Katika miaka ya hivi karibuni zimekuwapo taarifa mbalimbali za kusikitisha za kuongezeka idadi ya wanafunzi wanaotoroka au kuamua kutokwenda shule Zanzibar.
Hali hii imetolewa maelezo ya kila aina na viongozi wa Serikali, walimu na wazee katika nyakati mbalimbali.
Kuna wakati watu wa makundi haya wamekuwa yakinyoosheana kidole cha lawama.
Uchunguzi umeonyesha mahudhurio ya wanafunzi katika shule nyingi za Pemba huporomoka zaidi wakati wa msimu wa karafuu ambao huchukua zaidi ya mwezi mmoja.
Kisiwa cha Pemba huzalishwa zaidi ya asilimia 80 ya karafuu kwa Zanzibar na kwa kweli zao hili ndiyo tegemeo kubwa la kipato kwa wakulima wengi wa kisiwa hicho.
Mapato yatokanayo na karafuu ndio husaidia watu kujenga nyumba nzuri, kusomesha watoto wao na kukidhi mahitaji muhimu ya kila siku ya maisha.
Hapana ubishi hata kidogo kwamba mahudhurio mabaya ya shule ya wanafunzi huwa na matokeo mabaya ya masomo kwa wanafunzi na maisha ya baadaye kwa vijana mbao mahudhurio yao ya shule si mazuri.
Hapa suala la kujiuliza ni kwa nini hali ipo na inazidi kukua kila siku na nini kifanyike ili kuirekebisha? Njia pekee ya kupata suluhisho mwafaka ni kutafuta sababu na si kukurupuka kwa kutoa lawama hizi na zile, zikiwamo za kisiasa, na kufumbia macho mambo ya msingi yanayopelekea kuwapo kwa hali hii. Kwanza tuangalie hali ilivyo katika shule zetu badala ya kuendelea kujigamba tu kwamba elimu Visiwani inatolewa bila ya malipo.
Ukweli ni kwamba yapo matatizo mengi katika shule zetu, za Serikali na binafsi. Kwa mfano, madarasa katika shule nyingi za Visiwani, na hasa za Serikali, yana msongamano mkubwa.
Baadhi ya shule madarasa huwa na wanafunzi zaidi ya 100, wakiwamo wale wanaokaa chini na darasa moja kuwa na walimu wawili au watatu wanasomesha kwa wakati mmoja. Hii si hali ya kuridhisha au kufurahisha.
Suala la kumaliza tatizo la madawati limekiwa likisikika kila baada ya siku chache kwa zaidi ya miaka 20 sasa, lakini bado haujapatikana ufumbuzi na kinachosikika ni tupo mbioni kulimaliza.
Ukiuliza mbio hizi ni za nyika, masafa marefu ya kati au mafupi na zinaanzia wapi na kumalizikia wapi unaambiwa ni mjuba.
Mahudhurio ya walimu katika baadhi ya shule zetu ni mabaya na kwa kiasi fulani yanachangia kwa baadhi ya wanafunzi kuamua kutokwenda shule kwa vile badala ya kusoma wanakwenda kutumia muda mwingi kucheza.
Kwa hiyo, si ajabu wanafunzi hawa wanaotoroka wakawa wanaona bora wacheze nje ya shule kuliko kufanya hivyo madarasani. Hili nalo litupiwe jicho.
Hivi karibuni tu tumemsikia Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein akiahidi wakati alipokuwa na ziara kisiwani Pemba kwamba Serikali yake imeamua kuwafukuza kazi walimu wote watoro.
Hatua hii ninaipongeza kwa sababu haiwezekani kulipa mishahara walimu ambao hawafiki shule kusomesha watoto wetu.
Lakini, lipo jambo lilionishangaza. Nalo ni kumsikia Dk Shein akiwataka wakuu wa wilaya kuongoza zoezi hili la kuwatafuta walimu watoro kwa kufanya ukaguzi wa kina wa shule katika wilaya zao nakuwafukuza kazi watakaobainika kuwa watoro. Baada ya hapo nafasi za walimu watakaofukuzwa zijazwe na walimu wanaosubiri ajira.
Nimeshangaa kwa sababu wapo maofisa wanaoitwa wakaguzi wa elimu au waratibu wa elimu na moja ya kazi zao ni kuangalia mahudhurio ya walimu katika shule zilizokuwa chini ya mamlaka yao.
Sasa kama hawa wakaguzi hawaifanyi kazi hii kwa uadilifu na kwa mujibu wa majukumu waliokabidhiwa kwa nini na hawa nao wasikufuzwe kazi, au hapana watu wenye ujuzi wa kujaza nafasi zao kwa vile hawatimizi wajibu wao?
Labda hapa niulize: Je, kama madaktari na wauguzi nao watakuwa wanatoroka kazini itabidi na wakuu wa wilaya pia kuwashughulikia? Lazima utaratibu uliopo uruhusiwe kufuata mkondo wake.
Jambo jingine muhimu linalofaa kuzingatiwa kwa umakini ni ratiba (mihula) ya kufungua na kufunga shule Visiwani kama ni rafiki kwa wanafunzi. Hapa nataka kukumbusha kwamba hapo zamani shule zilikuwa zinafungwa kwa wakati wa msimu wa karafuu. Hii ilitokana na kuelewa kwamba huu ni wakati kwa watoto kusaidia wazee wao kujipatia kipato.
Wakati huu watoto walitumia muda kidogo kuokota karafuu zinazoanguka ambazo zinaitwa mpeta, kuanika karafuu asubuhi na kuzianua nyakati za jioni.
Bila ya shaka utaratibu wa ratiba ya shule ulipangwa wakati wa ukoloni na kuendelea kwa muda baada ya Mapinduzi ya 1964 kwa kuzingatia hali halisi ya Zanzibar na kuelewa kwamba shule zikiwa wazi wakati wa msimu wa karafuu patakuwapo mahudhurio mabaya ya wanafunzi, hasa kisiwani Pemba.
Hili nalo linafaa kuangaliwa upya, hasa wakati huu ambapo kila mtu analalamikia hali ngumu ya maisha. Kama iliwezekana kuwa na mpango wa shule kufungwa pale msimu wa kuchuma karafuu ulikiwa umepamba moto hapo zamani kumetokea nini hata ikawa hili haliwezekani haiwezekani siku hizi.
Wapo atakaosema kwamba si vizuri kushabikia ajira kwa watoto, lakini ajira ya mtoto ni jambo moja na kwa mtoto kutumia muda mfupi kumsaidia mzee wake wakati wa msimu wa karafuu ni jambo jingine.
Lakini jambo jingine muhimu ambalo linafaa kuzingatiwa ka undani ni kwamba kushiriki kwa watoto kwa muda mfupi kila siku katika harakati za kuokota au hata kuchuma na kuanika juani na kuanua karafuu zinawapa maarifa, kuwajengea uwezo na kuwapa uzoefu wa kulishughulikia zao hili vilivyo wanapokuwa wakubwa.
Tujifunze kwa uzoefu tuliopata katika miaka ya nyuma na hali tunayoiona hivi sasa. Tusione taabu wala aibu kukosolewa na tuwe tayari kujirekebisha ili tupate suluhisho la utoro uliopo katika shule
zetu, hasa wakati wa msimu wa karafuu.
No comments:
Post a Comment