litaielekeza nchi hiyo katika uchumi wa kisasa. Zaidi ya hayo, Kenya ni mlango muhimu wa Afrika kuelekea Asia. Pale barabara na bandari zake zikizuilika kufanya kazi, basi eneo lote la Mashariki ya Afrika lita

No comments:

Post a Comment